Phil Klerruu
Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
Afisa Milki Mwandamizi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyesimamishwa kazi, Phil Klerruu, amepinga hatua hiyo akisema Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, hana mamlaka hayo kulingana na sheria na kanuni za ajira za Jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Klerruu alisema mamlaka yake ya ajira na nidhamu ni Baraza la Mawaziri la EAC ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kumwajibisha baada ya kupokea tuhuma na mapendekezo kutoka kwa Katibu Mkuu.
“Katibu Mkuu alipaswa kunipa kwa maandishi hati ya mashtaka yenye tuhuma dhidi yangu, kuunda tume kunichunguza na kuwasilisha mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi iwapo tuhuma zitathibitishwa,” alisema Klerruu
Alisema pamoja na kukiuka sheria na kanuni za ajira EAC, katibu Mkuu pia alishindwa kutaja mali anazodaiwa kujimilikisha wala thamani yake licha ya ukweli kwamba kazi ya kuhamisha vitu siyo moja ya kazi zake kulingana na majukumu yaliyoanishwa kwenye barua yake ya ajira.
Klerruu alisema anaamini barua yake kwa Katibu Mkuu, Dk Sezibera akimwomba kuchukua hatua dhidi ya Naibu Katibu Mkuu (Fedha na Utawala), Jean-Cloud Nsengiyumva anayetuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kubagua wafanyakazi kwenye ajira za muda ndiyo imemponza.
Akijibu madai ya Klerruu mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake, Dk Sezibera alisema sheria na kanuni za ajira zinampa mamlaka ya kumchukulia hatua za kiutawala ikiwemo kumsimasha kazi afisa huyo kupisha uchunguza kabla ya kuwasilishwa suala hilo Baraza la Mawaziri.
Akipokezana na Mkurugenzi wa Utawala wa EAC, Richard Ochwada, Dk Sezibera alikiri kupokea barua ya Klerruu akimtuhumu Naibu Katibu Mkuu Nsengiyumva kwa matumizi mabaya ya madaraka lakini tuhuma hizo hazikuthibitishwa na baada ya uchunguzi kufanyika na kukana kuwa chanzo cha Afisa huyo kusimamishwa.
No comments:
Post a Comment