Profesa Sospeter Muhongo siku alipojiuzulu Januari 24, 2015
Na
Daniel Mbega
UTEUZI wa Baraza la Mwaziri umepokelewa kwa
hisia tofauti ambapo wapo wanaosema Rais Dk. John Magufuli amekosea kuwateua Profesa
Sospeter Muhongo na Dk. Harrison Mwakyembe.
Wanaokosoa uteuzi wa mawaziri hao wawili
kuwemo kwenye baraza wanawahusisha na ufisadi, hali wanayosema inaweza isilete mabadiliko
ambayo yalianza kuonekana katika serikali ya awamu ya tano.
Prof. Muhongo anahusishwa na kashfa ya
uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow wakati Dk. Mwakyembe anahusishwa
na ununuzi wa mabehewa mabovu ya TRL kutoka India.
Lakini Prof. Muhongo, ambaye amerejeshwa
kwenye Wizara ya Nishati na Madini, ndiye anayeonekana kuwaumiza vichwa wengi,
kwani uteuzi wake umezua mjadala mkubwa kila mahali.
Wanaopinga uteuzi wake wanasema waziri huyo
alilazimishwa kujiuzulu na Bunge kufuatia kashfa hiyo ya Escrow, katika
wanashindwa kutambua kwamba, kujiuzulu kwake kulikuwa kwa uwajibikaji wa
kawaida katika kutuliza hali ya hewa iliyokuwepo baina ya Bunge na Serikali.
Prof. Muhongo alijiuzulu Januari 24, 2015. Lakini kiuhalisia, hakutuhumiwa
ufisadi wowote kwenye kashfa ya Escrow, bali ni kuhusishwa na uamuzi mbovu.
Kilicho dhahiri hapa ni kwamba, wanaompinga
wote ‘wanasingizia’ tu kashfa ya Escrow, lakini hawataki kusema kurudi kwa
Muhongo pale Nishati na Madini ni kuendelea kuiziba mianya yote ya rushwa
iliyokuwa imetamalaki.
Inafahamika namna vitalu vya mafuta na gesi
vilivyozua mvutano mkubwa tangu Muhongo alipoichukua wizara hiyo kutoka kwa
William Ngeleja na jinsi alivyosimamia suala la ugawaja wa vitalu hivyo.
Wafanyabiashara wazawa walilalamikia
msimamo wake usioyumba katika mafuta na gesi, wakapiga kelele nyingi kwamba
wanabaguliwa, lakini kwa kuzingatia maslahi ya taifa, Muhongo akasema lazima
utaratibu ufuatwe na siyo kugawa tu vitalu hivyo kwa sababu ya uzawa ambao
hautaweza kuinufaisha nchi.
Yalifichuka mambo mengi yaliyokuwa
yamefichwa, kwamba wapo wafanyabiashara wazawa ambao walitaka kujilimbikizia
vitalu vya gesi na mafuta wakati uwezo wao ni mdogo, kumbe wanataka watumie
umiliki huo kufanya udalali na wawekezaji wa nje.
Kama hawana uwezo, ni kwa nini basi wawe
madalali? Si afadhali serikali iingie moja kwa moja mikataba na wawekezaji hao
wageni wenye uwezo kuliko kuwaacha wajanja wachache waanze ‘kupiga dili’ kwa
rasilimali za wananchi? Tatizo liko wapi?
Inafahamika kwamba wapo wafanyabiashara
ambao wamejilimbikizia vitalu vya uchimbaji madini, lakini kwa miaka nenda
rudi, hawajawahi kuchimba badala yake wanatafuta wawekezaji wageni ili waingie
nao mikataba. Unafanyaje udalali kwa mali ya umma kwa sababu tu una uwezo wa
kupenya na kujipatia mikataba hiyo?
