Bakary Papa Gassama (Gambia)
Afrika itawakilishwa na waamuzi wa kati watatu kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil kwa mujibu wa orodha ya waamuzi 25 iliyotolewa na Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA. Kila mwamuzi ataongoza timu ya wasaidizi wawili na hivyo kufanya idadi ya waamuzi wasaidizi kutoka Afrika kuwa nane kati ya 50.
Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitafanyika nchini Brazil kuanzia Juni 12 mpaka Julai 13 ikiwa ni mara ya pili kwa fainali hizo kufanyika kwenye nchi hiyo kigogo katika soka duniani. Mara ya kwanza fainali hizo zilifanyika Brazil mwaka 1950.
Waamuzi hao ni Doue Noumandiez kutokaIvory Coast, Papa Gassama (Gambia) na Djamel Haimoudi (Algeria) ambao wataongoza timu ya waamuzi watatu kila mmoja kwenye fainali hizo, kwa mujibu wa utaratibu wa FIFA.
Doue atachezesha mechi za fainali hizo pamoja na waamuzi wasaidizi kutoka Burundi, Songuifolo Yeo na Jean Claude Birumushahu.
Gassama ataunda timu itakayowajumuisha waamuzi wasaidizi Evarist Menkouande kutoka Cameroon na Kabanda Felicien kutoka Rwanda, wakati Haimoudi ataongoza waamuzi wasaidizi Abdelhak Etchiali wa Algeria na Redouane Achik wa Morocco.
Mwamuzi wa akiba kutoka Afrika Kusini Daniel Bennett na Neant Alioum kutoka Cameroon wanakamilisha orodha hiyo ya waamuzi kutoka Afrika. Katika orodha hiyo pia wamo Djibril Camara (Senegal) na Marwa Range (Kenya).
Afrika imeendelea kushikilia idadi yake ya waamuzi watatu wa kati kwenye fainali hizo.
Kwa mujibu wa orodha ya FIFA waamuzi wengine ni Ravshan Irmatov kutoka Uzbekistan, Yuichi Nishimura (Japan), Nawaf Shukralla (Bahrain), Benjamin Williams (Australia), Joel Aguilar (El Salvador), Mark Geiger (Marekani), Marco Antonio Rodriguez (Mexico), Enrique Osses (Chile), Nestor Pitana (Argentina), Sandro Ricci (Brazil), Wilmar Roldan (Colombia), Carlos Vera (Ecuador), Peter O’Leary (New Zealand), Felix Brych (Ujerumani), Cuneyt Cakir (Uturuki), Jonas Eriksson (Sweden), Bjorn Kuipers (Uholanzi), Milorad Mazic (Serbia), Pedro Proenca (Ureno), Nicola Rizzoli (Italia), Carlos Velasco (Hispania) na Howard Webb (England).
Mbali na Afrika, bara la Ulaya litatoa waamuzi tisa, Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (CONMEBOL) litatoa waamuzi watano, huku waamuzi wanne wakitoka Asia (AFC), watatu kutoka Shirikisho la Soka la vyama vya Amerika ya Kaskazini na Visiwa vya Carribea (CONCACAF) na mmoja kutoka Oceania.
Akizungumzia uteuzi wa waamuzi hao 25, Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke alisema: “Waamuzi hao walichaguliwa kutokana na uwezo wao, uelewa wao wa mchezo wa soka, uwezo wa kuusoma mchezo na kuelewa timu zinazocheza zinatumia mbinu gani.”
Hata hivyo Valcke alisema kuna baadhi ya waamuzi na wasaidizi wao wanaweza kuachwa Juni 12 wakati watakapowapima kwa mara ya mwisho ili kujua kama wapo fiti kabla ya kuanza kwa mashindano.
Alisema: “Fifa ina utaratibu wa kuchagua waamuzi bora ambao wapo fiti kwa ajili ya kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia. Huwa tunachagua waamuzi ambao wapo katika ubora wa juu kabla ya mashindano.”
Noumandiez Doue (Ivory Coast)
Doue, ambaye alizaliwa Septemba 29, 1970, ni mwamuzi kutoka Ivory Coast ambaye amekuwa na beji ya Fifa tangu mwaka 2004. Doue amechezesha mashindano mbalimbali ya kimataifa. Amechezesha mechi za fainali za Mataifa ya Afrika 2010, 2012 na 2013. Pia Doue amechezesha mechi za fainali za Kombe la Dunis kwa vijana walio na umri chini ya miaka 20 mwaka 2011. Alichezesha mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2011 na mechi za mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia 2011. Doue pia amechezesha mechi za kuwania kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2010 na 2014. Mwaka 2011, Doue alishinda tuzo ya mwamuzi bora wa Afrika.
Akizungumzia uteuzi huo, Doue alisema: “Waamuzi wote wanataka kuchaguliwa kuchezesha mashindano makubwa, kwa hiyo hii ni heshima kwangu, kwa Gassama na Haimoudi kuchaguliwa kuchezesha fainali za Kombe la Dunia 2014.”
Bakary Papa Gassama (Gambia)
Gassama, ambaye alizaliwa Februari 10, 1977, ni mwamuzi kutoka Gambia ambaye amekuwa kwenye jopo la Fifa tangu mwaka 2007. Tayari ameishachezesha mechi za Michezo ya Olimpiki 2012. Pia alichezesha Fainali za Mataifa ya Afrika 2013 na mechi za kuwania kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2014.
Djamel Haimoudi (Algeria)
Haimoudi alizaliwa Desemba 10, 1970 mjini Oran, Algeria. Ni mwamuzi wa soka wa Algeria. Amekuwa mwamuzi wa Fifa tangu 2004. Alichezesha mashindano mengi kwani, ikiwa ni pamoja na fainali za Mataifaya Afrika 2008, Kombe la Dunia za U-20 mwaka 2011, Mataifa ya Afrika 2012, Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi za awali za Kombe la Dunia.
Desemba 2012, Haimoudi alichaguliwa kuwa mwamuzi bora wa Afrika. Miezi miwili baadaye alichezesha mechi ya fainali ya mataifa ya Afrika kati ya Nigeria na Burkina Faso. Pia alichezesha mechi ya mshindi wa tatu wa Kombe la Mabara kati ya Uruguay na Italia.
Akizungumzia uteuzi huo, alisema: “Kuwa katika fainali za Kombe la Dunia ni muhimu. Natarajia kupata uzoefu tofauti kwa hiyo nimefurahi sana.”
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou aliwapongeza waamuzi hao akisema: “Kwa niaba yangu na kamati ya utendaji ya CAF, nawapongeza waamuzi wa Afrika waliochaguliwa kuchezesha fainali za Kombe la Dunia 2014”
Afrika itawakilishwa na Algeria, Ghana,Cameroon, Nigeria na Ivory Coast.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment