Mraghibishi Alex John maarufu kwa jina Mafuriko akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Herieth Makwetta alipotembelea kijijini hapo
Na Krantz Mwantepele, Geita
“Huku tupo tu
tunahangaika na kilimo, tunalima kila mwaka, lakini ukweli ni kwamba kilimo
chetu wala hakina faida basi tu bora siku ziende”.
Lilikuwa ni jibu toka
Alex Jonh maarufu kwa jina la “Mafuriko” mmoja wa wanaharakati na waraghbishi
wa kijiji cha Lugunga, kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita baada ya
kuulizwa swali kuhusu maendeleo ya kijiji chao na mmoja wa waandishi wa habari
za mitandao Ali Masoud maarufu kwa jina la Kipanya.
Kijiji hiki kina wakazi
wanakadiriwa kuwa na wakazi 3,685 wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo wadogo.
Kilimo kinaajiri karibu 75% ya wakazi wa vijijini. Lakini ni ukweli pia, ni
kilimo ambacho bado kinategemea jembe la mkono na mvua na hivyo kuathiri sekta
hiyo kwa kiasi kikubwa. Tukiacha hiyo pia upatikanaji wa pembejeo kwa mifumo
iliyomo kwenye sera ya kilimo, bado ni changamoto kubwa.
Waraghbishi wengi ni
wakulima, ingawa wapo pia walimu, viongozi wa dini, wenyeviti wa vijiji, na
watendaji wa kata lakini ukweli unabaki kwamba wengi wao wanategemea
kilimo. Changamoto wanazokutana nazo wakulima ndiyo sababu inayopelekea kilimo
kutokuwa cha faida hali inayowakatisha tamaa na kusema bora liende.
Akielezea masikitiko
yake kuhusu hali yetu, mraghbishi Alex John ama Mafuriko anasema:
“Ndugu zangu sisi huku
tumesahaulika kabisa, kilimo chetu tunacholima ni kilimo cha bora liende maana
hatuna kabisa elimu yoyote hapa kijijini. Kila mtu analima na kupanda anavyojua
maana tumeshazoea maisha ya hivi.”
Katika ufafanuzi wake
Mafuriko ameendelea kusema kuwa kijiji chao kina ardhi yenye rutuba na
inayokubali mazao mengi yakiwemo mahindi, maharage, mpunga na karanga lakini
licha ya kuwa na ardhi nzuri kama hiyo bado kilimo hakina faida kwao.
Mchora Katuni Ali Masoud
(mwenye miwani) akizungumza na waraghbishi na wananchi wa kijiji cha Lugunga
Lakini ni sababu gani
inayowafanya wakose faida katika kilimo chao licha ya kuwa na ardhi nzuri
inayokubali zaidi ya mazao ya aina tatu. Hapo ndipo waraghbishi walipoanza
kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo.
Akifafanua ukubwa wa
tatizo linalowakabili wakulima wa kijiji hapo raia mwamilifu na mraghbishi
Gabriel Jonathan anasema:
“Unajua ndugu mwaandishi
hapa kijijini tatizo ni moja, asilimia kubwa ni wakulima na wakulima wengi
hawana elimu. Unaona, wengi wao wameishia darasa la saba na wengine hawajasoma
kabisa, hivyo hata kilimo chao wanalima ili mradi msimu upite hata akilima heka
mbili akatoa gunia tano kwake anaona sawa.”
Ni kweli kilimo ni suala
la kitaalamu na hivyo kuna uhitaji mkubwa wa ufahamu kwa mkulima, na hapo ndipo
serikali inapomwajiri Afisa Kilimo. Ambaye kimsingi ndio mwenye jukumu hilo
katika kuhakikisha anawatembelea wakulima na kuwasaidia kitaalamu ili waweze
kuzalisha mazao mengi na yenye ubora.
Hali hii iliibua hamu ya
kutaka kujua iwapo kijijini hapo yupo Afisa wa Kilimo ama Bwana Shamba kama
anavyojulikana na wengi, katika hali ya kutokuridhishwa na kiwango cha huduma
anachotoa mtaalamu huyo wa mashamba, mraghbishi Mafuriko alisema,
“Bwana Shamba yupo tena
yupo sana lakini hana ushirikiano kabisa na wakulima wa Lugunga, kwanza hakai
hapa kijijini. Pili wengine hawamjui kabisa yaani kwa wiki anaweza kuja mara
mbili au msimuone mwezi mzima ila mshahara analipwa”
Akiongezea kuhusu upatikanaji
wa Afisa huyo Yohana Julius alisema:
“Tunasikia anaishi
Masumbwe na anapoishi hatujui ni mtaa gani na wala mimi simjui licha ya kwamba
nakaa hapa katikati (Center) hata nikikutana naye bila kuambiwa simjui je mwananchi
anayeishi Mahameni itakuwaje”
Mahameni ni kitongoji
kilichopo pembeni ya kijiji cha Lugunga ambapo pia bwana Shamba wa kijiji hicho
anatakiwa kufika katika kutimiza wajibu wake.
Mraghbishi Gabriel (wa
kwanza kushoto) akiwa na wananchi wenzake wa kijiji cha Lugunga, wakisikiliza maswali
toka kwa mwandishi
Umbali wa kutoka
Masumbwe hadi Lugunga ni kilometa 17 hali inayodhihirisha kuwepo umbali mrefu
kati ya anapoishi Afisa kilimo huyo Dickson Silvester na kituo chake cha kazi.
Kukaa tu na kulaumu
hakusaidii sana hivyo ni jukumu la waraghbishi kujua nini wanachotakiwa
kufanya,
“Mimi naona hapa
tuandamane mpaka ofisi ya Mkurugenzi, yeye ni mwajiri wake na inawezekana akawa
hana hata taarifa ya nini kinafanyika huku, alisikika mmoja wa wananchi
aliyetambulika kwa jina moja la Hassan.
Katika hatua nyingine
wananchi hao wakapaza sauti kwa kumtaka afisa kilimo huyo kurudi kuishi
kijijini na kuongeza kuwa kama alikubali kuja kufanya kazi na kupokea mshahara
basi akubali kuishi katika kijiji hicho cha Lugunga kama wanavyoishi wananchi
alioenda kuwatumikia.
Safari ya kujua ukweli
wa kwanini afisa kilimo huyo haishi katika kituo chake cha kazi ilizidi kusonga
mbele na ndipo mwandishi wa makala hii alipomtafuta kwa njia ya simu na kufanya
naye mahojiano yaliyodumu kwa dakika kumi na tano.
Katika mahojiano hayo
afisa kilimo huyo Dickosn Silvester alikiri kuwa yeye ndiye afisa kilimo wa
kijiji cha Lugunga na kukanusha taarifa za kuwa haishi katika kituo chake cha
kazi.
“Mimi ni afisa kilimo wa
Lugunga kweli na ninaishi hapo hapo Lugunga Center aliyekwambia siishi hapo ni
nani? Mana huo ni uzushi”, alisikika akisema Dickson kwa njia ya simu wakati
akiongea na mwandishi wa makala hii.
Baada ya kupata majibu
ambayo hayakuniridhisha kutoka kwa afisa kilimo huyo nilirudi Lugunga kwa njia
ya simu na kumtafuta mwenyekiti wa kitongoji cha Lugunga Kati (Center) bwana
Mashiba Dioniz ili kupata ukweli yalipo makazi ya afisa kilimo huyo.
“Mimi ndiye mwenyekiti
wa kitongoji cha hapa Senta, kwakweli mwandishi huyo afisa kilimo hana makazi
hapa mimi nazijua kaya zangu zote, Ila huwa namuona mara moja kwa wiki basi ila
kusema anaishi hapa ni uongo kabisa.’ Alisema Bwana Mashiba mwenyekiti wa
Lugunga.
Lakini waraghbishi hawa
si tu wanajaribu kufuatilia upatikanaji wa huduma za ugani katika kijiji chao,
ila wameendelea kutoa elimu kwa wanakajiji wengine wa kijiji hapo. Mfano mmoja
ni migogoro baina ya wakulima wenyewe. Na kwa kuwa waraghbishi hawa hawaitishi
mikutano ya vijiji mara nyingi wamekuwa wakitumia maeneo ya migogoro kama
sehemu yao ya kutolea elimu.
Akifafanua hilo Felix
Daudi, mraghbishi mwingine katika kijiji hicho anasema,
“Kuna kesi tunakutana
nazo ambazo tunazitumia pia kutoa elimu. Moja ya kesi hizo ni zile na mtu
kuacha mifugo yake bila uangalizi na mwishowe inaingia kwenye mashamba ya watu
na kuanza kula mazao. Utakuta mtu hajui wapi akapeleke tatizo lake ama
akishaikamata mifugo hiyo afanye nayo ni nini,”
Hivyo ni vizuri watendaji
wa serikali wakashirikiana na waraghbishi na muda mwingine kuwapatia ujuzi
mdogo mdogo. Hii itasaidia kufanikisha shabaha ya Maendeleo kwani pande zote
watakuwa wanategemeana. Na si katika hali hii ambayo watu wanashutumiana. Hivyo ni jukumu letu sote kucheza nafasi zetu
katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Moja ya mashamba ya
mpunga yaliyopo katika kijiji cha Lugunga
No comments:
Post a Comment