Prof. Muhongo aliguswa
guswa tu kwenye kashfa ya Escrow, hakuhusika. Lakini ugumu alioupata wakati
ule, na ambao kuna uwezekano atakabiliana nao sasa, ni kuwepo hata kwa maofisa
wa serikali wanaotumiwa na wafanyabiashara hao kuhujumu juhudi za serikali
katika sekta ya mafuta na gesi.
Watumishi hao wasio
waaminifu wanaihujumu serikali kwa manufaa yao binafsi, jambo ambalo haliwezi
kuleta maendeleo kwa taifa, hivyo sasa wameunganisha juhudi na ‘wapiga dili’
wanaokwenda kwa mwamvuli wa wafanyabiashara ili kumkataa Muhongo.
Prof. Muhongo siyo
mwanasiasa na kimsingi amerudishwa pale ili kulinda mikataba ya gesi, mafuta,
madini na dili zote za tanesco. Hajarudi kwa bahati mbaya.
Katika serikali ya Dk.
Magufuli inayowataka watendaji na siyo wanasiasa wapiga dili, Muhongo ni chaguo
sahihi kwa sababu licha ya utendaji wake, yeye ni mtaalamu wa mambo hayo na
alidhihirisha hayo katika kipindi alichokaa wizarani hapo.
Zile dili za kuzima ovyo
umeme ili watu wauze majenereta zilikufa katika kipindi chake na haukushuhudiwa
mgao wa ajabu wa umeme.
Wakati alipokuwa
madarakani, Mradi wa Nishati Vijijini (REA) ulikuja kwa kasi, lakini tangu
alipoondoka mradi huo umezorota, hivyo kwa asilimia kubwa kurejea kwake
kutawanufaisha wananchi wa vijijini wakiwemo wa kule Kamsamba wilayani
Sumbawanga na kwingineko nchini ambao wanaonekana wako kisiwani kutokana na
jiografia ya maeneo hayo.
Katika zama ambazo Tanzania
imeshuhudia mikataba ya mibovu sana ya madini iliyohusisha kampuni kama
Meremeta, Tangold, TanzaniteOne, Buzwagi na mingineyo, pamoja na kuchotwa kwa
mchanga wa dhahabu na kusafirishwa Ulaya ili ukasafishwe, tunahitaji mtu kama
Muhongo ambaye anaweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli kuondoa uchafu huo.
Wale wanaolalamikia uteuzi
wa Muhongo, pengine walitaka watu wao ndio washike wizara hiyo, lakini kwa
staili ya Magufuli, hakuna mwanya wa kujipenyeza kwenye kufanya ‘ushawishi’
(lobbying) kama ilivyokuwa huko nyuma.
Mambo ya ‘kumshawishi’ Rais
amteue fulani kwa maslahi ya wachache hata kama hana uwezo ndiyo yamesababisha
utawala unayumba kwa sababu watu wamekuwa wakiangalia sura badala ya utendaji,
matokeo yake tunawaweka wapiga dili watupu.
Wanaolalamika wanajua
kwamba hawatakuwa na nafasi ya kumwita hoteli Prof. Muhongo ili wasaini
mikataba ya kulifilisi taifa, hivyo wanaona ndoto zao zimeyeyuka.
Kuna kila dalili kwamba,
mikono ya mafisadi hata sasa inaweza kutumika kukwamisha utendaji wa Muhongo,
kwani hata watendaji wake wa chini wanaweza kutumika kumhujumu.
Hata hivyo, ni afadhali
asiyeweza kazi, ama aliyeizowea kazi, akaondoka mwenyewe kwa sababu Tanzania ya
sasa inahitaji mabadiliko chanya ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ndoto
ambazo zilipotezwa na tamaa ya baadhi ya watendaji waliopita.
Rais Magufuli ana makusudi
yake, siyo maamuma, na tusubiri tuone kitakachotokea badala ya kulalamika na
kwa wale wanaompinga Muhongo, naweza kuwaambia kwamba hawana namna zaidi
kukubali matokeo kwani ‘msiyempenda kaja’!
0656-331974
No comments:
Post a Comment