Mangara Tabu Mangara (kulia) na kocha Tambwe Leya (kushoto) mwaka 1974.
Na DANIEL MBEGA
WENGI wamekuwa na maelezo tofauti kuhusu
chanzo cha mgogoro wa Yanga kilichozaa timu ya Pan African mwaka 1977. Wapo
wanaosema kupoteza ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1976 ndiko
kulikosababisha kutokea mgawanyiko. Lakini maelezo hayo si sahihi, kwani wakati
ubingwa huo unatoweka Januari 1976 mjini Mombasa, Kenya, tayari kulikuwa na
mgawanyiko wa Yanga Raizoni na Yanga Kandambili, na zaidi tayari uchaguzi mkuu
ulikuwa umefanyika (Desemba 1975) na Mangara Tabu Mangara kudondoshwa.
Kwanza kabla ya kuingia kwa undani kuhusu
mgogoro huo ni vyema mtu akaielewa kwa undani historia ya Yanga kuanzia mwaka
1968. Wengi wanasema kwamba Mangara Tabu ndiye aliyefanikisha ujenzi wa jengo
la Yanga la Jangwani. Si kweli! Suala la ujenzi wa jengo lile lilianza tangu
mwaka 1968, kweli, lakini kwanza lilitanguliwa na uandaaji wa Katiba ya kwanza
ya Yanga.
Katiba hiyo iliandaliwa na kisha
kuchapishwa mwaka huo, lakini ndani yake kulikuwa na vipengele ambavyo baadaye
vikaja kuonekana vinawabana baadhi ya watu. Mojawapo ya vipengele hivyo ni kile
kilichoelezea kuhusu udhamini wa jengo la klabu lililokuwa linatarajiwa
kujengwa, ambacho kilisema kwamba, mdhamini ni lazima awe na nyumba iliyojengwa
kwa usimamizi au utaratibu wa serikali na pia awe na pato la shilingi 1,500 kwa
mwezi.
Rais wa Yanga wa wakati huo, Kondo Kipwata
ndiye aliyestahili sifa zote za maendeleo ya klabu hiyo ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa tatu, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kaunda.
Vyote hivi vilijengwa kutokana na michango mbalimbali ya wananchi, serikali (ya
Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar) na taasisi mbalimbali za umma na
binafsi.
Wazo la ujenzi lilipotolewa Mzee Kondo
Kipwata alikuwa na nyumba zake, lakini kutokana na kutokuwa na hati za
kiserikali na kutokuwa na kazi, kipato chake hakikuwa kile kilichoainishwa
kwenye Katiba, hivyo kumuwia vigumu kuwa mmoja wa wadhamini wa jengo hilo.
Wakati huo Makamu wa Rais, Mangara Tabu, alikuwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali
na kipato chake kwa mwezi kilikuwa shilingi 1,500. Yeye ndiye aliyeandaa Katiba
hiyo na kuichapa, hivyo ilikuwa rahisi kwake kuweka kipengele hicho.
Lakini tayari Mangara alikuwa akipingwa na
wanachama wengine kama Mathew Kashindye na David Mwambungu. Hali hiyo ikamfanya
Mangara kutafuta njia ya kumwezesha kuwa mmoja wa wadhamini wa jengo hilo, na
kwa vile alikuwa na nyumba Mtaa wa Swahili na pia alikuwa na kazi ya mashahara,
wana-Yanga wakaamua kumweka kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi.
Hata Rais Julius Kambarage Nyerere
alipotembelea ujenzi huo mwaka 1970 alikuta Mangara ndiye msimamizi mkuu.
Wakati huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia klabu ya Wananchi (zamani
ikijulikana kama African Sports), chini ya Sheikh Abeid Amani Karume, ilikuwa imetoa
shilingi milioni 2.0 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo. Jiwe la Msingi
liliwekwa na Sheikh Karume mwaka 1971.
Pamoja na hayo, bado kuliendelea kuwepo na
migogoro. Mwanzoni mwa mwaka 1973 Mzee Kondo Kipwata alifariki dunia, na kwa
mujibu wa Katiba, Makamu wake, Mangara Tabu, ndiye aliyekaimu nafasi yake.
Lakini katika mechi ya kwanza chini yake dhidi ya Simba mwaka huo 1973, Yanga
ilichapwa bao 1-0 na kisha kuvuliwa ubingwa wa Taifa ilioushikilia kwa miaka
mitano mfululizo (1968-1972). Kipigo kile kikachochea kabisa mgogoro uliokuwa
unazidi kukomaa, hivyo wanachama wakaamua kumshinikiza Mangara kuhakikisha
kwamba timu inaandaliwa vya kutosha kwa ajili ya michuano ya Ubingwa wa Taifa
wa mwaka 1974.
Ndipo mwaka 1974 Yanga ikaendea kuzuru
Brazil kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo iliyofanyika Mwanza. Baada ya
kurejea Yanga ilikuwa inatisha na ilipoingia fainali ikakumbana na Simba Jumanne
ya Agosti 10, ambapo ilishinda kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Mapema mwaka 1975 ikaivua tena Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini
Zanzibar kwa kuifunga mabao 2-0.
Pamoja na mafanikio hayo, bado wanachama
waliendelea na mgogoro huo na walionyesha dhahiri kutokuwa na imani na Mangara
hasa kutokana na kushindwa kujengwa kwa viti (jukwaa) kwenye Uwanja wa Kaunda
ingawa wanachama walikuwa wamechangishwa fedha kwa ajili hiyo. Mpaka leo
haijulikani fedha zile ziliingia wapi.
Mangara alikuwa ametengeneza sefu ya fedha
kwenye klabu ya Yanga pale Jangwani na nyingine, kwa mujibu wa waliokuwepo,
aliiweka nyumbani kwake. Wachezaji au wanachama walipokuwa na shida ya fedha
walikwenda kupanga foleni pale nyumbani kwake. Kitendo hicho kilikuwa
kinapingwa sana na kocha Tambwe Leya, ambaye alikuwa akiidhinisha fedha kwa
wachezaji wenye matatizo. Wale wanachama waliokuwa wakimuunga mkono Mangara
walikuwa wakijiita ‘Raizoni’, yaani watoto wa mjini wanaojua kuvaa, na wale
wengine waliokuwa wakimpinga walionekana makabwera tu. Ni katika mgawanyiko
huo, ambapo siku moja baada ya timu kumaliza mazoezi pale Kaunda, wanachama
fulani wakamzonga mchezaji Juma Shaaban ‘Uncle J’ na kuanza kumshambulia kwa
maneno, lakini kipa huyo akasema, ‘Yaani hata nyie mnaovaa kandambili mnaweza
kusema mbele ya wenye fedha?!’ Hapo ndipo lilipoanzia neno ‘Yanga Kandambili!’
Wakati huo Yanga ilikuwa inamiliki magari
matano. Kulikuwa na Isuzu iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 65, Isuzu
nyingine ya kubeba watu 30, Ford ya kubeba watu 35, Pundamilia Isuzu ya kubeba
watu 18, ambayo mara nyingi ilikuwa ikibeba wachezaji wanapoingia uwanjani, na
gari aina ya Honda iliyokuwa ikitumiwa na kocha Tabwe Leya.
Wakati Mangara alikuwa kaimu Rais wa klabu,
mdogo wake Mtaruke Mangara alikuwa
Makamu wa Rais, Katibu Mkuu alikuwa David Mwambungu, Katibu Msaidizi alikuwa
Mohammed Misanga, Mweka Hazina alikuwa Ngakonda, Mweka Hazina Msaidizi alikuwa
Punzi, Abdul Masoud (mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam –RTD sasa
marehemu) alikuwa Katibu Mwenezi na Mathew Kashindye alikuwa Katibu Mipango.
Lakini baada ya kutwaa ubingwa kule
Nyamagana mwaka 1974 mgogoro ukazidi na wanachama wakashinikiza uchaguzi
ufanyike. Serikali ikaona kwamba hali hiyo ingeweza kuvuruga amani nchini hasa
katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa mwaka 1975, hivyo ikaamua kuwafungia
Mwambungu na Kashindye kutojishughulisha na michezo maisha.
Tamko hilo la serikali halikuwakatisha
tamaa wanachama, ambapo mwaka 1975 wakaamua kufanya mapinduzi baridi kwa
kuchagua uongizi wa muda uliokuwa chini ya uenyekiti wa Omar Mussa Chitenje
pamoja na Mohammed Misanga (Katibu Mkuu), Punzi (Mweka Hazina), Edson
Mwandemane (Katibu Mipango), na Abdul Masoud (Katibu Mwenezi). Hatua hiyo ya
kufanya mapinduzi baridi ilifuatia kutolewa kwa Yanga na Enugu Rangers ya
Nigeria katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mnamo Juni 1975. Katika mchezo
wa kwanza huko Lagos timu hizo zilitoka suluhu, lakini ziliporudiana mjini Dar
es Salaam zikafungana 1-1, hivyo Wanigeria wakapata ushindi wa sheria ya bao la
ugenini.
Wanachama wa Yanga walimtuma Hamad Abdallah
Kiluvia kwenda kuipokea timu ya Enugu. Alipofika Uwanja wa Ndege alianza
kusalimiana na golikipa wa Enugu, Emmanuel Okala, kipa mrefu sana ambaye pia
alikuwa akiidakia timu ya taifa, Green Eagles, wakati huo (sasa inaitwa Super
Eagles).
Lakini upande wa Mangara inasemekana
haukuwa radhi kuona Yanga inashinda, hivyo baadhi ya waliokuwa wakimuunga mkono
wakawashawishi wachezaji wa Yanga wacheze chini ya kiwango. Wachezaji hao
wakasikika wakisema kwamba, siku hiyo ya mchezo hakuna mtu kufunga goli. Maneno
hayo yalitamkwa wakati wako ndani ya gari wakienda uwanjani siku hiyo ya
mchezo, lakini viongozi hawakujua. Hata kocha Tambwe Leya hakuwa na habari.
Baada ya kuingia uwanjani, Enugu ndio
walianza kupata bao, lakini baadaye Kitwana Manara akasawazisha, hali
iliyosababisha kutokee ugomvi mkubwa hapo uwanjani baina ya kambi ya Mangara,
ambao walikuwa wakilaumu kwa nini Kitwana alifunga bao hilo. Hata hivyo,
matokeo yakabaki 1-1 na Yanga ikawa imetolewa.
Nilipata kuzungumza na mmoja wa viongozi wa
Yanga wa wakati huo, Kennedy Kanyanka, ambaye alikuwa na haya ya kusema: “Baada
ya wanachama kugundua njama hizo, ndipo walipofanya uchaguzi Julai 1975 na
Mwenyekiti akawa Omar Mussa Chitenje. Hata hivyo, serikali ikaingilia kati na
kusema kwamba uchaguzi huo ulikuwa batili kwa sababu walichofanya wanachama ni
kama kuteua Kamati ya Muda tu kinyume na Katiba.
“Lakini mgogoro huo ulipoendelea ikabidi
serikali iridhie kufanyika kwa uchaguzi mwingine wa Yanga mnamo Desemba 28,
1975, Jumapili, chini ya usimamizi wa Umoja wa Vijana wa TANU (TLY). Ndipo kwa
mara nyingine akachaguliwa Omar Mussa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti
alikuwa Juma Shamte, Katibu Mkuu alikuwa Mohammed Misanga, Katibu Msaidizi
Hassan Lupindo, Katibu Mwenezi Abdul Masoud, Katibu Mipango Kennedy Kanyanka,
Mweka Hazina Kanduru Msusa, Mweka Hazina Msaidizi Edson Mwandemane,” anakumbuka.
Unaweza kuona kwamba mpaka wakati huo
tayari kulikuwa na makundi mawili; Kundi la Mangara na kundi la wanachama
wengine, wakiwemo na wale waliochaguliwa kushika uongozi. Lakini kundi la
Mangara lilikuwa linaungwa mkono na serikali, ndiyo maana hata baada ya Yanga
kuvuliwa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka 1976,
baada ya uongozi kupeleka basi la kukodi (UDA-Ikarus Kumbakumba) kule Uwanja wa
Ndege ili kuwapokea wachezaji, wachezaji hao wote hawakuingia kwenye basi hilo
na badala yake wakaingia kwenye magari ya mawaziri, mkuu wa mkoa, RPC na magari
mengineyo ya serikali. Kitendo hicho kilizidisha hasira za wanachama, ambapo
wakaazimia kuwafukuza wote na kuanza kuunda kikosi kipya.
Serikali ikatoa amri ya kutoruhusu
uandikishwaji wa klabu ya michezo kutokana na migogoro. Wachezaji wale
walioondoka awali walitaka kujiunga na klabu moja pale Manzese, lakini kutokana
na amri hiyo ya serikali, ikabidi watimkie Morogoro walikojiunga na timu ya
Nyota Afrika iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Taifa.
Katika mahojiano mwaka 2002, Kanyanka
alipata kuniambia: “Viongozi wa serikali waliokuwa nyuma ya Mangara, Mshindo
Mkeyenge na Shiraz Shariff, walikuwa Waziri wa Michezo, Utamaduni wa Taifa na
Vijana Mirisho Sam Hagai Sarakikya, Mkuu wa Mkoa wa Pwani (wakati huo) Clement
Rwegasira, Katibu Mkuu wa Rais Sammy Mdee, Mkurugenzi wa Radio Tanzania Dar es
Salaam Paul Andrea Sozigwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani (Dar) Ismail
Lazaro, ambao waliona Mangara alikuwa ameonewa tu na wanachama hao,” anasema.
Baada ya kutimuliwa kwa wachezaji hao,
Yanga haikuwa na kikosi kibaya sana, ingawa mwaka huo 1976 walifungwa na Simba
2-1. Hali hiyo ikawashangaza hata wapinzani wao, na hata serikali nayo
ikachanganyikiwa kuona timu iliyokuwa na migogoro mingi kama Yanga iliweza
kuunda kikosi imara katika muda mfupi. Hii ilitokana na kuwa na kocha mzuri,
Tambwe Leya, ambaye aliamini vijana ndio walikuwa nguzo imara.
Ndipo likatolewa agizo la kuwataka Tambwe
Leya na kocha wa Simba wa wakati huo, Nabby Camara kutoka Guinea, kuondoka
nchini haraka sana kwa madai kwamba walikuwa makachero wa Shirika la Kijasusi
la Marekani (Central Intelligence Agency – CIA). Mwaka 1977 ndipo ikazaliwa Pan
African baada ya wachezaji wale kurejea kutoka Morogoro na pia ndio mwaka ambao
Yanga ilichabangwa na Simba mabao 6-0.
Awamu ya pili baada ya kuondoka Mangara na
kipindi cha Mzee Omar Mussa Chitenje kumalizika ilikuwa ya Dakta Daudi Aziz
aliyekuwa Mwenyekiti na Christopher Mahimbo (wakati huo alikuwa Meneja Mkuu wa
UDA) kuanzia mwaka 1978-81. Awamu iliyofuata ilikuwa ya Hassanar Salum
(1981-84), ambaye alikuwa Hakimu katika Mahakama ya Magomeni kabla ya kuwapisha
akina William ‘Bill’ Bandawe (1984-87).
Uongozi wa Bill Bandawe ulikuwa na matatizo
makubwa sana na almanusura mgogoro huo uzae matunda kama yale ya mwaka 1976.
Huu ndio ukweli kuhusu mgogoro uliozaa
Yanga Kandambili na Yanga Raizoni.
NB: Daniel Mbega
ni mwandishi mkongwe na mtafiti wa michezo nchini ambaye anaandaa vitabu vya
‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ na ‘SIMBA VS YANGA: VUTA-NIKUVUTE’.
No comments:
Post a Comment