Profesa Ibrahim Lipumba akitetea jambo na Edward Lowassa siku kada huyo wa Chama cha Mapinduzi alipojiunga na Chadema/Ukawa Julai 28, 2015.
Lowassa akiwa na viongozi wa Chadema siku chama hicho kilipotangaza kumpokea Julai 27, 2015. Dk. Slaa anaonekana kushoto.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akimkabidhi kadi ya uanachama Edward Lowassa baada ya kujiunga Julai 28, 2015.
Na Daniel Mbega
TAFSIRI ya haraka ya neno ‘Propaganda’ ni
taarifa, mawazo au uvumi unaosambazwa kwa makusudi kumsaidia au kumharibia mtu,
kundi la watu, harakati, taasisi, taifa na kadhalika.
Propaganda pia inatafsiriwa kama namna ya
mawasiliano yanayolenga kuwashawishi baadhi ya watu waunge mkono jambo fulani.
Lakini tafsiri nyingine ya Propaganda ni
taarifa ambazo siyo sahihi zinazotumika kwa msingi wa kushawishi hadhira na
kuchochea agenda, mara nyingi kwa kuwasilisha taarifa zilizopangwa ama
kutengenezwa (pengine kudanganya hapa na pale) ili kuhamasisha kundi linalolengwa
liamini kinachoelezwa na liunge mkono.
Neno hili kwa sasa limebebeshwa mtazamo
hasi kwa kulihusisha na harakati za kurubuni kwa maslahi ya kundi linaloendesha
harakati hizo na kwamba wanaofanya propaganda wanaweza kuwaaminisha watu kwamba
ile rangi ‘nyeusi’ ni ‘nyeupe’ na kinyume chake.
Hata hivyo, asili yake ilikuwa ni ya usawa
na ilikuwa na malengo chanya, kama kuhamasisha masuala ya afya ya jamii, mabango
kuhamasisha jamii ishiriki kwenye sensa na uchaguzi, ama ujumbe kuwahamasisha
wanajamii kuripoti matukio ya uhalifu.
Pengine hakuna mtu katika historia
aliyetumia nguvu ya propaganda kwa mafanikio ya kutisha kama alivyofanya Paul Joseph
Goebbels, ambaye alikuwa Waziri wa Propaganda wa chama cha Nazi cha Ujerumani kati
ya mwaka 1933 hadi 1945 wakati wa Hitler. Wakati wote wa Vita Kuu ya Pili ya
Dunia, yeye ndiye aliyedhibiti mawasiliano yote nchini Ujerumani na kufanikiwa
kulibadilisha taifa lote kuwa kakamavu na la kijeshi.
Inaelezwa kwamba, isingekuwa mbinu za Goebbels,
chama cha Nazi kisingeweza kutawala Ujerumani kwani licha ya kuhamasisha magwaride
ya kijeshi, ndiye aliyewafanya Wajerumani wawe makatili hata wakati wa vita
kiasi cha kufanya mauaji ya kutisha, ikiwa ni pamoja na kuwateketeza Wayahudi.
Goebbels ndiye aliyehamasisha hadi
kuanzishwa kwa somo la propaganda shuleni, ambapo watoto walianza kuaminishwa
mambo mbalimbali tangu wakiwa wadogo, hata kama yalikuwa ya uongo.
Watoto walifundishwa na kulishwa uzalendo
kwamba Ujerumani ilikuwa ni ya Wajerumani tu, hivyo Wayahudi na watu wengine
hawakutakiwa kuishi humo!
Propaganda za Ukawa
Kiongozi wa chama cha National Socialism (au
kwa Kijerumani: Nationalsozialismus), ambacho ni maarufu zaidi kama Nazi, Adolf
Hitler, alitenga sura tatu za kitabu chake cha Mein Kampf kilichochapishwa 1925/26,
ambacho chenyewe ni silaha ya propaganda, katika somo na mafundisho ya propaganda.
Alidai alijifunza faida za propaganda wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia
kwamba propaganda za Waingereza zilikuwa na nguvu kuliko za Wajerumani. Mjadala
kwamba Ujerumani ilipoteza vita hivyo kwa sababu ya nguvu za propaganda za
Waingereza umeelezwa kwa kina kwenye kitabu cha Mein Kampf, na ndio ulioakisi
harakati za Ujerumani kupigania utaifa wao. Ingawa madai hayo ni ya uongo –
propaganda za Wajerumani zilikuwa na nguvu sana kwenye vita hivyo kuliko za
Waingereza – mjadala huyo ukawa ndio ukweli wa chama cha Nazi na kupandikiza ‘imani’
kwa Wajerumani kwa msaada wa Hitler.
Hitler anasema katika kitabu cha Mein Kampf
Sura ya VI (nanukuu kwa tafsiri ya Kiswahili): "Daima propaganda lazima ijidhihirishe kwa watu wengi. (...) Propaganda
zote lazima ziwasilishwe katika mfumo maalumu na lazima zijikite kwanza kwa wasomi
ili zisiwe juu ya vichwa vya watu wenye uelewa mdogo ambao ndio walengwa. (...)
Sanaa ya propaganda hasa inahusisha uwezo wa kuamsha matamanio ya watu kwa
ushawishi wa kutumia hisia zao, ili kutafuta mfumo mzuri wa kisaikolojia ambao
unaweza kuteka umakini na kuchochea msukumo mioyoni mwa wananchi wengi. Makundi
makubwa ya wananchi hayaundwi na wanadiplomasia au maprofesa wala hayahusishi
watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi baada ya tafakuri katika kadhia
husika, bali ni makundi ya vijana ambao wanayumbishwa na wazo moja baada ya
jingine. (...) Kundi kubwa la wananchi katika taifa lina tabia za kike na
mtazamo ambao mawazo na mwitikio wao unatawaliwa na huruma badala ya tafakuri
makini. Halitofautiani sana, lakini lina mtazamo hasi na chanya wa kupenda na
kuchukia, sahihi na isiyo sahihi, ukweli na uongo." Mwisho wa kunukuu.
Hapa Tanzania, vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) – Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD – vinaendesha propaganda
kubwa ya kisiasa ambayo haijapata kutokea tangu mfumo wa vyama vya siasa
ulipoanzishwa mwaka 1992.
Vyama hivyo vya upinzani, ambavyo Jumamosi
ya Septemba 15, 2007 pale kwenye Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es
Salaam – wakati huo vikiwa chini ya Umoja wa Vyama vya Upinzani – ndivyo vilivyofichua
orodha ya kutisha ya watu 11 mafisadi wanaolitafuna taifa.
Orodha hiyo ilitajwa na Dk. Willibrod Slaa
kwa niaba ya wenzake iliwataja Gavana wa zamani wa Benki Kuu Dk. Daudi Balali,
Rostam Aziz, Nimrod Mkono, Andrew Chenge, Basil Mramba, Gray Mgonja, Patrick Rutabanzibwa, Nazir
Karamagi, Edward Lowassa, Benjamin William Mkapa na Rais Jakaya Kikwete. Lowassa
akalazimishwa kujiuzulu Uwaziri Mkuu.
Hapo ndipo
propaganda za ‘Vita dhidi ya Ufisadi’ nchini zilipoanza na Chadema wakatumia
harakati mbalimbali wakizunguka kote nchini kuelezea kwamba Chama cha Mapinduzi
(CCM) kinawalinda mafisadi. Kila mahali walikokwenda waliita tafsiri ya CCM kuwa
ni ‘chama cha mafisadi’.
Propaganda hizi
zimesaidia kuinyoosha Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Kikwete, na
tuliweza kushuhudia vigogo wengi – mawaziri na wafanyabishara wakubwa
wasioguswa (the untouchables) – wakifikishwa mahakamani na baadhi yao hivi sasa
wako jela wanatumikia vifungo mbalimbali.
Mbali ya
kuendelea kufichua maovu ya watendaji wa serikali na kuilazimu kubadili Baraza
la Mawaziri mara kadhaa, lakini wapinzani wamesaidia – kwa propaganda hizo –
kuwahamasisha Watanzania kuielewa elimu ya uraia, haki zao za msingi na wapi
ambako serikali haitekelezi waibu wake. Haya ni mambo muhimu sana na ndiyo
majukumu ya upinzani kokote ulimwenguni. Kama wapinzani watashindwa kuyafanya
haya, basi hawajui wajibu wao.
Ni kwa mtaji
huo ndiyo maana Chadema iliweza kujiimarisha vyema hata uchaguzi mkuu wa mwaka
2010, ambapo mbali ya mgombea wake wa urais, Dk. Slaa, kushika nafasi ya pili,
lakini kwa mara ya kwanza iliweza kushinda majimbo 23 ya ubunge na kwa hivyo
kikawa ndicho chama kikuu cha upinzani bungeni. Lakini pia kilishinda madiwani
wengi na kuongoza baadhi ya halmashauri.
Ujio wa Lowassa Chadema
Ujio wa
Lowassa kutoka CCM kwenda Chadema baada ya mwasiasa huyo kuenguliwa katika mbio
za kuwania urais umeleta tetemeko katika siasa za Tanzania, maana ndiye mwanasiasa
pekee aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano kuweza kuthubutu kwenda
upinzani. Huko Zanzibar ilitokea kitambo wakati aliyepata kuwa Waziri Kiongozi
wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad, alipojitosa mapema
kwenye vyama vingi mwaka 1992.
Tetemeko la
Lowassa limekuwa na mafanikio makubwa kwa Chadema na Ukawa kwa ujumla, kwani
ameondoka na wanaCCM wengi waliokuwa wakimuunga mkono tangu mwanzo, hivyo
kuongeza idadi ya wanachama katika upinzani lakini pia imesaidia kulainisha
harakati za upinzani kuiondoa CCM madarakani.
Hata hivyo,
propaganda ambazo zimetumika tangu wakati huo zimewaacha watu wengi midomo
wazi. Chadema na Ukawa kwa ujumla hawataki tena kuzungumzia kuhusu ufisadi wa
Lowassa na kauli mbiu yao kubwa ni kwamba ‘Heri kuwa na fisadi mmoja kuliko
kundi la mafisadi’.
Yule yule ambaye
walimwita fisadi, leo hii ni ‘mtakatifu’ na kipenzi cha wengi. Kauli mbiu ya ‘Vita
dhidi ya Ufisadi’ ilikwisha muda wake kitambo na hakuna mpinzani yeyote kati ya
wanaounda Ukawa ambaye anathubutu kuitamka.
Ukawa wanachukua
jukumu la ‘kukanusha’ uhusika wa Lowassa kwenye mkataba tata wa kifisadi wa
kampuni za kufua umeme za Richmond na baadaye Dowans, kwamba hakuhusika bali
alitumwa. Hawazami kwa undani kuhusu nafasi ya Lowassa katika Serikali kabla
hajajiuzulu. Hawazungumzia kwamba, kama Lowassa alilazimishwa, na kama kweli
alikuwa mzalendo na hakupenda kulazimishwa, kwa nini hakujiuzulu kama
alivyofanya Ali Hassan Mwinyi!
Hakuna anayehoji
kwamba Lowassa amtaje basi mtu aliyemlazimisha, na ikibidi amtaje hata mmiliki
wa Richmond na hata Dowans.
Ukawa hawazungumzii
kabisa uadilifu wa Lowassa tangu akiwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC) na hata alipoingia kwenye Baraza la Mawaziri wakati
wa Awamu ya Pili ya Alhaj Mwinyi. Hawazungumzii mikataba mbalimbali ya kifisadi
iliyosainiwa kwa maazimio ya Baraza la Mawaziri wakati wa Awamu ya Tatu ya
Benjamin Mkapa huku Lowassa akiwa mmoja wa mawaziri hao.
Hata baada ya
waziri mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, kujiunga na Chadema, hakuna
anayethubutu kuelezea maovu ya Sumaye ambaye amekuwepo kwenye Baraza la Mawaziri
tangu mwaka 1985 hadi 2005.
Hakuna anayejisumbua
kuhoji ni kwa nini kilimo kiliyumba na vyama vya ushirika vilikufa wakati
Sumaye alipokuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika katika ya 1985 na 1994
kabla ya kuwa waziri kamili katika wizara hiyo mwaka 1994 hadi 1995
alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Hakuna anayehoji
ni kwa vipi yeye akiwa mtendaji mkuu wa serikali waliuza mashirika ya umma,
wakaua viwanda, wakajilimbikizia ardhi, mambo ambayo huyo huyo leo hii
anasimama kwenye majukwaa kuahidi kwamba Chadema ikiingia Ikulu itarejesha
viwanda hivyo. Ni propaganda.
Leo hii yeyote
atakayemsema vibaya Lowassa, Sumaye ama Ukawa, ndiye anayeshambuliwa kwa maneno
kwamba ama ametumwa au hataki mabadiliko, bila kuali kama mabadiliko
yanayozungumza na kushabikiwa ni ‘mabadiliko bora’ au ‘bora mabadiliko’.
Hapa pia
naikumbuka kauli ya Adolf Hitler katika kitabu hicho cha Mein Kampf kuhusu
mbinu zinazotumika kwenye propaganda, ambapo anasema (namnukuu): "Propaganda haihitaji kufanya uchunguzi wa ukweli wa jambo
(objectively) na, kwa namna inavyotamaniwa na upande na upande mwingine,
inatakiwa kuwasilishwa kwa mujibu wa nadharia ya utawala wa haki; lakini lazima
iwasilishwe kwa misingi ya ukweli ambao upande husika unataka. (...) Uwezo wa
wananchi wengi umedumaa, na uelewa wao ni mdogo. Kwa upande mwingine, ni wepesi
sana wa kusahau. Kwa msingi huo, propaganda zote zinatakiwa kujikita katika
mambo machache muhimu na hayo yanapaswa kuhubiriwa katika fomula nyepesi
inayofanana. Kauli mbiu hizo zinatakiwa kurudiwa kila wakati ili kumfanya mpaka
mtu wa mwisho aweze kuelewa na kushawishika na yanayosemwa. (...) Kila badiliko
linalofanywa kuhusu hoja fulani ya propaganda lazima kila wakati iwe na
suluhisho moja. Kauli mbiu kubwa lazima iwekwe katika njia tofauti na kwa namna
mbalimbali, lakini mwisho wa siku lazima kurejea kwenye fomula ile ile."
Agosti 6, 2015 Profesa Ibrahim Lipumba
alijivua uenyekiti wa CUF na kusema kwamba hawezi kuendelea kuwemo kwenye chama
hicho na umoja huo baada ya kumkaribisha Lowassa kwa kuwa dhamira yake
inamsuta.
Awali kabla ya ujio wa Lowassa, CUF
walikuwa wamejitenga kinyemela na ndiyo maana hata kikao cha Ukawa kilichofanyika
tarehe Julai 14, 2015 pale Collesium Hotel jijini Dar es Salaam, wao
hawakushiriki.
Lipumba alisema ameamua kujiuzulu kwa
sababu ya mambo makuu mawili; moja ni Ukawa kukubali kupokea waliotoka CCM
ambao walikuwa kikwazo kwenye Bunge la Katiba, na pili ni CUF kutothamini
mchango wake na hivyo kuonekana yeye ni kikwazo.
“Nimeamua kwa ridhaa yangu kuachia madaraka
rasmi ndani ya CUF, nitabaki mwanachama wa kawaida, dhamira yangu inanisuta.
Tumechukua watu waliotoka CCM ambao waliipinga Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa
na Jaji Warioba… mimi ndiye mwanzilishi wa Ukawa, sasa tumewapokea wanasiasa
waliotoka CCM, tumeshindwa kuenzi na kuzingatia maamuzi yetu kwenye vikao vya
Ukawa,” aliongeza.
Lakini mara tu baada ya kujiuzulu kwake,
propaganda nyingine za nguvu zikaanza kuenezwa, kwamba Profesa Lipumba
amehongwa na kwamba alifanya hivyo ili kulinda ajira ya mmoja wa maswahiba wake
wakubwa serikalini.
Mwandishi na mwanasiasa (mgombea ubunge
Jimbo la Ubungo – Chadema), Saed Kubenea, aliandika kupitia MwanahalisiOnline (http://mwanahalisionline.com/siri-za-prof-lipumba-kujiuzulu-zafichuka/)
kwamba, taarifa kutoka serikalini, ofisi kuu ya CCM, Lumumba, Idara ya Usalama
wa Taifa (TISS) na kwa watu waliokaribu na Prof. Lipumba mwenyewe zinasema,
kiongozi huyo alijiuzulu baada ya wakubwa ‘kufika bei’ ili kulinda kibarua cha
mmoja wa vigogo kutoka idara nyeti serikalini, ambaye ni swahiba wake wa karibu.
