Bandari ya Dar es Salaam ambayo kutokana na ufisadi na rushwa, watendaji wa serikali wanaikosesha mabilioni ya fedha za kodi na ushuru mbalimbali. (Picha ya mtandao).
Na Daniel Mbega
NAKUMBUKA hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere wakati wa Mei
Mosi 1995 pale kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Alisema mambo mengi sana, yote
yenye maana, lakini kubwa ninalolikumbuka leo, alisisitiza umuhimu wa kukusanya
kodi.
Alisema wazi kwamba, hata hao IMF (Shirika la Fedha Duniani)
na Benki ya Dunia, ambao ndio walioshinikiza tuyabinafsishe mashirika yetu ya
umma, walikuwa wanahimiza tukusanye kodi.
Na hawahimizi tukusanye kodi kwa sababu nao wamechoka kutusaidia,
bali ndio wajibu wa serikali yoyote makini, kwani kodi ndiyo chanzo kikuu cha
mapato ya serikali.
Hata hivyo, hili haliko hivyo katika serikali yetu, serikali
iliyojisahau ama kupuuza wajibu wake na kila mmoja aliye madarakani anaona
kwamba jambo la msingi zaidi kwake ni kuangalia maslahi yake, siyo ya umma.
Tunashuhudia kila uchao namna ambavyo maofisa wa serikali
wanavyokumbwa na kashfa mbalimbali za ufisadi, wizi na ubadhilifu katika idara
wanazoziongoza.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilikumbwa na kashfa kubwa
ya kutokusanya kodi kwa magari yanayoagizwa kutoka nje na badala yake watu
wachache wakajinufaisha kwa mamilioni ya fedha zilizopaswa kuingia serikalini,
wakatoa vibali kwa magari yasiyo na viwango.
Tumeshuhudia jinsi vigogo wa Mamlaka ya Bandari
wanavyoitumia bandari yetu kama kitega uchumi chao na familia zao kwa kushindwa
kutoza ushuru wa serikali, badala yake ule wanaokusanya, ambao ni kidogo, nao
unaingia kwenye akaunti zao zilizofurika huko nje.
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) nayo imeendelea kuandamwa na
zimwi la rushwa na ufisadi kwa maofisa wake kujineemesha kwa fedha za umma,
wakikusanya fedha chache kupitia mlango wa nyuma huku nyingi zikiendelea
kubakia kwa wafanyabiashara wenye uroho wa fisi, makupe wanaopenda kufonza
mpaka waone damu imekauka.
Sekeseke lililotokea hivi karibuni la kupitishwa kwa
makontena 349 bila kulipiwa ushuru ni mfano mmojawapo tu wa namna mabilioni ya
kodi yanavyochotwa pale Bandari kwa ushirikiano na TRA.
Tunaipongeza serikali ya awamu hii chini ya Rais John
Magufuli, ambaye ameamua kupambana kuhakikisha kodi za umma zinakusanywa na
wahusika wote wanashughulikiwa.
Aliahidi kwenye kampeni na ameendelea kurudia kauli yake
kwamba lazima apambane na wafanyabiashara wakubwa ‘wasioguswa’ ambao wamekuwa
wakikwepa kulipa kodi, na hii ya sasa pengine ni picha ya utangulizi tu.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 11, Rais Magufuli
alitamka bayana kwamba, ameamua kubana matumizi yasiyo ya lazima pamoja na
kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi. Amefuta safari za ng’ambo zisizo za lazima
ili kubana matumizi ikiwa ni pamoja na sherehe mbalimbali ambazo zimekuwa
zikigharimu mabilioni ya fedha.
“Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa
ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali
ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza
ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili
kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote
atakayekwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila
mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili
kulipa kodi alipe,” alisema kwa msisitizo.
Aliahidi kwamba, serikali yake itahakikisha kila senti
inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora
zaidi kwa wananchi na kwamba wataziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali
ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.
“Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za
Serikali: Kwanza, safari zote
zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini tutazidhibiti na badala yake
tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale
inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba
haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za
kufanya katika safari hizo.
“Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha
zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za
Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika
kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo: Tiketi za ndege zilitumia shilingi bilioni 183.160;Mafunzo nje
ya nchi zilitumika shilingi bilioni 68.612; Posho za kujikimu (Per
Diem Foreign) zilitumika shilingi bilioni 104.552,” alifafanua.
Alizitaja Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari
za nje kuwa ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa
Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa
Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, na kadhalika.
Kwa mdomo wake akasema: “Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri
kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme
n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza
kutengeneza zahanati ngapi? nyumba za walimu ngapi?, madawati mangapi? … Tunapodhibiti
safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na
mtuunge mkono.”
Akabainisha kwamba, atahakikisha anadhibiti
safari na ziara za mafunzo nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo
yanapatikana hapa nchini, lakini pia kudhibiti warsha, semina, makongamano, na
matamasha ambayo yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na
wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya
Serikali.
Inaonekana wazi kwamba Rais Magufuli
amedhamiria, kwani aliahidi pia kusimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya
Umma ili kuhakikisha mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi
hafifu inazibwa huku akisisitiza kusimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na
maelekezo mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu
ununuzi wa bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali.
“Samani zote kwa ajili ya matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe
zile zinazozalishwa hapa hapa nchini,” akasema na kuongeza: “Serikali ya Awamu
ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa
ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa Serikali; na tutaendelea
kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na Taasisi zake zote yasiyo na
tija kwa uchumi wa taifa letu.”
Ni jambo
lililo wazi kwamba, mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa mapato hazikuwajibika
ipasavyo huko nyuma, watumishi hawakuwa waadilifu, wakageuza taasisi kama
visima vya kuchota mali ya umma, matokeo yake yakaifanya serikali ikose mapato
stahiki na kugeuka ombaomba kila siku kutembeza bakuli kwa wahisani ili kukidhi
hata bajeti yake ya kila mwaka.
Walalahoi
ndio waliobanwa na kodi kwa sababu wanakamuliwa katika kila bidhaa wanayonunua,
lakini wafanyabiashara husika, wakiwemo wale wakubwa, licha ya kuwakamua
walalahoi, bado wameendelea kukwepa kulipa kodi hiyo kama wanavyopaswa.
Deni la
serikali linaongezeka kila siku, asilimia arobaini ya bajeti ya serikali
inategemea fedha za wahisani ambao nao hutuwekea masharti ya ajabu ndipo
watupatie fedha hizo. Tukishindwa kutekeleza, basi hatupati.
Mara
kadhaa serikali imenyimwa fedha hizo za bajeti kutoka kwa wahisani, matokeo
yake miradi mingi ya maendeleo inakwama.
Kwa upande
mwingine, tangu tupate uhuru, ardhi ya
Tanzania iliyopimwa, ambayo ndiyo serikali inategemea kukusanya kodi, ni
asilimia moja tu! Haya ni masikhara.
Ufisadi umejaa mno katika sekta ya ardhi. Viongozi wa
serikali ni washirika namba moja wa ufisadi huo ambapo tunatambua namna
walivyojiuzia wenyewe nyumba za watumishi wa serikali kwa bei ya kutupia,
halafu wameingia ubia na ‘wenye fedha’ kujenga mahekalu huku serikali
ikihangaika kuwatafutia watumishi wapya nyumba nyingine. Wizi mtupu!
Naam, nyumba za kule Masaki, Oysterbay, Ada Estate na pale
Kinondoni ambazo zilijengwa kwa ajili ya watumishi wa umma, walijiuzia vigogo
wa serikali, tena kwa bei waliyoipanga wao. Wakati wanajiuzia, sote tulitegemea
wangekaa huko, lakini ajabu ni kwamba, nyumba hizo kwa sasa zimepangishwa na
zinaendelea kupangishwa kwa bei ya kati ya Dola 3,500 na Dola 15,000 kwa mwezi!
Ni kwa mwezi, siyo kwa mwaka.
Nyumba hizi hizi walizojiuzia kwa vijisenti, zimekuwa mradi
mkubwa kwa waheshimiwa hawa, huku serikali ikishindwa kukusanya kodi yake
ambayo kama ingepatikana, ingeweza kuongeza pato la taifa.
Uzembe wa serikali kutokupima ardhi umefanya wananchi wengi,
hasa mijini, kuishi katika maeneo yasiyopimwa, hivyo kuinyima fursa serikali ya
kukusanya kodi. Matokeo yake serikali inaendeleza tabia yake ya kutembeza
bakuli kwa wahisani kuomba fedha za maendeleo badala ya kutumia vyanzo
tulivyonavyo!
Mwalimu Nyerere alisema; “… Serikali corrupt haikusanyi kodi…!” Naam, ndivyo ilivyo serikali yetu katika
awamu tatu zilizopita, ilikuwa corrupt
iliyojaa mafisadi wengi kila idara kiasi kwamba hivi sasa badala ya kuwaza
namna gani tubuni na kusimamia miradi ya maendeleo, tunaanza kutumia gharama
kubwa kuchunguza nani anakwiba sana fedha za umma na mambo kama hayo.
Naamini
kitu kimoja. Kwamba ndani ya serikali wamekuwepo watu makini, waadilifu ambao
wanaishauri vyema serikali kila siku, lakini hawakuwa wakisikilizwa. Zaidi tu
ni kwamba, ukiendelea kujifanya mchokonozi watakutafutia visa, mwishowe
utajikuta uko benchi bila sababu zozote. Ukihurumiwa, utahamishiwa huko ‘Tanganyika’,
ambako kunywa maji yenye viluwiluwi na yaliyo machungu utadhani tunaishi jirani
na Uvinza ni jambo la kawaida.
Kama
serikali haikusanyi kodi na haina utamaduni huo, hivi tunawezaje kujidanganya
na kudanganyika kwamba uchumi wetu umekua? Hizi takwimu za kwenye makaratasi
tunazopewa na watawala wetu zina ukweli kiasi gani?
Maisha ya wananchi yako chini mno, wengi hawana hata uhakika
wa mlo mmoja, huduma za jamii kama maji, afya na kadhalika siyo za kuridhisha –
mwili ukichemka unapewa Dawa Mseto, ukiumwa malaria unapatiwa panadol na mambo kama hayo.
Ndiyo, serikali imejitahidi kuimarisha miundombinu ya
barabara, lakini bidhaa ngapi zinazopitishwa humo ambazo zimetozwa kodi halali?
Maofisa wa TRA mipakani ni mamilionea, biashara za magendo zinaingia na fedha
zinakusanywa kupelekwa mfuko wa kushoto huku serikali ikikosa mapato.
Jambo baya zaidi ni kwamba, kwa ulafi wao Watanzania
wanaletewa bidhaa feki, zenye sumu na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu,
halafu mwisho wa siku tunadanganywa kwamba uchumi wetu umekua! Umekua wapi
wakati watu wachache ndio wamevimba matumbo huku maelfu kwa mamilioni wakiishi
kwa utapiamlo?
Sekta ya kilimo, ambayo kimsingi ndiyo mkombozi wa
Watanzania walio wengi, kwa muda mrefu inatumiwa kisiasa na watawala wetu
wakiwahadaa wananchi kwa nyimbo nzuri, mapambio na ngonjera kwamba wataleta
hiki na kile, lakini hakuna chochote kinachofanyika kivitendo.
Mwisho wa siku asilimia kubwa ya bajeti yetu inategemea
wahisani na mikopo, na kwa asilimia zilizosalia tunategemea tukusanye kwenye
‘pombe na bangi’ tu! Ni aibu!
Tunataka serikali ikusanye kodi.
0656-331974
No comments:
Post a Comment