Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 30 March 2014

WAJUMBE BUNGE LA KATIBA WAANZA KUFUNGA VIRAGO

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akimsikiliza Samuel Sitta, ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba

Dodoma/Dar. Wakati Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuanza kujadili Rasimu ya Katiba kesho, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wameanza kuondoka bungeni, kupinga mwenendo wa Bunge hilo.
Hatua hiyo ya wabunge hao inakuja wakati Bunge Maalumu la Katiba juzi lilipitisha azimio la kutumia kura ya siri na wazi katika kuamua vifungu vya rasimu.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Saluhu alisema baada ya kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura za siri na wazi katika Bunge hilo, kuanzia Jumatatu wataanza kujadili sura ya kwanza na sita ambayo inahusu Muundo wa Muungano.
Katika sura ya kwanza, mambo ambayo yanatakiwa kujadiliwa ni Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa wakati sura ya sita mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa ni Muundo wa Muungano.
Lema atangaza kurudi jimboni Arusha
Mjumbe wa Bunge hilo, Godbless Lema alisema anakusudia kuondoka bungeni, kutokana na kutoridhishwa na maridhiano ya kupiga kura za siri na wazi katika kufikia uamuzi katika Bunge hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema hakubaliani na utaratibu uliopitishwa, kwani unalenga kulazimisha kila jambo ambalo chama tawala kinalitaka lipitishwe.
“Huu utaratibu wa kura kupigwa kwa wazi na siri katika kitu kimoja, haupo sehemu yoyote duniani. Sasa sisi kukubali ni kuwasaliti wananchi, kwani hata Dodoma tunaandaa rasimu ya Katiba ya wananchi wote siyo ya CCM pekee,” alisema Lema.
Alisema pia hakubaliani na utaratibu wa kujadili rasimu ya Katiba, ambao umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuanza na sura ya kwanza na ya sita, kwani vinalenga kufumua Rasimu ya Jaji Warioba.
“Hapa CCM wanataka kulazimisha Serikali mbili kwa kujadili kwanza vifungu hivi, kama vitapita basi watakuwa na uwezo wa kubadili rasimu yote kitu ambacho mimi siwezi kukaa kwenye Bunge hili na kusaliti wananchi waliotoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji JosephWarioba,” alisema Lema.
Jussa atabiri Bunge kuvunjika.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mjimkongwe, Ismail Jussa, alisema uchaguzi wa vifungu hivyo ambavyo ndivyo vinabeba Rasimu ya Katiba, vinaashiria kuvunjika kwa Bunge hilo katika hatua za awali.
“CCM msimamo wao ni Serikali mbili na sisi ni Serikali tatu na tunaanza kujadili vipengele vinavyobeba Katiba na hakuna atakayekubali kuachia msimamo wake na hapo ndipo Bunge litakapovunjika,” alisema.
Kuhusu utaratibu wa kupiga kura za wazi na siri, Jussa alisema utaratibu huo utaleta mgawanyiko mkubwa, kwa sababu ya msimamo wa CCM ni kura za wazi na hivyo hakuna mjumbe wa chama hicho atakayethubutu kupiga kura ya siri.
Mnyika
Naye mjumbe mwengine wa Bunge hilo, John Mnyika, alisema, CCM ina mpango wa kubadili rasimu kutoka Muungano wa Serikali tatu kuwa wa Serikali mbili ili kufanikisha msimamo wao na maelekezo ya Rais kwenye hotuba yake bungeni.
Mnyika alieleza kuwa kwa mazingira hayo, Ukawa unahitajika kutetea maoni ya wananchi na kwamba CCM wakiendelea na njama zao wakati wa kujadili sura ya kwanza na ya sita, itawalazimu kurudi kwa wananchi ambao ndiyo wenye nchi.
“Hatua ya kurejea kwa wananchi inatarajiwa kuchukuliwa kabla ya kuendelea na sura zingine mbili za Rasimu ya Pili ya Katiba,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema mpango huu ulianza kwa wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka CCM wakati wa kujadili rasimu ya kanuni waliwasilisha majedwali ya marekebisho kutaka ibara zipangwe mbili mbili zinazofanana.
Katibu wa Bunge
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Yahya Khamis Hamad akizungumzia kuondoka kwa baadhi ya wabunge alisema, suala hilo amelipata jana kupitia Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge lakini si msimamo wa kundi.
“Taarifa hii tulipata kwenye kamati, lakini tukaulizana kama kuna kundi linataka kuondoka, ikabainika hakuna kundi.”
Kuhusu uamuzi wa kuanza kujadili sura ya rasimu ya kwanza na sita alisema tayari yalifikiwa na Kamati ya Uongozi na kwamba kwa mujibu wa kanuni ya 58 kifungu kidogo cha tatu, Kamati ya Uongozi ndiyo yenye jukumu la kupanga utaratibu wa kujadiliwa rasimu.
Kuhusu CCM kuwa na rasimu yake
Akizungumzia taarifa kuwa CCM ina rasimu yake ambayo ndiyo wanataka ijadiliwe alisema hakuna suala hilo.
“Mimi binafsi sijalisikia hilo na sitegemei kuwapo, kwani wajumbe watajadili rasimu iliyo mbele yao ambayo ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Hamad.
Wasomi
Wasomi nchini wamesema mfumo wa kupiga kura ya wazi na siri uliopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, hautapunguza nguvu ya mijadala katika Bunge hilo katika vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na aina ya muundo wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema kuwa badala yake mfumo huo utawalazimisha baadhi ya wajumbe wasiokubaliana na misimamo ya vyama vyao kupiga aina ya kura wasiyoitaka.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema mjadala mkali unatarajiwa kuendelea bungeni hasa katika hoja ya aina ya muundo wa Serikali, kwa kuwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliashiria kutotaka muundo wa Serikali tatu.
Profesa Shumbosho alisema kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa CCM hawakubaliani na muundo wa Serikali mbili, lakini watalazimika kupiga kura ya wazi ili kukiridhisha chama chao.
“Kuna watu hawana ujasiri. Ndani ya CCM wapo wanaopenda Serikali tatu lakini wanaogopa,” alisema Profesa Shumbusho.
Pia, alisema kuwa kwa namna hali inayoonekana kuendelea bungeni, kuna dalili kuwa maoni ya rasimu ya CCM kuhusu Katiba ndiyo yatakayopita na hivyo kurudisha mambo mengi yaliyopo katika Katiba ya sasa.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kuwa upigaji kura wa wazi au siri hautazuia wajumbe kuendelea na misimamo yao na kwamba badala yake mjadala utakuwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Alisema ingawa yapo baadhi ya mambo ambayo wajumbe wanaweza kukubaliana bila kupiga kura, suala la Muungano litakuwa na mvutano kwa kuwa tayari hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji JosephWarioba na Rais Kikwete bungeni, zimeshaleta ‘msuguano’.
“Mjadala utakuwa mkali, suala lenyewe tu limeanza kuwa kali tangu mwanzo. Warioba alieleza Serikali tatu, Rais Kikwete akapinga,” alisema Profesa Mpangala.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Hamad Salim alisema suala la kupiga kura ya siri au wazi limechukua muda mrefu kujadiliwa bila sababu za msingi.
Akifafanua, Salim alisema kuwa wanaotaka kura ya wazi wanajenga hoja kuwa wanataka masuala yote yawe wazi kwa wananchi, lakini wanashindwa kusema ni lini walipewa maoni hayo na wananchi.
“Sikubaliani na kura ya wazi, hawakutumwa na wananchi, walitakiwa kuridi kwao na kuwauliza aina gani ya kura wanataka,” alisema Salim na kuongeza:
“Kwa muda mrefu upigaji kura ulikuwa wa siri, sasa imekuwaje leo wanataka kura ya wazi?”
Sendeka
Mjumbe wa Bunge hilo, Christopha Ole Sendeka alisema matokeo ya kura za kupitisha kanuni ya 37 na 38 ya upigaji kura yamewashangaza Ukawa, lakini muhimu kwao ni kukaa bungeni na kujenga hoja.
“Matokeo ya jana (juzi) yamewakatisha tamaa kwa ushindi wa idadi nzuri ya kura, walidhani CCM haina theluthi mbili, lakini licha ya wabunge wengi hatohudhuria tumeshinda,” alisema Sendeka.
Alisema wingi wa CCM siyo ndani ya Bunge tu, kwani hata nje wengi wanakiunga mkono chama hicho.
“Vizuri wangekaa tu kwani CCM inaweza kupitisha mambo kwa kura nyingi zaidi, lakini wakiwepo tunaweza kufikia maridhiano katika baadhi ya mambo,” alisema Sendeka.
Umoja wabunge Wanawake
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wabunge, (TWP), Suzan Lyimo alisema utaratibu wa kura za wazi na siri utaleta vurugu na utekelezaji wake ni mgumu.
“Utaratibu huu ni mgumu kutekelezeka sasa sijui wanaopiga kura za wazi watakaa upande wao na wale wa siri upande wao, lakini ni mgumu kutekelezeka na hakuna nchi ambayo umeshawahi kutumika,” alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya wabunge wanawake kutoka vyama vya upinzani, Suzan Lyimo alisema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete imeleta madhara makubwa kwa wananchi hasa wale ambao hawana itakadi za vyama.
“Hotuba hiyo imeleta mpasuko mkubwa miongoni mwa Watanzania..., sisi kama wajumbe wa Bunge hili tunawahakikishia wananchi kwamba tutajadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Sabrina Sungura alisema mchakato huo wa Katiba unaweza usifike mwisho na kwamba mtu wa kwanza wa kulaumiwa ni Rais Kikwete ambaye alitoa hotuba ya kuwagawa wabunge.
“Tulipaswa kuambiwa kuwa Rais anatumia nafasi yake kama sehemu ya Bunge kuleta maoni yake na si kulizindua Bunge kama tulivyoambiwa katika ratiba,” alisema.
Naye Moza Abeid ametaka kurekebishwa upungufu uliojitokeza katika mchakato wa Katiba ili wananchi waweze kupata Katiba waitakayo.

HAYA NDIYO MAFANIKIO YA BANDARI YA DAR ES SALAAM


TAARIFA YA MAFANIKIO YA UTENDAJI KAZI YA BANDARI YA DAR ES SALAAM KWA KIPINDI CHA MIEZI SITA (JULAI – DISEMBA 2013)

Katika kipindi cha miezi sita ya Julai – Disemba 2013, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam. Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la shehena, kuongezeka kwa tija katika kuhudumia shehena na meli, kupunguza msongamano wa meli na mlundikano wa mizigo bandarini na kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo wateja bandarini.

1.HUDUMA KWA SHEHENA

Katika kipindi cha miezi sita ya Julai – Disemba, 2013 bandari ilihudumia tani milion 7.50 ukilinganisha na tani 
million 6.38 zilizohudumiwa katika kipindi cha Julai – Disemba, 2012, ongezeko la 17.6%. Sababu za kuongezeka kwa shehena ni pamoja na:

(i)Kukua kwa uchumi wa nchi zinazotumia bandari.

(ii)Jitihada zinazofanywa na serikali katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji

(iii)Jitihada za kimasoko zinazofanywa na bandari pamoja na wadau

(iv)Kuwepo kwa amani na utulivu bandarini kutokana na uhusiano mzuri 

2.HUDUMA KWA MELI

Idadi ya meli (Ships call) katika kipindi cha miezi sita ya Julai – Disemba, 2013 bandari ilihudumia jumla ya meli 868 zenye ukubwa wa GRT million 15.4 ukilinganisha na meli 677 zenye ukubwa wa GRT million 11.7 zilizohudumiwa kipindi cha Julai – Disemba, 2012. Ongezeko la meli ni 28.2% na ongezeko la GRT 31.6%.

3. UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI
Ufanisi na utendaji kazi bandarini umeongezeka katika kipindi cha nusu mwaka Julai – Disemba, 2013 ukilinganisha na Julai-Disemba, 2012 kwa kutumia viashiria mbali mbali ikiwa ni pamoja na:

(i)Idadi ya siku meli kukaa bandarini imepungua katika kipindi cha Julai – Disemba 2013, ilipungua hadi siku 5.6 ukilinganisha na siku 5.9 kipindi cha Julai – Disemba, 2012, ikiwa ni asilimia 5.1 za kupungua

(ii)Muda wa ukaaji wa kontena bandariniumepungua kutoka wastani wa siku 9.5 kipindi cha Julai-Disemba, 2012 hadi wastani wa siku 8.5 kipindi cha Julai-Disemba, 2013, punguzo la asilimia 10.5.

(iii)Katika kipindi cha Julai – Disemba 2012, utendaji wa krini kwa upande wa TPA (Kitengo cha Mizigo mchanganyiko) uliongezeka kutoka mizunguko 249 kwa saa 24 Julai-Disemba, 2012 hadi mizunguko 418 kwa saa 24 Julai-Disemba, 2013, ongezeko la asilimia 67.9. Kwa upande wa TICTS utendaji ulikuwa mizunguko 605 kwa saa 24 kipindi cha Julai – Disemba 2012 ukilinganisha na mizunguko 611 kwa saa 24 kipindi cha Julai-Disemba, 2013, ongezeko la asilimia 1.0.

(iv)Upakuaji wa magari umeongezeka hadi kufikia magari 672 kwa shifti (kuna shifti 3 kwa saa 24 na kila shifti ina saa 8) kwa kipindi cha Julai-Disemba, 2013 ikilinganishwa namagari 634 kwa shifti kwa kipindi cha Julai-Disemba, 2012, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.7.

3.1 SABABU ZA KUONGEZEKA KWA UFANISI

(i)Hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi katika kusimamia kwa karibu utendaji kazi wa Mamlaka.

(ii) Ununuzi wa vitendea kazi kwa ajili ya kuboresha huduma kwa meli na mizigo.

(iii) Mafunzo kwa wafanyakazi

(iv) Kuongezeka kwa maeneo ya kufanyia kazi nakuhifadhiamizigo,mfano “EX-AMI” (1,200 TEUS) na “EX-NASACO” (3,600 TEUS), ICDS 10 (15,550 TEUs) naCFS3 (Magari 5,630).

(v)Matumizi ya TEHAMA katika kuhudumia wateja (Harbour View, Cargo System, Billing System na epayment)

(vi) Kuanzishwa kwa One Stop Centre: Wadau wa bandari wamepewa ofisi bandarini ambapo kwa sasa wanapatikana katika eneo moja na hivyo kurahisisha huduma kwa wateja.

(Vii)baadhi ya mizigo (ya Tanzania) bandarini mara tu inapoteremshwa (direct delivery)

(viii)Kuwepo na nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha na iliyo motishwa

4.MATUMIZI

Mapato ya bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha Julai – Disemba, 2012 yalikuwa ni jumla ya shilingi 191,637,360,000 wakati kwa kipndi cha Julai – Disemba 2013, mapato yalikuwa ni jumla ya shilingi 224,196,470,000/= hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.9

5.ULINZI NA USALAMA

Ulinzi na usalama katika bandari ya Dar es Salaam umekuwa unaboreshwa na kuimarishwa kila wakati. Ulinzi na usalama ni changamoto ambapo mikakati inachukuliwa ili kuweza kufanya bandari kuwa salama kwa wafanyakazi, wateja, meli, mizigo na mali kwa ujumla. Matukio ya uhalifu/wizi yamekua yakipungua kila mwaka kwa sababu ya juhudi za Mamlaka katika kukabiliana na changomoto hizo. Mikakati ya kupambana na wizi kwa lengo la kuondoa kabisa vitendo vya wizi ni pamoja na:

(i)Matumizi ya TEHAMA katika upokeaji na utoaji wa mizigo bandarini, ambao umepunguza matumizi ya karatasi zilizokuwa zikighushiwa.

(ii)Kutoruhusu bandari kutumika kama sehemu ya kuhifadhia mizigo.

(iii)Kutofumbia macho udokozi wa mali za wateja (Zero tolerance).

(iv)Kuwashirikisha wafanyakazi na wateja katika ulinzi wa mali za wateja na wafanyakazi (Ulinzi shirikishi).

5. CHANGAMOTO

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Julai – Disemba 2013 kuna changamoto kadhaa ambayo bandari imekutana nazo katika utendaji kazi wake. Changamoto hizo ni pamoja na:

(i)Ufinyu wa maeneo ya kuhudumia meli na shehena

(ii)Mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuboresha na kupanua huduma za bandari

(iii)Kina kifupi cha maji na ufinyu wa lango la kuingilia meli

(iv)Mabadiliko ya teknologia ya meli

(v)Huduma hafifu ya reli

6. MIKAKATI YA KUBORESHA ZAIDI HUDUMA

(i)Kuongeza kina cha gati Na. 1 hadi 7 na lango la kuingilia bandarini ili kuwezakuhudumia meli kubwa.

(ii)Kujenga gati Na. 13 na 14 kwa ajili yakuhudumia shehena ya makasha.

(iii)Kuunganisha wateja katika mtandao mmoja wa mawasiliano ya kompyuta (PortCommunity System).

(iv)Kuimarisha ulinzi na usalama bandarini kupitia mradi wa “Integrated Security System.”

(v)Kuboresha mifumo ya kompyuta kwa ajili ya upakuaji, upakiaji, na uotaji wa mizigo bandarini.Tayari mifumo ya kompyuta yaHarbour view, Cargo system na billing system inafanya kazi. Mfumo wa billing system umewezesha wateja kulipa malipo moja kwa moja kupitia benki, k.m. CRDB.

(vi)Kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi ili kuboresha ujuzi wao.

(vii)Kujenga maeneo ya kuhudumia shehena ya makasha (Mfano; Kisarawe ICD naEx-Copper Yard).

(viii)Ujenzi wa matanki ya kuhifadhi mafuta (tank farms) huko Ras Mjimwema.

(ix)Ujenzi wa kituo cha kuhudumia mizigo cha Kisarawe (CFS). Wilaya ya Kisarawe imeipa TPA eneo la eka 1,760 za ardhi. TPA imeomba Halmashauriya Kisarawe kuthamini na kutoa gharama za fidia.

(x)Kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji na uendeshaji wa shughuli zabandari.

7.HITIMISHO

Serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania itaendelea kuwekeza katika bandari ya Dar es salaam kwa kujenga uwezo wa rasilimali watu namiundombinu pamoja na vitendea kazi vya kutosha na vya kisiasa. Msisitizo umewekwa katika matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha bandari hii inatoa huduma bora kwa wateja wake.

IMETOLEWA NA
MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA

SERIKALI YATAKIWA KUSAIDIA SHULE ZA PEMBEZONI


Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

Serikali imeombwa kuendeleza utoaji wa misaada katika shule zilizopo nje ya miji ili kuweza kuinua kiwango cha elimu na ufaulukwa wanafunzi walioko katika maeneo yaliyo nje ya miji.
Ombi hilo limetolewa na Daniel Josiah mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya sekondari ya City Boys iliyopo katika kata ya Olasiti jijini Arusha wakati akiongea na gazeti hili mapema leo.
Josiah alisema kuwa serikali iendelee kutoa misaada yake katika shule zote zilizopo nje ya mji wa Arusha kama vile vitabu,vifaa vya kujifunzia ili kuweza kupunguza mzigo kwa wazazi ama walezi pamoja na utengenezaji wa miundombinu ya barabara na nishati ya umeme ili kuwasaidia wanafunzi kujisomea katika mazingira mazuri.
Aidha Josiah alieleza kuwa shule hiyo iko chini ya uongozi wa kanisa katoliki lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana wa kiume ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo yao baada ya kuhitimu elimu ya msingi ikiwa ni pamoja na luwaandaa kitaaluma katika masomo ya sayansi.
Aliendelea kuwa katika kuwaandaa kitaaluma pia wana waandaa wanafunzi katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ili waweze kumudu maisha ya baadaye baada ya kumaliza masomo yao,wanawaandaa kinidhamu kuwa raia bora katika jamii zao.
"Wanafunzi walio wengi hawawezi kujishughulisha na kazi za mikono hali inayo wafanya wengi wao wakimaliza masomo wanashindwa kujiajiri hivyo uongozi wa shule hii umeamua kuwafundisha wanafunzi kazi za mikono wawapo shuleni kama vile kilimo ili hata watakapo maliza masomo yao wasikae bure manyumbani wajishughulishe na kazi mbalimbali"alisema Josiah.
Aliwataka wazazi na jamii kwa ujumla kujali elimu na kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu bora ikiwa ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya watoto wao,ambapo kazi kubwa wanayoifanya walimu ni kuwaandaa vyema wanafunzi katika masomo ili kuwajengea uwezo wa kuelewa nini wanachofundishwa.
Hata hivyo uongozi wa shule hiyo umeandaa mfumo mpya wa Global Getway inayowahusisha watoto hasa wanafunzi kupata udhamini wa masomo kutoka nchi ya British na kuweza kuwasomesha bure ambapo pia wanawasaidia wanafunzi ambao ni yatima kupitia huduma ya mtoto yesu kuwasomesha bure.

OFISA MWANDAMIZI JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI APINGA KUSIMAMISHWA KAZI


Phil Klerruu

Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

Afisa Milki Mwandamizi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyesimamishwa kazi, Phil Klerruu, amepinga hatua hiyo akisema Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, hana mamlaka hayo kulingana na sheria na kanuni za ajira za Jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Klerruu alisema mamlaka yake ya ajira na nidhamu ni Baraza la Mawaziri la EAC ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kumwajibisha baada ya kupokea tuhuma na mapendekezo kutoka kwa Katibu Mkuu.
“Katibu Mkuu alipaswa kunipa kwa maandishi hati ya mashtaka yenye tuhuma dhidi yangu, kuunda tume kunichunguza na kuwasilisha mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi iwapo tuhuma zitathibitishwa,” alisema Klerruu
Alisema pamoja na kukiuka sheria na kanuni za ajira EAC, katibu Mkuu pia alishindwa kutaja mali anazodaiwa kujimilikisha wala thamani yake licha ya ukweli kwamba kazi ya kuhamisha vitu siyo moja ya kazi zake kulingana na majukumu yaliyoanishwa kwenye barua yake ya ajira.
Klerruu alisema anaamini barua yake kwa Katibu Mkuu, Dk Sezibera akimwomba kuchukua hatua dhidi ya Naibu Katibu Mkuu (Fedha na Utawala), Jean-Cloud Nsengiyumva anayetuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kubagua wafanyakazi kwenye ajira za muda ndiyo imemponza.
Akijibu madai ya Klerruu mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake, Dk Sezibera alisema sheria na kanuni za ajira zinampa mamlaka ya kumchukulia hatua za kiutawala ikiwemo kumsimasha kazi afisa huyo kupisha uchunguza kabla ya kuwasilishwa suala hilo Baraza la Mawaziri.
Akipokezana na Mkurugenzi wa Utawala wa EAC, Richard Ochwada, Dk Sezibera alikiri kupokea barua ya Klerruu akimtuhumu Naibu Katibu Mkuu Nsengiyumva kwa matumizi mabaya ya madaraka lakini tuhuma hizo hazikuthibitishwa na baada ya uchunguzi kufanyika na kukana kuwa chanzo cha Afisa huyo kusimamishwa.

Saturday, 29 March 2014

TRENI YA MIZIGO YAPATA AJALI ENEO LA GULWE WILAYA YA MPWAPWA

Wafanyakazi walioajiriwa na shirika la Reli Tanzania (TRL) wakitoa mchanga kwenye kichwa cha treni ya mizigo kilichopata ajali usiku wa kuamkia katika stesheni ya Gulwe, Wilaya ya Mpwampwa. Katika ajali hiyo watu wawili wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa na kulazwa katika hospital ya Benjamin Mkapa Wilayani Mpwampwa.

Sehemu ya mabehewa ya mafuta na ngano ambayo hayakusombwa na maji katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika stesheni ya Gulwe, hiyo imetokea saa 9.15 usiku. Treni hiyo ya Mizigo ilikuwa ikitokea Dar es Salaam na kuelekea Mkoani Kigoma na ilikuwa na mabehewa yaliyobeba ngano, sukari na mafuta.
Njia ya Reli iliyoondolewa na maji katika stesheni ya Gulwe Wilaya ya Mpwampwa kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneno mbambali nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka akitoka kwenye maji baada ya kuangalia kichwa cha treni kilichopata ajali na kusombwa na maji katika stesheni ya Gulwe, Wilaya ya Mpwampwa, usiku wa kuamkia leo.

CHANZO: GPL

JK ATUNUKU TUZO YA RAIS YA MZALISHAJI BORA

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na washindi walionyakua tuzo mbalimbali wakati wa hafla ya kutunuku Tuzo ya Rais ya  Mzalishaji Bora wa mwaka 2013 iliyofanyika katika Hoteli ya Serena  jijini Dar es Salaam jana ijumaa.
(Picha na Freddy Maro)

WANAWAKE ELFU SABINI WAKUTANA KULIOMBEA TAIFA


Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

ZAIDI ya wanawake elfu sabini kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wamekusanyika katika viwanja vya Stadium Jijini Arusha huku lengo halisi likiwa ni kuombea mahitaji yao mbalimbali pamoja na mahitaji ya Taifa la Tanzania.
Aidha wanawake hao waliweza kukutanishwa mapema jana na kituo cha Radio cha Safina katika kongamano la wanawake na mabinti kwa makusudio ya kuwabadilisha mitizamo yao mbalimbali.
Akizungumza na maelfu ya wanawake hao Meneja wa kituo hicho Jovin Abel Msuya alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwasaidia wanawake ili waweze kufika katika malengo yao mbalimbali ambayo wamejiwekea.
Jovin alidai kuwa wanawake wakipewa nafasi nzuri ya kumjua Mungu katika maisha yao basi wataweza kubadilika kwa kiwango kikubwa sana na hata taifa nalo litaweza nalo kubadilika na kisha kupiga hatua
Alifafanua kwa kudai kuwa asilimia kubwa ya familia za sasa zinaharibikiwa sana kwa kuwa wengi wa wanafamilia hasa wanawake wanakosa hofu ya mungu hali ambayo wakati mwingine inasababisha hata taifa kupata wakati mgumu sana.
Amedai kuwa kutokana na hali hiyo sasa kuna umuhimu wa taifa kuwakutanisha wanawake kwa pamoja na waweze kupiga hatua kwani hali hiyo itaweza kusadia sana taifa la Tanzania katika mikakati yake mbalimbali.
"Mwanamke akisimama vema kuanzia kwenye ndoa yake basi hata nchi nayo itakuwa kwenye wakati mzuri na hivyo kila kusudi litaweza kufanikiwa na hapo matatizo mbalimbali ambayo yapo yataisha kabisa kwaiyo ni lazima hata wanawake nao wajue kuwa wana nafasi kubwa sana ya kutetea nafasi yao walionayo kwenye jamii"aliongeza Jovin
Mbali na hayo alidai kuwa kwa sasa nao wanawake wanatakiwa kuinuka katika nafasi zao na kuachana na tabia ambazo wakati mwingine huzaa matunda mabaya kwenye familia zao na hata nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuachana na tabia ya kuamini nafasi za nguvu za giza ambazo wakati mwingine husababisha mafaa makubwa zaidi.
Kwa upande wa wanawake ambao wamehudhuria katika kongamano hilo ambalo liliwahusisha wanawake na mabinti walidai kuwa kwa sasa kuna umihimu wa taasisi za dini kuendelea kuitisha makongamano ya wanawake na mabinti ili kuweza kusaidia jamii kupambana na changamoto mbalimbali.
Wanawake hao walidai kuwa katika makongamano hayo huwa wanapata fursa za kujifunza kwa undani juu ya maadili mema katika ndoa zao lakini hata jinsi ya kutii Amri za Mungu pamoja na ile ya serikali kama walivyokutanishwa na kituo cha Radio Safina.

TAHA YATANGAZA NEEMA KWA VIJANA KWENYE MASOKO YA KILIMO HAPA NCHINI




Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
Chama cha Wakulima wa Maua, Mboga na Matunda Tanzania (TAHA) kimesema kuwa kwa sasa kina mikakati mbalimbali ya kuwasaidia vijana kuwekeza zaidi kwenye kilimo huku lengo likiwa ni kupunguza tatizo la uhaba wa ajira hapa nchini.
Aidha lengo halisi la kufanya hivyo ni kuongeza ajira kwa vijana wa tanzania husani wale wahitimu wa vyuo vikuu ambao wakati mwingine humaliza masomo lakini hawana ajira.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa TAHA Bi Jacqline Mkindi wakati akielezea mikakati ya chama hicho kwa mwaka huu ambapo mikakati hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa chama hicho pamoja na sekta zake.
Aliendelea kwa kusema kuwa vijana ndio nguzo kubwa hapa nchini ambayo ina uwezo wa kujijenga na kujiimarisha kwenye maslai ya taifa endapo kama watapewa fursa ya kufanikisha malengo yao.
Mbali na hilo pia alisema kuwa mkakati huo utaweza kuwa na faida kubwa sana kwa vijana hasa wale ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu hapa nchini kwani kwa sasa asilimia kubwa ya vijana ambao wanamaliza vyuo vikuu hukosa ajira na hivyo kujikuta wakiwa wamebaki mitaani.
"Vijana wa Tanzania wana uwezo mkubwa sana wa kuweza kufanya mabadiliko kwenye sekta ya kilimo na hivyo sasa tumepanga wahitimu wa vyuo hasa hivi ambavyo wanajifunza masuala ya kilimo waweze kujiajiri wenyewe na wasisubirie ajira kwani uwezo huo sisi kama TAHA tunao kabisa aliongeza,"Jacqline.
Pia alisema ili kuhakikisha kuwa wanawafikia walengwa ambao ni vijana tayari wameshakubalina na vyuo vya Sokoine pamoja na Tengeru ambapo wahitimu wake wataweza kujiunga moja kwa moja na mpango huo ambao unatekelezwa chini ya TAHA.
Aliwataka vijana wote hata wale ambao sio wahitimu wa vyuo vikuu hapa nchini kuhakikisha kuwa wanatumia kilimo kama ajira na pia kushirikiana na TAHA ili kuweza kufanikisha malengo yao mbalimbali.

TASO ARUSHA YAANZA MCHAKATO WA KUWAPATA VIONGOZI WAPYA


Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
CHAMA cha wakulima na wafugaji kanda ya kaskazini TASO, kimeaanza mchakato wa kupata viongozi ngazi za kata katika uchaguzi unaoendelea ambao umeaanza February mwaka huu  kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi waishio vijijini  ambao huwa hawapati fursa ya kushirikimaonyesho ya kilimo ya ngazi ya kanda.
Hayo yamebainisha na Katibu mkuu wa Taso, Peter Ngasamiakwi,mapema jana wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo kwa mwaka huu.
Alisema  kuwa  uchaguzi huo unatokana na mabadiliko ya katiba ya TASO, yanayoelekeza lazima viongozi wa chama hicho  wapatikane kuanzia ngazi za kata bada yawilaya kama ilivyokuwa kabla.
Alifafanua kuwa Kulingana na mabadiliko hayo kila halmashauri ya wilaya inatakiwa inapaswa kuwa na viwanja vya maonyesho ya shughuli zawakulima na wafugaji ili kuwzesha wataalam wa ugani kutoa elimu sahihi itakayosaidia kuleta mapinduzi katika kilimo na mifugo.
"Kupatikana kwa viongozi hao kuanzia ngazi za kata  kutahamasisha uboreshaji wa shughuli za kilimo na mifugo na kuwezesha walengwa kubadilisha shughuli zao na kuwa ni zenye tija na kuepuka kuziendesha kwa mazoea," aliongeza Ngassa.
Hataivyo alidai kuwa wakulima pamoja na wafugaji wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia vema chama hicho kwa ajili ya kuongeza na kuimarisha ufanisi kwenye kilimo kwanza
Ngassa alisema kuwa lengo la chama hicho ni kuona kuwa makundi hayo mawili yananufaika kila msimu wa mwaka na wala sio kwa msimu wa maonesho ya nane nane kama ilivyo kwa baadhi ya wananchi
"Tunatamani sana kuona kuwa haya makundi mawili yanabadilika sana yaani yanafikia malengo tunatamani kuona kuwa wanakuja hata hapa ofisini kwetu na kisha wakapewa elimu ya shamba darasa kama wakifanya hivyo nchi itabadilika sana"aliongeza Ngassa.

HAWA NDIO VIBARAKA WA KAGAME WANAOMCHAFUA RAIS KIKWETE

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Waandishi wa habari watatu nchini, wametajwa kuwa vinara wa utoaji taarifa za kumkashifu rais Jakaya Kikwete kwa serikali ya Rwanda.


Taarifa zinasema waandishi hao wawili wanafanyakazi katika vyombo vya habari binafsi na mwingine yuko Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete. 

Tayari waandishi hawa mashuhuri nchini wamefanya ziara katika nchi za Rwanda, Kongo (DRC), Ufaransa, Ubelgiji, Uganda na Uingereza, ambako pamoja na kukutana na raia wa Rwandwa wanaoishi nchini humo, wamekutana pia na "majasusi ya Kagame."

Aidha, waandishi wamekutana na rais Paulo Kagame, Joseph Kanambe Kabila, Yoweri Museveni na rais wa Ufaransa kwa shabaha ya kumsaidia Kagame kuidhoofisha Tanzania.

“Nakuambia hivi kijana wangu. Wanaosaidia na Kagame kumtukana rais Kikwete, wako humuhumu ndani ya nchi. Kundi ni kubwa mno; lakini ndani yake kuna waandishi wa habari watatu wandamizi nchini,” ameeleza kiongozi mmoja serikalini.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja mwezi mmoja baada ya mtandao mashuhuri nchini Rwanda, NEWS of Rwanda (NR), kuchokomoa kinachoweza kuitwa, "Maisha binafsi ya Rais Kikwete."

Katika taarifa hiyo, mtandao huo wa Rwanda unadai mke wa Rais (Mama Salma Kikwete), ni ndugu wa Hayati Jevenalis Habyarimana, aliyewahi kuwa rais wa Rwanda; na kwamba Rais Kikwete mwenyewe ni mtu dhaifu katika masuala ya mapenzi. 

Rais Kikwete na Paul Kagame wamekuwa na vita ya maneno kwa muda mrefu sasa; huku Rwanda ikiituhumu Tanzania kutumiwa na mabeberu wasioitakia mema nchi hiyo.

Tayari waandishi hawa mashuhuri nchini wamefanikiwa kupenya mitego ya maofisa usalama wa taifa mkoa wa Mwanza waliokuwa wanafuatilia nyendo zao, wakati walipokutana na watu wa RPF - Chama cha Kagame, nchini Uganda, miezi mitano iliyopita.

Hiki kilikuwa kipindi ambacho rais Kikwete alifanya ziara mkoani Kagera, ambako pamoja na mengine, aliagiza kutekelezwa “operesheni wahamiaji haramu."

Ugomvi wa Kagame na Kikwete kwa kiasi kikubwa unatokana na serikali ya CCM kukisaidia chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda ili kimuondoe madarakani Kagame na RPF yake.

UJENZI WA MNARA WA KATIBA DODOMA


Ndugu zangu,
Kwa yanayoendelea mjini Dodoma katika Bunge Maalum la Katiba, hivi kweli tunategemea tutaipata Katiba mpya yenye kuzingatia maslahi ya Watanzania wote?
Ikiwa wawakilishi wetu tuliowaamini na kuwateua wakajidili mustakabali Katiba ambayo haitaleta kero kama tunazozishuhudia wanaendelea kulumbana, wengine wakipiga kelele almradi siku iende na wao waingize posho, hivi tunayo matumaini tena ya mjadala huo kuzaa matunda?
Naungana na Kipanya katika tafakuri hii kwamba mnara wa Katiba unabomolewa hata kabla ya kujengwa. Kila mmoja anajifanya fundi kuliko mwingine, wengine midomo yao haina tohara wanatema matusi ovyo, wengine wamevimbiwa na posho zinazotokana na kodi zetu na wanaona liwalo na liwe tu, wengine wenzangu na miye wamekwenda kule kuchuma fedha, kwani mbali ya 300,000 wanazopewa, bado wanaangalia upepo unaelekea wapi kwenye neema na kuungana nao ili tu wajaze mifuko yao.
Hii ni hatari sana kwa Watanzania wa leo, ambao daima hao hao ndio wamekuwa wakipiga kelele majukwaani mpaka mishipa ya shingo inawatoka kwamba Katiba ya sasa inahitaji kurekebishwa. Sasa wamelishwa nini Yarabi?
Lakini wakumbuke jambo moja tu, wakifanya mchezo, hata makaburi yao yatakuja kuchapwa viboko na watoto na wajukuu zetu.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa
0715 070109