Akaandika kwamba, haifahamiki ni kiasi gani cha fedha alicholipwa ili
kumshawishi kujiondoa katika wadhifa wake, ingawa kuna taarifa kuwa zaidi ya Shs.
3.7 bilioni zimetumika kwa kazi hiyo.
Taarifa hizo (propaganda) zikasema, miongoni
mwa vyeo ambavyo Prof. Lipumba ameambiwa atakabidhiwa baada ya CCM kushika Dola,
ni kufanywa kuwa waziri wa fedha katika serikali ya John Magufuli au kuwa
mshauri mkuu wa uchumi wa serikali hiyo, ahadi ambazo zimefanya asaliti mageuzi.
Wakati hayo yakiendelea, Septemba Mosi,
2015, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa aliibuka ghafla na kueleza
uamuzi wake wa kujiuzulu, huku akitoa tuhuma nyingi kwa Chadema, Ukawa, Lowassa
na Sumaye, pamoja na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
ambaye anadaiwa kwamba ndiye ‘mshenga’ aliyefanikisha ‘uhamisho’ wa Lowassa
kutoka CCM kwenda Chadema.
Zile propaganda zilizotolewa na Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, kwamba Dk. Slaa alikuwa mapumzikoni (likizo)
zikakanushwa vikali na Slaa mwenyewe, ambaye alisema alijiuzulu tangu Julai 18,
2015.
Kama kawaida, propaganda zinaendelea,
ambapo imeelezwa kwamba Dk. Slaa amenunuliwa ndiyo maana ameamua kuyasema hayo
wakati huu.
Wengine wanasema ni shinikizo la mkewe,
Josephine Mushumbuzi, ambaye alitarajia kwamba Dk. Slaa atagombea urais kupitia
Ukawa na yeye atakuwa ‘Mke wa Kwanza’ (First Lady) wa Tanzania.
Ukawa wametekwa
Propaganda, kama tulivyoona hapo juu, ni
mbaya kama zinatumiwa na kikundi cha watu kueneza uongo na kupindisha ukweli. Anayeendesha
propaganda yuko tayari kuliita jiwe kwamba ni mkate.
Propaganda za mabadiliko ya nguvu ndizo
zinazoenezwa Tanzania, na kitendo cha wapinzani sasa kumwita kila
anayewanyooshea kidole kwamba wamekosea kuwa ni ‘msaliti’, ‘amenunuliwa’, ‘amehongwa’
na mambo kama hayo, kinaondoa dhana halisi ya mabadiliko hayo tarajiwa.
Ukawa, na kwa maana halisi Chadema,
kuwasema wote wanaotoa hoja za kupinga mwenendo wao wa sasa wa kuifunika hoja
ya ufisadi kwamba wamenunuliwa ni kuupindisha ukweli huo.
Au pengine, kama wanataka Watanzania
waamini propaganda hizo za Profesa Lipumba na Dk. Slaa kuhongwa ama kununuliwa,
basi Watanzania pia waamini kwamba Ukawa nao wametekwa.
Tena basi watakuwa wametekwa na mambo
mawili: Kwanza; ni kwa wingi wa watu wanaomshabiki Lowassa kwamba ndio
utakaofanikisha kukaa Ikulu. Inafahamika kwamba, hivi sasa Chadema haitaki
jambo lolote lile isipokuwa kuingia Ikulu tu bila kujali itaingia na watu
wasafi ama wachafu. Kuiondoa CCM Magogoni ni agenda yao kubwa na haihitaji
mjadala wa ufisadi wala nini.
Nilipata kusema wakati fulani, Lowassa
anautaka urais, lakini wapambe wake – na sasa Chadema na Ukawa – ndio wanaoutaka
zaidi. Imani ya madaraka watakayoyapata baadaye ndiyo kubwa zaidi.
Pili; Chadema watakuwa wametekwa na fedha
za Lowassa. Ni ukweli ulio wazi kwamba, hakuna mgombea urais wa mwaka huu
anayeweza kumfikia Lowassa kwa umaarufu na pia utajiri. Kwa fedha
alizojilimbikizia kwa kujinyima – iwe za mfukoni mwake ama kutoka kwa rafiki
zake – Lowassa anaweza kufanya kampeni nchi nzima bila hata kutegemea ruzuku ya
serikali.
Imeelezwa mara kadhaa kwenye duru za siasa
na katika mitandao ya kijamii, kwamba Chadema wamelambishwa Shs. 10 bilioni na
Lowassa na ndiyo maana wengine wanalalamika kwamba chama kimeuzwa!
Kwamba makubaliano ya Chadema kumuuzia
Lowassa chama hicho yalifanywa Jumapili Julai 26, 2015 kati ya Mwenyekiti wa chama
hicho Freeman Mbowe na Lowassa, ambaye anadaiwa kukubali kutoa kiasi hicho cha
fedha ili aweze kutimiza safari yake ya matumaini ya kugombea urais baada ya
kuenguliwa na CCM.
Pengine fedha hizo ndizo ‘zilizofuta’ hata
ile Orodha ya Mafisadi (List of Shame) kwenye mtandao wa Chadema (link: http://www.chadema.or.tz/tamko/tamko.php?id=16&pg=110) kwa kuogopa wadaku na wadakuzi
wasije wakaishikia bango! Lakini wameshindwa kutambua kwamba hawawezi kufuta
kumbukumbu kwenye vichwa vya watu.
Wakati Zitto Kabwe alipofukuzwa Chadema,
baadaye ilielezwa kwamba mwanasiasa huyo alikuwa amepewa rushwa na Nimrod
Mkono, mmoja wa watuhumiwa 11 wa ufisadi.
Tuhuma hizo zilitolewa na Mwanasheria machachari
wa Chadema, Tundu Lissu mwaka 2014, ambaye alisema ulikuwepo mkakati wa
kuwachafua viongozi wa chama ulioendeshwa na Zitto baada ya kuyanasa
mawasiliano yake na aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis
Msacky (sasa Mhariri Mtendaji wa Mtanzania) tangu mwaka 2009.
Lissu akasema Zitto wakati huo alikuwa na magari
mawili ya Nimrod Mkono, na kwamba Mkono mwenyewe ndiye amewaambia taarifa hizo.
Lakini Zitto akauanika ufisadi wa Mbowe,
akisema: “Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na
Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe Shs.
40 milioni ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini.
“Nadhani (Mkono) alimwambia pia mwaka 2008
(baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) alimpa Freeman Shs. 20 milioni za
uchaguzi (mdogo) wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na
akalipwa.”
Zitto akaendelea: “Nadhani alimwambia pia
kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe Shs. 200 milioni za kampeni ya Slaa. Pia
hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe Shs. 100 milioni za kampeni.
Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha
za chama kutoka Conservative Party?
“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya
mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda. Lissu awaambie waliomtuma wamwambie
ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, mimi namtaka mama wa kifaranga
ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani
na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati
yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas. They must know I am not a push over. Chacha died, I won't (Lazima
watambue kwamba mimi siyo mjinga. Chacha alikufa, mimi siwezi). Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake
aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili,” alisema Zitto.
Nakubaliana
na maneno ya Mwalimu Ndimara Tegambwage anayesema: “Siasa haijawahi kuwa mchezo
mchafu… Bali kuna watu wachafu kwenye siasa – na vyama vya siasa.”
Naam.
Fedha inaweza kununua kila kitu: inaweza kununua nafasi katika Ukawa na mwenye
tuhuma za ufisadi akateuliwa kugombea nafasi yoyote bila hata kufuata
utaratibu.
Hizo ndizo
propaganda na hiyo ndiyo michezo inayoendelea ndani yake. Sishangai kuona leo
Chadema wamemuona yule yule waliyemwita fisadi, amekuwa muadilifu na ‘mtakatifu’.
0656-331974
Kumbuka: Haya ni maoni ya mwandishi, hayana uhusiano na
msimamo wa blogu hii.



No comments:
Post a Comment