Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday, 9 April 2014

WILAYA NNE ARUSHA ZAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA UZAZI, LISHE


Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

IMEELEZWA kuwa mkoa wa Arusha bado unakabiliwa na changamoto ya huduma za uzazi pamoja na lishe bora hali ambayo inasababisha malengo ya Milenia kukwama huku idadi ya vifo vya mama na watoto ikiendelea kuongezeka.
Aidha kwa wilaya nne kati ya saba bado zinaendelea kuzalisha watoto majumbani huku Wilaya nne nazo tena zikiendelea kukabiliwa na changamoto ya lishe duni kwenye jamii.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Frida Mokiti wakati akiongea na wadau pamoja na wataalamu wa sekta ya afya wa mkoa wa Arusha ambao walikutanishwa na shirika la EGPAF mapema wiki hiii huku lengo likiwa  ni kuweza kujadili agenda za afya kwa mkoa wa Arusha.Dkt Mokiti alisema kuwa kwa sasa wilaya ambazo zina jamii ya wafugaji zinakabiliwa na changamoto ya uzazi hafifu pamoja na lishe duni  hali ambayo inasababisha malengo yaliweza kuweka na mkoa kufifia.Aliendelea kwa kusema kuwa wilaya ambazo zinatoa huduma ya uzazi chini ya asilimia 50 kuwa ni pamoja na wilaya za Monduli, Longido, pamoja na Ngorongoro hali ambayo inaendelea kusababisha vifo vya  mama na mtoto kutokea kila mara.Mbali na hayo alidai kuwa wilaya za Meru, Jiji la Arusha,Karatu, ndizo ambazo zimeweza kurahisisha huduma za uzazi kwa mama wajawazito na watoto ambapo wao wanatoa huduma kwa kiwango cha asilimia 70  huku lengo likiwa ni asilimia 80."Hapa tunaweza kuona kuwa hizi asilimia za wilaya nne kwa kweli ni mbaya sana na zinahitaji msaada mkubwa sana kwani hii inasababisha vifo vya watoto na mama zao kuzidi kuongezeka lakini kwa sasa tunampango wa kuweka mikakati itakayoweza kusaidia afya za wananchi wetu kuimarika kwani pia kutokana na hili linasababisha  wengi kuzalia majumbani"aliongeza Dkt MokitiKutokana na hilo pia alisema kuwa utoaji wa huduma za uzazi kwa wanawake na watoto pia bado zinakabilia na changamoto ya lishe duni hali ambayo ni chanzo kikubwa sana cha vifo hasa vya watoto wadogo Dkt Mokiti alisema kuwa Mpaka sasa wilaya ambazo zinakabiliwa na changamoto hiyo ya lishe Duni kuwa ni pamoja na Wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro,pamoja na Wilaya ya Karatu.Katika hatua nyingine naye Meneja wa shirika la EGPAF kutoka katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro Ponsiano Riziki alisema kuwa ili kuatatua changamoto zote hizo kunahitajika umoja baina ya watendaji wa serikali na asasi binafsi.Ponsiano alisema kuwa kwa sasa Shirika hilo limeeka mikakati ya kuwakutanisha kwa pamoja wadau wote ili kuwa na kauli moja ambayo itaweza kutoa majawabu ya afya za jamii kwenye mkoa wa Arusha.

WASUSI 200 WAPEWA MBINU ZA USUSI BORA

Picha ya Mtandaoni

Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

Zaidi ya wasusi 200 kutoka katika mkoa wa Arusha na Manyara wamefanikiwa kupatiwa elimu na mbinu bora za kuboresha biashara zao huku lengo likiwa ni kuongeza kipato kutokana na kazi zao 
Aidha elimu hiyo pia ilienda sanjari na mbinu bora za ususi wa kimataifa ambao unafanywa na nchi ambazo zimeendelea duniani na hivyo kufanya kazi ya ususi kuwa bora zaidi
Elimu hiyo ilitolewa mjini hapa na kampuni ya Hair Tanzania Indusry mapema jana ambapo pia iliweza kuwakutanisha wasusi wote wa mji wa Arusha lakini pia mji wa Manyara.
Akiongea mara baada ya kumalizika kutolewa kwa elimu pamoja na mbinu bora za ususi Meneja wa kampuni hiyo kwa kanda ya kaskazini Bw Noah Mfinanga alisema kuwa kuna sababu kubwa ambazo zimesababisha waweze kuwakutanisha wasusi hao.
Alitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kuwafanya waweze kukubali kazi zao za ususi kwani wanaweza kufanya kazi hiyo kwa kiwango cha hali ya juu sana na hivyo wanaweza kuongeza uchumi wa familia zao lakini pia hata nchi kwa ujumla.
Pia aliongeza kuwa sababu nyingine ni pamoja na kuwapa mbinu za kimataifa za ususi lakini pia namna ya kuendelea kutunza na kuimarisha ususi wao ambao utaweza kulinda utamaduni wa mwanamke wa kitanzania.
"Ususi ni moja ya kazi lakini pia ni moja ya kazi ambayo kila mara inadharaulika sana kwa jamii wakati ni kazi ambayo inaweza kuwajenga watu katika uchumi wa hali ya juu ila kwa sasa tumeweka mpango maalumu wa kuhakikisha kuwa hawa wasusi wa mikoa hii wanajijua na kutambua kazi zao"aliongeza Bw Mfinanga
Wakati huo huo aliwataka hata watanzania kuhakikisha kuwa wanajijengea utaratibu wa kupenda kununua bidhaa za Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kuruhusu nchi kujijenga kiuchumi zaidi.
Hata hivyo wasusi hao ambao wengi wao ni wanawake walisema kuwa wanashukuru kuweza kupewa mbinu mbalimbali za kuongeza ufanisi wa kazi zao lakini ni changamoto kwa makampuni mingine kuhakikisha kuwa wanajiwekea tabia ya kutoa elimu kwani uwepo wa bidhaa nyingine bado haziwanufaishi watanzania ingawaje ni bidhaa za Tanzania.

JIHADHARINI NA MTANDAO WA TCRA FOUNDATION

JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAHADHARI NA MTANDAO WA UTAPELI UNAOJIITA TCRA FOUNDATION


Mamlaka ya Mawasiliano imebaini kuwa kuna mtandao wa matapeli wanaotumia jina la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutumia tovuti inayojiita “TCRA Foundation” na inayodanganya kutoa mikopo kwa maendeleo kwa watu.

Mtandao huu umetengenezwa wa kutumia picha zilizopo kwenye mitandao mbalimbali zikiwaonyesha Raisi Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Makawe Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Prof. John Nkoma.

Aidha mtandao huu unadai kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na Kampuni za Simu za Vodacom na Tigo pamoja na Benki ya CRDB na NMB zinashirikiana kuendesha Foundation hiyo.

Mamlaka ya Mawasiliano inawatahadharisha wananchi kuwa haina “Foundation” yoyote ya kutoa misaada ya fedha. Mtandao huu unatumika kuwalaghai wananchi na kuwaibia fedha zao kwa kuwataka watume fedha za kujiunga na mtandaqo huo kwa number za simu za Tigo na Vodacom zinazoonesha kusajiliwa kwa jina la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Sio kweli na ni wizi na udanganyifu.

