Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya
Siku ya Haki za Binadamu Duniani, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee
jijini Dar es Salaam,leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Maimuna
Tarishi, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mhe. Makamu wa Rais kuhutubia wakati
wa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani,
yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo Dec 10, 2015. Picha
na OMR
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania,
Joyce Mends-Cole, akizungumza kabla ya Mhe. Makamu wa Rais kuhutubia wakati wa Maadhimisho
ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani, yaliyofanyika kwenye
Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu,
Bahame Nyanduga, wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya
kupokea maandamano ya wananchi wakati wa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku
ya Haki za Binadamu Duniani, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar
es Salaam,leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond
Mushi, wakati wa mapokezi ya maandamano ya wananchi wakati wa Maadhimisho ya
Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani, yaliyofanyika kwenye
Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam,leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na mtoto, Ahana Gloria Massey (5) wakati
alipowasili kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, leo Dec 10, 2015
katika ufunguzi wa maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu
Duniani. Picha na OMR
Baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria
ufunguzi huo wakimsikiliza Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, wakati
akihutubia kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za
Binadamu Duniani, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es
Salaam,leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na
washiriki wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za
Binadamu Duniani, baada ya ufunguzi huouliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee
jijini Dar es Salaam,leo Dec 10, 2015. Picha na OMR
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA NANE YA KITAIFA YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI, UKUMBI WA KARIMJEE - DAR ES SALAAM,
TAREHE 10 DESEMBA 2015
Mhe. Said Meck
Sadick
Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam;
Mhe. Bahame Tom
Nyanduga
Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
Mhe. George
Masaju
Mwanasheria Mkuu
wa Serikali;
Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria;
Mwakilishi Mkazi
wa Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania;
Waheshimiwa
Mabalozi wa Nchi mbalimbali
mliopo hapa;
Viongozi
mbalimbali wa Serikali;
Wawakilishi wa
Asasi za Kiraia;
Wageni Waalikwa;
Waandishi wa
Habari;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na
Mabwana.
Nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha
kukusanyika hapa leo ili kushiriki katika Maadhimisho haya ya Siku ya Haki za
Binadamu ambayo husherehekewa Duniani kote Desemba 10 kila mwaka. Hii ni siku
muhimu kwetu na kwa mataifa mengi duniani.
Niwashukuru pia wale
wote waliofanikisha maadhimisho haya kwa njia moja ama nyingine. Kipekee
niwashukuru Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Ofisi ya Umoja wa
Mataifa Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Nchi za Ulaya Tanzania, asasi za kiraia,
na wadau wengine wote kwa jitihada zao kubwa za kuratibu na hatimaye
kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni
Sana!
Aidha, niwashukuru wale wote
walioshiriki katika maandamano, mmeonesha kuthamini Siku hii ya leo - Nawapongeza Sana!
Ndugu
Wananchi;
Mabibi
na Mabwana;
Leo t unaadhimisha Siku ya Haki za Binadamu
tukikumbuka miaka 67 tangu Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu likubaliwe
na kupitishwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1948. Azimio hilo
limekuwa chimbuko la utetezi wa haki za
binadamu ulimwenguni na heshima ya utu wa mwanadamu katika nchi zote
ulimwenguni zinazotekeleza matakwa ya Azimio hilo. Mikataba mingi ya kikanda na
kitaifa imeridhiwa na nchi nyingi ulimwenguni na misingi ya haki za binadamu
iliyomo kwenye Azimio imeingizwa kwenye katiba za nchi nyingi, ikiwemo
Tanzania.
Kitaifa tumekuwa
tukiadhimisha siku hii kutokana na ukweli kuwa sisi Tanzania ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ambako
ndiko chimbuko la Haki za Binadamu, na kwamba kama Serikali, tunaamini na tunawajibika moja kwa moja kukuza, kulinda
na kutekeleza haki hizo hapa nchini.
Kaulimbiu ya
Kimataifa ya Siku hii ya Haki za Binadamu mwaka huu ni– “Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima” (Our Rights, Our Freedoms Always)
inaakisi hamu ambayo kila mmoja wetu aliyonayo popote pale alipo na wakati
wowote ule ya kuona kuwa haki na uhuru wake kama binadamu unatambuliwa,
unalindwa na kuheshimiwa wakati wote.
Natumaini wote
tutatafakari kaulimbiu hii ya “Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima”
tukijikumbusha kuwa haki za binadamu siyo bidhaa ya anasa bali ni kitu muhimu
katika maisha yetu sote, wanawake kwa wanaume, watoto, vijana wote, wasichana
na wavulana, pamoja na wazee wanahitaji kufurahia uhuru wao na haki zao
kuheshimiwa.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inao wajibu wa kulinda na kukuza uhuru na haki
hizi, kwa kuzingatia misingi iliyopo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ya Haki za Binadamu na
sheria mbalimbali za nchi, katika jitihada zake za kutimiza wajibu huu muhimu,
wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu.
Tanzania
imeridhia mikataba mingi ya kimataifa inayohusu Haki za Binadamu. Baadhi ya
mikataba hiyo ni pamoja na; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za
Ubaguzi wa mwaka 1965; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa
1966; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni 1966;
Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya Wanawake wa
mwaka 1979; Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka
1981; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto 1989; Mkataba wa Afrika wa Haki na
Ustawi wa Watoto wa mwaka 1990, Itifaki ya Afrika ya Haki za Wanawake, (Maputo
Protocol) ya 2003, na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa
mwaka 2008.
Ili kuhakikisha
kuwa ulinzi wa haki za binadamu unaimarishwa, Serikali yetu imekwisha ingiza
baadhi ya mikataba hii katika sheria zetu za nchi, ama kwa kuunda sheria mpya au
kurekebisha zile zilizopo.
Isitoshe,
Serikali imekuwa ikiandaa ripoti za utekelezaji wa Haki za Binadamu kwa mujibu
wa mikataba tajwa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwenye vyombo vya kimataifa
kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya utekelezaji.
Ndugu
Wananchi;
Mabibi
na Mabwana;
Maadhimisho haya
yanatoa fursa nzuri kwetu sote kujiuliza; tumefanya nini katika kipindi cha
mwaka mzima uliopita, changamoto zinazokabili suala zima la haki za binadamu na
tunatarajia kufanya nini siku za usoni. Tunafanya haya yote tukikumbuka kuwa
utekelezaji wa haki za binadamu ni mchakato, hivyo siku zote ni lazima
tuendelee kuboresha haki hizo hatua kwa hatua.
Sisi katika
Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuziwezesha taasisi zinazosimamia
utekelezaji wa sheria na kutoa haki ili kutimiza wajibu wake. Napenda
kuwahakikishia kuwa haki na uhuru wa kila Mtanzania itaheshimiwa, itahifadhiwa
na kulindwa.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na juhudi
kubwa za Serikali kuboresha mazingira ya upatikanaji na utoaji wa Haki za
Binadamu nchini, matukio ya ukiukaji wa haki hizo yameendelea kuongezeka.
Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari na ripoti za kitafiti, zimeonesha na
kuthibitisha uwepo wa matukio kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.
Baadhi ya matukio hayo ni kama yale ya mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye
ualbino, mauaji ya wanawake vikongwe, ghasia zinazohusiana na vurugu za
makundi; Mahabusu kuwekwa rumande muda mrefu kabla ya kesi kusikilizwa,
unyanyasaji dhidi ya wanawake, unyanyasaji wa watoto ikiwemo ukeketaji, ukatili
wa kijinsia, ndoa za utotoni, mauaji kwa wanaozaliwa na ulemavu, utekaji nyara,
ajira mbaya n.k.
Nawahakikishieni
kuwa Serikali imejipanga vema kukabiliana na kutokomeza uovu huo bila kumwonea
huruma mtu yeyote anayejihusisha na maovu hayo.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Mtakumbuka kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imepokea
kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita
kutokana na kutokukamilika mapema kwa uandikishaji wapiga kura. Napenda
kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya
awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba
na Bunge Maalumu la Katiba lililotupatia Katiba inayopendekezwa. Serikali
itatekeleza wajibu wake kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Marekebisho ya
Katiba ya mwaka 2013, na iwapo Katiba inayopendekezwa itapitishwa hapo baadaye, itachangia sana
ukuaji wa haki za binadamu nchini.
Hatua nyingine ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuzichukua ili
kuboresha haki za wananchi nchini kadiri alivyofafanua hivi karibuni Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na
kupambana na rushwa na ufisadi, umaskini,
upungufu wa ajira, kuboresha elimu
na afya.
Tutaendeleza
mapambano dhidi ya ubadhirifu, wizi na ufujaji wa fedha za umma. Yote haya
yatafanyika kwa kuzingatia sheria, na matamko ya haki za binadamu. Mathalani
watuhumiwa kufikishwa kwenye vyombo vya haki ili sheria ichukue mkondo wake
bila ya kumwonea mtu yeyote. Ikumbukwe kwamba ubadhirifu, wizi, rushwa na
ufisadi umechangia katika kudumaza ukuaji wa uchumi na hivyo kuendeleza
umasikini na kuwaacha wananchi walio wengi, kukosa haki za msingi za maisha. Hali hiyo haikubaliki, kwani ikiachiwa
iendelee, itarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Malengo ya
Kimataifa ya Maendeleo Endelevu, (Sustainable Devevelopment Goals), Mpango
ambao umezinduliwa na Umoja wa Mataifa
Septemba 2015, unatarajiwa kuanza rasmi
tarehe 1 Januari, 2016 ukiwa na malengo kumi na saba (17). Mpango huu
unachukua nafasi ya Mpango wa Maendeleo wa Millenia (Millenium Development
Goals) baada ya kufikia tamati.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua elimu ya awali, msingi,
sekondari na vyuo vikuu na kuongeza ubora wa elimu inayotolewa. Serikali
itahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi
kidato cha nne inatolewa bure. Aidha, tutahakikisha wanafunzi wengi zaidi wa
elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati na pia haki za walimu zinaboreshwa kwa
kiwango kinachostahili.
Kwa upande wa huduma za afya,
pamoja na mambo mengine Serikali ya Awamu ya Tano inakusudia kuanzisha na
kuimarisha huduma kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuongeza wataalamu,
kutoa vifaa tiba bora na vya kisasa, kuongeza bajeti ya dawa, kuboresha mfumo
wa upatikanaji wake na kuhamasisha wananchi wajiunge na mifuko ya bima ya afya.
Tunatambua afya
haiwezi kuimarika iwapo wananchi hawapati maji safi na salama, hivyo Serikali ya
Awamu ya Tano itahakikisha inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia
asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya
mijini ifikapo 2020.
Ndugu wananchi,
Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu
kwa kushirikiana na wadau wengine, zikiwemo taasisi za Serikali, taasisi zisizo
za kiserikali na wananchi kwa ujumla.
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nitumie fursa
hii pia kuwaasa Watanzania wenzangu kuanzisha kampeni maalum za kukuza maadili
mema katika ngazi mbalimbali zikiwemo zile za utumishi wa umma, taasisi za
dini, taasisi za elimu na katika nyanja zote za maisha ya kila siku. Suala hili
likifanyika vizuri, naamini sote kwa pamoja, tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kulinda haki za binadamu, kwani bila
maadili mema, itakuwa vigumu kuheshimu utu wa mwanadamu ambao ndio msingi mkuu wa haki za binadamu, na
hivyo kutekeleza kaulimbiu ya Haki Zetu, Uhuru Wetu Daima.
Jukumu la kukuza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu
ndani ya jamii yetu, ni letu sote, mtu mmoja mmoja, familia au kaya, na
Serikali kwa ujumla. Serikali ya Awamu ya Tano
itaendelea kuhakikisha kuwa haki
za binadamu na misingi ya utawala bora
inazingatiwa hapa nchini.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima natamka
kuwa Maadhimisho
ya Nane ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu, yamefunguliwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment