Kuala Lumpur. Polisi nchini Malaysia wamevamia nyumba aliyokuwa akiishi rubani wa ndege iliyopotea na kuendesha msako mkali, ikiwamo kukusanya nyaraka muhimu ambazo zinazamiwa kuwa zitasaidia kufichua ukweli kuhusu tukio la kupotea kwa ndege hiyo.
Ripoti zilisema kuwa upekuzi huo, ambao pia
umefanyika katika nyumba aliyokuwa akiishi rubani msaidizi, umefanyika
baada ya kuibuka kwa taarifa zinazodai kuwa rubani huyo, Zaharie Ahmad
Shah alikuwa na mrengo wa siasa kali.
Shah alikuwa ni shabiki na mfuasi wa wazi wa
mwanasiasa wa upinzani, Anwar Ibrahim ambaye sasa yupo gerezani baada ya
kukutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya fedheha.
Inaaminika kuwa rubani huyo alikuwapo mahakamani
wakati mwanasiasa huyo alipopandishwa kizimbani mwezi Machi mwaka huu na
pengine hakufurahishwa na hukumu hiyo.
Kwa sasa polisi wanashikilia nyaraka kadhaa,
ikiwamo kompyuta ambayo inadhaniwa kuwa na taarifa muhimu
zilizohifadhiwa na rubani huyo.
Polisi hao wameenda mbali zaidi kwa kuanzisha
uchunguzi wa kimazingira ambao utasaidia kupata historia binafsi kuhusu
maisha ya rubani huyo aliyetajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa urushaji wa
ndege.
Wataalamu wa saikolojia na wale wanaohusika na
usalama wa anga wameitwa kuongeza nguvu ili kusaidia kuchambua taarifa
zinazoendelea kukusanywa kuhusu mwenendo wa rubani Shah ambaye nyumba
yake bado inaendelea kulindwa.
Kitendo cha polisi kuifanyia upekuzi nyumba ya
rubani huyo pamoja na kukusanya taarifa zake binafsi kimeelezwa kwamba
ni jitihada za Serikali kutaka kujiridhisha hasa kutokana na mazingira
yanayohusisha upotevu wa ndege hiyo.
Wachunguzi hao wanataka kujua kama kumekuwa na
tukio lolote la matatizo ya kiakili na kumewahi kujitokeza kwa
changamoto za kifamilia kwa marubani hao au kwa yeyote aliyekuwamo
kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur na kuelekea
Beijing.
Pamoja na kwamba marubani wa ndege hiyo ya
Malaysia walikuwa na rekodi nzuri, kuna wasiwasi pengine walikutwa na
tukio lililosababisha kujiingiza kwenye hali ambayo ingepoteza umakini
wa kuongoza ndege.
Uchunguzi pia unawalenga abiria waliokuwemo kwenye
ndege hiyo iliyokuwa na umri wa miaka 11 na kwamba hatua hiyo inaweza
kusaidia upatikanaji ukweli halisi juu ya tukio hilo.
Serikali yaomba msaada
Malaysia imeomba msaada zaidi kutoka nchi kadhaa kwa ajili ya
kusaidia kuitafuta ndege hiyo ya abiria iliyopotea kwa zaidi ya wiki
moja iliyopita huku kukiwa na taarifa za kusitishwa uchunguzi kwenye
Bahari ya Hindi mpaka pale tathimini ya kina itakapofanyika.
Wizara ya uchukuzi ilisema kwamba imeomba msaada
kutoka nchi za Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzistan, Turkmenistan na
Pakistan. Nchi nyingine zilizoombwa kushiriki ni pamoja na Indonesia,
Thailand, Marekani, Australia na Ufaransa.
Msaada huo ni pamoja na takwimu za Satelaiti
zilizonasa safari ya ndege hiyo iliyokuwa na watu 239 na ambayo ilipotea
tarehe 8 mwezi huu, baada ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kuala Lumpur.
Awali Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak alisema
wachunguzi waligundua kwamba ndege hiyo, iliyokuwa ikielekea Bejing
nchini China, ilibadili njia na kuelekea Magharibi kabla ya mitambo yake
ya mawasiliano kuzimwa.
Akizungumza na waandishi habari katika mji mkuu wa
Kuala Lumpur, Najib Razak alisema: “Wachunguzi wanaamini kwa kiwango
kikubwa kwamba kulikuwa na kitendo cha makusudi cha kuzima mfumo wa
mawasiliano katika ndege aina ya Boeing 777-200ER ya shirika la ndege la
Malaysia Airlines.
Kwa msingi huo, ndege hiyo haingeweza kuwasiliana na kituo cha kudibiti trafiki angani.”
Waziri Mkuu wa Malaysia aliongeza kuwa baada ya
kuzimwa mfumo huo wa mawasiliano, ndege hiyo ilibadilisha mkondo wake na
kuelekea upande wa Magharibi baharini jambo ambalo linaashiria kulikuwa
na hatua za makusudi.
Alisema pamoja na kuwepo taarifa kuwa ndege hiyo
ilitekwa nyara, bado hakuna lolote lililo wazi kwani uchunguzi ungali
unaendelea ili kubaini ni kwa nini ndege hiyo ilichepuka kutoka katika
mkondo wa safari yake.
Pamoja na ukweli kuwa nchi kadhaa zinahusika
katika juhudi za kuitafuta kwa kutumia teknolojia ya kisasa, bado
haijatangazwa kama ndege hiyo iliyotegenezwa Marekani imepata athari
gani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment