Na Daniel Mbega
MITAALA yetu imebadilika sana kiasi
kwamba kizazi cha sasa hakipati fursa ya kujifunza hata historia yetu kwa
undani. Ingawa wahusika wanajitetea kwamba wanakwenda na mabadiliko ya sayansi
na teknolojia, lakini binafsi naamini tunakosea sana kutowafundisha vijana wetu
mambo ya msingi, hususan yaliyotokea nchini mwetu kabla ya ukoloni, wakati wa
ukoloni na hata baada ya uhuru.
Binadamu kuishi bila kumbukumbu ya
mambo yaliyopita kamwe hakuwezi kumfanya akabadilika na kujua nini afanye ili
kuyaboresha maisha yake. Hata tunapojifunza mambo ya imani za kiroho ni
historia, sasa wahusika wa elimu wanaposhindwa kuandaa mitaala thabiti kwa
vizazi vyetu wanakuwa wanafanya makosa makubwa.
Ndugu zangu, leo nataka kuwakumbusha
tu kuhusu usafiri mkubwa uliozoeleka wakati wa ukoloni na hata baada ya uhuru.
Usafiri wa treni. Sitaki kuzungumzia historia ya usafiri huo hapa nchini, bali
nitazungumzia kuhusu reli ya kwanza kabisa kujengwa ndani ya Tanganyika, au
Koloni la Kijerumani Afrika Mashariki (German East Africa) kama lilivyokuwa
likijulikana wakati huo likizihusisha Tanganyika (Tanzania Bara ya sasa),
Rwanda na Burundi.
Kwa wale wasiojua ni kwamba, reli ya
kwanza kabisa kujengwa hapa nchini ni ile ya Usambara (Usambara-Railway). Reli
hii ilijengwa baada ya kuanzishwa kwa kampuni moja ya reli mwaka 1891 ikiwa na
dhamira ya kuiunganisha bandari ya Tanga katika Bahari ya Hindi na Ziwa Nyanza
(Ziwa Victoria) kupitia kusini mwa Milima ya Usambara. Wahusika walipanga
kwamba reli hiyo iwe na geji 1,000mm (futi 3 na inchi 3 3⁄8).
Tangu Junie 1893 ujenzi wa reli hiyo
ukaendelea kuanzia Tanga kwenda bara. Kutokana na ukosefu wa mtaji ilibidi
kampuni hiyo itaifishwe na serikali (ya Kikoloni chini ya Wajerumani) mwaka 1899.
Baada ya hapo reli hiyo ikawa chini ya Shirika la Reli la Kijerumani
lililofahamika zaidi kama Ostafrikanische Eisenbahngesellschaft (East
African Railway Cooperation), kampuni ambayo ilikuwa imeundwa ili kujenga na
kuendesha Reli ya Kati ya Tanganyika (Zentralbahn) kutoka Dar es Salaam
hadi Kigoma.
Kati ya Pongwe
na Ngommi kwenye Reli ya Usambara kulikuwa na michepuko miwili (double
hairpin turn).
Mnamo Septemba 26, 1911 reli hiyo ilifika
Moshi kwenye Mlima Kilimanjaro ukiwa ni umbali wa kilometa 351.4 kutoka
Bandari ya Tanga. Safari kwenye njia hiyo zilianza Oktoba 4, 1911 na uzinduzi
rasmi ulifanyika Februari 7, 1912. Mwaka 1914 treni moja ilifanya safari kati
ya Tanga na Buiko na kurejea kila siku na kwa siku mbili kwa wiki safari zilifanyika
kati ya Tanga na Moshi. Safari nzima kwa umbali huo ilitumia saa 14 na dakika
40.
Kutoka katika stesheni ya Tengeni hadi mji wa Sigi kulikuwa na njia-panda ya reli
yenye urefu wa kilometa 23.3 iliyojengwa kwa kutumia geji 750mm (futi 2 na
inchi 5 1⁄2) ikiwa na michepuko minne (four hairpin turns).
Kuanzia Juni 4, 1912 – Mei 12, 1913 reli
hiyo ikaitwa Reli ya Kaskazini (Nordbahn - Northern Railway) kwa kipindi
kifupi. Mipango ya kuiendeleza reli hiyo hadi Arusha ilikuwa inafanywa na fedha
tayari zilikuwa zimetolewa lakini haikuweza kujengwa kutokana na kuanza kwa
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Waingereza walipoanza kuitawala
Tanganyika wakaamua kuiunganisha Reli ya Usambara kati ya Moshi na Voi na ile
Reli ya Uganda nchini Kenya na kuiongezea mwaka 1929 hadi katika kituo chake
cha sasa cha Arusha.
Baada ya Tanganyika kupata uhuru
Reli ya Kati na Reli ya Usambara zikaunganisha kati ya Mruazi na Ruvu. Wakati
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyohusisha nchi za Kenya, Tanzania na Uganda,
Reli ya Usambara ilikuwa chini ya Shirika la Reli la Afrika Mashariki (EAR).
Jumuiya hii ilipovunjika mwaka 1977 Reli ya Usambara ikawa chini ya Shirika la
Reli Tanzania (TRC) ambalo nalo lilibinafsishwa mwaka 2007 na kuchukuliwa na
kampuni ya RITES ya India.
Chini ya utawala wa Wajerumani mwaka
1913, Reli ya Usambara ilikuwa na injini 18, mabehewa 31 ya abiria na mabehewa
199 ya mizigo pamoja na wafanyakazi 562 ambapo 35 kati yao walikuwa Wazungu.
Baada ya kujengwa kwa njia ya
kuunganisha Voi, safari kati ya Arusha, Moshi na pwani zilielekezwa kwenye
bandari ya Mombasa na sehemu ya kaskazini ya Reli ya Usambara ikawa kwa ajili
ya huduma za ndani. Treni la abiria liliongozwa na watumishi (DMU) wanne wakati
huo.
No comments:
Post a Comment