Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 23 March 2014

MARIJANI RAJABU: MIAKA 19 NDANI YA KINYWA CHA MAUTI


Na Daniel Mbega
ILIKUWA siku ya Alhamisi miaka 19 iliyopita, tarehe kama ya leo, yaani Machi 23, 1995, wakati umma wa Watanzania  ulipopata pigo kubwa kufuatia kifo cha 'Jabali la Muziki nchini Tanzania', Marijani Rajabu, au 'Bulldozzer' kama alivyokuwa akiitwa na wanamuziki wenzake kwenye bendi ya Dar International 'wana-Super Bomboka'.
Halikuwa pigo la Watanzania tu, bali hata Wafrika kwani alitunga nyimbo nyingi, ukiwemo wa 'Kumekucha' ambao ulikuwa ukiwahimiza watu kuacha shuka na kwenda kazi, pamoja na nyingine nyingi.
Marijani na mapenzi, ndoa:
Kwa ujumla Marijani alikuwa akijua nini alichokuwa anakifanya. Alipozungumzia mapenzi au ndoa alikuwa kama anajielezea mwenyewe yanayomsibu, na kwa kweli nyimbo hizo zilisikitisha, kuhuzunisha na pia kufurahisha.
Nyimbo kama Mama Watoto na Ndoa ya Mateso zilimuonyesha Marijani kama mtu wa familia aliyekuwa akikabiliwa na matatizo mbalimbali, na kwa kiasi kikubwa akaweza kuiteka jamii na baadhi ya wanajamii waliokuwa na matatizo kama hayo kwenye ndoa zao walifanikiwa kujirekebisha.
Alipokuwa akiimba nyimbo zenye mchanganyiko wa mapenzi na huzuni, Marijani angeweza kukufanya ulie bila kutaka. Nyimbo kama Salama na Zuwena, alioupiga mara tu baada ya kujiunga na Dar International akiwa na akina Abdallah Mensah, ni mfano mmojawapo wa tungo za aina hiyo.
Katika wimbo wa Salama, sauti ya Marijani inayoonyesha masikitiko ya kukosa 'kitu moyo unapenda' inasikika zaidi hasa pale anaposema:
"Nikilala naota sura yako,
Nikitembea nasikia waniita,
Nageuka sikuoni Salama mama.
Wapi Salama,
Salama nakuomba, Salama nakuita...."
Na hata wanamuziki wenzake wanapojaribu kumsihi anyamaze kwa kuahidi kwamba apoe tu Salama atakuja, bado Marijani, akiwa katika hali ya kukata tamaa, anasikika zaidi katika wimbo huo akilalama:
"...Poa, siwezi poa,
Mpaka nimuone Salama,
Na kula, siwezi kula,
Mpaka nimuone Salama!!..."
Katika nyimbo za Zuwena na Sikitiko, Marijani alidhihirisha wazi kuwa ni mwanamuziki aliyejua kuziteka nyoyo za hadhira yake na uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa namna inayostahili.
Kama alivyosikika katika wimbo wa Zuwena, Marijani anasema kuwa, alipokuwa nyumbani kwake asubuhi wakati jua ndio kwanza linachomoza, alisikia taarifa za ajali ya kutisha iliyokuwa imetokea kwenye daraja la Sealander jijini Dar es Salaam. Je, alifanyaje?
"...Nilitoka bila kujitambua,
Mikono kichwani huku ninalia...
Mbio kwenda hospitali,
Kwenda kumuona, mpenzi Zuwena,
Sijui kama yuko hai,
Ama Zuwena amekwisha kufa,
Maringo na mikogo yangu
Siku hiyo vyote vilikwisha...".
Marijani ambaye alilenga zaidi kufikisha ujumbe wake jinsi alivyokuwa anampenda Zuwena kwa njia inayotia simanzi zaidi, anazidi kueleza zaidi sababu zilizokuwa zikimfanya kumpenda kimwana huyo.
"...Zuwena, ningempata wapi,
Zuwena mwingine sawa na yeye,
Mtoto aliyeumbika, mwenye tabia za kupendeza,
Zuwena, Zuwena kweli nampenda x2
...Moyo ulianza kutulia
Kukuta Zuwena angali mzima,
Ingawa ana majeraha mengi
Haidhuru kuwa namuona,
Zuwena, Zuwena, Zuwena mama,
Zuwena bibi ee, kweli nampenda.
...Sijui ningefanya nini
Kama Zuwena angenitoweka,
Tumeishi kwa muda mrefu
Wote wawili tumezoeana,
Zuwena, Zuwena, Zuwena bibi kweli nampenda..."
Mbali na sauti nzito yenye simanzi na inayomfanya kila ausikiaye wimbo huo kuvutiwa nao, upigaji wa ala katika wimbo huo na hasa kinanda vinazidi kuufanya muziki huo upendwe zaidi.
Marijani pamoja na kuonekana 'fundi' mzuri katika uimbaji wa nyimbo za mapenzi, alikuwa hodari wa kuwasakama akina mama waliokuwa wakishindwa kujitunza na kujijua kuwa walikuwa wanawake waliotakiwa kuonyesha kila aina ya adabu na heshima. Wimbo wa Mayasa ingawa ulitungwa zaidi ya miaka 20 iliyopita lakini ni dhahiri unaonekana zaidi kuwafaa kwa wakati huu akina dada wengi ambao wameonakana kujikwatua kupita kiasi!
Marijani na jamii:
Mwanamuziki huyo alifahamu fika kuikosoa jamii kwa staili ambayo ilimfanya kila mwanajamii kujijua yuko kwenye kundi gani. Aliweza kuwasema wale wenye tabia ya kutaka kuvunja ndoa za watu, hususan wanawake, ambao utakuwa wanawapenda waume za watu kwa lengo la ama kuwakomoa wanawake wenzao au kuwakomoa wanaume wenyewe.
Hayo aliyaeleza bayana katika wimbo wa Mwanameka, kibao kinachoendelea kutamba mpaka sasa kikiwa kimeingizwa kwenye mashule ya sekondari na Wizara ya Elimu kikitumika katika fasihi simulizi, ambapo wanafunzi wamekuwa wakikumbana na maswali kwenye mitihani ya taifa hasa ya kidato cha nne tangu mwaka 1992.
Baadhi ya maneno yaliyoko kwenye kibao hicho ni haya: "Mwanameka eeeh, Mwanameka jirani yangu...uliposikia eeeh, kwamba Mussa ameoa, kaoa mke wa ndoa...ukabadilisha njia eeeh, ukienda sokoni kwa Mussa, naye Mussa macho yakaona, kakutamkia neno la mapenzi...penzi nalo eeeh, penzi nalo halina siri, na siri si ya watu wawili, mkewe Mussa agundua eeeh, hakupikiki wala hakuliki, akaanza kudai talaka, Mussa naye akatoa talaka..."
Yapo maneno mengi sana aliyoyasema katika wimbo huu ambayo yana maana kubwa kwa jamii nzima, hali ambayo inawafanya hata wale wanawake wenye tabia kama hiyo, pamoja na wanaume wenye kupenda kuwadanganya wake za watu, waache tabia hizo na kushika mwenendo mpya wa maisha katika jamii.
Aidha, nyimbo zake nyingi zilikuwa zikihusu matukio ya kweli kabisa; kwa mfano wimbo wa 'Masudi amekuwa jambazi'. Wimbo huu uliopendwa sana katika miaka ya 1980 ulikuwa ni tukio la kweli lililomkuta kijana mmoja Masudi aliyekuwa akiishi Kigogo Luhanga, ambaye alikuwa hatari kweli kweli kwa kukwapua vitambaa vya akina, kofia na fedha...
Inasemekana baada ya kuimbwa na Marijani, Masudi aliacha ukwapukwapu na kuamua kutumia nguvu zake kusukuma mkokoteni, kwani mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe!
Wimbo wa 'Kumekucha' ulikuwa unatumika Redio Tanzania kuwahamasisha watu asubuhi kuacha shuka zao na kwenda kazini.
Aliwaasa watoto wa shule, kama alivyofanya katika wimbo wa 'Roza nenda shule' na 'Unakwenda wapi mwana', akina mama kama alivyofanya katika nyimbo zilizotajwa hapo juu na hata wanaume walevi kama alivyofanya katika wimbo wa 'Pombe siyo chai'.
Aliimba kuhusu wanadamu walivyogeuka kuwa wadanganyifu na kukosekana kwa imani duniani, hakuna uaminifu, watu wanadhulumiana, ndugu wanagombea urithi wakati yatima wanahangaika, na mengine mengi. Ni katika kibao cha 'Dunia Imani Imekwisha.' Anasema:
"Aeeh aeeh walimwengu x2
Walimwengu fungueni masikio msikie,
Mazingira ya dunia yanatuhusu wenyewe,
Tujihadhari na wanadamu tunaoishi nao hatari eeeh.
Mwanadamu hana wema usimwamini,
Hana hizo fadhila wala shukrani,
Tenda wema kwake fadhila yake punda mateke..
Usimpe siri yako rafiki hata nduguyo,
Kwani kikulacho ki nguoni mwako,
Utajikuta pabaya halafu ushangae eeeh eeeh.
Kiitikio:
Dunia sasa imani imekwisha,
Nyoyo za watu zimebadilika,
Wala hakuna uaminifu tena,
Si wanawake, si wanaume,
Si kwa wazee, wala si vijana,
Wote tunakwenda mzabwa mzabwa,
Kwenye watu kumi binadamu mmoja.
Hata walaghai ndio mmezidi,
Watu wamezidi kudhulumiana,
Kila mahali unafiki na dhuluma,
Utu umekwisha umebakia unyama.
Bwana fulani amefariki,
Kafa lakini kaacha watoto,
Ndugu waliobaki akili zimewaruka,
Mawazo yote ni kwenye mali,
Wanataka uana sababu ya nyumba,
Wanasahau hata watoto,
Watoto wenyewe bado wadogo,
Wanadhulumu hata watoto yatima.
Fundi cherehani kaletewa vitambaa,
Mwenyewe kataka suruali tatu,
Fundi kajibu hewala vimefika,
Kumbe mfukoni fundi kachacha,
Vitambaa kauza na pesa katia ndani,
Wiki iliyofuata mwenyewe kafika,
Anauliza wapi suruali zangu,
Fundi alia yoo yoo,
Anauliza fundi walia nini,
Ati anajibu leo nimeibiwa.
Ndugu kauzeni kaachiwa duka,
Mwenyewe kaenda Kilwa Kivinje,
Kauzeni kasema, "Sasa watanijua!!
Hasa yule Kabuta atanitambua,"
Kapita Kabuta akamhonga unga,
Karudi jioni kapewa sukari,
Wiki mbili duka limefilisika,
Anajiuliza nitajibu nini,
Kila akiwaza hakuna la kufanya,
Akaiba mapesa na vitu vyote akapotea."
Lakini kama alivyowahi kuimba yeye mwenyewe katika wimbo wake wa 'Rufaa ya Kifo', Mwenyezi Mungu akaamua kumuita akiwa bado mbichi. Marijani anasema katika wimbo huo: "...Lakini Mola eeeh, kazi yake haina makosa, tena hairekebishwi na binadamu yoyote..."
Achukuliwa na Simba:
Pengine linaweza likawa jambo la kushangaza. Lakini ndio ukweli wenyewe. Kwamba, mbali ya kutunga, kupiga na kuimba muziki, lakini pia Marijani alikuwa mwanasoka mzuri sana enzi zake akichezea nafasi ya golikipa.
Alikuwa akiutumia muda wake wa ziada kwenda kufanya mazoezi pale kwenye uwanja wa Karume, zamani ukijulikana kama Uwanja wa Ilala, si mbali sana kutoka pale mtaa wa Somali alikokuwa akiishi.
Kutokana na uhodari wake aliouonyesha akiwa na timu za mitaani, Marijani alijikuta akichukuliwa na viongozi wa Simba ili akaidakie timu hiyo. Hiyo ilikuwa katika miaka ya 1970.
"Kwa kweli fani yetu ilipata pigo kubwa kipindi hicho na tulidhani kwamba tungempoteza mwanamuziki muhimu sana hasa kama angeamua kukubali kuichezea Simba, ambayo alikuwa na mapenzi nayo makubwa. Hata hivyo, aliamua kuachana na wazo la kuichezea timu hiyo na kurejea kwenye jukwaa la muziki," alipata unisimulia, Abdallah Mensah (sasa marehemu), rafikiye wa karibu enzi hizo.
Mensah alisema kuwa, mbali ya kusoma na marehemu Marijani katika shule ya msingi Kisarawe na baadaye shule ya sekondari Tambaza, lakini pia aliimba naye kwenye bendi ya Safari Trippers na baadaye wakaenda kuanzisha Dar International.
Kuzaliwa:
Marijani alizaliwa mwaka 1954 jijini Dar es Salaam na kulelewa katika mazingira ya kidini ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kusomeshwa Qur'an kwenye Madrasa, ambako pia alikuwa mwimbaji wa kaswida na mpiga dufu.
Alipofikisha umri wa miaka 18 tu akajitokeza kuwa gumzo katika midomo mingi ya Watanzania katika uimbaji. Tangu alipokuwa na bendi ya STC, Marijani, ambaye kwa wakati huo pia alikuwa bado mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Tambaza, alionyesha wazi kuwa alizaliwa kwa ajili ya kuburudisha, kufundisha na kukemea yale yote ambayo yalikuwa hayampendezi Mwenyezi Mungu na wateule wake.
Wimbo wa Ewe ndugu yangu na Shida alizotunga na kuimba wakati akiwa na bendi ya STC mwaka 1971 ni ushahidi tosha wa kuonyesha kuwa Marijani tangu awali aliamua kutumia kipaji chake kwa ajili ya kuonya dhid ya matendo mabaya.
Kipaji cha Marijani kilichanua zaidi wakati alipochukuliwa na Saleh Amour aliyekuwa Mkurugenzi wa Bendi ya Safari Trippers pia ya jijini Dar es Salaam mwaka 1973, ambako aliibuka na nyimbo za Matilda, Hanifa, Salama, naMwana mpotevu.
Mwaka 1978 alihama bendi hiyo pamoja na wanamuziki kadhaa na wakaanzisha bendi ya Dar International na kibao chake cha kwanza kilikuwa Zuwena kilichofuatiwa na nyinginezo nyingi.
Bendi hiyo 'ilisinzia' na kupotea katika miaka ya 1980, lakini mwaka 1990 Jabali la Muziki liliibuka likiwa na vyombo vya kisasa na kuja na bendi nyingine iliyoitwa Afri Culture ikiwa na mtindo wa 'Mahepe ngoma ya wajanja'. Bendi hiyo ilikaa miaka takribani mitatu halafu ikapotea kabisa.
Mkewe Amina binti Ibrahim alifariki mwaka 1992 na kumwachia watoto watatu; Aisha, Wahida na Rajabu. Mtoto wake mwingine Hanifa alifariki.
Kama alivyowahi kuimba mwenyewe katika wimbo wake wa Rufaa ya Kifo, Mwenyezi Mungu aliitwaa roho yake Alhamisi, Machi 23,1995 baada ya kuugua kwa zaidi ya mwezi mmoja. Alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Siku hizi bendi nyingi zimekuwa zikipiga baadhi ya nyimbo zake katika maonyesho yao na wale wanaotumia mitindo ya 'Chuna Buzi', yaani wenye vinanda wanaopiga kwenye sherehe. Hii ni kuonyesha kwamba, nyimbo hizo bado ni 'peremende' kwa mashabiki.
'Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. AMINA'.

No comments:

Post a Comment