Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday, 29 December 2015

ZAMU YA KURUDISHA MABILIONI YA VIGOGO YALIYOFICHWA USWISI

Zitto Kabwe, ambaye aliibua kashfa ya vigogo walioficha mabilioni nchini Uswisi.


Na Daniel Mbega
IJUMAA Mei 16, 1997 mara tu baada ya Laurent Kabila kuipindua serikali ya mwanahabari Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za Banga nchini Zaire, alitangaza kutaifisha mali zote za dikteta huyo aliyeitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa miaka 32.
Siku moja baadaye, yaani Jumamosi Mei 17, 1997 serikali ya Uswisi nayo ikatangaza kuzuia mali za Mobutu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa utawala mpya wa Kabila. Hadi kufikia mwaka 2009 mali hizo, karibu Dola 6.7 milioni, zilikuwa hazijarudishwa.
Mali zilizozuiliwa kufuatia uamuzi wa serikali ya Uswisi ni pamoja na hekalu lake lenye vyumba 300 lililokuwa eneo la Savigny pembezoni mwa ziwa huko Lausanne, ambalo kwa wakati huo thamani yake ilikuwa Dola 5 milioni. Hili lilikuwa miongoni mwa vitegauchumi vyake vingi barani Ulaya ambako ilielezwa vyote kwa pamoja vilikuwa na thamani ya takriban Dola 37 milioni kwa wakati huo.
Ingawa kulikuwa na taarifa kwamba Mobutu alikuwa ameficha karibu Dola 4 bilioni, lakini serikali ya Uswisi ilichunguza katika benki zote 400 nchini humo na haikuona fedha zozote zilizowekwa kwa jina lake au jina la wanafamilia wake.
Taarifa iliyotolewa na taasisi ya Transparency International kupitia Bribe-Payers Index ilieleza kwamba, Mobutu na Mohammed Suharto wa Indonesia na Ferdinand Marcos wa Ufilipino kwa pamoja walifisidi nchi zao jumla ya Dola 50 bilioni, kiasi ambacho kwa wakati huo kilikuwa sawa na bajeti nzima ya mwaka ya misaada kutoka nchi wahisani.
Suharto alikomba takriban Dola 35 bilioni katika kipindi cha utawala wake wa miongo mitatu kabla ya kupinduliwa wakati ambapo Mobutu yeye alichota nusu ya Dola 12 bilioni za misaada ambazo zilitolewa na Shirika la Fedha Dunia (IMF) kwa kipindi chote cha utawala wake na kuifanya nchi hiyo ibaki na madeni makubwa hadi sasa.
Joseph-Desiré Mobutu, kama alivyoitwa kabla ya kutawala Zaire, ambaye alithubutu kulipa Dola 10 milioni kwa mabondia Muhammad Ali na George Foreman (Dola 5 milioni kila mmoja) ili wakapigane jijini Kinshasa Oktoba 30, 1974, hakuona shida kutumia fedha hata kwenda kufanya ‘shopping’ Ulaya na ndiye rais pekee Afrika kutumia midege mikubwa na ghali zaidi duniani, Concorde.
Mwaka 1989, Mobutu alikodi dege la Concorde lenye namba za usajili F-BTSD kutoka Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) kwa ajili ya safari ya Juni 26– Julai 5 kwenda kuhutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Julai 16 akakodi dege hilo kwenda Paris, kuhudhuria sherehe za Ufaransa baada ya kualikwa na Rais François Mitterrand, Septemba 19 akakodi dege hilo kutoka Paris hadi mjini Gbadolite, Zaire na safari nyingine ya moja kwa moja kutoka Gbadolite hadi jijini Marseille akiwa na kwaya ya vijana wa Zaire.
Kwa kutumia fedha za Wazaire, aliamua kujenga uwanja maalum mjini Gbadolite, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko alikotokea, ili kuliwezesha dege la Concorde kutua na kuruka.  Uwanja huo uliokuwa kwenye kilele cha meta 460 kutoka usawa wa bahari, njia yake ya kurukia ilikuwa na urefu wa meta 3,200 (kilometa 3.2) na upana wa meta 60.
Lakini kama tulidhani zama za akina Mobutu, Suharto na akina Marcos zimekwisha, tutakuwa tunajidanganya, kwa sababu hivi sasa bado viongozi na maofisa wa kawaida wa serikali zetu, hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, wanaendelea kukomba fedha za wananchi na kuzificha ughaibuni – mara nyingi wakitumia majina ya washirika wao kwa kuhofisa yasiwapate kama yaliyowakumba wengine.
Kwa miaka kadhaa sasa tumeelezwa kwamba wapo vigogo wengi wa Tanzania – viongozi wa serikali, wanasiasa, wafanyabiashara na hata viongozi wa dini – ambao mbali ya kumiliki mahekalu ughaibuni, pia wameficha mabilioni huko ng’ambo.
Wapo ambao majina yao yamekuwa yakitajwa kwa minong’ono, lakini kuna wale ambao licha ya kuanikwa hadharani, baadhi yao wamewahi hata kutoa kauli za kejeli kwamba “ni vijisenti tu”, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Andrew Chenge, mwaka 2008 baada ya kubainika kwamba alificha karibu Dola 1 milioni huko Uingereza.
Taarifa zinasema, orodha iliyopo ni ya Watanzania walioficha zaidi ya Dola 3.5 milioni kila mmoja, ambapo inaelezwa kwamba fedha nyingi za wanasiasa zimewekwa na makampuni ya nje yenye shughuli Tanzania.
Katika majina ambayo yamekuwa yakinong’onwa, wamo vigogo waliopata kuwa mawaziri katika serikali zilizopita, lakini pia Julai 2015, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika mkutano wake jijini Dar es Salaam, alitoa orodha ya Watanzania 99 wenye asili ya Kiasia ambao wameficha takriban Dola 114 milioni katika benki ya HBSC nchini Uswisi wakitumia akaunti 288.
Inafahamika kwamba Uswisi ni ‘kisiwa’ salama kwa watu kuficha fedha zao kutokana na mfumo na sheria za kifedha za nchi hiyo, ambapo wahusika hawaulizwi ‘maswali ya ajabu’ wanapotaka kufungua akaunti zao, hali ambayo inafanya hata fedha chafu zote zihifadhiwe huko.
Kati ya waliotajwa na Zitto, wapo wafanyabiashara ambao wametajwa katika kashfa nyingi za mikataba inayoendelea kulitafuna taifa hadi sasa, zikiwemo kashfa za ufisadi za EPA, Richmond, na mikataba ya Radar, ununuzi wa ndege na magari ya jeshi na kadhalika.
Swali ni kwamba, vyombo husika vina taarifa? Kama taarifa zipo, zimefanyiwa kazi? Kama kazi imefanyika, matokeo yake yakoje? Ikiwa havina taarifa, viko hapo vinafanya nini? Kuna umuhimu wowote wa kuendelea na vyombo hivyo kama haviwezi kufuatilia hata minong’ono na kuchunguza kama minong’ono hiyo ina ukweli wowote?
Jibu ni kwamba taarifa zipo. Kama ilivyo kawaida ya nchi hii, hakuna anayejali. Lakini hapana, wanajali sana. Tatizo ni kwamba, hata huyo anayetakiwa kushughulikia wahusika, naye ni mhusika. Hapo ndipo penye tatizo.
Julai 2012, Benki Kuu ya Tanzania kupitia kitengo chake cha Financial Intelligence Unit (FIU) ilisema kwamba imeanza kuchunguza madai ya Watanzania walioficha fedha Uswisi kama wanavyofanya wenzao wa mashirika ya kijasusi ya CIA (Marekani), MI6 (Uingereza), RAW (India), DGSE (Ufaransa), FSB (Urusi), ISI (Pakistan), Mossad (Israel) na MSS (China), ambayo yamekuwa yakifuatilia nyendo za fedha haramu hasa za kighaidi dunia.
Inaelezwa kwamba, fedha nyingi kati ya hizo zilizofichwa huko zinadaiwa kutokana na biashara zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Serikali ya awamu ya nne kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mwaka 2012 ilianza kuwachunguza baadhi ya mawaziri wake pamoja na wabunge kutokokana na kujilimbikizia mali nyingi tofauti na kipato chao halali, lakini hakuna matokeo yoyote yaliyowekwa hadharani.
Ripoti ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008 ilionyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la kiasi cha fedha kinachotoroshwa katika nchi mbalimbali duniani kutoka Dola za Marekani 1.06 trilioni za mwaka 2006 hadi kukaribia Dola 1.26 trilioni za mwaka 2008.
Katika kiasi hicho cha fedha, wastani wa Dola 725 bilioni hadi 810 bilioni zilitoroshwa kwa mwaka tangu mwaka 2000 hadi 2008 kutoka katika nchi zinazoendelea.
Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini zinaongoza kwa asilimia 24.3, nchi zinazoendelea za Ulaya asilimia 23.1, Afrika asilimia 21.9 na Asia asilimia 7.85.
Miaka mitatu iliyopita Benki ya Dunia (WB) ilianzisha mpango wa Kurejesha Mali na Fedha Zilizoibwa (Stolen Asset Recovery Initiative - StAR), juhudi ambazo zinafanywa kila nchi na taasisi kama BoT.
Ni wakati muafaka sasa kwa serikali ya awamu hii kulivalia njuga suala la mabilioni hayo ya Uswisi, wahusika wahojiwe walivyoyapata, kama hakuna majibu ya kuridhisha, wataifishwe kwa sababu huo ni uhujumu uchumi.

0656-331974


No comments:

Post a Comment