Dar es Salaam. Waandishi wa habari wanawake wameibuka kidedea kwenye tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2013, baada ya kunyakua tuzo 13, huku Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikishinda tuzo tano kati ya tuzo 19 zilizoshindaniwa.
Sherehe ya utoaji tuzo hizo, ambazo mgeni rasmi
alikuwa Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Harold Nsekela
ilifanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, ambapo kazi 907
zilishindanishwa kuwania tuzo katika vipengele 19, ikiwemo ya mshindi wa
jumla.
MCL inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The
Citizen na Mwanaspoti iliendeleza historia yake ya ushindi katika tuzo
hizo baada ya kuwaingiza wateule 15, huku mwandishi wa Mwananchi,
Kalunde Jamal akinyakua tuzo mbili (Michezo na Burudani na Afya).
Waandishi wengine wa MCL walioshinda tuzo zao
kwenye mabano ni Musa Juma (Kundi la wazi) na Beldina Nyakeke (Watoto)
kutoka gazeti la Mwananchi na Zephania Ubwani (Mazingira) kutoka The
Citizen.
Kwa upande wa zawadi, mshindi wa kwanza kwa kila
kipengele alipewa tuzo, cheti na simu ya Samsung S3 na mshindi wa pili
na wa tatu walipewa kisimbuzi na dishi la DSTV.
Waandishi wa Habari wa MCL wamekuwa wakifanya
vizuri katika tuzo mbalimbali nchini. Katika Tuzo za EJAT zilizotolewa
mwaka jana, waliotwaa tuzo hizo ni pamoja na mshindi wa jumla Lucas
Liganga wa Gazeti la The Citizen.
Mbali na kutoa mshindi wa jumla, waandishi sita
walioshinda na tuzo zao katika mabano ni Edward Qorro (Uchumi na
Biashara), Lucas Liganga (Mazingira na Malaria), Fredy Azzah (Ukimwi na
Elimu), Anthony Mayunga (Utawala Bora) na Florence Majani aliyetwaa tuzo
ya Sayansi na Teknolojia na Afya ya Uzazi.
Redio zilizong’aa
Kwa upande wa tuzo za redio, Afya Redio ya mkoani
Geita ndiyo iliyong’ara zaidi kwa kushinda tuzo 10 kati ya 19, huku
ikitoa mshindi wa jumla, Idd Juma Yusuph ambaye alikabidhiwa zawadi ya
cheti na Dola 4,000.
Tuzo zilizochukuliwa na redio hiyo ni Biashara na
Uchumi (Harith Jaha), Mazingira (Idd Juma Yusuph), Ukimwi (Peninah
Kajura), Sayansi na Teknolojia (Cecilia Ndabigeze), Elimu (Noel Thomson)
na Afya ya Uzazi (Regina Kulindwa).
Tuzo nyingine ni Kundi la Wazi na Afya (Clara Patrick), Ulemavu na Kilimo (Idd Juma Yusuph).
Wengine walioshinda tuzo za redio ni Gervaz Hubile
wa TBC FM (Malaria), Hawa Halifa Msangi wa Kili FM (Utawala Bora),
Grace Kiondo kutoka Hits FM (Watoto), Makwaiya Jumanne wa Victoria FM
(Jinsia) na Abdallah Majura kutoka ABM FM (Uchunguzi).
Kwa upande wa waandishi wa magazeti, tuzo zilimwendea John Bwire
kutoka Raia Mwema (Uchumi na Biashara), Romana Mallya wa Nipashe
(Ukimwi na VVU), Khadija Musa kutoka Uhuru (Utawala Bora) na Richard
Makole wa Nipashe (Jinsia).
Pia wamo Mwantanga Vuai kutoka Zanzibar Leo
(Sayansi na Teknolojia), Peter Orwa wa Uhuru (Elimu), Manyerere Jackton
kutoka Jamhuri (Utalii na Uhifadhi), Anthony Siame wa Mtanzania (Mpiga
picha), Mashaka Mgeta kutoka Nipashe (Afya ya Uzazi kwa vijana),
Polycarp Machira wa The Guardian (Uchunguzi) na Deus Bugaya wa Raia
Mwema aliibuka na tuzo ya Kilimo.
Tuzo zakosa washiriki
Akielezea namna upigaji kura ulivyofanyika,
Mwenyekiti wa majaji wa Ejat, Gervas Moshiro alisema waandishi wa habari
wanapaswa kuongeza zaidi ubora wa kazi zao kwa kuwa nyingi
zilizoangaliwa hazikuwa na kiwango kinachotakiwa.
Akitoa mfano, Moshiro alisema mpiga picha bora wa
televisheni hakupatikana kutokana na kukosa sifa ingawa kazi nyingi
ziliwasilishwa kushindaniwa.
Alisema kuwa televisheni ndiyo zilizokosa zaidi
washindi kuliko redio na magazeti kwa kushindwa kupata tuzo katika
habari za kilimo na biashara, Ukimwi na VVU, uchunguzi, Malaria, watu
wenye ulemavu, sayansi na teknolojia, vijana na afya ya uzazi na michezo
na utamaduni.
“Washindani walikuwepo lakini kazi hizo
zilipowekwa kwenye ubora wa kufuata vigezo zilishindwa kabisa na ikabidi
jopo liseme hakuna mshindi,” alisema Moshiro.
Magazeti yalishika nafasi ya pili kwa kukosa
washindi, ambapo waandishi wa habari za malaria na watu wenye ulemavu
walikosekana, huku redio zikishindwa katika kipengele cha uhifadhi na
utalii.
“Magazeti kama chombo yamepata washindi 46, redio
washindi 39 wakati runinga ikipata washindi 19 na kukosa washindi kwenye
maeneo tisa,” alisema.
Katika kazi zilizopelekwa kushindaniwa, vipindi
vya redio ndivyo vilivyotajwa kuwa na ubora kuliko kazi za vyombo
vingine, ikifuatiwa na magazeti na televisheni.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Kajubi Mukajanga, alisema kazi zinazopokelewa zimeongezeka kutoka
304 mwaka 2009 hadi 907 mwaka 2013.
Pia idadi ya wateule nayo imepanda kutoka 89 mwaka
jana hadi 101 mwaka 2013, na kwamba ongezeko hilo linaonyesha kuwa kazi
bora zimeongezeka.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment