Yanga Bwanga (kushoto). Picha kwa hisani ya zenjdar.co.uk
Na Daniel Mbega
NAMKUMBUKA mtangazaji nguli wa kipindi cha michezo cha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTC
wakati huo - sasa TBC Taifa), marehemu Abdul Masoud, katika siku ambayo
Yanga ilimsajili kiungo mshambuliaji machachari Yanga Fadhil Bwanga
kutoka kwa 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union mwaka 1976 kama sikosei.
Nilikuwa mdogo sana wakati huo, lakini ndiyo kwanza nilikuwa ninapenda
michezo hasa tukiwa tunajikusanya nyumbani kwa Balozi wa Nyumba Kumi
aliyekuwa na redio ya 'Mkulima' kila siku saa mbili kasorobo.
Siikumbuki
vizuri siku hiyo, lakini ninachokikumbuka ni utangulizi wa habari kuu
ya siku hiyo ambapo Abdul Masoud alisema: "Haya tena, mambo kangaja
huenda yakaja... Leo katika Uwanja wa Mkwakwani Coastal Union yaifunga
Yanga... Lakini Yanga Fadhil Bwanga ajiunga na Yanga!"
Naam,
yalikuwa ni maneno mazito hasa ikizingatiwa ushabiki wa mpira wakati
huo ulivyokuwa juu tofauti na sasa ambapo utandawazi umewafanya wengi
wanashabikie timu za Ulaya wanazoziona kwenye luninga.
Siku
hiyo Yanga ilikuwa imefungwa na Coastal Union katika mchezo mkali wa
kirafiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Mwaka huo Coastal Union haikufika
fainali ya Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu) baada ya kutolewa kwenye hatua
ya Kanda.
Lakini
kikosi chake kilikuwa imara mno. Ikumbukwe pia kwamba, Abdul Masoud
wakati huo ndiye alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga baada ya kuchaguliwa
katika uchaguzi uliosimamiwa na serikali kufuatia mgogoro mkubwa
uliokuwa umeikumba klabu hiyo na kuwafukuza wachezaji 20, ambao baadaye
ndio waliounda Pan Africans, akiwemo Rais wa sasa wa TFF, Leodgar Tenga,Gibson Sembuli, Sunday Manara, Boi Idd 'Wickens', Ally
Yusuf, na wengineo.
Pamoja na kuwa na wachezaji chipukizi, lakini Yanga ilishindwa kufua dafu mbele ya Wagosi wa Kaya.
Baada
ya mchezo huo Yanga wakamtorosha Yanga Fadhil Bwanga na kwenda
'kumhifadhi' kwa ndugu zake Pangani ili Coastal wasiushtukie mchezo huo.
Coastal walipopata fununu waliweka mtego barabarani na kukagua kila
gari iliyopita. Ilivumishwa kwamba Yanga Bwanga alisafirishwa na lori la
mkaa, lakini (watanisahihisha wakongwe) inaelezwa kwamba baada ya
kupumzika siku kadhaa Pangani, alipitia Bagamoyo na kuingia Dar. Hiyo
ndiyo hadithi yake, naamini wakongwe wanaweza kunisahihisha katika hili.
Hata
hivyo, hapa nazungumzia tukio lililofanywa na Yanga Bwanga katika mechi
baina ya Yanga na Simba mwaka 1977 ambapo alivunja pambano hilo.
Siku hiyo ya Jumapili Novemba 27, 1977 kwa
mara nyingine Simba iliifunga tena Yanga kwa mabao 2-1 katika pambano ambalo
lilivunjika dakika 12 kabla ya wakati wake kutokana na mchezaji Yanga Bwanga wa
Yanga kukataa kutoka nje baada ya kuamuliwa na mwamuzi kufanya hivyo.
Bwanga, kwa makusudi kabisa, alimpiga daluga
Nicodemus Njohole wa Simba kifuani ikiwa ni kulipiza kisasi kwa mchezaji huyo
ambaye alikuwa amemtegea wakati wakiwania mpira. Bwanga alikuwa ameonywa mara
ya kwanza kwa kadi ya njano katika dakika ya 16 alipomfanyia rafu Nicodemus
tena na hivyo baada ya rafu mbaya kwa mara ya pili ikalazimika atolewe nje.
Lakini mchezaji huyo hakushtuka kwa amri hiyo
badala yake akaendelea kurukaruka uwanjani akifanya mazoezi mepesi. Mwamuzi
Stephen Lutayangirwa baada ya kusubiri kwa dakika 10 alipuliza kipenga cha
kumaliza mchezo.
Mchezo wenyewe ulikuwa wa kwanza wa kuwania
Kombe la Jitegemee, ambapo uliharibiwa kabisa kutokana na uchezaji mbaya wa
wachezaji wa timu zote ambao walikuwa wakitembezeana madaruga na kuonyeshana
ubabe wa dhahiri.
Kulikuwa na vipindi vichache sana vyenye
msisimko na mara nyingi kulikuwa na rafu na mchezo wa hasira. Mwamuzi naye
alistahili lawama kwa kufanya mchezo kuharibika zaidi. Hakuwa mkali inavyopasa
kila wachezaji walipokuwa wakifanya makosa uwanjani.
Ukali pekee aliouonyesha wenye busara ni
alipomtoa nje ya uwanja Daudi Salum 'Bruce Lee' wa Simba na Ayubu Shaaban wa
Yanga walipokingiana ngumi. Kabla ya hapo alikuwa amewaonyesha kadi za njano
Omar Mahadh na Daudi Salum wa Simba, na Yanga Bwanga wa Yanga.
Mameneja wa timu hizo Mohammed Viran wa yanga
na Abdulrahman Khamis Muchacho wa Simba ndio walioonyesha urafiki baada ya
kuvunjika kwa mchezo huo kwani walitoka nje wakiwa wameshikana mikono huku
wapenzi wa timu hizo mbili wakilaumiana kwa mchezo mbovu wa timu zao.
Simba iliwazidi kimchezo wapinzani wao katika
dakika za mwanzo hadi walipojipatia bao lao la kwanza katika dakika ya 18.
Mpira uliotoka kwa Abdallah Kibadeni aliyeupeleka mbele ulimkuta Jumanne Hassan
Masimenti ambaye naye alitoa pasi ya kichwa kwa George Kulagwa ambaye aliachia
mkwaju mkali ambao kipa wa Yanga Isega Isindani alishindwa kuukumbatia. Rahim
Lumelezi aliyekuwa karibu akauwahi na kuutumbukiza wavuni.
Kuanzia hapo hadi mapumziko mchezo ulipooza
sana ingawa Yanga ilikuwa ikicheza kwa ufundi zaidi ambao ungewaletea goli la
kusawazisha kunako dakika ya 22 kwa kiki ya nguvu iliyopigwa na Karabi Mrisho
lakini ikapaa juu ya goli.
Yanga
iliwaingiza Ramadhan Mwinda na Danny Mwalusamba badala ya Karabi Mrisho na
Burhani Hemed kipindi cha pili kilipoanza, lakini mabadiliko hayo hayakuleta
tofauti sana.
Katika
mojawapo ya hatari langoni mwa Simba, Filbert Rubibira aliunawa mpira na
mwamuzi akaamuru penalty ipigwe. Wachezaji wa Yanga walitegeana kupiga mpaka
Charles Mwanga alipojitolea lakini alipopiga mpira ukaota mbawa kwa kupaa juu
ya goli.
Simba ilijiongezea bao la pili dakika ya 54.
Bao hilo lilianzia na mpira wa kona iliyochongwa na Abdallah Kibadeni na kusababisha
kizaazaa langoni, Nico Njohole akatokea na kufunga kirahisi.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na Ezekiel
Grayson dakika ya 64. Mohammed Kajole ndiye aliyesababisha bao hilo baada ya
kuuachia mpira ambao angeweza kuokoa akidhani kipa wake Omar Mahadh atauwahi.
Ezekiel akatokea na bila taabu akafumua mkwaju uliotinga wavuni.
Yanga ikaanza kucheza vizuri kuanzia hapo
hadi mchezo ulipovunjika, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.
Yanga: Isega Isindani, Charles Mwanga,
Fadhil/Boniface Makomole, Selemani Jongo, Hashim Kambi, Sam Kampambe, Burhani
Hemed/Danny Mwalusamba, Ezekiel Grayson, Karabi Mrisho/Ramadhan Mwinda, Yanga
Bwanga, Ayoub Shaaban.
Simba: Omar Mahadh, Daudi Salum, Mohammed
Kajole, Aloo Mwitu, Filbert Rubibira, Athumani Juma, Rahim Lumelezi, Nico
Njohole, Jumanne Hassan, Kibadeni, George Kulagwa.
NB: Makala haya
ni sehemu ya kitabu chake cha VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA ambacho kimeandikwa
na mwandishi mwandamizi wa michezo nchini Tanzania, Daniel Mbega ambacho kiko
karibuni kutoka.
No comments:
Post a Comment