Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 21 March 2014

NYERERE, KARUME WANATUMIWA KUPINGA SERIKALI TATU KWA MASLAHI YA CCM


Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Ndugu zangu,
Nakubaliana kabisa na kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aliyoitoa Januari 2, 2014 akionya kwamba Mwalimu Julius Nyerere asitumike kupinga muundo wa Muungano wenye serikali tatu.
Kinachoonekana katika hotuba ya Rais Kikwete inayoendelea Bungeni kinanitia mashaka sana, kwa sababu kinaonekana kama yanayohutubiwa humo ni ule msimamo wa Chama cha Mapinduzi ambao kwa miaka mingi kimeendelea kupinga kufufuliwa kwa Tanganyika kwenye Muungano.
Inaonekana dhahiri kwamba anaikosoa hata Tume ya Warioba kwamba takwimu walizozitoa siyo sahihi kuhusu Watanzania 'wengi' wanataka serikali tatu, lakini akakumbusha kuwaenzi waasisi wa Muungano huo, Nyerere na Sheikh Karume.
Kwa mtazamo wangu, hili ni janga kubwa na kuna uwezekano mjadala unaweza kuvurugika. Sikutegemea kama Rais angetoa hotuba kama hiyo, alipaswa kuwa 'nyutro'. Vinginevyo kutoa maelekezo ya serikali ipi ndiyo bora, basi ni kuwapa majibu ya mtihani wajumbe na zaidi kuwapasisha mtihani wajumbe wanaobeba msimamo wa CCM wanaopinga serikali tatu na ndiyo maana makofi na vigelele vinasikika kila anapoonekana kukosoa maoni ya serikali tatu.
Jaji Warioba alisema hivi wakati huo:

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewashangaa watu wanaodai kuwa mapendekezo ya kuanzishwa muundo wa Muungano wa serikali tatu ni kumgeuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye enzi za uhai wake aliukataa.
Pia amesema suala la gharama haliwezi kuwa tatizo kwa kuwapo muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Jaji Warioba alisema hayo katika mkutano kati yake na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri (TEF) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuwapa fursa wahariri kupata ufafanuzi kutoka kwa Tume hiyo kutokana na mapendekezo iliyoyatoa kuhusiana na rasimu ya pili ya Katiba mpya.

MWALIMU HAKUWA NA MAWAZO MGANDO
Jaji Warioba alisema watu wanaotoa madai hayo wana upeo finyu wa kufikiri, hasa kuhusu hali aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere kimawazo.
“Wanafikiri Mwalimu (Nyerere) angekuwa na mawazo mgando wakati wote, asingebadilika,” alisema Jaji Warioba.
Alisema enzi za uhai wa Mwalimu Nyerere kuna mambo kadhaa yalibadilika, ukiwamo mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa, ambao yeye alikuwa kinara wake mkubwa.
Hata hivyo, alisema Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipokuja na ripoti iliyopendekeza kuanzishwa mfumo mpya wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Watanzania wengi waliupinga.
“Lakini Mwalimu (Nyerere) akasema tumefika mahali hatuwezi kwenda na chama kimoja. Dunia imebadilika. Hata ukuta wa Berlin umevunjika,” alisema Jaji Warioba akimnukuu Mwalimu Nyerere.

GHARAMA HAZIEPUKIKI
Aidha, aliwashangaa wanaoshikilia kwamba, serikali tatu zitatumia gharama kubwa katika kuziendesha, huku wakisahau kuwa wakati Watanganyika walipoanza kujitawala, walianza na mikoa, wilaya, tarafa na vijiji vichache, lakini leo vimeongezwa na hivyo, kuongeza gharama za uendeshaji wake.
“Hizi ni gharama, lakini ni za kimaendeleo,” alisema Jaji Warioba.
Hata hivyo, alisema njia pekee ya kupunguza gharama kubwa katika uendeshaji wa serikali za muundo wowote wa Muungano, ni kuondoa matatizo yanayousibu Muungano.
“Bado tutaongeza mikoa. Hizo ni gharama. Na bado watu wanadai mikoa iongezwe…tunaamini gharama siyo tatizo kwa kuwa na muundo wa Muungano wa serikali tatu,” alisema Jaji Warioba.
Alisema rasimu ya katiba mpya iliyopo siyo ya Warioba wala ya Tume, bali ni ya wananchi.
Hivyo, akasema Tume haitaki kuhusishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wala makundi yoyote ya kijamii.
Jaji Warioba alisema wanakataa hilo kwa kuwa waliotoa maoni hawakuwa wakifanya hivyo kwa misingi ya vyama wala makundi.
Alisema hadi wananchi wanafikia kutoa maoni waliyoyatoa kwa Tume, ni dhahiri kuwa waliona sababu za msingi.
Hivyo, akasema kama Tume nayo isingeona sababu za msingi katika maoni yaliyotolewa na wananchi, isingependekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu.

BUNGE LA KATIBA
“Sisi kazi yetu tumemaliza. Tutajiandaa vizuri kwenda kuwasilisha (rasimu ya katiba mpya) kwenye Bunge la Katiba ili wajumbe wajue nini tumependekeza,” alisema Jaji Warioba.
Awali, alisema kwa namna rasimu ya katiba mpya ilivyo sasa kama Tume ingekuwa na uwezo, ingeipitisha na kuwa katiba rasmi.
Lakini akasema sheria inaibana Tume kwa kuwapa wananchi mamlaka ya kuwa ndiyo mwamuzi wa mwisho kuamua ama kuikubali au kuikata rasimu hiyo.
Alisema nia kubwa ya mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi, ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, katiba itakayopatikana iwe inakidhi matumaini ya Watanzania.
Lakini akasema wasiwasi mkubwa juu ya kufikia lengo hilo, unatokana na namna vyombo vya habari kwa kiwango kikubwa vilivyojikita kwenye kutangaza habari zinazohusu uongozi na kuacha mambo mengine muhimu, ambayo wananchi waliyatolea maoni.
“Kwamba mambo, ambayo yanahusu uongozi ndiyo, ambayo yamepewa kipaumbele. Ikiwa pendekezo, chombo cha habari hakisemi kama kimetoka kwa wananchi, kinaona kama ni kundi fulani, ama kundi fulani limepata, kundi fulani limepoteza,” alisema Jaji Warioba.
Alisema wao kama Tume wanayaona yaliyo ya msingi, ambayo yataleta mapinduzi katika kutengeneza katiba mpya, ni yale yaliyotoka kwa wananchi.
Jaji Warioba alisema katiba ni maisha ya kawaida na kwamba, kila kitu kinachofanywa na watu kiko ndani yake.
Alisema wananchi katika kutoa maoni, walizungumzia mambo mengi sana ya maisha yao ya kila siku, zikiwamo shughuli zao za kiuchumi, matatizo ya kilimo, usafiri, mambo ya jamii, afya, hifadhi ya jamii, maadili katika taifa na haki za binadamu.
“Katika kutoa habari kwa kweli vyombo vya habari havioni kama haya ni muhimu. Lakini yakija mambo ya urais, mambo ya ubunge, mambo ya mgombea binafsi, yale yanayohusu wakubwa, haya yanafahamika sana,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza: “Kwa hiyo huko tunakokwenda mjue kwamba, kuna mambo ya wananchi, ndiyo mategemeo yao.”  
SOURCE: NIPASHE     

No comments:

Post a Comment