Nje ya nyumba yupo mtoto mdogo akiwa amelala juu ya
kipande cha mkeka. Kwa kumtazama tu utajua anasumbuliwa na maradhi
kadhaa kutokana na afya yake kudorora.
Ukimtazama kwa haraka haraka anaonekana kuwa na
umri wa miaka minne labda, la hasha! Ni mtoto wa miaka saba ambaye kama
afya yake ingekuwa nzuri, kwa wakati huu alitakiwa kuwa darasani na
wenzake.
Anaingia mwanamke akiwa na mzigo kichwani, anautua
na kupokea ugeni uliofika kumtembelea. Ni mwanamke mkarimu
anayejitambulisha kuwa bibi wa mtoto aliyelala hapo nje.
Anasema siyo huyu tu, anao wajukuu wengine wawili
ambao ni wadogo zake yule aliyelala katika kipande cha mkeka, lakini kwa
wakati huo wamekwenda kucheza.
Mwanamke huyu anajitambulisha kwa jina la Amina
Rajab anasema, kwa miaka minne sasa amekuwa akiishi na wajukuu zake hao
baada ya wazazi wao wote wawili kufariki. Amina anasema, kuachiwa
wajukuu kwake sio tatizo isipokuwa wakiwa na maradhi kama hawa wajukuu
kwake.
Anasema wajukuu wawili kati ya hao watatu, kwa
muda mrefu wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali kama vile
kukohoa na magonjwa ya ngozi.
“Kuachiwa wajukuu wakiwa na afya nzuri siyo
tatizo, ila wakiwa wanaumwa kama hawa wa kwangu ndiyo ugumu, kwani mguu
mmoja, hospitalini, mwingine kutafuta sembe, sasa katika umri huu kwa
kweli kwangu ni mtihani mkubwa,” anasema Amina.
Mwanamke huyo anasema amekuwa akipata ugumu wa
kufuatilia afya za wajukuu zake, kwa kuwa mzigo wa kuwatafutia chakula
una mwelemea.
“Mwanangu hapa unaponiona ninatoka sokoni Buguruni
kununua ndizi na machungwa ya biashara, kila siku kiguu na njia
kuwatafutia chakula, suala la kwenda hospitalini mara kwa mara
linanishinda kwani nitawaua na njaa hawa watoto,” anasema Amina.
Anafafanua kuwa kwa mtaji wake wa Sh12,000, kila
siku analazimika kwenda sokoni kwa kuwa huisha tofauti na angekuwa na
mtaji mkubwa.
Kwa wengine Sh50,000 ni fedha ya matumizi ya
siku, pengine ni zaidi ya hiyo. Lakini kwa Bibi Amina ni tofauti, yeye
ndoto yake ni kupata mtaji mkubwa ambao ni kati ya Sh50,000 au
Sh100,000.
Ndoto ya mama huyo ni kupata mtaji mkubwa wa
angalau kuanzia Sh50,000 mpaka Sh100,000 na maisha yake yatabadilika,
kwani ataweza kununua bidhaa nyingi na hivyo kutolazimika kwenda sokoni
kila siku.
“Katika vitu vinavyoniumiza ni hii hali ya kuamkia sokoni kila
siku, sina mtu wa kumuachia wajukuu zangu kwa hiyo ninaamka alfajiri
kuwaandalia kifungua kinywa halafu ninakimbilia sokoni kufanya ununuzi,”
anasema Amina.
Maisha yake yako vipi
Amina anaishi Tabata Kisiwani katika chumba kimoja
anacholipia Sh 20,000 kwa mwezi. Anasema ingawa anatakiwa kulipa kodi
yake kila baada ya miezi sita lakini mwenye nyumba amemruhusu kulipia
kila baada ya miezi mitatu pale anapopata pesa.
Ni chumba kilichojazana vitu kutokana na kuwa
kidogo. Usiku unapoingia wajukuu zake watatu hulala juu ya vitanda naye
husogeza vyombo vilivyopo chini na kutandika mkeka hapo.
Anasema: “Ninashukuru wasamaria wema ambao mara
kwa mara huniwezesha, nikidunduliza nalipia kodi hiyo miezi mitatu
maisha yanaendelea.”
Huamka asubuhi kwaajili ya kuwaandalia kifungua
kinywa wajukuu zake kisha huelekea sokoni kununua matunda ambayo huyauza
kwaajili ya kupata faida inayomsaidia kuendesha maisha yake. Mchana
hufanya shughuli za nyumbani kama kuwaogesha, kuwafulia na kuwaandalia
chakula cha mchana na jioni.
Saa kumi na moja jioni hujongea barabarani ambako ndipo huuza ndizi na machungwa. Saa tatu usiku au saa nne hurudi nyumbani.
Matibabu ya wajukuu zake
Ingawa hazungumzii moja kwa moja maradhi
yanayowasumbua wajukuu zake, Bibi Amina anasema anataka kuanza
kufuatilia matibabu yao ili wapate nafuu na ikibidi waanze masomo.
“Wajukuu zangu wawili hali yao ni kama hivi, huyu
unayemuona hapa amedhoofu sana kwasababu aliwahi kugongwa na gari,
lakini nia yangu hasa ni kuangalia zaidi matibabu yao kwani wakiwa
wazima wa afya na mimi nitaweza kufanya kazi zangu kwa ufanisi,” anasema
Bibi Amina.
Anasema zaidi anataka kujua afya ya huyu aliyepo
nyumbani akisema: “Huyu anakohoa sana, ninataka nikampime Kifua Kikuu
ikibidi, kwani nimemaliza kila ina ya dawa na bado hakiponi.”
Amina anasema atafurahi iwapo atapata msaada wa
mtaji mkubwa kwani kawa hatua hiyo ataweza kufuatilia afya za wajukuu
zake ambazo zimekuwa zikitetereka kila kukicha.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment