Korongo Taji-kijivu.
Korongo Domo-ngazi.
Korongo Mfuko-shingo.
Na Daniel Mbega (Mhifadhi Asilia)
WATANZANIA wa sasa hawachoki kwa visa. Watakwambia
mji una joto au baridi kali, mara watasema foleni zinachosha. Lakini hakuna
hata mmoja anayewaza kubadili mazingira hayo yanayomchosha japo kwa muda.
Naam, sehemu pekee ambayo unaweza kupata
mawazo mapya ni kwa kutembelea hifadhi zetu za taifa, ambazo ziko 16! Huko utakutana
na mazingira ya asili kabisa, upepo mwanana ukivuma usio na vumbi wala moshi wa
magari mabovu ya mitumba, mengi yakiwa ya mikopo ya Saccos.
Tunahitaji japo mara moja kwenye kuangalia
hizi rasilimali zetu ambazo zimeendelea kuwa vivutio vya wageni kutoka nje
kuliko sisi wenyewe. Ni aibu sana.
Hii inatokana na ukweli kwamba, mtaji uliopo
ni wa asili kwani kuna vivutio vingi kama wanyama, ndege, mimea na mbuga nzuri
ambazo macho ya binadamu yeyote anayependa kubadilisha mtazamo wake yangependa
kuvinjari.
Hata hivyo, wananchi wengi wa Tanzania
wameonekana kutokuwa na utamaduni kwa kwenda kutembelea vivutio vyetu vya asili
vya utalii, badala yake wengi wao wako tayari kununua mikanda mingi ya filamu
za Kimagharibi na kupoteza muda mwingi kuangalia.
Hii ni mbaya kwa sababu siyo tu tunawajengea
utamaduni mbovu hata watoto wetu, bali tunaikosesha Tanzania mapato ya ndani
huku tukijenga hisia mbovu kwamba mbuga za wanyama ziko kwa ajili ya Wazungu
pekee, jambo ambalo siyo sahihi.
Tunatambua kwamba watalii kutoka nje wamekuwa
wakivifuata vivutio hivi tunavyovielezea hapa, lakini kwa bahati mbaya wengi
wetu tumekuwa hatuna utamaduni wa kwenda kutembelea wala kuvitazama vivutio
hivyo, hususan katika mbuga za wanyama.
Hatuhitaji kuwa na fedha nyingi sana wala
pasipoti au viza kwenda kwenye mbuga zetu za wanyama, bali kiasi kidogo tu
kinatosha kabisa kutufikisha huko kama gharama za usafiri, chakula na gharama
kidogo tu za kuingilia hifadhini ili kuchangia pato la taifa.
Kwenye hifadhi zetu wamejaa ndege hawa
wanaoitwa Korongo, ambao unaweza kuwaita Storks au Cranes kwa jamii zao.
Korongo
wamegawanyika katika makundi mawili – wale wa familia ya Ciconiidae wanaoitwa
Storks wenye domo refu na nene.
Pia wanafahamika kama Kongoti, hususan korongo mfuko-shingo. Mabawa yao ni
marefu sana ambapo yale ya korongo mfuko-shingo yana urefu wa meta 3.2, ni
marefu kuliko yale ya ndege wote ghairi ya tumbusi wa Andes (Andean condor). Spishi nyingine huishi mahali pa majimaji
nyingine mahali pakavu. Hula vyura, samaki, wadudu na nyungunyungu, hata
ndege na wanyama wadogo. Korongo hawa hawawezi kutoa sauti. Lakini kwa
tago hupiga kelele na midomo yao.
Spishi za korongo wa familia hii ambazo
zinapatikana Afrika ni Korongo Domo-wazi (African Openbill Stork), Korongo
Samawati (Abdim’s Stork), Korongo Mweupe (White Stork), Korongo Shingo-sufu (Woolly-necked
Stork), Korongo Mweusi (Black Stork), Korongo Domo-ngazi (Saddle-billed Stork),
Korongo Mfuko-shingo, Kongoti au Marabu (marabou Stork), na Korongo Domo-njano (Yellow-billed Stork).
Aina ya pili ya Korongo ni wale wa Familia ya
Gruidae wanaoitwa Cranes ambao pia wanajulikana kama Mana. Hawa wana midomo
mifupi na myembamba kuliko wale wa familia ya Ciconiidae. Spishi nyingi
hutembea kwa mikogo na madoido. Madume hubembeleza jike kwa mbwembwe huku
wakitoa sauti kubwa. Wakikubaliana huishi maisha yao yote. Makorongo
hawa hupenda kuwa pamoja na huhama kwa makundi makubwa. Hula kila
kitu kinachopatikana, kama panya, wadudu watambaao, amfibia au samaki,
hata nafaka na matundamadogo. Spishi za makorongo zinatokea mabara yote
ghairi ya Amerika ya Kusini.
Spishi zinazopatikana Afrika ni Korongo Buluu (Blue Crane), Korongo Tumbo-jeusi (Demoiselle Crane),
Korongo Taji-jeusi (Black Crowned Crane), Korongo Taji-kijivu (Grey
Crowned Crane), Korongo Ndevu (Wattled Crane), na Korongo
Paji-jeusi (Eurasian au Common Crane).
Ndege hawa wanaopatikana katika hifadhi zetu nyingi
nchini kitaalamu ama kisayansi wako katika Himaya ya Animalia (Wanyama), Faila
ya Chordata (yaani Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni), Nusufaila ya
Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo), Ngeli ya Aves (Ndege), Oda ya
Ciconiiformes (Ndege kama makorongo), Familia ya Ciconiidae na Gruidae, na
Jenasi mbalimbali kama zilivyotajwa hapo juu.
Jamani, nendeni kwenye mbuga za wanyama
mkatazame vivutio hivi, maana vipo kwa ajili yetu na siyo Wazungu tu peke yao
kuja kuangalia.
* Mwenye
maoni, au anayewajua ndege hawa kwa majina ya kienyeji, anitumie kupitia namba
0715 070109, au e-mail: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment