Kutoka
kushoto ni Katibu wa Bunge maalum la Katiba Bwana Yahya Khamis
Hamad,Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue. Waziri Mkuu Mizengo
Pinda ,Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh.Samuel Sitta,Makamu
Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Mh.Samia Suluhu, Makamu wa pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Sefu Iddi, Naibu Katibu
wa Bunge Maalum Dkt.Thomas Kashilila na kulia ni Mwenyekiti wa muda wa
Bunge maalum la katiba aliyemaliza muda wake Mh.Pandu Ameir Kificho.
UONGOZI wa juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kesho utahamia katika Makao Makuu ya Tanzania, Dodoma, kushuhudia hotuba ya kihistoria itakayotolewa na Rais Jakaya Kikwete mbele ya Bunge Maalumu la Katiba.
Hotuba hiyo ya Rais inasubiriwa kwa hamu na Watanzania, kutoa dira kwa wajumbe wa Bunge hilo
Maalumu la Katiba, wakati watakapokuwa wakiandika Katiba mpya.
Mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wakongwe, aliliambia gazeti hili kuwa anatarajia hotuba ya Rais Kikwete itakuwa ya kujenga Bunge na sio kubomoa kwa kuzungumzia misimamo ya vyama.
“Yeye ni kiongozi wa Taifa, hivyo natarajia atakuja hapa kutupa njia na namna ya kushughulikia changamoto zilizopo wakati tunapoenda kuandika Katiba mpya,” alisema mwanasiasa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema Rais atahutubia Bunge saa 10 jioni na wageni waalikwa watatakiwa kuwa wameketi katika maeneo yao saa tisa alasiri.
Hamad alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza na kikao cha Bunge saa 9.10 na baadaye kikao hicho kitaahirishwa saa 9.20 kwa ajili ya kumpokea Rais Kikwete.
Wageni mashuhuri
Hamad alisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, amewaalika wageni mbalimbali kushuhudia tukio hilo muhimu la kitaifa, wakiwemo viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu kutoka pande zote za Muungano.
Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba Mh.Samuel Sitta(kushoto) na Makamu Mwenyekiti
Mhe.Samia Suluhu(kulia).
Wengine ambao wamealikwa kuhudhuria tukio hilo ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, wajumbe wenzake na makamishna wote wa Tume hiyo.
Pia watakuwepo viongozi wengine wastaafu wa kitaifa ambao ni mawaziri wakuu wastaafu, Waziri Kiongozi mstaafu na maspika wa Bunge.
Wageni wengine walioalikwa ni kutoka taasisi za dini, taasisi zisizo za kiserikali, wawakilishi wa tasnia ya habari, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na taasisi za elimu ya juu.
Pia vipo vyama vya watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi na wakulima pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi.
Kuwasili kwa JK
Baada ya Rais kuwasili katika eneo la Bunge, atapokewa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kwenda katika jukwaa maalumu kupokea salamu za heshima na kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Polisi.
Katibu wa Bunge alisema baada ya shughuli zote zitakazofanyika katika viwanja vya Bunge kumalizika, utaratibu umewekwa kwa viongozi kuingia bungeni kwa maandamano maalumu.
Viongozi watakaotangulia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Gharib Mohammed Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Rais Kikwete ambaye atakuwa amefuatana na mwenyeji wake ambaye ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Baada ya Rais kumaliza kuhutubia Bunge Maalumu, wajumbe wote wa Bunge Maalumu watapata fursa ya kupiga picha ya pamoja mbele ya jengo la Bunge.
Rais atalihutubia Bunge ili kutoa nafasi kwa bunge hilo kuendelea na mjadala baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya pili ya Katiba, Jumanne wiki hii.
Hotuba ya Jaji Warioba ambayo ilijaa tafiti nyingi inaonekana kuwachanganya wajumbe wengi kwa kuamini kuwa imeibua mambo mengi ambayo yalikuwa yamefichika.
Sendoro
Katika hatua nyingine, Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Elinaza Sendoro alimpongeza Jaji Warioba na Tume kwa kazi kubwa waliyoifanya kuandaa Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo, Sendoro aliyezungumza na gazeti hili jana Dar es Salaam, baada ya Misa ya Jubilee ya miaka 30 ya Uaskofu wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliwaonya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuwataka waache vurugu na misimamo binafsi katika suala la kitaifa.
