Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), iliyo chini ya Pan Africa Power Solutions (PAP), Bw. Harbinder Sethi (Kushoto), akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) maboresho yaaliyofanyika katika kiwanda hicho tangu PAP ilipochukua uongozi wa IPTL. Wakishuhudia ni baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya IPTL.
Na
Daniel Mbega
ACHANA na Shs. 240 bilioni
za akaunti ya Tegeta Escrow, tunazungumzia mabilioni ambayo Serikali imeilipa
kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa miaka
20.
Mkataba wake umekwisha
mwaka huu 2015 kwa staili ya aina yake, ukitanguliwa na wakubwa kugawana
mabilioni yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow, huku wengine
wakiziita fedha hizo kwamba ni ‘za mboga’.
Jambo linalotia simanzi ni
kwamba, licha ya wakubwa hao wakiwemo wa Ikulu, kugawana mabilioni hayo, lakini
mkataba wake pia ulikuwa na utata mkubwa tangu awali, huku ukiliingiza taifa
katika hasara kubwa kwa miaka yote 20, hali inayowalazimu Watanzania waiombe
Serikali ya Awamu ya Tano ipitie ripoti zote za mradi huo na kuwawajibisha
wahusika wote kwa sababu wanafahamika.
Taarifa zilisema kwamba,
baadhi ya mawaziri waliotajwa pamoja na watendaji wengine serikali walipewa
rushwa ya Dola 200,000 kila mmoja ili kufanikisha, lakini wapo wengine
wazalendo, akiwemo Patrick Rutabanzibwa aliyekuwa Kamishna wa Nishati wakati
huo, ambao walikataa rushwa hiyo.
Wakati mkataba huo unasainiwa
mwaka 1995 ili IPTL izalishe umeme wa megawati 100 na kuliuzia Shirika la Ugavi
wa Umeme Tanzania (Tanesco), Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa Andrew Chenge
wakati Waziri wa Maji, Nishati na Madini alikuwa Jakaya Kikwete, rais mstaafu
wa awamu ya nne.
Kwa mujibu wa mkataba huo,
IPTL ilijenga mtambo wa SSD Tegeta jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola
163.5 milioni.
IPTL ilianzishwa mwaka 1994
ikiwa ni kampuni ya ubia baina ya Mechmar Corporation ya Malaysia iliyokuwa na
hisa 70% na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited inayomilikiwa na
mzawa James Rugemalira iliyokuwa na hisa 30%.
Mchakato wenyewe wa
kuipatia zabuni IPTL ulitandwa na rushwa kubwa na pamoja na ushauri kutolewa na
wataalamu wa uchumi, bado viongozi wa serikali waliamua kuipatia zabuni hiyo
bila hata kurekebisha baadhi ya vipengele kama ilivyoshauriwa.
Ripoti ya Profesa Mark
Mwandosya, wakati huo akiwa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Taasisi ya Nishati,
Mazingira, sayansi na Teknolojia (CEEST – Centre for Energy, Environment,
Science and Technology) kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, iliyowasilishwa kwa Rais Benjamin Mkapa Januari 1998 ilibainisha kuwepo
kwa rushwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kiserikali katika kuipatia IPTL
mradi huo mkubwa.
Katika ripoti hiyo ambayo
haijawahi kuwekwa hadharani kutokana na kuwagusa moja kwa moja vigogo wa
serikali, wakiwemo mawaziri wanne waliokuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu
pamoja na mbunge mmoja, ilielezwa kwamba rushwa hiyo ndiyo iliyowafumba macho
watendaji wa serikali na hivyo kuliingiza taifa mkenge katika mzigo huo mkubwa.
Kulingana na mkataba huo,
Serikali/Tanesco ilikuwa inailipa IPTL Dola za Marekani 2,865,920 kila mwezi
ambazo kama zitakokotolewa kwa thamani ya Shs. 1,500 kwa Dola moja kama
ilivyokuwa miaka mitano iliyopita, ni sawa na Shs. 4,298,879,847 (bila Kodi ya
Ongezeko la Thamani – VAT) hali inayomaanisha kwamba, katika kipindi cha miaka
20, Tanzania imekamuliwa jumla ya Dola 687,820,800 (kwa kiwango cha miaka
mitano iliyopita, ni sawa na Shs. 1,031,732,000,000).
Inaelezwa katika ripoti
hiyo kwamba, Wamalaysia walipowasili tu nchini, baada ya muda mfupi walipata baraka
za kuanza kazi kwa kuwa inaaminika walitumia mwanya wa kufahamiana na ‘wakubwa’
kurahisisha kukubalika kwa IPTL.
Ripoti hiyo inaeleza
kwamba, unzishwaji wa IPTL ulikuwa wa mashaka kwa sababu ilikosa ‘chanzo’ cha
maana cha kupewa kazi hiyo kubwa, ikawa inabainishwa kwamba ‘mwenyeji’ wake
hapa nchini, Rugemalira alikuwa na ufahamu mkubwa wa ‘kunusa’ mahali pa kupata
fedha nyingi.
Aidha, ripoti inasema
kukubalika na hatimaye kupewa kazi kwa IPTL kusingewezekana kama siyo kwa njia
nyingine zilizojificha.
Itakumbukwa kwamba, taasisi
ya Decision Strategies Fairfax International (DSFX) ya Marekani nayo ilieleza
kutokana na ripoti ya Mwandosya kwamba, profesa huyo alibainisha namna baadhi
ya viongozi wa serikali wasivyokuwa waaminifu.
DSFX ilipewa kazi na
Serikali ya Rais Mkapa kupitia upya mradi mzima wa IPTL na kwa kushirikiana na
Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB wakati huo – sasa PCCB) ilibainisha kwamba baadhi
ya watendaji wa serikali, wakiwemo mawaziri, waliwezesha IPTL kupata zabuni
kubwa ya kufua umeme ulioelezwa kuwa wa dharura na kwamba walipewa rushwa ili
kufanikisha kazi hiyo.
Licha ya taarifa zote hizo
za uchunguzi na ushauri wa wataalamu wa uchumi, sheria za mikataba na wahandisi
wa nishati, lakini serikali ilipuuza na hakuna kilichofanyika zaidi ya ripoti
hiyo kuwekwa kabatini.
Mwaka 2002 suala hilo
lilitua mikononi mwa PCB, na taarifa za baadaye zikasema tayari faili
limepelekwa Polisi kwa ajili ya kushughulikiwa kisheria, ikiwemo kuwafikisha
mahakamani wahusika, lakini mpaka nukta hii hakuna kilichofanyika.
Mtiririko mzima wa mchakato
mzima hadi IPTL ikapewa mkataba wa kuzalisha umeme ghali upo, umeandaliwa
vizuri, umehifadhiwa na unafahamika kwa viongozi wengi wa juu serikalini.
Mwanzoni
mwa 1992
Tanzania inakabiliwa na
uhaba wa umeme kutokana na ukame ulioikumba na kukausha maji katika mabwawa ya
kuzalisha umeme. Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi
inaanza kupitia mapendekezo kadhaa ya wataalamu kuhusu namna ya kukabiliana na
tatizo hilo.
Novemba
1994
IPTL, kampuni iliyosajiliwa
Tanzania kwa ubia kati ya Mechmar Corporation ya Malaysia na VIP Engineering
and Marketing Limited ya Mtanzania James Rugemalira, inapeleka mapendekezo ya
kutatua tatizo la umeme kwa kuanzisha mradi wa haraka wa kufua umeme.
Desemba
1994
Wawakilishi wa Mechmar wanaitembelea
Tanzania na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Tanzania
inayowakilishwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Maji, Nishati na
Madini, Tanesco na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wakati huo Andrew Chenge.
Januari
1995
Wizara ya Maji, Nishati na
Madini inapeleka mapendekezo katika kikao cha Kamati ya Ufundi ya Baraza la
Mawaziri (IMTC) na kupendekeza IPTL ipewe zabuni. IMTC inakataa mapendekezo ya
Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kuwa yalikosa tathmini ya kifedha na
kiuchumi kuhusu mradi huo. Baada ya uamuzi wa IMTC, Tanesco chini ya Mkurugenzi
Mtendaji wake wakati huo Baruany Luhanga inaipa zabuni kampuni ya Economics
International ya London, Uingereza kufanya tathmini ya kina kuhusu mradi huo
kifedha na kiuchumi. Economics International inasema mkataba utakuwa ni gharama
kubwa kwa serikali ingawa inapendekeza IPTL itekeleze mradi. Economics
International ilipendekeza vipengele vya mkataba vifanyiwe tathmini ya kina
kabla ya kufanya mkataba wowote.
Mei
3, 1995
Bila kuzingatia ushauri wa
Economics International juu ya masuala ya uchumi, Baraza la Mawaziri
linapitisha uamuzi kuwa mkataba utiwe saini kama ulivyowasilishwa awali.
Mei
26, 1995
Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco inapitisha mkataba baada ya kupewa idhini na uongozi wa Wizara ya Maji,
Nishati na Madini. Mkataba wa kifisadi ulioliumiza taifa kwa miaka 20
mfululizo.
Julai
16, 1996
Wizara ya Nishati na Madini
chini ya Waziri Dk. William Shija inatoa leseni kwa IPTL na Tanesco
zishirikiane kuwaumiza watumiaji umeme kwa kuongeza gharama.
Februari
1997
IPTL inaweka mkataba wa
kiufundi na kampuni iitwayo Stork-Wartsila ya Uholanzi. IPTL inakiuka vipengele
vya mkataba na Tanesco/Serikali kwa kufunga mitambo ya kufua umeme wa bei ghali
inayotumia kasi ya kati (Medium Speed Diesel – MSD) badala ya kasi ndogo (Slow
Speed Diesel – SSD) iliyokubaliwa katika mkataba. IPTL inafanya hivyo bila hata
kuitaarifu Tanesco wala serikali.
Septemba
1997
Rais Benjamin Mkapa
anaagiza mkataba wa IPTL upitiwe upya na kuagiza Wizara ya Nishati na Madini
kuanza majadiliano na wawakilishi wa IPTL.
Oktoba
13, 1997
Baraza la Mawaziri
linapitisha uamuzi kwamba IPTL izingatie vipengele vyote vya mkataba na kuuza
umeme kwa bei nafuu.
Januari
1998
Ripoti ya upitiaji upya
mkataba huo inawasilishwa kwa Rais Mkapa na kubainisha kwamba kulikuwa na
rushwa na ukiukwaji wa maadili katika kuipatia IPTL zabuni.
Machi
1998
Tanesco inapewa kibali cha
serikali kuipa notisi IPTL kuhusu ukiukwaji wa mkataba. IPTL nayo inafungua
madai Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ikidai Tanesco iendelee kulipa gharama
za umeme kila mwezi na kushinda, lakini uamuzi wa kesi ukasogezwa Mahakama ya
Rufaa. Baadaye shauri linavuka mipaka ya nchi na kuamuliwa katika mahakama ya
kimataifa iitwayo International Centre for the Settlement of Investment Disputes
(ICSID) iliyoko London, Uingereza baada ya IPTL kushindwa kutoa vielelezo vya
kuthibitisha madai yake.
Februari
2001
ICSID inatoa uamuzi kuwa
IPTL ilionewa kkidogo na kwamba Tanesco ilitambua mabadiliko ya vipengele vya
mkataba kutoka matumizi ya mitambo ya SSD hadi mitambo ya MSD.
2002
hadi 2013
Mbia wa IPTL – VIP
Engineering and Marketing Limited ya Tanzania inafungua kesi ya madai Mahakama
Kuu ikitaka kufungwa kwa kampuni ya IPTL. Hata hivyo, kesi hiyo ikarushwa tena
hadi London kwa majaji wa Labour Court of International Arbitration (LCIA).
Wabia wa IPTL kutoka
Malaysia, Mechmar Corporation wanasema uamuzi wa VIP Engineering ni ujanja tu
wa kutaka kupandisha thamani ya hisa zake ndani ya IPTL.
Serikali ya Tanzania
inaamriwa kulipa Dola 30 milioni kila mwaka kwa IPTL hadi mwaka 2015 ambazo zinawekwa kwenye
akaunti maalum ya Tegeta Escrow. Wamalaysia wanakataa kata kata kuuza mitambo
yao ya IPTL kwa Tanesco au serikali kwa sababu za wazi kwamba walikuwa wanafaidi
uhondo wa mamilioni hayo.
Wizara ya Nishati na Madini
chini ya Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete inaamua kunyamazia
suala hilo.
Mwaka 2013 VIP Engineering
inashinda kesi, ndipo ufisadi mkubwa wa Shs. 240 bilioni kutoka akaunti ya
Tegeta Escrow unafanyika, tena bila kuzingatia sheria za usimamizi wa fedha.
2014
Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi) David Kafulila, anatoa hoja binafsi Bungeni kuhusu ufisadi wa
akaunti ya Tegeta Escrow. Anapingwa lakini baadaye hoja hiyo inashika nguvu na
kuikisa serikali.
Januari
2015
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anajiuzulu kufuatia kashfa hiyo. Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akafukuzwa kazi
baada ya kupokea Shs. 1 bilioni kutoka kwa Rugemalira huku maelezo yake
yakishindwa kujitosheleza, lakini yeye akasema hizo zilikuwa ‘fedha za mboga’.
0656-331974
No comments:
Post a Comment