Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 31 January 2016

VIWANDA VITANUSURU ZAO LA NYANYA IRINGA


Na Daniel Mbega, Iringa

CHINI ya miti ya mikaratusi, kando ya Mto Mlowa, vijana wanaonekana wakijaza nyanya kwenye matenga ya mbao huku pembeni yao kukiwa na malundo makubwa ya zao hilo.
“Hii ni hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini inaonekana yametoka thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika (masalo) ambazo haziwezi kwenda mahali popote,” anasema Jacob Kamota, mkulima wa nyanya kutoka Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.
Jacob analalamika kwamba, huko shambani pia ameacha malundo ya nyanya zisizofaa kusafirishwa, ingawa zinafaa kwa matumizi ya nyumbani au hata kwa kusindikwa, hali ambayo inazidi kumtia umaskini badala ya kujikwamua kiuchumi.
“Sina mahali pa kuzipeleka, laiti kungekuwepo na kiwanda ningeweza kuuza nyanya zote na kupata faida, lakini sasa hata gharama zangu sidhani kama zinaweza kurudi,” anasema.
Mkulima huyo anasema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja zilikuwa Sh. 1 milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga 80, lakini matenga 30 yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20 yakiharibika wakati alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya mto huu.
Bei ya soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000 tu kwa tenga moja, hivyo kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30 ambayo yalionekana yanafaa kusafirishwa.
Jacob ni miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa wanaojishughulisha na zao la nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Inaelezwa kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya, ambalo ndilo kuu la biashara mkoani Iringa, inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu bora, hasa barabara.
Wakulima ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo.
Hali hiyo imewafanya wakulima wengi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini, huku wengine wakipunguza ukubwa wa mashamba yao ama kutolima kabisa kutokana na kukosa uwezo wa kuyahudumia.
Maulid Kiboma ‘Papara’ ni mfanyabiashara ambaye anasema nyanya inayoharibika ni kiasi kikubwa zaidi kuliko inayofika sokoni.
“Nyanya ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa inakuwa masalo, hivyo inabidi ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.
“Kabla ya kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na kuyaacha masalo shambani, lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana matenga 10, anaweza kujikuta amebaki na manne tu ambayo ndiyo tunanunua,” anasema Papara.
Papara anasema, wafanyabiashara pia wanapoifikisha nyanya hiyo kwenye masoko makubwa, hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo kiasi kinachobakia kwa ajili ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya kilichozalishwa.
Anaongeza kwamba, wakati mwingine bei katika soko la Dar es Salaam inaporomoka kiasi kwamba hata wafanyabiashara wenyewe huamua kutonunua zao hilo kwa ajili ya kusafirisha kwa kuhofia kupata hasara.
Mfanyabiashara huyo anasema, bei inaposhuka katika masoko makubwa inakuwa hasara zaidi kwao wafanyabiashara wa kati, ambapo hata wakipewa nyanya hizo bure na wakulima hawawezi kuchukua.
“Suluhisho pekee litakalomkomboa mkulima ni kujenga kiwanda cha kusindika matunda na mboga mboga ili wakulima waweze kuuza nyanya zote na kukuza kipato chao,” anasema.
Anasema kiwanda pekee cha Dabaga kilichoko Iringa mjini hakitoshelezi, hivyo kuitaka serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria namna ya kuwakomboa wakulima hao.
Masoud Said, mfanyabiashara wa nyanya kutoka Dar es Salaam, anasema serikali, pamoja na kufikiria kujenga viwanda, lakini pia ijenge masoko ya uhakika vijijini ambayo yatawafanya wakulima wawe na mahali pa kupeleka bidhaa zao badala ya eneo la sasa lililoko katikati ya vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata hiyo ya Image.