Aliwataka wajumbe hao wasirudie walichokifanya juzi baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya Katiba mpya, ambapo alisema kila mmoja alirejea kwenye misimamo binafsi, ya taasisi na vyama vya siasa.
Badala yake amewataka kutafakari kwa kina aliyosema Warioba na kuleta kwa wananchi kitu kitakachojenga umoja wa Kitaifa.
“Mchakato mzima wa kuwa na Bunge la Katiba ni sawa kabisa, lakini mara nyingine wajumbe wale wana vurugu zisizo za lazima, baada ya Rasimu ya II, walisimama wengine na kuanza kuzungumza maneno mengi, wakarejea kule kule kwenye misimamo yao na vyama vyao. “Wangekaa kwanza kimya, watafakari alichosema Warioba, wajadili, wachuje ili watoke na kitu kitachojenga umoja wetu, wameacha alichosema Warioba na inavyoonekana, watu wameamua kuwa misimamo yao ndio yao, hii si sawa, kila mtu akishikilia msimamo wake pale tutapata Katiba? Alihoji Sendoro.
Akizungumzia Muungano, Askofu Sendoro alisema pamoja na kwamba Taifa lipo katika mchakato wa Katiba utakaoamua pia muundo wa Serikali uweje, ni wazi Muungano uliopo hivi sasa umeleta umoja wa Kitaifa.
Muungano
“Siku zote umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, Muungano umetuletea umoja, wakati huu tunapaswa kuangalia kwa makini kama tunachagua muundo wa kutuongoza, tuangalie tunauendeshaje Muungano, tulifikishwa na waasisi wetu kuwa nchi moja,” alisema Sendoro.
Kwa mujibu wa Askofu huyo mstaafu, suala la Zanzibar kujitokeza kuwa na Katiba yake inayoitambua kama nchi kamili, ni dosari inayopaswa kufanyiwa kazi kwani inaleta utengano badala ya umoja. Alisisitiza Katiba ijayo ibebe sera ya umoja wa kitaifa.
Akimzungumzia Kardinali Pengo, Askofu Sendoro alisema ni mtu wa pekee, mwenye kumpenda Mungu na kuhudumia watu hasa wahitaji na alisema kwa ushirikiano waliokuwa nao tangu mwaka 1992 Pengo alipokuwa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, umejenga umoja wa kiimani na maendeleo makubwa ya kiroho na kimwili kwa Wakristo wa Jiji hilo.
Ubinafsi
Awali akihubiri katika Ibada hiyo ya Misa, iliyofanyika katika Viwanja vya Kituo cha Msimbazi, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo la Morogoro, alisema ubinafsi umezidi kuongezeka katika jamii na chanzo ni tabia ya kila mtu kuona yeye ndio yeye na mwingine hana maana kwake.
“Tunaona mambo yanayoendelea katika jamii leo, katika Bunge, wanasiasa, kila mtu anaona chama chake kikisema na kuamua ndio kimesema, hakuna kingine kinaweza kusema, huu ni ubinafsi ambao ulisababisha ndugu kuuana kama Kaini na Abeli katika Biblia Takatifu,” alionya Askofu Mkude.
Alimpongeza Pengo kwa kutii sauti na mwito wa Mungu, kujitoa si kwa manufaa yake bali ya Taifa la Mungu kwa ujumla, jambo alilotaka watu waige kwa maslahi ya umma.
Alisema Kanisa linatambua mchango wa watumishi wake ndio maana Aprili 27 mwaka huu litawatangaza rasmi Baba Mtakatifu Yohana Paulo II na Yohana wa XXIII kuwa Watakatifu.
Mkude aliwashukuru wazazi wa Kardinali Pengo (wote marehemu), kwa kumleta duniani kiongozi huyo na kuwataka waumini wote popote nchini, kumuombea afya njema ili aendelee na kazi ya Mungu.
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dodoma na Gloria Tesha, Dar es Salaam.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment