Mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa, akizungumza siku aliyotangaza kujiunga na Chadema Julai 27, 2015. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbati na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe.
Na Daniel Mbega
MASHAIRI
ya sasa ya siasa hayana mizani wala vina, tena hayana urari! Hata ngonjera na
tenzi vyote huwa na beti, mizani na vina.
Tanzania
imegubikwa na tufani ya Ukawa, hususan Edward Lowassa. Wimbi kubwa la wanaohemka
ni la vijana, wengi wao wakiwa waliozaliwa katika miaka ya 1980, ambao kwa
hakika ndio viongozi wa sasa wanaotakiwa kuleta mabadiliko. Vijana siyo taifa
la kesho tena, ni la leo.
Naam. Wale
wazee na vijana hirimu yangu wanaogelea katika wimbi la mageuzi hayo ambapo
wapiga kasia ni vijana. Wengi wanafurahia upepo unakoelekea na wanaomba usije
ukabadilisha mwelekeo – pepo za Kusi na Kaskazi huwa hazitabiriki wakati
mwingine na zinaweza kuleta madhara.
Wanasiasa
wakongwe wanaona huu ndio wakati muafaka wa kupata neema nyingine. Ndiyo. Wapo
waliokuwa wabunge kwa miaka mingi, wapo waliokuwa wanaongoza vyama vya siasa
kwa miaka mingi. Wengi kati ya hawa wamechokwa na wananchi waliokuwa
wanawaongoza. Wametemwa na vyama vyao na sasa wameona kimbilio pekee ni
kudandia mashua inayopelekeshwa na upepo wa mabadiliko – ya vijana!
Japokuwa
tayari mashua imempata nahodha, ambaye ni Lowassa, lakini kwa kiasi kikubwa
vijana ndio wanaoisukuma, tena kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba kama litatokea
wimbi kubwa linaweza kukipaisha chombo na wote wakazama. Ni mtazamo wangu tu
miye ambaye niko ng’ambo naangalia.
Lowassa
ametoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya chama hicho kumbwaga akiwa
ndiyo kwanza anataka kuianza safari yake ya matumaini. Amekaa akatafakari wee
akaona hapana, safari ya matumaini inaweza kuendelea, hata kwa kutumia ngalawa.
Akapokelewa
kwa huba na mahaba huko Chadema na hata Ukawa kiasi kwamba ndani ya siku mbili
tu, tayari akawa amekabidhiwa mikoba ya kuwania urais. Mikoba ambayo kabla ya
kuelekea huko wapinzani hao walikuwa wameafikiana kwamba aibebe yule Paroko
mstaafu, Dakta Wilbrod Peter Slaa.
Na mara tu
Lowassa alipotua Ukawa, Dk. Slaa akaingia mitini, kukaa kidogo, Profesa Ibrahim
Lipumba naye akatimua. Wale waliokuwa nguzo ya upinzani wameondoka kabla chombo
hakijang’oa nanga.
Yanaendelea
kusemwa mengi kutokana na kuondoka kwa wanasiasa hao wawili ndani ya Ukawa.
Wanatuhumiwa kwamba wamelambishwa sukari guru, ndiyo maana wameondoka ili
wakidhoofishe chombo hicho na kukwamisha safari ya matumaini ya Lowassa pamoja
na ndoto za Chadema za kukaa pale Magogoni kwa mara ya kwanza!
Kuvuja kwa
pakacha, nafuu kwa mchukuzi, maana mzigo utakuwa mwepesi. Ukawa inabidi
wafurahie kuondoka kwao. Unadhani wakichukua nchi si watakuwa na nafasi mbili
za Paroko na Profesa ambazo lazima wangepewa hao kama wangekuwepo?
Leo hii
wanaozisubiri nafasi hizo ni wengi mno – Ukawa kuna orodha ndefu, halafu
Lowassa kama taasisi ameondoka CCM pamoja na ‘watu wake’ ambao alikuwa nao
kitambo na wengi walikwishaahidiwa nyadhifa nyeti kama wakifanikisha safari ya
matumaini. Uongozi mzuri bwana, asikwambie mtu, na hasa unapopigiwa mizinga 21!
Lakini tayari
Profesa Lipumba amekwishasema kwamba ameondoka Ukawa na CUF – alikoachia nyadhifa
zake zote – kwa sababu dhamira yake inamsuta. Yawezekana anayajua mengi yaliyo
nyuma ya pazia kuhusu mchakato wa kuingia kwa Lowassa.
Dk. Slaa
kwa upande wake ndiye amemwaga sumu Septemba Mosi, 2015 wakati alipoeleza
bayana kwamba mchakato uliyumbishwa na viongozi wenzake ndani ya Chadema na
Ukawa kwa ujumla, kiasi kwamba hata barua yake ya kujiuzulu ilichanwa na Makamu
Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari.
Yapo mengi
aliyoyasema pia kuhusu ujio wa waziri mkuu mstaafu mwingine Frederick Sumaye
ndani ya Chadema, lakini kuna mengine amesema ni silaha zake za maangamizi,
ambazo ninaamini atakuwa nazo kwenye faili. Tayari Sumaye ndiye ameteuliwa kuwa
Meneja wa Kampeni wa Lowassa, kuhakikisha ushindi unapatikana.
Alipotua
Ukawa, mara moja Lowassa akatamba kwamba yeye tayari ni rais, anasubiri
kuapishwa kwa sababu siku ya Oktoba 25, 2015 atanyakua ushindi asubuhi tu!
Nadhani itabidi tutoke saa tisa alfajiri kama tulivyokuwa tunafanya tulipokuwa
tunajiandikisha kwenye BVR ili tufanikishe safari ya matumaini!
Hakuishia
hapo, akasema anazijua fitna zote za CCM na atahakikisha anakomaa mpaka
kinaeleweka. Wewe vihunzi vyote alivyoruka mpaka sasa anajaza nyomi kila
anakopita na kumhakikishia safari ya matumaini unadhani usingizi unaweza kuja?
Lakini
Lowassa lazima azijue fitna za CCM kwa sababu yeye alikuwa miongoni mwa
‘wajumbe wa kamati ya usajili’ na pia kocha mchezaji. Anajua vyema harakati
zake za safari ya matumaini zilizoanzia mwaka 1995. Tena anajua vyema namna
walivyouanzisha ‘Mtandao’ ndani ya CCM mwaka 2005 ili kufanikisha ushindi wa
Jakaya Kikwete.
Lowassa ni
dhahiri anajua mchezo uliofanyika mwaka 2005 wa kumkata mapemaaa Mzee
Cigwiyemisi John Samuel Malecela mpaka akashindwa kuingia kwenye tano bora.
Sijui kwanini yeye safari hii amelia na kuomboleza baada ya kukatwa mapema. Hakika
kidonda kiko kwako, kwa mwenzako hakiumi!
Naam.
Lowassa pia atakuwa anakumbuka kilichotokea mpaka mwanadiplomasia
ninayemheshimu sana, Dk. Salim Ahmed Salim, akafanyiwa fitna kwa picha yake
kutengenezwa na kuzushiwa kwamba ati aliwahi kuwa mwanachama wa Hizbu, kile
chama kilichokuwa na Waarabu wengi ambacho kilikuwa kinapinga harakati za
ukombozi Visiwani zilizokuwa zinafanywa na vyama vya African Association na
Shirazi Association ambavyo baadaye vikaungana na kuunda Afro-Shiraz Party.
Zile
zilikuwa ni fitna mbaya sana na wahusika walioucheza mchezo huo nadhani nafsi
zao zinawasuta. Wengi dhambi ile inawatafuna kwa sasa.
Duru za
siasa zinaeleza kwamba ati kuna ‘Mafaili ya Lowassa na Sumaye’ yanayoandaliwa
na baadhi ya watu – ndani na nje ya CCM wanaopinga hatua yake ya kugombea urais
kwa sababu siyo msafi kama anavyojinasibu – ambayo pengine yanasubiri wakati
muafaka tu yatolewe hadharani wakati mapambano ya hoja za majukwaani
yatakapoanza. Sijui kama kama kauli ya Dk. Slaa ni mwanzo wa kuyafumua faili hayo
ama la.
Mimi
nalisubiri sana mafaili hayo ili kujua kuna nini ndani. Sijui kama yatakuwa yanazungumzia
kuhusu kuanzishwa kwa ‘mtandao’ ambao ndio umekivuruga chama ingawa Lowassa
mwenyewe anayedaiwa kuwa mhusika naye analia kwamba chama kimeharibika?
Natamani
nione mafaili hayo ili kujua hasa chanzo cha ‘chuki’ ya Lowassa kwa Malecela.
Sijui kama ilianza wakati ule alipokuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu na
Makamu wa Kwanza wa Rais akishughulikia Haki na Mambo ya Bunge miaka ile ya
1990 wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, au ilianza kipindi kile cha mwaka 1997
wakati vijana wa CCM walipotaka kumwangusha Malecela kwenye nafasi ya Makamu
Mwenyekiti Bara na kumpa Frederick Sumaye kabla Mwalimu Julius Nyerere hajaenda
Dodoma kuzima jaribio hilo!
Bila shaka
mafaili hayo yatakuwa na kashfa za uuzaji wa viwanja vya Kariakoo jijini Dar es
Salaam akimtumia mfanyabiashara Baghdad wakati yeye akiwa Waziri wa Ardhi
wakati wa Mwinyi, au pengine wanataka kuanika ukweli wa zilikopelekwa fedha za
msaada zinazodaiwa kutumika kwenye ujenzi wa nyumba ya Lowassa ambayo
kaupangisha Ubalozi wa Afrika Kusini kule Masaki.
Pengine
faili la Lowassa litakuwa linaeleza bayana namna alivyohusika kwenye mchakato
wa mkataba wa Richmond, tofauti na utetezi wake alioutoa wakati akienda Ukawa.
Naamini nyaraka za Baraza la Mawaziri hasa Kikao
cha Baraza la Mawaziri kilichoketi Februari 2, 2006 (takriban mwezi mmoja na
nusu tangu Lowassa ateuliwe kuwa Waziri Mkuu), zitakuwemo na zitaeleza ni
kwanini baada ya kikao cha Februari 2, 2006, saa 10 jioni ya siku hiyo hiyo,
Ibrahim Msabaha (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo), aliufuta
mchakato ulioanzia kwenye Serikali ya Mkapa na kubarikiwa na Baraza la Mawaziri
na hatimaye kampuni ya Richmond ikapewa zabuni ya kufua umeme wa dharura.
Au pengine
linaeleza uamuzi wake, akiwa Waziri wa Maji na Mifugo, wa kuruhusu mifugo
itawanyike nchi nzima bila maandalizi yoyote wala elimu kwa wakulima na
wafugaji, hatua ambayo imesababisha mauaji makubwa kutokana na migogoro baina
ya jamii hizo mbili.
Kama
sivyo, basi huenda faili hilo litakuwa limejaa kashfa za rushwa, kwamba alikuwa
anatumia jumuiya mbalimbali za CCM ili kumuunga mkono kwenye safari yake ya
matumaini ya kwenda pale Magogoni.
Nalisubiri
kwa hamu faili hili kama kweli litatoka. Pengine basi litakuwa na orodha ya
watu – wakiwemo wanahabari – ambao wanadaiwa wanalipwa ili kufanya kazi maalum
ya kumpamba na kumtakasa kwa nia ya kumsindikiza hadi Magogoni.
Au pengine
faili hilo, mbali ya kuwa na orodha ya utajiri wa Lowassa na familia yake, na
jinsi ulivyopatikana, pia linaweza kuwa na orodha ya marafiki zake ambao
wanamsaidia ama kumchangia fedha – zikiwemo zile ambazo amekuwa akizitoa kwenye
harambee mbalimbali au namna marafiki zake hao walivyozipata fedha hizo ingawa
sina imani kama hilo haliwezi kuiathiri Benki ya CRDB!
Kwa upande
wa Sumaye, nasubiri kuona lina nini ndani ili kulinganisha na ‘madongo’
aliyoyaporomosha kwa serikali ya sasa.
Inawezekana
faili hilo litaeleza ushiriki wake katika kudidimiza kilimo kwa maana amekuwepo
kwenye Wizara ya Kilimo na Ushirika tangu mwaka 1985 hadi 1995 – kwanza akiwa
naibu waziri na baadaye waziri kamili.
Pengine litaeleza
namna mashamba ya umma (NAFCO, DAFCO na NARCO) yalivyobinafsishwa na hata
kuuzwa baada ya wakubwa kuyatafuna watakavyo.
Yumkini faili
la Sumaye litaeleza yaliyotokea akiwa waziri mkuu kwa miaka 10, mwezi mmoja na
siku tatu. Huenda tukajua mikataba yote mibovu ya nishati na madini
ilivyosainiwa ama wakubwa walivyojitwalia mashirika ya umma.
Naamini yapo
mengi, na Watanzania wanatamani kuyaona ama kuyasiki sasa ili waweze
kuyajadili, maana mambo yaliyofanyika wakati huo ndiyo yameongeza ugumu wa maisha
kwao.
Kama kweli
yapo, mafaili hayo ni muhimu kuyaona na ninawashauri wenye nayo wayalete haraka
tuyachambue na kuyajadili. Mimi nayasubiri!
Alamsiki.
0656-331974

No comments:
Post a Comment