Rais
Jakaya Kikwete akizungumza na wanamuziki wa bendi ya DDC Mlimani Park
'Sikinde' waliotumbuiza hafla ya uzinduzi wa kuchangia ujenzi wa Kituo
cha Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Januari 22, 2011.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, zaidi ya shilingi bilioni 1.6
zilikusanywa katika hafla hiyo ya uzinduzi ambapo Rais Jakaya Kikwete
alichangia jumla ya shilingi milioni kumi.(PICHA NA RICHARD MWAIKENDA).
Yuko na Sikinde, hapa ilikuwa wakati wa bethdei yake ya miaka 60 Oktoba 7, 2010 kwenye Viwanja wa WAMA.
Kama kuna maoni kuhusiana na historia hii, tafadhali nipigie: +255 715 070 109
Yuko na Sikinde, hapa ilikuwa wakati wa bethdei yake ya miaka 60 Oktoba 7, 2010 kwenye Viwanja wa WAMA.
Na Daniel Mbega
JAMANI miye siyo mchokonozi, lakini najaribu kusema kile ambacho
nimekiona katika tafiti zangu za michezo na burudani nchini Tanzania. Kila binadamu
ana utashi wake – wala siyo dhambi, na katika masuala ya burudani yeyote
anaweza kushirika bila kujali wadhifa alionao.
Ukizungumzia kandanda hapa nchini basi unazitaja klabu mbili kongwe –
Simba na Yanga. Hata kama zipo klabu nyingine, lakini dhahiri ni kwamba, ndani
ya wanachama na wapenzi wa klabu hizo nao wamegawanyika kwa kuzishabikia Simba na
Yanga.
Tangu ukoloni timu hizi zimekuwa na wafuasi wengi – kuanzia wananchi wa
kawaida kama akina siye mpaka kwa viongozi – hakuna anayebisha. Hata Mwalimu
Julius Nyerere anatambulika kwamba yeye na Sheikh Abeid Amani Karume walikuwa
mashabiki wa Yanga. Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rashid Kawawa, Samwel Malecela na
wengineo walikuwa mashabiki wa Simba.
Ben Mkapa na hata Rais wetu wa sasa Jakaya Kikwete wanatajwa kwamba ni
mashabiki wa Yanga. Hili linajidhihirisha hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje
katika awamu ya tatu, Rais JK alifanya kazi ya ziada kutulia mgogoro mkubwa
ulioibuka Yanga wakati huo na kuzaa Yanga-Kampuni, Yanga-Asili na
Yanga-Academia.
Kwa upande wa burudani, ambapo kwa miaka mingi tulikuwa tunazithamini
bendi zetu za dansi, nako kulikuwa na ushabiki mkubwa kama ilivyokuwa kwenye
mpira. Zamani zile haikushangaza kuona watu wakishindana kwa bendi za Dar Jazz iliyokuwa
Mtaa wa Kidongo Chekundu na Western Jazz iliyokuwa Kariakoo.
Hata ulipoibuka ushindani wa Marquiz du Zaire na Orchestra safari Sound
au Juwata Jazz na DDC Mlimani Park haikushangaza, maana ilileta raha ya aina
yake.
Kwa hiyo basi, wengi walikuwa wakizishabikia mojawapo ya bendi hizo
kama wanavyoshabikia mpira, ingawa kadiri siku zilivyosonga mbele ushabiki
umepungua na kubaki mapenzi yale ya moyoni tu. Leo hii mtu akisikia wimbo wa
bendi aliyokuwa akiihusudu tangu miaka hiyo, lazima atatikisika kidogo bila
kujali ana wadhifa gani. Siyo dhambi maana mtu anaonyesha hisia zake.
Naam, hili nilishudia mwaka 2008 wakati wa uzinduzi wa maghorofa mawili
ya Shirika la Nyumba la taifa (NHC) pale Chalinze karibu na Msolwa. Bendi iliyokuwa
ikitumbuiza hapo ni DDC Mlimani Park Orchestra wana Sikinde Ngoma ya Ukae.
Muda mfupi kabla ya mgeni rasmi kuwasili, Rais Jakaya Kikwete, bendi
hiyo ilikuwa ikiendelea na kibao chake cha zamani cha ‘Fikirini Unisamehe’,
lakini mara tu baada ya JK kuwasili na kuketi mezani bendi hiyo ikapiga moja
kwa moja kibao cha ‘Mnanionyesha Njia ya Kwetu’ badala ya kile cha mwanzo
kilichokatishwa kwa sababu ya kuwasili wa JK.
Kibao cha Mnanionyesha Njia ya Kwetu’, ambacho ni utunzi wake King
Michael Enoch kilichoimbwa na Cosmas Chidumule, kilipopigwa tu hapo nikamuona mheshimiwa
JK akiinuka mezani kwake na kuanza upiga makofi kwa furaha. Waliokuwepo mezani
nao wakainuka kumuunga mkono.
Maneno ya wimbo huo yanasema: “Mnanionyesha
njia ya kwetu, Huku mnanisimanga kuwa sina changu tena wala faida kwenu x2, Hata
tanga halijaishaa mnaanza kugawana mali, Ya Marehemu Mume wangu ee, Ninapouliza
yamekuaje jibu ni kwamba mnagawana mali ya mwaanenu x2”
Baadaye nikamfuata Hussein Jumbe Totoro, mmoja wa waimbaji wa bendi
hiyo, na kumuuliza kulikoni hawakuendelea na kibao cha ‘Fikirini Unisamehe’,
akaniambia kwamba Mheshimiwa Rais ni shabiki mkubwa wa ‘Nginde’ na anakipenda
zaidi kibao cha ‘Mnanionyesha Njia ya Kwetu’, ndiyo maana waliamua kupiga
mwanzoni kwa vile hawakujua kama wangeweza kupata nafasi baadaye.
Naam. Nikafarijika na miye hasa kwa kuona mtu akishindwa kujizuia
kuonyesha hisia zake katika kitu kinachomvutia, hususan nyimbo kama hizo ama
kibao hicho ambacho kimebeba ujumbe mzito kwa yanayofanyika ndani ya jamii yetu
kuhusu kunyang’anya mali za wajane mara tu wanapofiwa na waume zao.
Kwa kuendeleza tu makala haya naona nizungumze ukweli kwamba, Sikinde
ni moja ya bendi kongwe nchini ikiwa na miaka 35 tangu ilipoanzishwa. Baadhi ya
mnaosoma makala haya hamkuwa mmezaliwa wakati huo.
Lakini bendi hiyo imepitia madhoruba mengi yaliyotishia uhai wake. Ukisikiliza
maneno ya wimbo mmoja wa bendi ya OTTU Jazz wana-Msondo Ngoma usemao Manahodha ni wengi; "Chombo kimeumbika, tena kinapendeza, lakini chaenda
mrama...nikitaka kukiokoa, kina manahodha wengi...," utatambua kwamba,
hicho ni kijembe dhidi ya mahasimu wao wakubwa, DDC Mlimani Park Orchestra.
Ni kijembe kwa sababu, baadhi ya wanamuziki wa Mlimani Park walikuwa
wakijiona wamekomaa na kila mtu kufanya mambo kivyake, hali iliyosababisha meli
hiyo, maarufu kama MV Mapenzi Meli ya Wapendanao, kuwa katika hatihati za
kuzama baharini!
Mbaya zaidi ni kwamba, waamuziki hao hawakuwa wakimtumia vilivyo
mwalimu na mwanzilishi wa bendi hiyo, Michael Enoch Chinkumba, au maarufu kama
King au Teacher, ambaye enzi ya uhai wake alikuwa nguzo ya bendi hiyo.
Na kwa kweli, ingawa bendi hiyo imekuwa na wanamuziki wazuri wanaojua
kutunga na kuimba kwa ustadi, lakini tangu mwaka 1993 walikuwa wakitumia ujuzi
wao tu binafsi, kila mmoja kivyake, kutokana na kinachoelezwa na wengi kuwa ni
chuki binafsi miongozi mwao na kusababisha bendi kupoteza mwelekeo wake
uliotishia uhai wa Msondo Ngoma tangu mwaka 1978 ilipoanzishwa.
Katika miaka ya mwisho ya uhai wake hadi mauti yalipomfika mwaka 2004,
King Enoch ambaye alipooza tangu mwaka 1989, alikuwa msikilizaji tu na siyo
mpangiliaji wa muziki kama ilivyokuwa zamani, na sababu kubwa ni kuwa
wanamuziki wengine walimuona mzee huyo kama hana umuhimu kwa kuwa wao tayari
wanafahamu kutunga na kuimba.
ILIANZAJE SIKINDE?
Bendi hii iliyokumbwa na dhoruba nyingi zilizotishia uhai wake ina
historia ndefu, ikiwa inamhusisha Mzee Michael Enoch, na kwa namna moja ama
nyingine inazihusisha bendi za Dar es Salaam Jazz na Dar International ambazo
mzee huyo alizipigia. (Nimeizungumzia hii katika makala ya King Enoch).
Sikinde ilianza mwaka 1978 ikiwa inamilikiwa na Tanzania Transport
& Taxes Services - TTTS na ilikuwa na wanamuziki kama Cosmas Thobias
Chidumule, Ally Rajabu, Salehe ‘Belesa’ Kakere, Joseph Mulenga (bass), Abel
Baltazar kutoka NUTA Jazz (solo), Michael Enoch (sax), Abdallah Gama (rhythm),
Haruna Lwari (tumba), Saidi (drum), Joseph Bernard (sax), Machaku Salum
(trumpet), Ibrahim Mwinchande (trumpet) na Betto Julius (trumpet).
Wanamuziki wengine waliokuja kuanzisha Mlimani Park ni Muhidini Maalim
Gurumo, Hassan Rehani Bitchuka, Juma Hassan 'Town', Selemani Mwanyiro na
Abdallah Omar 'Dullah' wote kutoka Msondo Ngoma.
Baadaye wakaja akina Hamisi Juma Kinyasi ‘Maalim Kinyasi’, Benno Villa,
Francis Lubua, Max Bushoke, Henry Mkanyia, Michael Bilali, Abdallah Gama, Muharami
Saidi, Mohamed Iddi, Huruka Uvuruge, Julius Mzeru, Habibu Abbas ‘Jeff’,
Chipembere Saidi, Ally Omari, Mashaka Shaban, George Kessy Omojo, Boniface
Kachale, Ibrahim Mwinchande, Machaku Salum, Hamisi Mirambo, Ally Yahya, Joseph
Bernard, na Shaban Lendi.
Wakaibuka na nyimbo tatu za kwanza ambazo zilikuwa Celina piga konde moyo (Joseph Mulenga), Barua kutoka kwa mama (Chidumule), Kassim Kafilisika (Gurumo), Talaka
ya Hasira na Pata Potea (Mulenga)
na Nalala kwa taabu na Penzi la Mwisho (Chidumule).
Mwaka 1983 waliokuwa wamiliki wa bendi hiyo TTTS walifilisika na
hatimaye bendi hiyo ikachukuliwa na Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC)
na hapo ndiyo ikaanza kuvuma kwa jina la DDC Mlimani Park Orchestra.
MADHORUBA YAANZA...
Madhoruba ya kuhamwa na wanamuziki katika bendi hii yalianza rasmi
mwaka 1985, miaka mitatu baada ya bendi hiyo kutwaa ushindi wa Bendi Bora
Tanzania ikifuatiwa na Mwenge Jazz wana-Paselepa iliyokuwa ikiongozwa na Duncan
Njilima.
Wanamuziki Hassan Rehani Bitchuka na Muhidin Maalim Gurumo
walichukuliwa na Hugo Kishimba kwenda kuimarisha bendi ya Orchestra Safari
Sound na kuibuka na mtindo wa ‘Ndekule’. Abdallah Omar 'Dullah' alikuwa
ameondoka mapema kwenda kutafuta maisha Ulaya, lakini baada ya wimbi hilo,
Joseph Mulenga, Abdallah Gama na Shaaban Dede nao wakatimua kwenda Bima Lee
Orchestra iliyotamba na mtindo wa ‘Magnet Tingisha-Magnet Ndere’.
Sikinde sasa ikawa imebakia na waimbaji Chidumule, Hamisi Juma Kinyasi ‘Maalim
Kinyasi’, Maximilian Bushoke, Francis ‘Nassir’ Lubua, Benno Villa Anthony,
Fresh Jumbe na wapiga ala walikuwa Abel Baltazar (solo), Kassim Rashid Kizunga
(solo) na Ally Makunguru (rhythm), Henry Mkanyia (rhythm), Michael Bilali
(solo), Muharami Saidi (rhythm), Juma Mzeru (bass) na Ally Jamwaka (tumba).
Ikatamba na vibao kama Naijibu
Telegramu, Penzi Kileo cha Fikara na Aza
(Max Bushoke), Ziada ya Uvumilivu
(Benno Villa), Mtoto akililia wembe,
Usitumie pesa, MV Mapenzi na Mkataa
pema (Chidumule), na nyinginezo ambazo ziliimarisha hadhi ya bendi hiyo na
kumudu ushindani dhidi ya Msondo Ngoma (JUWATA), Marquis, Kimulimuli, Vijana,
Mwenge Jazz na nyinginezo.
Pigo kubwa zaidi likaja mwaka 1988 wakati wanamuziki Max Bushoke,
Hamisi Juma Kinyasi, Kassim Rashid Kizunga, Chidumule na Fresh Jumbe walipohamia
OSS.
Wakati hao wanakwenda OSS, Gurumo na Bitchuka wakarejea Sikinde walikoungana
na bwana mdogo Hussein Jumbe, Mohammed Hamisi Mwinyikondo, Tino Masenge ‘Arawa’,
Francis Lubua, Huruka na nduguye Fadhil Uvuruge aliyekuwa akipiga gitaa la
rhythm.
Mwaka 1989 Bitchuka na Gurumo wakarejea Msondo Ngoma na kuzidisha
ushindani huku Chidumule naye akirejea Sikinde, na mwaka 1991 Shabani Dede
akajiunga na Sikinde kuungana na Hussein Jumbe, Hassan Kunyata na Adam Bakari
'Sauti ya Zege'.
Mwaka 1994 Sikinde ikakimbiwa na wanamuziki Henry Mkanyia, Tino Masenge
na Julius Mzeru, ambao walikwenda kuanzisha bendi yao, ingawa Tino baadaye
akarejea.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 1999 wanamuziki karibu sita nyota Tino Masenge
'Arawa', Charles John 'Ngosha', Mashaka Shaaban, Abdallah Hemba, Mjusi
Shemboza, Kassim Rashid walikwenda kuanzisha bendi ya Super Sikinde Academia
kwa lengo la kuisambaratisha Sikinde, lakini Super Sikinde ikafa kabla hata
haijarekodi.
Sikinde iko kwenye ushindani, ingawa inajitegemea baada ya ‘kutemwa’ na
Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC), kama ilivyo kwa Msondo Ngoma
iliyotemwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi.
Angalia kibao chao kisemacho Mnanionyesha
Njia ya Kwetu, ukiwa ni utunzi wake King Enoch. Lakini kiliimbwa na Cosmas
Thobias Chidumule alishirikiana na Hassan Rehani Bitchuka, Benno Villa, Hamisi
Juma Kinyasi na Muhidin Maalim Gurumo:
Mnanionyesha njia ya kwetu
Huku mnanisimanga kuwa sina changu
tena wala faida kwenu x2
Hata tanga halijaishaa mnaanza
kugawana mali
Ya Marehemu Mume wangu ee
Ninapouliza yamekuaje jibu ni
kwamba mnagawana mali ya mwaanenu x2
Mbona mmesahau ya kuwa mali hiyo
haswa ni ya watoto
Na msimamizi ni mimi Mama yao
ambae leo mnanikana x2
Chorus
Kama ni mila tuache ooo ooo
tuache kwa sababu
Madhara yake ni makubwa
(Bichuka)
Mlikuwa mkiniita Mkwe ooo Wengine
Shemeji
Wengine wifi ee lakini hayo
mmeyasahau
Kama ni msiba ni wa kwetu sote
(Wote)
Kama ni mila tuache oo oo tuache
kwa sababu madhara yake ni makubwa
(Bichuka)
Wengine huniita Shemeji
Wengine huniita wifi
Wengine huniita Shangazi
[Wote]
Madhara yake ni makubwa
No comments:
Post a Comment