“Walikuja hapa watu sijui wa Techno Save, wakajenga kijibanda kidogo pale Iyayi kwamba ndilo soko. Pale wamewachezea tu wananchi na kutafuna bure fedha za mradi kwa sababu nyanya zinazozalishwa kwenye maeneo haya ni nyingi kuliko kijibanda kile.
“Jambo jingine ni kujenga barabara imara ambazo zitapitika katika majira yote, tofauti na sasa ambapo barabara ya kutoka Ilula hadi huku Image iko kama mgongo wa mtumbwi kiasi ambacho magari mawili hayawezi kupishana,” anaongeza Masoud.
Martin Kazingumu Kutika, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Image, akizungumzia changamoto ya soko la nyanya, anasema inawatesa wakulima wengi, ingawa juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali kuboresha mazingira ya soko hilo.
“Nyanya nyingi zinaharibika japokuwa wakulima wanakuja huku kuzifuata. Bei nayo inapanda na kushuka kiasi kwamba ni vigumu kwa mkulima kunufaika moja kwa moja,” anasema.
Anaongeza kwamba, kujengwa kwa soko katika Kijiji cha Iyayi kutapunguza kero kwa wakulima na wafanyabiashara, kwani eneo lililopo soko la sasa siyo rasmi na linamilikuwa na Shule ya Msingi Uhominyi.
Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, anakiri kuongezeka kwa uzalishaji wa nyanya mkoani humo, ambapo anasema kwa msimu wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817 zililimwa kwa umwagiliaji na tani 115,514 zilivunwa.
Hata hivyo, anasema changamoto ya masoko inaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama mashirika ya Techno Save, Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).
Anasema kujengwa kwa masoko hayo kutawawezesha wakulima kufikisha mazao yao mahali pamoja na kujua bei inayozunguka sokoni, hivyo kuwaepusha na walanguzi ambao wanawapunja.
“Kuna mwekezaji mmoja ambaye alikuwa amejitokeza kutaka kujenga kiwanda katika Kijiji cha Viwengi, ingawa sijajua amefikia hatua gani, lakini naamini kikijengwa kitasaidia uchumi hasa kwa zao la nyanya ambalo kwa kweli linategemewa na wakulima wengi mkoani Iringa,” anasema.
Lakini tayari kampuni ya Darsh Industries Limited inayozalisha bidhaa maarufu nchini za Redgold imekamilisha ujenzi wa kiwanda katika Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, takriban kilometa 12 kutoka Iringa mjini na iko katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji.
Mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo anayeshughulikia masuala ya ujenzi huo, Pratap, anasema uzalishaji utakapoanza kiwanda hicho kitahitaji jumla ya tani 200 (kilogramu 200,000) za nyanya kwa siku, sawa na kreti 4,500 au magari 20 aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba tani 10 kila moja.
“Tunahitaji tani 200 kwa siku, ndio uwezo wa kiwanda, na tunawahakikishia wakulima kwamba soko la uhakika litapatikana wala wasiwe na hofu,” anasema Pratap.
Ofisa huyo anasema, kiwanda kitanunua nyanya za madaraja yote bila kubagua, hivyo hakutakuwa na ‘masalo’ yatakayomwagwa na kwamba wakulima wawe na imani watapata tija kutokana na kilimo hicho.
Anaongeza kusema kwamba, watapeleka makreti ya kubebea nyanya kwenye vituo vyote vya kukusanyia zao hilo ambavyo vitateuliwa na kwamba wakulima hawatagharamia usafiri wa kupeleka kiwandani.
“Wakulima kazi yao itakuwa kupeleka nyanya kwenye vituo ambako tutakuwa tumepeleka makreti ya kubebea, usafiri utakuwa ni juu ya kiwanda,” anafafanua na kuongeza kwamba, pamoja na kununua nyanya kwa wakulima, ambayo ni malighafi ya kiwanda hicho, lakini uongozi utatoa huduma za ugani kwa wakulima ukishirikiana na Mradi wa Tanzania Agricultural Productivity (TAPP) pamoja na maofisa ugani wa vijiji na kata husika linakolimwa zao hilo.
Ujenzi wa viwanda ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao yanayolimwa Tanzania ni moja ya ahadi za serikali ya sasa chini ya Rais John Magufuli, ikiwa na lengo pia la kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Aidha, uzalishaji wa bidhaa za ndani ukiimarika, kuna uwezekano wa kuuza bidhaa hizo nje, hivyo kuongeza pato la serikali pamoja na fedha za kigeni.

0656-331974

No comments:

Post a Comment