Ndugu zangu,
Mambo mengi yameendelea kuzungumzwa kuhusu marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia kwenye mchakato wa kukusanya maoni, mjadala wa rasimu ya kwanza na hata kwenye Bunge Maalum, watu wengi wanazungumzia zaidi muundo wa Muungano - ama kuwa na serikali mbili kama ilivyo sasa au kuwa na serikali tatu kwa maana ya kufufuliwa kwa 'hayati' Tanganyika.
Kila mmoja anasema lake analolijua, kwa utashi wake, si kuna uhuru wa kutoa maoni bwana!
Wanaotaka serikali mbili wana hoja, haziwezi kupuuzwa, na wanaotaka serikali tatu, nao pia wana hoja za msingi kabisa.
Inafurahisha kuona hoja za pande zote, na hasa nikiwa Mtanzania mwenye kupenda kupima mambo kabla ya kuyazungumzia.
Wanaotetea serikali mbili, ambao wengi ni wa Chama cha Mapinduzi, wanahisi kwamba kama Tanganyika itafufuliwa basi Muungano utakufa kibudu!
Lakini wanaotetea kufufuliwa kwa Tanganyika ndani ya Muungano, wakiwemo Wazanzibari ambao ndio wako mstari wa mbele kutaka kuona serikali-mwenza ya muungano huo, wanaamini haki na demokrasia itatendeka ikiwa Tanganyika itakuwepo. Kama kuna agenda nyingine ya siri kwa Wazanzibari, hakuna anayejua zaidi ya shaka tu ya CCM.
Binafsi NAUNGANA na wale wote wanaotaka serikali tatu, kwa sababu hakuna ndoa ya upande mmoja! Kama Zanzibar wanayo serikali kwenye Muungano, basi Tanganyika nayo inapaswa kuwa na serikali yake.
Kimsingi, watu wasibezane, kwa sababu kinachotafutwa ni kutengeneza Katiba ya Tanzania miaka 50 ijayo, watu wasifikirie maslahi yao ya sasa, bali wanapaswa kuwafikiria watoto na wajukuu zetu.
Jambo muhimu ni kwamba, Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wanapaswa kutumia hekima na busara katika suala hili kwa sababu ndilo pekee ambalo linaweza ama kudumisha umoja na mshikamani pamoja na amani au linaweza kuvuruga kabisa ikiwa uamuzi utakuwa wa kufuata utashi wa makundi.
Katika kipindi ambacho serikali inatuhumiwa na kusimangwa kwa rushwa iliyokithiri, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, kukosekana kwa uzalendo na kumong'onyoka kwa maadili ya uongozi, hakika Katiba Mpya ndio urithi (legacy) pekee ambao Rais Kikwete atakapotoka madarakani mwaka 2015 atakuwa amewaachia Watanzania.
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0715 070109
No comments:
Post a Comment