Mwanasiasa mwenye historia ya kipekee nchini, James Mapalala amesema ufafanuzi wa Rasimu ya Katiba uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, umekiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye wakati mgumu.
Mapalala, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba, amesema ufafanuzi huo ni wa kisayansi kwa kiwango cha juu kiasi kwamba atakayetaka kubishana naye, atakabiliwa na kazi pevu ya kujenga hoja.
“Ripoti yake (ya mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba) imekuwa very scientific (ya kisayansi sana). Kila kitu alichoeleza amekitolea ushahidi ulio hai katika maisha ya kila siku ya Watanzania,” alieleza Mapalala.
Mapalala alisema pamoja na kuwa una manufaa kwa mustakabali wa taifa, ufafanuzi huo umeiweka pabaya CCM kutokana na kujibu hoja zote ambazo chama hicho kilipanga kuzitumia kuipinga hotuba hiyo.
“Labda watumie nguvu kubwa lakini kwa mtindo wa kutumia hoja, hakuna Mtanzania mwenye akili timamu atakayeshindwa kubaini hali halisi inayolikabili taifa, kwa sababu ukweli umewekwa peupe,” alieleza Mapalala.
JK akoleza mjadala
Kauli hiyo ya Mapalala imekuja wakati tayari Rais Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge na kueleza kwamba inavyoonekana Muundo wa serikali tatu hautekelezeki.
Mbali na kupinga muundo wa serikali tatu na kupendekeza serikali mbili, Rais Kikwete ameonyesha shaka kuhusu utekelezaji wa ukomo wa ubunge uliopendekezwa na Tume ya Katiba.
Mapalala alisema madai yanayotolewa na baadhi ya wanaotaka serikali tatu kwamba sehemu kubwa ya maoni yaliyo katika rasimu iliyowasilishwa ni maoni binafsi ya Jaji Warioba, yanakosa mashiko kwa sababu sasa kila “mwenye macho haambiwi tazama.”
Anasema hata madai kwamba mahitaji ya serikali tatu ni ya kisiasa; ikielezwa kuwa CUF inaamini itatawalaZanzibar kadhalika Chadema ikijiamini kuwa kitatawala Tanzania Bara, hayana msingi.
Alisema haoni mantiki ya CCM kumpinga Jaji Warioba kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeundwa na Serikali ya chama hicho tawala chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
“Hata marekebisho ya sheria hiyo, yaliyofanyika Septemba mwaka jana yalipitishwa huku vyama vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni vikiwa havipo ndani ya vikao; ikaidhinishwa kuwa tume ikimaliza kuwasilisha rasimu uhai wake uwe umekoma. Ikiwa kwenye mchakato huu kuna siasa, basi zinaletwa na CCM na si vinginevyo,” alieleza Mapalala.
No comments:
Post a Comment