Ameteuliwa baada ya Jose Mourinho kufutwa Alhamisi.
"Nimefurahia kurejea Stamford Bridge. Chelsea ni moja ya klabu kubwa duniani lakini haimo pale inakofaa kuwa kwa sasa. Hata hivyo nina uhakika tunaweza kubadilisha mambo,” amesema Hiddink baada ya kuteuliwa. “Nasubiri kwa hamu kufanya kazi na wachezaji na wakufunzi wenzangu wapya katika klabu hii kubwa na kufufua uhusiano wangu mzuri na mashabiki wa Chelsea.”
Mholanzi huyo alikuwa uwanjani Stamford Bridge kutazama mechi ya Ligi ya Premia dhidi ya Sunderland ambayo ilisimamiwa na Steve Holland akisaidiwa na Eddie Newton, ambaye sasa atakuwa kocha msaidizi wa timu.
The Blues wamo nambari 16 ligini kwa sasa baada ya kushindwa mechi tisa kati ya 16 walizocheza msimu huu Ligi Kuu Uingereza.
Hiddink alishinda mataji sita ya ligi ya Uholanzi na Kombe la Ulaya akiwa meneja wa PSV Eindhoven ya Uholanzi katika vipindi viwili.
Pia aliongoza timu za taifa za Korea Kusini, Australia na Urusi kabla ya kujiunga na Chelsea mara ya kwanza kujaza pengo lililoachwa na Luiz Felipe Scolari Februari 2009.
Alijiuzulu wadhifa wake kama mkufunzi wa timu ya Taifa ya Uholanzi mwezi Juni, baada ya kutofanya vyema katika juhudi za kuwasaidia kufuzu kwa Euro 2016.
Mwishowe Uholanzi hawakufuzu kwa michuano hiyo.
BBC/SWAHILI
No comments:
Post a Comment