Ni tatizo ambalo limewasumbua wazazi wake kwa muda mrefu sasa, kiasi cha kuomba misaada.
Waswahili husema ‘kuzaa si kazi, bali kazi ni
kulea’. Kuzaa ni jambo la kawaida kwa wazazi ambao hufurahia watoto
wao. Kwa wale wanaokosa watoto kutokana na sababu mbalimbali inakuwa
balaa kwao.
Mwaka 2006 ilikuwa furaha kwa Angolwisye Ntalima
kupata mtoto wa kwanza wa kike aitwaye Vera. Hata hivyo furaha hiyo
imekuwa ikiyeyuka kadiri mtoto wao anavyokua hadi sasa amefikisha miaka
saba. Mtoto huyo hadi sasa hawezi kusimama, kuongea, wala kujisaidia
bila kupata msaada.
“Awali mtoto huyu alipozaliwa alikuwa na afya njema tu,” anasema Ntallima huku akionyesha picha za utotoni za Vera.
“Tulianza kugundua tatizo lake pale alipokuwa
akijifunza kusimama na kutembea akiwa na mwaka mmoja na nusu. Alikuwa
akisimama kwa vidole na anakosa mwelekeo na kuanguka vibaya.”
Anasema walimwanzishia matibabu Hospitali ya CCBRT ambako alipewa viatu vya kumsimamishia na kumfanyia mazoezi.
Chanzo cha tatizo
Akizungumzia chanzo cha tatizo hilo, Ntalima
anasema inawezekana ni wakati wa kuzaliwa kwani mama yake alionyesha
dalili zote za kujifungua, lakini hakupata uchungu.
“Madaktari walimchoma sindano ya uchungu tangu saa
sita mchana wakamwambia arudi baadaye. Ilipofika jioni nikampeleka
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako aliongezwa sindano nyingine ya
uchungu aliyokaa nayo hadi saa 6:00 usiku. Mwisho wakampeleka kwenye
upasuaji ambao ulimalizika saa 8:00 usiku na mtoto alikuwa na hali
nzuri,” anasema.
Anataja sababu ya pili akisema inawezekana ni ugonjwa wa degedege alioupata akiwa bado mdogo.
Kuhusu mazoezi waliyopata CCBRT, Ntalima anasema licha ya kukamilika, bado hayakumwezesha mtoto wake angalau kwenda shule.
Mbali na CCBRT, Ntallima anasema aliwahi kumpeleka
kituo cha YWCA kilichopo Buguruni Malapa kwenye shule ya wenye mtindio
wa ubongo, lakini hakupata nafuu.
“Wakati huo nilikuwa nikiishi Kisarawe, hivyo nilikuwa
nikimpandisha gari hadi Gongo la Mboto ambako anachukuliwa na gari la
shule, kisha namfuata jioni na kurudi naye Kisarawe. Yalikuwa mateso
matupu.
“Mwaka jana nilimpeleka hadi Iringa ambako kuna
kituo cha watoto wenye matatizo kama haya, lakini hali ilizidi kuwa
mbaya. Ilibidi nimrejeshe baada ya miezi sita tu,” anasema.
Mbali na hayo anasema mazoezi aliyopatiwa
yamemwezesha walau kutambaa kwa kuinama na kupata nguvu. Licha ya
kuendelea kutokwa na udenda mdomoni na kushindwa kuongea.
“Unavyoona hali hii ni kwa sababu tuliwahi
kumpeleka hospitali kufanya mazoezi, vinginevyo angelemaa kabisa. Watu
wanaowafungia ndani watoto kama hawa wanaishia kulemaa moja kwa moja,”
anasema.
China kwa ajili ya matibabu
Ntallima anasema alikuwa akipitia mitandao ya
intaneti ili kujifunza kuhusu ugonjwa huo na alioona anwani ya Hospitali
ya Beijing Shizhentang.
“Wanasema moja kati ya huduma zao ni matatizo ya
ubongo na wanaweza kutibu kwa asilimia 70 na ukiwahi inaweza kuzidi.
Ndipo nikawasiliana nao na kuwaeleza hali niliyonayo,” anasema.
Anasema hospitali hiyo ilimjibu ikimtaka awape
historia ya ugonjwa wa mtoto na matibabu aliyopata na kuambatanisha
picha mnato na video ili kufafanua tatizo lake.
“Walinijibu kuwa tatizo alilonano ni la ubongo
(cerebral pars). Walisema watachukua uboho wa mifupa na kuuwekea dawa
kisha kuurudisha kupitia uti wa mgongo. Walifafanua kwamba mzazi
atafundishwa jinsi ya kumwongelesha.
“Waliopata matibabu hayo wanasema ndani ya wiki
tatu, mtoto anaweza kuongezeka kwa angalau nusu nchi na atatamka hadi
neno la tatu na nguvu kwenye viungo itarejea.”
Anasema gharama za matibabu hayo ni kubwa na
hawezi kuimudu. “Kinachonisumbua ni gharama kwa sababu wao wanataka Dola
27,000 za Marekani (sawa na Sh43 milioni) kwa ajili ya matibabu ya wiki
nne, malazi ya mtoto na wasindikizaji na baada ya tiba kuna dawa zenye
gharama ya Sh3 milioni,” anasema.
Anasema hadi sasa amefanya jitihada za kuomba msaada kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.
“Mtoto tumemfungulia akaunti Na 015221931200 katika Benki ya CRDB.
CHANZO: MWANANCHI
“Mtoto tumemfungulia akaunti Na 015221931200 katika Benki ya CRDB.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment