Posted Ijumaa,Marchi14 2014 saa 24:0 AM

Kwa ufupi

Kiasi kilichofichwa kimebaki Sh291.96 bilioni, kinaweza kujenga barabara ya Morogoro hadi Iringa

Dar es Salaam. Mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za Uswisi yameanza kuhamishwa kimyakimya.


Ripoti ya Benki za Uswisi ya 2012 inaonyesha kuwa fedha zinazotoka Tanzania zimepungua kwa karibu Sh.36.4 bilioni ikilinganishwa na zilizokuwapo 2011 nchini humo, lakini haielezi sababu ya kupungua kwake.

Taarifa za kuhamishwa kimyakimya kwa fedha hizo ambazo zinaaminika kuwekwa na Watanzania waliowahi kuwa katika utumishi wa umma, imekuja wakati ambao Serikali inasubiriwa kutoa taarifa yake kuhusu vigogo walioficha fedha nchini humo, ambazo zinaaminika walizipata kwa njia zisizo halali.

Awali, kiasi cha fedha kilichotajwa kufichwa katika benki hizo ni Sh.327.9 bilioni (Dola za Marekani 204.96 milioni), lakini taarifa mpya ya 2012 inaonyesha kuwa kiasi hicho kimepungua hadi Dola za Marekani 182.2 milioni (Sh.291.5 bilioni).

Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi Iringa.

Akizungumzia ripoti hiyo, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema: “Hadi mwisho wa 2012, fedha zilizopo kutoka Tanzania zimebaki Faranga za Uswisi 160 milioni (Dola za Marekani 182.2 milioni) na siyo zile za awali ambazo ni Faranga za Uswisi 180 milioni (Dola za Marekani 327.9 milioni)……. hivyo ndiyo kusema kuwa fedha hizo zinapungua,” alisema Chave na kuongeza:

“Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za nchi nyingine. Sisi Serikali ya Uswisi tunapochapisha ripoti kama hizi kuonyesha jumla ya fedha kwa nchi zote duniani, haimaanishi kuwa fedha zote hizo ni haramu.”

http://www.mwananchi.co.tz/habari/Ki...f/-/index.html