Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,
akiondoka bungeni chini ya ulinzi wa askari wa Bunge baada ya vurugu kutokea jana. Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele
ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana
na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya
Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa
11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe
kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema:
“Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge
hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani
Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya
wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo
kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba
kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe
wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari,
Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya
Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi
(hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata
kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na
kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti
chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher
Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji
Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili
za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye
mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino
Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza
sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo,
naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo
tutakapotangaziwa tena.”
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Dakika-tatu-za-Warioba-mbele-ya-mimbari-ya-Bunge/-/1597296/2248080/-/11ag114z/-/index.html
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, akiondoka bungeni chini ya ulinzi wa askari wa Bunge baada ya vurugu kutokea jana. Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Dakika-tatu-za-Warioba-mbele-ya-mimbari-ya-Bunge/-/1597296/2248080/-/11ag114z/-/index.html
No comments:
Post a Comment