Friday, 28 March 2014

MAPALALA: WARIOBA AMEWAVURUGA CCM

James Mapalala (kulia) akiwa na Rais Jakaya Kikwete

Mwanasiasa mwenye historia ya kipekee nchini, James Mapalala amesema ufafanuzi wa Rasimu ya Katiba uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, umekiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye wakati mgumu.
Mapalala, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba, amesema ufafanuzi huo ni wa kisayansi kwa kiwango cha juu kiasi kwamba atakayetaka kubishana naye, atakabiliwa na kazi pevu ya kujenga hoja.
“Ripoti yake (ya mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba) imekuwa very scientific (ya kisayansi sana). Kila kitu alichoeleza amekitolea ushahidi ulio hai katika maisha ya kila siku ya Watanzania,” alieleza Mapalala.
Mapalala alisema pamoja na kuwa una manufaa kwa mustakabali wa taifa, ufafanuzi huo umeiweka pabaya CCM kutokana na kujibu hoja zote ambazo chama hicho kilipanga kuzitumia kuipinga hotuba hiyo.
“Labda watumie nguvu kubwa lakini kwa mtindo wa kutumia hoja, hakuna Mtanzania mwenye akili timamu atakayeshindwa kubaini hali halisi inayolikabili taifa, kwa sababu ukweli umewekwa peupe,” alieleza Mapalala.
JK akoleza mjadala
Kauli hiyo ya Mapalala imekuja wakati tayari Rais Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge na kueleza kwamba inavyoonekana Muundo wa serikali tatu hautekelezeki.
Mbali na kupinga muundo wa serikali tatu na kupendekeza serikali mbili, Rais Kikwete ameonyesha shaka kuhusu utekelezaji wa ukomo wa ubunge uliopendekezwa na Tume ya Katiba.
Mapalala alisema madai yanayotolewa na baadhi ya wanaotaka serikali tatu kwamba sehemu kubwa ya maoni yaliyo katika rasimu iliyowasilishwa ni maoni binafsi ya Jaji Warioba, yanakosa mashiko kwa sababu sasa kila “mwenye macho haambiwi tazama.”
Anasema hata madai kwamba mahitaji ya serikali tatu ni ya kisiasa; ikielezwa kuwa CUF inaamini itatawalaZanzibar kadhalika Chadema ikijiamini kuwa kitatawala Tanzania Bara, hayana msingi.
Alisema haoni mantiki ya CCM kumpinga Jaji Warioba kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeundwa na Serikali ya chama hicho tawala chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
“Hata marekebisho ya sheria hiyo, yaliyofanyika Septemba mwaka jana yalipitishwa huku vyama vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni vikiwa havipo ndani ya vikao; ikaidhinishwa kuwa tume ikimaliza kuwasilisha rasimu uhai wake uwe umekoma. Ikiwa kwenye mchakato huu kuna siasa, basi zinaletwa na CCM na si vinginevyo,” alieleza Mapalala.

BALOZI SEIF AMPONDA MAALIM SEIF


Balozi Seif Ali Idd
Dodoma. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Balozi Seif Idd ametangaza vita kwa mtu yeyote anayepanga njama za kuvuruga mchakato wa Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo amebeza kauli ya makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif SharifHamad aliyoitoa juzi kwenye viwanja vya Kibandamaiti Zanzibar akisema kuwa kiongozi huyo hana uwezo wa kufanya chochote kisiwani humo.
Juzi katika hotuba yake Hamad alisema chama chake hakiko tayari kuunga mkono suala la Serikali mbili na wala suala la hotuba ya Rais Jakaya Kikwete bali wako katika misingi ya hotuba ya Jaji Warioba.
“Mheshimiwa Hamad hana uwezo wa kufanyajambo lolote visiwani Zanzibar. Zaidi ya yote ataishia kusema tu bila ya mafanikio na ndiyo maana Wazanzibari wameshatambua kuwa mzee yule ni mwongo,” alisema Balozi Idd.
Alisema hali ikiendelea hivyo na Serikali ya Mapinduzi haitasita kuwashughulikia watu wote wa aina hiyo.
Kuhusu nafasi ya Makamu wa Kwanza alisema kuwa alitoa kauli ile kwa nafasi yake ya katibu wa chama cha CUF, lakini hakuwa amesimama kama makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Makamu huyo alipinga kauli kwamba Wazanzibari hawataki serikali mbili kwa kuwa hakuna aliyeulizwa juu ya jambo hilo.
“Kule Zanzibar tuko karibu watu 1.3 milioni, sasa nani aliulizwa kama si uongo wa kutaka kuwagombanishwa watu. Wanafanya ubaguzi usio na maana na hiyo ni choyo tu,” alisema.
Aliwataka wananchi wa Serikali ya Zanzibar kupuuza kauli za makamu wa kwanza wa Serikali ya Zanzibar kwa madai kuwa kauli zake ni kwa masilahi yake na chama chake.
Alisema kwa sasa inaonekana kuwapo na baadhi ya wanasiasa ambao wana mpango wa kukwamisha mjadala wa kujadili Rasimu ya  Katiba, ikiwamo kikundi cha Ukawa.
Huku akionekana kuunga mkono hotuba ya mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ina mashiko na ni nzuri lakini akaponda suala la serikali tatu.
Aliwatupia lawama wanasiasa kuwa wamekosa uvumilivu na utashi wa kweli katika kupata Katiba ya nchi.