Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
Katika upatikanaji wa kilo 100 za mkaa wachomaji wa mkaa hulazimika kuchoma miti yenye kilo 1000 ili kupata nishati hiyo jambo ambalo linasababisha hasara kubwa na kuteketea kwa misitu.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika shirika la Jumuiko la Maliasili lenye makao yake jijini hapa, Mtemi Zombwe alipokuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake.
Mtemi amesema kuwa iko haja ya serikali na mashirika binafsi kuhamasisha matumizi mbadala ya nishati ili kuokoa misitu.
Mtemi amesema kuwa mfumo uliopo haujawaandaa watu wengi kuona kuwa wanaweza kuishi bila mkaa kwanzia watumiaji, wachomaji na wauzaji suala ambalo ni hatari kwa misitu.
Hata hivyo, ameshauri kuwa elimu itolewe kwa jamii ya watanzania pamoja na juhudi za makusudi za kuhamasisha nishati mbadala ili kunusuru misitu na nishati mbadala.
Pia ameitaka serikali na jamii kwa ujumla kuzingatia sheria na utaratibu katika uvunaji wa misitu ili kuepuka uvunaji holela wa misitu unaopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na upotevu wa mapato kwa serikali.
Amebainisha kuwa sababu kubwa ya uvunaji holela wa rasilimali za misitu ni rushwa kwani baadhi ya watendaji wa serikali wasio waaminifu hupokea na kuwaruhusu watu wachache wavune bila utaratibu na kupelekea watu wachache kunufaika hali inayosababisha wananchi kujichukulia hatua na kuvuna bila utaratibu.
“Hatusemi watu waache kutumia mkaa bali misitu ivunwe kwa utaratibu ili iweze kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo,serikali na mashirika binafsi yaongeze kasi katika kuhamasisha nishati mbadala ili kuokoa misitu,” alisema Mtemi.
No comments:
Post a Comment