Mwanafunzi
Nadhra Mresa (kulia) akipokea cheti cha ufadhili kutoka kwa Karimjee leo hii (Picha
zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).
Diana
Sosoka (kushoto) na Nadhra Mresa wakiwa a hati zao za ufadhili kutoka
taasisi ya karimjee Jivanjee Foundation. Wanafunzi hao kutoka Shule ya
Sekondari ya Wasichana Mtwara, waliibuka washindi wa jumla jumla katika
maonyesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2016
yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). Wanafunzi
hao
wameondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kwa maonyesho ya sayansi.
Na Daniel Mbega wa brotherdanny.com
HAMID
Mresa na mkewe Zakhia Ramadhan hawamini binti yao, Nadhra, amepata ufadhili wa
masomo ya chuo kikuu kutoka katika taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation ya
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shahada ya kwanza ya sayansi.
Na wazazi
hao wanashangazwa zaidi na mafanikio ya binti huyo anayetaka kusomea udaktari
wa binadamu ambaye miaka mitatu iliyopita, wakati akiwa kidato cha tatu, hakuwa
akifanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na aliyachukia.
“Kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha tatu Nadhra alikuwa akifanya vibaya masomo ya
sayansi, hakuyapenda au tuseme aliyaogopa… nilisikitika sana kwa sababu
nilitamani asome sayansi, ikabidi niwaite ndugu na jamaa zangu ambao baadhi ni
madaktari ambao walimhamasisha na akabadilika hatimaye kufaulu vizuri masomo
hayo wakati wa mtihani wa kidato cha nne,” ndivyo anavyoeleza Hamid.
Hamid,
ambaye yeye ana shahada ya Lugha ya Kiarabu na Dini ya Kiislam, anasema tangu
wakati huo, binti yake ameendelea kufanya vizuri na kuwahamasisha hata wadogo
zake watano, akiwemo kaka yake aliyetaka kusomea sheria, naye kupenda sayansi.
Hata hivyo,
kubwa zaidi ambalo wazazi hao wanalishukuru ni ufadhili huo alioupata,
wakieleza kwamba umewapunguzia mzigo wa ada ya chuo kikuu ikiwa atafaulu.
“Tulikuwa
tunafikiria, hivi akifaulu tutafanyaje na sisi uwezo hatuna? Mikopo yenyewe ni
ya ushindani mkubwa,” wanasema kwa pamoja wazazi hao na kuongeza kwamba
wanamuombea afanye vizuri na kufaulu ili ufadhili huo uweze kupatikana.
Lakini leo
hii, Nadhra na mwenzake Diana Sosoka, wanafunzi wa kidato cha sita katika shule
ya sekondari ya wasichana ya Mtwara wanaochukua mchepuo wa Kemia, Balojia na
Jiographia (CBG) wamekabidhiwa hati za ufadhili (scholarship) na taasisi hiyo
ya Karimjee Jivanjee.
Siyo hivyo
tu, wanafunzi hao wameondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kushiriki mashindano
ya kimataifa ya Sayansi na Teknolojia kutokana na ubunifu wao wa mashine za
kutotolesha vifaranga ambao ndio uliowapa ushindi wa jumla wakati wa mashindano
ya sayansi ya Young Scientists Tanzania (YST) yaliyofanyika Agosti 2016 jijini
Dar es Salaam.
Tofauti na
Nadhra, mwenzake Diana anasema alihamasishwa kupenda masomo ya sayansi tangu
akiwa mdogo na kwa ufadhili alioupata anaamini ndoto zake za kuwa daktari wa
binadamu akijikita katika afya ya mama na mtoto, itatimia.
“Naombea
nifaulu vizuri mtihani wa kidato cha sita, nataka niwe daktari niwasaidie
akinamama na watoto,” anasema.
Baba yake,
Sosoka Paul, anasema kwamba amekuwa akiwahimiza watoto wake kupenda sayansi kwa
kuwa anaamini masomo hayo ni kama masomo mengine.
“Hivi sasa
nyumbani kuna mradi mkubwa wa ufugaji na tunatotolesha vifaranga kutokana na
ubunifu wake, tumekuwa tukifuga miaka mingi na yeye amekulia katika mifugo,
nadhani ndiyo maana yeye na mwenzake wakaamua kubuni mashine za utotoleshaji wa
vifaranga,” anasema Sosoka, mkazi wa Mwanza.
Sosoka alikuwepo
wakati wanafunzi hao wakikabidhiwa scholarship zao ikiwa ni pamoja na
kumsindikiza uwanja wa ndege wakati akienda Ireland.
Kutokana
na ufadhili huo wa Karimjee Jivanjee Foundation, wanafunzi hao wawili ambao
wanatarajia kumaliza kidato cha sita mwaka huu, watasomeshwa na taasisi hiyo
chuo kikuu huku wakilipiwa ada pamoja na gharama nyingine zote kwa miaka yote
watakayokuwa wanachukua shahada zao.
Bi. Eliavera
Timoth, Meneja Msaidizi wa Masoko wa Taasisi hiyo, akizungumza kwa niaba ya
Meneja wa KJF Devota Rubama, alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009 na
kuanza kazi zake mwaka 2010 imejikita kwenye ufadhili wa huduma za kijamii hususan
elimu.
“Sekta ya
elimu ndiyo hasa iliyolengwa na taasisi yetu ambapo tumekuwa tukitoa ufadhili
wa masomo kwa vijana wa Kitanzania wanaotaka kusomea elimu ya juu, hasa masomo
ya sayansi tukiwa tunaunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha watoto
wapende masomo ya sayansi.
“Tumedhmiria
kuwahamasisha na kuwaunga mkono watoto wa Kitanzania kuendeleza stadi zao za
ubunifu kupitia sayansi kwa manufaa ya taifa,” alisema Eliacera.
Kuhusu udhamini
wao wa YST, Eliavera alisema tangu mwaka 2012 taasisi hiyo imetoa scholarship
17 kwa wanafunzi kupitia vitengo vya ushindi wa jumla na ushindi wa shule zenye
mahitaji maalum.
“Kila
mwaka KJF inatoa scholarship nne kwa washindi wa tuzo za YST kusoma elimu ya
juu. Tumetoa ufadhili kwa wanafunzi kutoka Kibosho Sekondari (2012 – wanafunzi
watatu washindi wa jumla); Ilongelo Sekondari - Singida (2013 – washindi wawili
wa jumla); na Fidel Castro –Pemba (2013 – washindi wawili wa shule zenye
mahitaji maalum),” alisema Eliavera.
Wengine waliopata
ufadhili huo ni kutoka Lumumba Sekondari – Zanzibar (2014 – washindi wawili wa
jumla); Ngongo Sekondari – Lindi (2014 – washindi wawili wa shule zenye
mahitaji maalum); Mzumbe Sekondari – Morogoro (2015 – washindi wawili wa jumla );
Nasa Sekondari – Simiyu (2015 – washindi wawili wa shule yenye mahitaji maalum);
Mtwara Girls (2016 – washindi hao wawili wa jumla); na Binza Sekondari – Simiyu
(2016 – washindi wawili wa shule yenye mahitaji maalum).
Hata hivyo,
Eliavera alisema, KJF ina mpango wa kuanzisha ufadhili wa program ya Shahada ya
Uzamili ya Uhifadhi Afrika katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland kwa pamoja
na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha.
Katika program
hiyo ya miaka miwili, kwa mujibu wa Eliavera, The programme, KJF itatoa
scholarship tatu kwa wanafunzi kusoma mihula miwili katika Chuo Kikuu cha Glasgow
na mihula nane katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
“Taasisi
imekuwa ikitoa scholarship za Madaktari kwa Shahada ya Uzamili katika Pediatric
Oncology kwenye Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi cha Muhimbili ambapo madaktari
wawili walihitimu mwaka 2015 na mmoja akahitimu mwaka 2016,” alisema Eliavera.
Mwenyekiti
wa Kundi la Makampuni ya Karimjee Jivanjee nchini Tanzania, Hatim Karimjee alisema:
“Tunajivunia kuunga mkono Tuzo za YST kwa sababu tunaamini elimu ni mmuhimu kwa
maendeleo ya kesho ya Tanzania, na kwa sababu elimu ya sayansi inaweza kufungua
fursa na maendeleo makubwa zaidi.”
Katika
maonesho ya 6 yaliyoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST) kwa
mwaka 2016 yalishirikisha jumla ya shule 240 na walimu 120 kutoka nchini kote
ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi zikiwemo fedha taslimu,
medali, vikombe, vifaa vya maabara pamoja na maktaba.
Dk. Gozibert
Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, ameishukuru
taasisi hiyo pamoja na Serikali ya Ireland kupitia Shirika la Kimataifa la
Misaada la Irish Aid na kuomba wadau wengine wajitokeze kufadhili maonesho
hayo.
(Imeandaliwa na www.brotherdanny.com)
No comments:
Post a Comment