Mamlaka ya Mawasiliano inawataka wananchi kuwa na tahadhari na watu hawa ambao hutumia mitandao ya Mawasiliano ya simu na intaneti kufanya utapeli. Usitume fedha wala kujiunga na mitandao ya namna hii.

Aidha Mamlaka ya Mawasiliano inawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa wanapobaini utapeli wa namna hii kwa kutoa taarifa kwa Mamlaka kwa vyombo vingine vya usalama ikiwa watahisi au kuwa na taarifa za watu wanaojihusisha na udanganyifu huu katika mitandao ya Mawasiliano ili kuzuia vitendo hivi vilivyoshamiri katika siku za hivi karibuni.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
8Aprili 2014


SABABU TANO ZA EDWARD LOWASSA KUWA RAISI 2015


Mheshimiwa Edward Ngoyayi Lowassa

HIZI NDIZO SIFA ZA LOWASSA BILA SHAKA KWENYE KWELI UWONGO HUJITENGA.!!

Sababu nzito Tano ambazo mimi binafsi naziona zinafaa sana kumtathmini Edward Lowasa kama Rais ambae Tanzania inamuhitaji kwa muongo mwingine ujao. Nikiri wazi kwamba kwa CCM ni Lowasa pekee mwenye sifa hizo labda nitamlinganisha na Dr. Slaa ambae kwa muono wangu kidogo anamkaribia Lowassa nikimaanisha kidoogo wanalandana na nitasema wapi Lowassa anampiku Slaa.
Kwa utangulizi tu ni kuwa Nchi hii ili iendelee inahitaji KIONGOZI kwa ufupi kabisa niseme hivyo inahitaki KIONGOZI SHUPAVU tena SHUPAVU KWELIKWELI sio masihara. Waziri mkuu Mizengo Pinda na Mbunge wa Monduli Erdward Lowassa. Tupo kwenye umaskini mkubwa, watu wanateseka bila sababu ya msingi. Vijana tunashabikia tuu kama wehu, wengine ni wasomi lakini tunapelekwa kama upepo tukisikia hiki "hewala" tukisikia kile "sawa" tukiambiwa hivi "alhamdulilah" tukiambiwa kile "poa tu". Hatutaki kuchambua na kuielewa siasa kwamba kwenye siasa kuna majungu,fitna,kuchongeana,uchu wa madaraka na mali na mambo meeeengi ambapo msipokua makini mnaweza KUMCHUKIA MZURI MKAMPENDA MBAYA. kwa misingi hii ninaanza uchambuzi wangu. Na uchambuzi huu nitauandika kwa facts and figures kama anavyosemaga Prof.Muhongo.
1.LOWASSA NA "BIG RESULTS NOW".
Nianze na hili.Tunajua wote kuwa serikali yetu sasa ipo kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa BRN.Mpango huu mbali na mambo mengine unahitaji kiranja mkuu (RAIS) ambae ni SHUPAVU, JASIRI, MTHUBUTU, MWENYE KUWEKA MALENGO NA KUSIMAMIA KUONA YANATEKELEZEKA lakini pia kama jina la mpango lenyewe lilivyo "MATOKEO MAKUBWA SASA" yaan we want things to happen now. Kwa minajili hiyo ni kiongozi gani mnaeona anaeweza kuleta matokeo makubwa sasa? Embu tuwe wakweli LOWASSA tunamjua alipoingia kuwa waziri mkuu alitangaza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ambacho angekuwa WAZIRI MKUU angetaka kata zote ziwe na shule za sekondari. Sote ni mashahidi alivyosimamia sera hiyo shule zilianza kumea kama uyoga yaani kama mazingaombwe.
Hata maeneo kama ya Kinondoni ambapo ardhi huuzwa kiholela hivyo ardhi kutopatikana lakini ilipatikana kuanzia vijijini hata mijini wananchi walianza kujenga
shule. Ni mashahidi kama sio fitna za yeye kupelekea kujiuzulu sijui leo kielimu tungekuwa wapi. HE HAD A MASTER PLAN OF OUR EDUCATION SYSTEM AND HE LEFT WITH IT BUT STILL HE HAS IT IN HIS HEAD. Naamini huyu mzee akipata nafasi tutafika. Si hilo tu tunajua mambo mengi aliyokuwa nayo kichwani ambayo mengi yapo kwenye huu mpango ni shupavu ambae angeweza na anaweza kuyasimamia yatekelezeke. Dr.Slaa ni mzuri wa kusimamia mambo lakini sometimes huwa analoose focus nitaliongelea kwenye point ya tatu.
2. LOWASSA ANAJUA KUWEKA VIPAUMBELE NA KUJUA TUNAVIFIKIAJE.
Jamani Nchi hii ili iendelee na ndivyo hata nchi zilizoendelea zilivyoanza ni kuwekeza katika elimu ya watu wake, Kilimo na Viwanda nikimaanisha sekta ya uzalishaji. Tunajua jinsi LOWASSA alivyo anza na hayo shule za kata nilishazizungumzia na mipango mingi
ya elimu ukitaka kuijua waulize walimu alipoanzisha program ya kuwajengea nyumba,alivyoanzisha program ya kuhakikisha watoto hawakai chini kila mtoto akae kwenye dawati,alivyoshusha ada n.k Tusisahau kwenye kilimo aliyoanzissha kilimo cha umwagiliaji
mpaka akataka kuleta Mvua ya kutengenezawa mimi huwa nasema hata kama isingewezekana lakini inaonyesha ile nia njema aliyonayo mzee huyu.
Ukitaka kuelewa vizuri waulize wakulima wakuhadithie jinsi alivyokua anawatimua kazi na kuwashtaki watu waliokua wanakula hela za mbolea za ruzuku. Jinsi alivyokua anatafuta
masoko ya nje ya mazao ya kilimo waulize wafanyabiashara wakuhadithie.
Ni kiongozi nani mwenye hulka na kariba hii ndani ya CCM? Tunajua wote kuwa mapinduzi ya kilimo na viwanda ndiyo yaliendeleza bara la ulaya historia inatuambia hivyo na elimu ndiyo
imeikomboa JAPAN na nchi nyingine LOWASSA ni jembe katika hili ana master plan ya mambo haya na anajua kusimamia haya sio siri wala kumpigia debe HE IS REAL.
3. LOWASSA SIO MTU WA KUPOTEZA UELEKEO (TO LOOSE FOCUS)
Lowassa siku zote akitaka kitu ni mpaka kitimie na kikishindikana basi ujue kumpata wa kukiweza ni shughuli pevu na akitaka kitu hakati tamaa ili mradi kiwe ni chema hata kama hakina maslahi kwake na ikitokea yeyote akasimama mbele yake kumzuia basi ama zake ama za huyo mtu. Wazungu wanasema "You are either with me or against me". Tunakumbuka jinzi alivyokua akitimua viongozi waliokuwa wakitaka kumkwamisha kwenye utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Hakujali urafiki wala nini anakuweka ukimzingua anakumwaga THAT IS THE TYPE OF THE PRESIDENT WE WANT kwa sifa hii hana tofauti na Dr. Slaa japo Slaa huwa wakati mwingine anapoteza uelekeo.
Mfano mzuri wa kutopoteza uelekeo ni kwamba mwaka 1995 alitaka kuwa Rais wakatoswa, 2005 akakubali swahiba wake achukue lakini akabaki kuwa focused, fitna zikajengwa akajiuzulu 2007 lakini hata sasa bado hajaloose focus japo anaface a lot of challenges.
Sio mfano mzuri sana huo kutoa lakini inaonyesha ni mtu wa namna gani kuwa siku akitaka vijana tukimaliza vyuo tupate kazi maana yake atalisimamia hilo by hooks or crooks
kama ni viwanda kufufuliwa vitafufuliwa idimradi tu vijana tulambe ajira THAT IS THE PRESIDENT WE WANT. A FOCUSED MAN
4. LOWASSA NI HALF DICTATOR HALF DIPLOMATIC
Hahahahaha nianze kwa kucheka maana tunajua hakuna nchi iliyoendelea kwa kiongozi kuwa full diplomatic yaani kitu kidogo "Tume iundwe" jambo dogo "NJOO MEZANI TUONGEE" kitu kidogo "TUSUBIRI UCHUNGUZI" jambo kidogo "DUNIA ITATUELEWAJE". jamani tunamjua LOwassa ni mtu wa action kwa kwenda mbele Ghorofa limeanguka nani mkandarasi piga chini. Halmashauri imekula hela za maendeleo nani mkurugenzi piga chini.
Wizara inatokota nani muhusika piga chini. Tunatatizo fulani solution ni nn tekeleza.yaani hakuna longolongo.Hii ndio type ya uongozi itakayotukomboa Tanzania. Na ukitaka kujua faida yake waulize wachina yaani watakwambia vizuri udictator kidogo unavyoharakisha maendeleo yao. Hakuna TANZANIA hii viongozi wa type hii mbali na LOWASSA na Dr. SLAA tatizo SLAA .... (nitamuonge lea wakati mwingine)
5. LOWASSA ANASIKILIZIKA, ANAFUATILIA, SI KIGEUGEU NA SI MVIVU.
Hii ni sifa kubwa kwa mtu kuwa RAIS unapoona unataka kuwa Rais au unamchagua mtu ambae kwa haiba yake tu hasikiliziki ujue unaturudisha nyuma. Rais anatakiwa awe akisema hili lifanyike huyo anaeambiwa linamuingia moyoni. Nirudie Rais anatakiwa anapoongea hata kwa simu tu ile pitch ya sauti iashirie kuwa jambo hili ni lazima lifanyike.Yaani kama anaongea mbele yako ukimwangalia kuanzia nywele mpaka unyayo uashirie kuwa kiongozi anataka hili lifanyike. LOWASSA yupo hivyo akisema jambo linatekelezwa na haiishi hapo anafatilia mwanzo mwisho si mvivu hata kidogo.kutwa anaizunguka Tanzania hii vijijini hadi mijini nyote ni mashahidi wa hili.
SIMAMA SASA NA UHESABIWE kuelekea safari ya matumaini na mafanikio 2015.!


CHANZO: WANABIDII

Wednesday, 2 April 2014

KIMBUNGA HELLEN BADO KIPO

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

WIZARA YA UCHUKUZI 
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA 

Simu: 255 22 2460735/2460706-8 
Faksi: 255 22 2460735/2460700 S.L.P. 3056 
Barua pepe: met@meteo.go.tz DAR ES SALAAM 
Tovuti: www.meteo.go.tz 

Kumb.No. TMA/1622 01 April, 2014 

TAARIFA KWA UMMA 
Mwelekeo wa Kimbunga “HELLEN” na hali ya Mvua 

Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kufuatilia kwa karibu mifumo ya hali ya hewa na 
mabadiliko yake pamoja na adhari zake kwa Nchi yetu na kutoa utabiri na tahadhari za hali 
mbaya ya hewa. Tarahe 28 Machi 2014 mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la Rasi ya 
Msumbiji kusini magharibi mwa bahari ya Hindi ulianza kuimarika zaidi na kusababisha 
kuwepo kwa makutano ya upepo na mwelekeo wa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo 
mengi nchini. Tarehe 29 Machi 2014 mgandamizo huo wa hewa (Tropical Depression) 
uliimarika zaidi na kuwa kimbunga kilichopewa jina ‘Hellen’ (Tropical Cyclone) uchambuzi 
ulionesha kuwa kimbunga ‘Hellen’ kilitarajiwa kuongezeka nguvu (Severe Tropical Cyclone) 
na kusababisha ongezeko zaidi la mvua na upepo mkali. 
Hivyo maeneo yafuatayo yalitabiriwa kuwa na adhari zaidi za mabadiliko hayo kuanzia tarehe 30 Machi hadi 01 April 2014 ; Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na mikoa ya Dodoma, Singida, Ruvuma, Katavi, Njombe, Iringa, Mbeya na Morogoro. 
Viwango vya mvua zaidi ya mm 50 kwa saa 24 zilizopimwa tarehe 30 Machi hadi Asubuhi 
ya tarehe 01 Aprili 2014. 
Tarehe 30 Machi- 01 April 2014 
Morogoro 71.9mm, Mahenge 70.2mm na Ilonga 64.7mm. 

Mwenendo wa Kimbunga Hellen katika kipindi cha saa 24 Zilizopita. 
Katika kipindi hicho nguvu ya Kimbunga ‘Hellen’ ilibadilika mara kwa mara na katika vipindi vifupi hususan kilipokaribia pwani ya kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagasca, hivyo kubadili pia mifumo ya hali ya hewa na viwango vya mvua vilivyotarajiwa katika baadhi ya maeneo ambayo tahadhari ilitolewa. 
Hata hivyo kimbunga ‘Hellen’ bado kipo katika eneo la rasi ya Msumbiji karibu na pwani ya Kisiwa cha Madagascar ambapo kitaendelea kusababisha mabadiliko ya mvua katika maeneo machache, hususan katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa. 
Mvua za Masika zinatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini kama zilivyotabiriwa. 
Mamlaka inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa na tahadhari kila 
inapobidi. 

Imetolewa na 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania 

BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI LAVUNJIKA


Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Margret Zziwa akitoka nje ya Bunge

Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeanza kuonekana kufanana na Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Bunge hilo jana limevunjika bila kujulikana litakutana tena lini baada ya kuibuka mabishano ya kisheria kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Spika, Margret Zziwa.
Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari vya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa na hatimaye kuwasilishwa jana na Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kwa niaba ya wenzake Shy-Rose Bhanji wa Tanzania, Nyiranilimo Odette wa Rwanda na Hafsa Mossi kutoka Burundi.
Awali Bunge hilo linalopaswa kuanza vikao vyake saa 8:00 mchana lilichelewa kuanza hadi Saa 9:44 alasiri baada ya wabunge kugoma kuingia ukumbini walipobaini kuwa hoja ya kumng’oa Spika haikuwa miongoni mwa shughuli za Bunge kwenye kikao cha jana.
Baada ya mashauriano ya muda mrefu kati ya ofisi ya spika, Mwanasheria wa EAC, Wakili Wilbert Kaahwa na Katibu wa Bunge, KennethMadete, Spika Zziwa alikubali hoja ya kumng’oa iongezwe kwenye orodha ya shughuli za Bunge ndipo Mbunge Mathuki alipopewa fursa ya kuwasilisha hoja.
Hata hivyo dakika moja tangu Mathuki alipoanza kusoma maelezo ya hoja hiyo, Mbunge Fred Mukassa Mbidde aliinuka na kuomba mwongozo wa Spika na alipopewa nafasi, alipinga hoja hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa kwa madai kuwa kuna kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) inayohusiana na hoja hiyo.
Akifafanua Mbidde alisema kesi hiyo inaomba mwongozo na ufafanuzi wa kisheria kuhusu kanuni ya 9 ya Bunge la EAC inayoelekeza utaratibu wa kumwondoa madarakani Spika wa Eala iwapo kutatokea haja ya kufanya hivyo.
Wakati Mbunge Mbidde akiwa bado amesimama huku akiendelea kutoa hoja yake, Mbunge JosephOmbasa kutoka Kenya aliinuka na kumpinga mbunge mwenzake akisema anataka kulipotosha Bunge kwani kifungu 38 (3) kinaruhusu Bunge hilo kujadili hoja yoyote yenye masilahi ya umma wa EAC ikiwamo hilo la kumng’oa Spika.
Baada ya hoja ya Ombassa, Mwanasheria wa EAC, Kaahwa alisimama kutoa ufafanuzi wa kisheria licha ya kukiri kuwapo kesi mahakamani alisema tayari mahakama hiyo imetoa uamuzi mdogo kuwa shauri hilo haliwezi kuzuia shughuli na mjadala wowote wenye nia ya kumwondoa Spika madarakani
Hoja hiyo ya Mwanasheria ilimwibua tena Mbunge Mbidde aliyehoji kwanini maelezo na ufafanuzi wa mwanasheria huyo yanatoa mwelekeo wa ulipo msimamo wake kuhusu hoja iliyokuwa mbele ya Bunge.
Katika hali iliyoashiria uwapo wa kimkakati kati ya kiti cha Spika na Mbunge Mbidde, Spika Zziwa naye aliunga mkono hoja ya mwanasheria kuonekana anaelemea upande unaotaka ang’olewe.
Kauli hiyo ilimwamsha kitini Mwanasheria Kaahwa aliyemhakikishia Spika kuwa hoja yake inalenga kusaidia uendeshaji bora wa Bunge na siyo kuegemea upande unaotaka kumng’oa.

WATANZANIA WALIOLIPULIWA NA OSAMA KUZOA SHS. 672 BILIONI

Osama bin Laden

Nairobi/Dar. Watanzania wanne waliojeruhiwa katika mlipuko wa bomu katika ubalozi wa Marekani mwaka 1998 na wengine watano waliofariki dunia katika mlipuko huo watalipwa fidia ya Sh672 bilioni, kiwango ambacho ni sawa na bajeti ya wizara nne za Tanzania.
Watanzania hao waliuawa na wengine kujeruhiwa katika moja ya mashambulizi pacha yaliyotokea kwa wakati mmoja jijini Dar es salaam na Nairobi, Kenya na ambayo yaliratibiwa na Osama Bin Laden akitumia mtandao wa kundi la Al Qaeda mwaka 1998 kwenye ofisi za balozi za Marekani.
Katika mashambulizi hayo yaliyotokea saa 4:00 asubuhi Agosti 7, 1998, Wakenya 200, Watanzania 10 na Wamarekani 12 walipoteza maisha na pia magaidi wawili nao walikufa.
Kati ya Watanzania 10, ni kesi za watu wanne tu waliouawa tu zilizofunguliwa kudai fidia ya watu hao kupoteza maisha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani, Thomas Bates alitoa hukumu hiyo wiki iliyopita, akiagiza pia kwamba serikali za Iran na Sudan lazima zilipe jumla ya Dola za Marekani 957 milioni (Sh1.53 trilioni) kwa Watanzania hao na Wamarekani 23 waliouawa au kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya kigaidi.
Jaji Bates alisema kiasi cha Dola 488 milioni za Marekani (Sh780.8 bilioni) kitalipwa kwa Wamarekani 12 waliouawa na familia zao. Dola 420 milioni za Marekani (Sh672 bilioni) zitalipwa kwa Watanzania wanne waliojeruhiwa katika mlipuko na Watanzania watano waliuawa katika shambulio hilo. Dola milioni 49 (Sh78.4 milioni) zitalipwa kwa raia wawili wa Marekani waliojeruhiwa katika milipuko hiyo.
“Milipuko ya mabomu katika balozi hizo mwaka 1998 iliwaathiri wanaoshtaki katika kesi hii, “Jaji Bates aliandika. Kupitia simulizi zao binafsi, inaonyesha kwamba hata zaidi ya miaka 15 baadaye kila mmoja bado ana kumbukumbu za kutisha za siku hiyo.
“Fidia hii haiwezi ikarudisha maisha ya wale waliokufa wala waliopata madhara. Badala yake, ni ya kutoa tu kifuta machozi. Lakini hiyo ni kidogo sana kwa wale wanaoshtaki.”
Hata hivyo, uamuzi wa Jaji Thomas Bates haujaeleza fedha hizo zitalipwa lini kwa waathirika hao.
Kiwango cha Sh672 bilioni ni sawa na bajeti za Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo katika mwaka wa fedha wa 2013/14 ilitengewa Sh20.4 bilioni, Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Sh21.3 bilioni), Uchukuzi (Sh491.1 bilioni ) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotengewa Sh138.3 bilioni.
Thomas Fay, wakili aliyewawakilisha Watanzania na Wamarekani, alisema kuwa juhudi zinazotakiwa sasa ni kuanza kutambua mali za Iran na Sudan ambazo zinaweza kutaifishwa ili kulipa fidia hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Washington alisema kuwa hukumu ya Jaji Bates ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Wamarekani na Watanzania walioathirika kwa ugaidi huo wanapata haki kwa mateso waliyoyapata.

SHEIKH ABUBAKAR SHARIFF 'MAKABURI' SHOT DEAD IN MOMBASA

Sheikh Abubakar Shariff alias Makaburi

By Benard Sanga and Stanley Mwahanga

Mombasa, Kenya: Riots broke out in several parts of Mombasa following the killing of radical islamist and terror suspect Sheikh Abubakar Shariff alias Makaburi outside the Shanzu Law Courts.
Eyewitnesses told The Standard that at approximately 6.30pm last evening, some men wearing white flowing robes in a white car opened fire on Makaburi and five other unidentified men as the group waited for a bus after appearing in the court. The gunmen sped towards Mombasa, according to eyewitness accounts.
Makaburi was killed two days after intelligence officials linked him to the March 23 killing of worshippers in a Mombasa church.
The officials indicated last weekend that the Anti-Terror Police Unit had concluded allegedly, after telephone intercepts that Makaburi aided militants allied to Al Hijra, an affiliate of Al-Shabaab in Mombasa, to procure guns and commit the March 23 church massacre allegedly on the orders of a Kenyan Yemeni based Al-Qaida fugitive Ahmed Iman Ali.
And Makaburi, who openly praised violence, Al-Shabaab and rationalized the September 22, 2013 Westgate terror attack was killed less than a week after he won Sh670,000 in damages from the State forillegal search of his home two years ago.
Makaburi and Iman were also linked to the booby-trapped car found at the Mombasa police headquarters on March 17.
In July last year the UN Monitoring Group linked Makaburi to Al Hijra activities in Mombasa, Nairobi, Tanzania and Burundi. The report that Makaburi and British terror suspect Jermaine Grant who is facing terrorism charges had assumed the leadership of Al-Qaida and its affiliates in Kenya and East Africafollowing the August 27, 2012 killing of his former comrade Sheikh Aboud Rogo.
A man who identified himself as Steve told The Standard that Makaburi and his group were coming from the court and were waiting for a matatu to go to town when two men dressed in kanzus inside a car shot them.
The Standard at the scene described Makaburi’s body as bloodied and spread-eagled by the road sidewith his head hanging in a ditch.
His chest had what appeared like bullet marks.  A second person who was in the company of Makaburi known only as Bahero was killed on the spot. Three other men who were  injured were still at the scene by the time of going to press.
The dead and injured were later  taken away by police to Bamburi Police Station.
Makaburi’s militant supporters poured out of Masjid Shuhadaa in Majengo, Mombasa to block roads and protest his killing. Until last month Masjid Shuhadaa was called Masjid Musa and is a known base for radical islamists in the mould of  Makaburi and his slain radical and comrade Sheikh Aboud Rogo.
 By the time of going to press dozens of Makaburi’s supporters blocked sections of the Malindi to Mombasa road. Police fired warning shots in a bid to disperse them.
The youth, who were demanding the bodies for burial, shouted: “Allahu Akbar we want our martyr we want to bury him according to Muslim tradition.”


Tuesday, 1 April 2014

JK KATIKA ZIARA YAKE UINGEREZA

1_3ed4b.jpg

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Bw. Hague alipomtembelea ofisini kwake jijini London kwa mazungumzo Machi 31, 2014
3_04702.jpg
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron alipomtembelea ofisini kwake 10 Downing Street jijini London kwa mazungumzo jana
2_c093a.jpg
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akibofya kitufe kuzindua rasmi mpango wa bima ya afya na maafa wa WESTADI wa mfuko wa Jamii wa NSSF jijini London, akiwa na Mkurugenzi wa NSSF Dkt RAmadhani Dau na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya mfuko huo Bw. Abubakar Rajabu (kushoto) . Mwenye miwani kati ni Bw. Aboubakar Faraji aliyekuwa mwongoza sherehe wa siku hiyo ambapo Dkt Kikwete alikutana na kuzungumza na Watanzania waishio Uingereza.

5_549d6.jpg
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wadau mbalimbali wa biashara na uchumi wa Uingereza aliokutana nao katika ukumbi wa Chatham House jijini London Machi 31, 2014

MALIASILI YALIPWA TSHS. 25 MILIONI, YAKAMATA MAJANGILI 544 NA MENO YA TEMBO

 

Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha

WIZARA ya Mali asili na utalii imefanikiwa kukamata majangili 544 wanaojihusuisha na ujangili kwenye hifadhi mbalimbali hapa nchini pamoja na mizoga ya tembo 39,meno ya tembo mazima,katika oparesheni maalumu ambayo imeftanyika kati ya Januari na Machi mwaka huu.
Hataivyo kukamatwa kwa vitu hivyo kunatokan na doria ambazo zinafanywa na baadhi ya askari wa wanyama pori ambazo zilikuwa zinaendelea kufanyika katika mapori na hifadhi mbalimbali.
Akiongea na vyombo vya habari mapema leo Mkurugenzi wa wanyama pori Taifa Paul Sarakikya alisema kuwa hiyo imetokana na oparesheni ambayo inaendelea kufanywa na wizara hiyo huku lengo lake likiwa ni kupunguza kasi ya ujangili.
Aidha alisema kuwa katika kipindi cha mwezi January hadi kufikia Machi Mwaka huu jumla ya doria zilizosababsisha kukamtwa kwa vitu hivyo ni doria Mandays 30,372 ambapo zilikuwa ni kwa ajili ya kukabiliana na ujangili  ndani na hata nje ya hifadhi za taifa,mapori ya akiba nchini
Aliendelea kwa kusema kuwa katika kipindi husika jumla ya mizoga ya tembo 39 ilionekana ndani na nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akibanchini huku meno mazima yakiwa ni 171 na vipande 22 vya meno ya tembo ghafi , vipande 302 vya meno ya tembo yaliyochakatwa yenye jumla ya kilo 662.62
Mbali na hilo pia alisema kuwa katika doria hizo waliweza kukamata vitu vingine ambavyo ni kama vile nyama pori za wanyama mbalimbali ambazo zilikuwa zinatolewa na majangili hayo kwa ajili ya viteo jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria ya nchi inavyosema na kufafanua zaidi
"tumefanikiwa kukamata hivi vitu kutokana na jitiada ambazo tumeziweka hapa kwetu na hata nje lakini bado tuna mikakati mingine mingi zaidi ya kuweza kuwateka majangili ambao wanasababisha madhara makubwa kwa taifa letu la tanzania"aliongeza Sarakikya
Katika hatua nyingine alifafanua kwa kudai kuwa waliweza kukamata hata vifaa mbalimbali ambavyo vilikuwa vinatumika na majangili hayo kwa ajili ya shuguli zao ndani ya mapori lakini hata hifadhi mbalimbali hapa nchini.
aliweza kutaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na Bunduki ya rashasha  moja, Rifle 3, shotgun 2, gobori 5 na jumla ya risasi 7 za aina mbalimbali  pamoja na malighafi kama vile  magari 5  ngombe 2663 misumeno 1 na mbao 745
kutokana na hilo pia watuhumiwa waliweza kulipa faini ya zaidi ya milioni 25 na pia hali hiyo iliweza kusababisha hata ujangili kushuka kwa kiwango cha asilimia 58 tofauti na mwaka jana ambapo ujangili ulikuwa ni mkubwa sana.

RAIS SHEIN AZUNGUMZA NA WAZIRI MATHIAS CHIKAWE IKULU ZANZIBAR

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akimkaribisha ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe. Waziri Chikawe alifika ofisini hapo kwa lengo la kujitambulisha kwa Rais huyo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Viongozi hao pia walijadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania Bara na Visiwani. Katikati ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pereira Ame Silima. (Picha zote na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza kwa makini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe (katikati) alipokuwa akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu ya Zanzibar leo.  Waziri Chikawe alifika ofisini hapo kwa lengo la kujitambulisha kwa Rais huyo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Viongozi hao pia walijadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania Bara na Visiwani. Kushoto ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pereira Ame Silima.  (Picha zote na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (watatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe (watatu kushoto), Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pereira Ame Silima (wapili kulia), Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (wapili kushoto). Kulia ni Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa, Ofisi ya Zanzibar, Vuai Suleiman. Kushoto ni Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omary Makame. Waziri Chikawe alifika Ikulu ya Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha kwa Rais Shein baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Viongozi hao pia walijadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania Bara na Visiwani. Kushoto ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pereira Ame Silima.  (Picha zote na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).

PICHA ZOTE NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

MIAKA 100 YA WW1: MWANAFUNZI ALIVYOSABABISHA VITA KUU YA KWANZA YA DUNIA

Gavrilloprincip_86c0f.jpg
Gavrilo Princip, muuaji wa Mfalme Franz Ferdinand
Franz_ferdinand_762b2.jpg
Mfalme Franz Ferdinand
Na Daniel Mbega

VITA Kuu ya Kwanza ya Dunia (WWI), ilianzia na kuhusisha mataifa ya Ulaya lakini ikasambaa ulimwenguni kote. Vita hii ilianza Julai 28, 1914 na kufikia tamati Novemba 11, 1918. Tangu kuanza kwa vita hiyo hadi kuibuka tena kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1939, ilikuwa inafahamika tu kama Vita Kuu. Zaidi ya wanajeshi milioni 9 waliuawa. Huo ulikuwa mgogoro wa tano mkubwa zaidi katika historia ya dunia, na kufungua mlango wa mabadiliko makubwa ya kisiasa, yakiwemo mapinduzi katika mataifa mengi yaliyohusika.
Vita hivi vilihusisha mataifa yote yaliyokuwa na nguvu za kiuchumi duniani, ambayo yalikuwa katika pande mbili zinazopingana kulingana na uchumi wao: Majeshi ya Washirika (yaliyotokana na Mkutano wa Utatu wa Uingereza, Ufaransa na Dola ya Russia) na Majeshi ya Kati (Central Powers) yaliyoundwa na Ujerumani na Austria-Hungaria. Ingawa Italia ilikuwa mjumbe wa Muungano wa Majeshi ya Kati pamoja na Ujerumani na Austria-Hungaria, haikuweza kuungana nayo kwani Austria-Hungaria ilikuwa imekiuka masharti ya umoja huo.
Majeshi hayo ya pande mbili yalikuwa yameundwa na kutanuka kadiri mataifa mengi yalivyoingia kwenye vita hivyo: Italia, Japan na Marekani wakajiunga na Majeshi ya Washirika (Allies), na Dola ya Ottoman na Bulgaria wakajiunga na Majeshi ya Kati. Maofisa milioni 70 wa kijeshi, wakiwemo milioni 60 kutoka Ulaya, wakajipanga katika mojawapo ya vita vikubwa kabisa katika historia ya dunia.

KUUAWA KWA MFALME FRANZ FERDINAND
Sarajevo_princip_bruecke_9da18.jpg
Daraja mjini Sarajevo ambapo Mfalme Ferdinand na mkewe Sophie waliuawa Juni 28, 1914
Japokuwa kuibuka kwa ubepari kulikuwa sababu ya msingi ya vita hivyo, lakini chanzo kikubwa kilikuwa ni tukio la Juni 28, 1914 la kuuawa kwa Archiduke Franz Ferdinand wa Austria, mrithi wa taji la ufalme la Austira-Hungaria. Ferdinand aliuawa mjini Sarajevo, Yugoslavia na manafunzi mwanaharakati Gavrilo Princip. Hii ilileta mgogoro wa kidiplomasia wakati Austria-Hungaria ilipopeleka sharti (ultimatum) kwa Ufalme wa Serbia, na umoja wa kimataifa uliokuwa umeundwa miongo kadhaa nyuma ukavunjika. Ndani ya wiki chache tu, mataifa makubwa yalikuwa vitani na mgogoro ukasambaa haraka dunia nzima.
Mnamo Juni 28, 1914, Mfalme Mkuu Franz Ferdinand wa Austria, ambaye alikuwa ndiye mrithi wa taji la ufalme la Austro-Hungaria, na mkewe Sophie, Duchess wa Hohenberg, waliuawa mjini Sarajevo na Gavrilo Princip, mmoja wa kundi la wauaji sita (watano Waserbia na mmoja Mwislamu wa Bosnia), mauaji yaliyoratibiwa na Danilo Ilic.
Madhumuni ya kisiasa ya mauaji hayo yalikuwa kuyavunja majimbo ya Slavia ya kusini katika himaya ya Austro-Hungaria ili yaungane na Serbia Kuu au Yugoslavia. Maofisa wa kijeshi wa Serbia walikuwa nyuma ya mauaji hayo yaliyoendeshwa katika harakati za Young Bosnia.
Mauaji hayo yalisababisha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia wakati Austira-Hungaria ilipotoa sharti la mwisho dhidi ya Serbia, ambalo lilikataliwa. Austria-Hungaria ikatangaza vita, na ndipo vita hasa ilipoibuka.
Kati ya maofisa wa jeshi la Serbia waliokuwa nyuma ya mpango huo walikuwemo Mkuu wa Ujasusi wa Kijeshi wa Serbia Dragutin Dimitrivajec, msaidizi wake wa karibu Meja Vojislav Tankosic, na Jasusi mkuu Rade Malobabić. Meja Tankosić aliwapatia wauaji mabomu na bastola na kuwapa mafunzo. Wauaji hao walipewa fursa kuingia katika mtandao maalum na kutumia nyumba za siri na mawakala wa usalama ambao Rade Malobabić aliwatumia wakati akipenyeza silaha na shughuli zake ndani ya Austria-Hungaria.
Wauaji hao, wafuasi wa mtandao ya kijasusi, na maofisa wa jeshi la Serbia waliohusika ambao walikuwa hai bado, walikamatwa, wakashtakiwa, wakakutwa na makosa na kudhibiwa. Waliokamatwa Bosnia walishtakiwa Sarajevu Oktoba 1914. Wengine walishtakiwa kwenye mahakama ya kangaroo ya Kiserbia katika eneo la Salonika Front lililokuwa linamilikiwa na Ufaransa kati ya mwaka 1916-1917 kwa mashtaka ya uongo yalisiyohusiana na mauaji hayo; Serbia iliwanyonga maofisa watatu wa jeshi.
Itaendelea kesho...
http://www.mjengwablog.com/habari-za-kijamii/item/10354-miaka-100-ya-ww1-mwanafunzi-alivyosababisha-vita-kuu-ya-kwanza-ya-dunia.html

UKAWA WAANZA MAPAMBANO NJE YA BUNGE


Mjumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), Ismail Jussa akionyesha moja ya nukuu za kitabu cha Profesa Issa Shivji wakati wa mkutano na waandishi Dodoma jana. Kushoto ni mjumbe mwenzake, Tundu Lissu. Picha na Salima Shao 


Dar /Dodoma/Mwanza. Ni dhahiri kwamba mjadala wa msomi wa Sheria, Profesa Issa Shivji umewavuruga wanasiasa waumini wa serikali mbili ambao baadhi yao jana walimshukia wakidai kuwa “mzee huyu ni ndumila kuwili na kigeugeu.”
Shivji juzi alitoa mjadala kuhusu muundo wa Muungano na kuishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza serikali tatu, kuwa ilipotosha maoni ya wananchi. Alipotakiwa kuzungumzia madai dhidi yake, Profesa Shivji alisema: “Nyie ni waandishi wa habari someni, angalieni wapi mimi nilisema Serikali tatu, wanaosema ninatumiwa na CCM hayo ni maoni yao siwakatazi kuzungumza wanachofikiria.”
Jana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kampeni yake nje ya Bunge la Katiba, ulimtaka Profesa Shivji kuwaomba radhi wananchi kwa kile wanachodai kwamba amekuwa kigeugeu kwenye maandishi na matamshi yake kuhusu muundo wa Muungano.
Katika mkutano wake wa kuelimisha wananchi kuhusu Katiba Mpya mjini Mwanza uliojaa polisi kila kona, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alisema wanamshangaa Profesa Shivji kwa mawazo yake yasiyoeleweka kuhusu muundo wa Muungano.
“Kwa kweli tunaamini watu ambao ni wasomi kama Profesa Shivji wanaweza kuwasaidia wananchi kupata katiba nzuri, lakini anachokifanya sasa ni siasa, jambo ambalo siyo jema,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Ukawa tunamtaka awaombe radhi wananchi, kwani amewadhalilisha kwa kuwa kigeugeu. Mara ya kwanza tunakumbuka alikuwa muumini wa Serikali tatu leo anageuka na kuanza kuhubiri serikali mbili, huu ni upuuzi kwa msomi kama yeye kufanya hivyo.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM wanaogopa Rasimu ya Katiba kwa sababu wamezoea uchakachuaji.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Abdulkarim Kambaya alisema Rais Kikwete amewachezea akili wananchi, kwani awali alikuwa anaonyesha yupo upande wao lakini kupitia hotuba yake bungeni amewakana na kuibeba CCM.
Lissu, Jussa nao wanena
Pia baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walimshambulia kwa maneno Profesa Isa Shivji kuwa ni ‘ndumilakuwili’.
Kwa nyakati tofauti, wajumbe Tundu Lissu na Ismail Jussa walisema kuwa Profesa Shivji “alibebwa na CCM na kulishwa maneno kwa masilahi ambayo hayajulikani.”
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa vitisho kwa wananchi.

BARUA YA WAZI KWA JK KUTOKA KWA CHAMA CHA WAZANZIBARI UINGEREZA

Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
Ikulu
P O Box 9120
Dar es Salaam


Yah: Hotuba Yako ya Kuwagawa Watanzania

Mheshimiwa Rais,
Tumelazimika kuandika barua hii kwako kama kiongozi wa juu wa taifa letu ili kukuonesha namna ambavyo tumesikitishwa na matamshi yako wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma. Tukiwa sehemu ya jamii kubwa ya Kizanzibari tuishio nje ya nchi yetu, hotuba yako imetutia khofu kubwa kulenga kwake zaidi kwenye kuvunja na sio kujenga mustakbali mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hotuba yako Mheshimiwa Rais, haikuzingatia maslahi ya Muungano wetu kwa misingi ya umoja unaonendana na matakwa ya wananchi walio wengi.
Tunakuandikia barua hii kukuzindua kile ambacho tumekiona kinakwenda tafauti na akhlaki zako. Ukweli ni kwamba kwa muda wote wa kipindi chako cha utawala tumekuwa tukikutazama kama ni tarajio jipya lililojengeka kwa misingi ya haki, insaaf na kioo cha uadilifu kwa pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.

Tunazungumza nawe moja kwa moja sio tu kama kiongozi wa taifa, bali pia kama mtu tuliyempa matumaini hayo. Wewe ni mtu wa mwisho kwetu kuamini kuwa anaweza kujenga khofu badala ya matumaini, batili badala ya halali, kitisho badala ya nasaha na mgawanyiko badala ya utangamano.

Mheshimiwa Rais,
Ulichokifanya siku ya tarehe 21 Machi 2013 ni kuzua taharuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano hasa kwa ndugu zetu wa Kizanzibari waishio upande wa pili wa Muungano huo. Ulichofanya ni kulihusisha jeshi letu linalothaminiwa dunia nzima kwa misingi ya heshima kwa kusaidia pakubwa kuifanya Jamhuri yetu kuwa ndio kisiwa cha amani kwa takribani miaka yote 50 ya Muungano wetu. Hakujawahi katika historia ya Tanzania kwa rais kuzuwa hisia za mapinduzi ya kijeshi kama hoja mbadala ya kuviza maoni ya walio wengi katika kiwango ambacho wewe umefanya.

Mheshimiwa Rais,
Ulikuwa umejizolea sifa kwa kuwa mmoja wa viongozi wachache wa Tanzania ambao hawakuonea haya mtafaruku wa kisiasa visiwani Zanzibar na ukaamua kuuvalia njuga ili kuhakikisha kuwa unatulizwa kwa amani. Kwa Wazanzibari wengi walio ndani na nje ya nchi, matarajio yao yalikuwa ni kwamba wewe ungelisimimia haki yao ndani ya Muungano kwa uadilifu mkubwa haidhuru maoni waliyonayo kuhusu muundo wa Muungano yanatafautiana na yako.

Tulikutegemea kuwa msimamizi wa haki uliyejizatiti kuhakikisha chembechembe za ubaguzi zinakufa katika kipindi chako cha utawala. Tulikutegemea usimame imara kusimamia hilo maana ndiyo misingi ya kiuongozi. Hatukutegemea hata kidogo uyumbe na uyumbishwe na kundi la wahafidhina ndani na nje ya Chama chako cha Mapinduzi (CCM), kwani maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi kuliko maslahi finyu ya makundi hayo ya kihafidhina. Lakini leo hii umekwenda kinyume hata na imani yako kwa kuwabeza Wazanzibari waishio Tanganyika bila ya kuthamini mchango wao mkubwa katika ukuwaji wa uchumi katika Muungano huu.

Tukukumbushe Mheshimiwa Rais, ikiwa umesahau, kuwa ni Zanzibar ndiyo iliyoungana na Tanganyika. Si Wapemba wala Waunguja. Sawa na sisi kusema kwamba hatukuungana na Wadengereko au Wanyamwezi waishio visiwani Zanzibar, bali ni Tanganyika kwa jumla kama nchi iliyo na makabila zaidi ya 100 ambayo tokea awali tumekuwa pamoja kwa misingi ya udugu kabla hata ya Muungano wa nchi zetu.

Pili tukukumbushe Mheshimiwa Rais kwamba suala la kuuvunja Muungano halijawahi kuwa sehemu ya mjadala mkuu kwenye Rasimu ya Katiba. Ni wewe na wenzako ndio ambao munalizusha kila mara kwa mintarafu hiyo hiyo ya kutisha. Lakini hata kama hayo yatakuwa ndio matokeo ya munayoyataka, basi tukukumbushe kuwa Waunguja na Wapemba waishio Tanganyika wataathirika sawa sawa na mtetemeko wa Muungano kama ilivyo kwa Watanganyika waishio visiwani. Si walima vitunguu tu ambao husaidia katika ulipaji wa kodi inayotumika kuijenga Tanganyika watakaoathirika na uvunjwaji wa Muungano, bali kila mmoja wetu.

Inashutsha sana kwa rais wa nchi mwenye heshima duniani kukiuka misingi ya usawa kwa kuwalenga jamii ya watu anaowaongoza kwa vitisho badala ya kuwahakikishia ulinzi hasa kwa vile ndie jemedari mkuu wa jeshi aliyeapa kuwalinda wananchi wote wa Muungano huu kwa nguvu zote alizopewa kikatiba.

Hatukuzuii kutetea na kulinda mfumo wa serikali mbili hasa ukiwa mwenyekiti wa chama chako kilichojizatiti katika mfumo huu wa sasa. Lakini ukiwa kama ni rais wa nchi inakupasa kuzitafautisha sehemu hizi mbili za kimamlaka ili kuwe na ufanisi wa demokrasia iliyokuchaguwa na kukupa hadhi ya rais wa Muungano huu.

Hivi kweli hakukuwa na hoja nzito za kuulinda mfumo wa sasa bila ya kuwaingiza wananchi katika mzozo mkubwa utaoleta nyufa katika taasisi tunayotarajia kuilinda na kuiimarisha? Umeamsha hisia kwamba ni Wapemba pekee – kama ulivyotuita – tunaofaidika na Muungano huu na kuendeleza kampeni ya chuki juu yetu, badala ya kuwazindua wananchi michango ya pande zote mbili katika ukuwaji wa uchumi na pia misingi ya amani tunayojivunia. Umekiuka maadili ya uongozi uliotukuka ulioapa kuitekeleza ukiwa ni mkuu wa Muungano huu na kudharau michango yetu Wazanzibari katika sekta zote za maendeleo ya Tanganyika.

Tukukumbushe tena Mheshimiwa Rais kwamba huna uhalali wa kuunganisha mfumo wa Serikali Tatu na uwezekano wa kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi. Umekuwa mmoja wa wapatanishi wa mzozo wa Madagascar, kwa mfano, na unajuwa kwamba mapinduzi ni zao la wapenda madaraka, wasiopenda kuwasikiliza wananchi walio wengi pamoja na uendeshwaji wa nchi kwa misingi isiyoendana na haki, uadilifu na ihsani.

Mfumo wa muungano unahitaji ithibati nzito kutoka kwa wananchi wa pande zote mbili. Haiwi sawa kuendeleza hamasa za kisiasa kwa kuzidharau hisia na matakwa ya walio wengi kwa kisingizio cha kuendeleza siasa za kuwaridhisha Wazanzibari pekee. Hiyo ni sawa na rushwa ya upande mmoja, na ulaghai wa hali ya juu kwa upande mwengine, kwa vile kero za Muungano hazipo kwa Wazanzibari pekee. Tunahitaji mfumo utaokuwa na nguvu ya matakwa ya pande zote mbili, utakaoweza kudumu na kuwa tunu kwa Afrika nzima.

Miaka 50 ya Muungano huu wetu mbali ya kwamba hakuna aliyejaribu kujiunga nasi kwa kutokuwa na manufaa, bali hata wengine walioungana hawakuwahi kuutazama huu wetu kama kigezo cha kuungana. Kwa kuendeleza mfumo wa sasa katika jitihada za kutiatia viraka, zipo ishara nzito kwamba sio tu kwamba Muungano hautadumu, bali pia utazua machafuko makubwa na kuzitia nchi zetu katika giza la historia chafu na dowa litaanza kwako kwa kuogopa kivuli chako mwenyewe. Ni vigumu kwa wakuu wa nchi kupima hali halisi ya nchi kwa kusikiliza wapambe waliojipenyeza kwa fitna na kukisema kile ambacho wakuu hupenda kukisikia. Kwa sasa angalizo kwako ni kuangalia mazingira yalivyo hasa katika Muungano na muamko wa wananchi katika mabadiliko waliyoyategemea zaidi kutoka kwako.

Mheshimiwa Rais,
Tunakuusia tena kama tunavyoziusia nafsi zetu, wasikilize wananchi walio wengi na matakwa yao katika ujenzi wa Muungano mpya utakaokuwa madhubuti na utakaoacha jina lako kuwa kwenye kumbukumbu njema kwa vizazi vijavyo. Haki, usawa na heshima baina ya pande hizi mbili ndio ziwe dira kwako katika kuleta mustakbali wa mabadiliko yatayotuweka katika Muungano utakaothaminiwa na kutunzwa na kila mdau. Matarajio yetu katika kipindi chako ni mageuzi ya kweli yanayoendana na wakati, yatakayoangalia matakwa ya wananchi na kuhakikisha hekima zako na busara zitaweza kuzaa matunda makubwa yatayoweza kuwa neema kwa vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Rais,
Khofu ni adui mkubwa wa mabadiliko ya kweli na yaliyo thabiti. Ulichaguliwa kwa matarajio makubwa kwa vile ulionyesha wazi kuwa miongoni mwa wachache walio na dira ya mapatano, ukuwaji wa amani na mapambazuko ya demokrasia nchini. Tanzania iliweza kubadili mfumo wa vyama vingi na kubeza waliokuwa na khofu ya mabadiliko. Zanzibar iliweza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo kwa upande mkubwa imerejesha imani kwa wananchi na hata wawekezaji na kuwa ni chombezo kwa wengine majirani kufuatia. Na kwa hili la mabadiliko ya mfumo wa Muungano tuna hakika ndio nafasi pekee ya Muungano mpya utakaobeba haki, usawa na heshima kwa kila mwananchi wa nchi zetu hizi.

Mheshimiwa Rais,
Tumekuandikia haya yote kwa kuwa tunaamini kuwa ukitaka unaweza kurekebisha pale ulipoteleza. Wewe ni mwanaadamu licha ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Una nafasi ya kufanya makosa, lakini una nafasi kubwa zaidi ya kusahihisha makosa yako, maana makosa yako yana uzito mkubwa na wa kipekee kwa hatima ya taifa. Tunakunasihi uipitie tena hotuba yako, weka sawa ulimopinda, safisha ulimochafua. Nchi inataka uongozi wako kukwamuka na kusonga mbele. Haitaki vitisho wala khofu zako. Ukihisi ni maamuzi magumu zaidi, rudi kwa wananchi na uwaulize tena kwa uwazi matakwa yao juu ya mfumo wa Muungano wa nchi zetu. Sote tunataka Tanzania kwanza pia hapana shaka, lakini kwa maana gani ya Tanzania kwanza?
Tanzania kwanza isiyobebwa na shengesha za mfumo butu wa sasa.
Tanzania kwanza isiyoviza ukweli wa kuwepo kwa Zanzibar na Tanganyika zinazojiendesha kwa ufanisi.
Tanzania kwanza iliyojidhatiti katika Muungano wa heshima, usawa na haki.
Tanzania kwanza iliyobebwa na matashi na matakwa ya wananchi.
Tanzania kwanza ya Serikali Tatu sio moja ya kuimeza Zanzibar na isiyotenda haki kwa Tanganyika.

Ahsante.

Hassan M Khamis
Mwenyekiti ZAWA UK

CHANZO: WANABIDII