Na Daniel Mbega
HATUA ya Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda, Biashara na Masoko, Uledi Mussa, kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuacha kasumba ya kutumia mabilioni
ya fedha kununua nguzo za umeme nje ya nchi ni sawa na serikali kujipiga kofi
na kulia yenyewe.
Na kilichofanywa na
mtendaji huyo wa wizara ni usanii na kuwazuga wananchi kwa kuwafanya mazezeta,
kwa sababu serikali inaufahamu fika mchezo uliokuwepo kwa muda mrefu wa kukataa
kununua nguzo za umeme hapa nchini, lakini inaagiza nje ya nchi nguzo zile zile
zilizotoka kwenye kampuni za kizalendo ambazo zinazalisha nguzo imara.
Wakati
akiwa katika ziara mkoani Njombe, Mussa aliagiza kwamba iwe mwisho kwa Tanesco
kuagiza nguzo hizo nje ya nchi kwa sababu viwanda kama Tanwat alichokitembelea
eneo la Kibena, vinazalisha nguzo imara ambazo alizikuta zimelundikwa
zikisubiri kusafirishwa kwenda Kenya na Afrika Kusini ambako ndiko liliko soko
lao kubwa.
Ni huko ambako
watendaji wa serikali, hasa Tanesco, wamekuwa wakisingizia Sheria ya Ununuzi ya
Umma (PPRA) kuwapa zabbuni wafanyabiashara wa nje wailetee nguzo zile ambazo
zimetokea Njombe au Mafinga, wakizinunua kwa bei mbaya kuliko kama wangezinunua
nchini, kwa sababu tu ama wanapata kamisheni kubwa kujaza viriba tumbo vyao au
kampuni zao ndizo zinazopewa zabuni hizo.
Tanwat siyo kampuni
pekee ya kizalendo inayotengeneza nguzo imara za umeme. Nenda pale Mafinga,
tena barabarani kabisa, utakuta kuna kampuni inayotengeneza nguzo hizo ambayo
walau kidogo imekuwa ikiiuzia Tanesco – pindi wakubwa wanapoamua ‘kuua soo’ ili
waonekane wanajali hata viwanda vya ndani.
Ni hivi karibuni tu
iliripotiwa kwamba Tanesco ilikuwa katika mchakato wa kuagiza nguzo 700,000
kutoka Afrika Kusini huku Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Felchesmi Mramba,
akiitetea hatua hiyo kuwa inatokana na mahitaji ya Sheria ya Ununuzi wa Umma
inayoweka ukomo wa zabuni kutangazwa kimataifa.
Hii siyo mara ya kwanza kwa serikali kuagiza Tanesco
isiagize nguzo nje, ndiyo maana nikasema, kinachofanyika sasa ni kama kuwazuga
wananchi waonekane mazezeta wasiojua kinachoendelea.
Nakumbuka mwaka 2012 wakati George Simbachawene akiwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini alipata kuiagiza Tanesco kuacha kuagiza nguzo za
umeme kutoka nje ya nchi na badala yake itumike bidhaa ya hapa nchini.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Simbachawene kutembelea baadhi
ya timba za nguzo wilayani Mafinga na kujionea hali halisi ya nguzo hizo
zikikosa soko, huku Tanesco ikiagiza bidha hizo kutoka Kenya na
Afrika Kusini.
“Sioni sababu ya
kuagiza nguzo kutoka Kenya au Afrika Kusini wakati hapa nchini tuna bidhaa hii
inakosa soko, hili ni jambo la ajabu sana, hili ni swali ambalo hata ukiulizwa
na mtoto mdogo unapata shida sana kulijibu,” alisema.
Akaongeza: “Haya ni maajabu makubwa, viwanda vyetu havina
kazi, lakini malighafi zipo, eti tunakwenda kununu nje ya nchi, sisi
tunaosimamia wizara hii, tunaambiwa na Tanesco kuwa tatizo kubwa ni nguzo za
umeme, na wananchi wetu wanahangaika kupata huduma hii ya umeme kwa gharama
kubwa, hapa kama kiongozi na naibu waziri nimesikitishwa sana, moja ya maamuzi
ya maana na ya haraka ni kuzuia huu uagizaji wa nguzo nje ya nchi. Haiwezekani
wakulima wakawa wanazalisha miti na kupata nguzo tena zenye ubora, halafu sisi
tunakwenda kununua nje ya nchi, wakati hao wanaotuuzia wanazinunua kwa gharama
nafuu hapa hapa nchini kwetu, hii haiwezekani.”
Aliongeza kuwa wakati sasa umefika kwa Tanesco kwa kutumia
bidhaa iliyopo nchini ili kuleta tija kwa viwanda vya ndani, hatua ambayo ingepunguza
mzigo wa ununuzi wa gharama kubwa kwa wananchi wanaohitaji nyumba zao
kuingiziwa umeme.
Akasisitiza kwamba hawezi kuruhusu tena nguzo ziendelee
kuletwa nchini, kwani hali hiyo inachangia kuua viwanda vidogo, inaua uchumi na
ajira, na inaleta madhara makubwa kwa taifa.
Lakini muuzaji wa nguzo katika mji wa Mafinga, Awadhi
Shedaffa, alisema hatua ya Tanesco kuagiza nguzo nje ya nchi inawanyima fursa
wazawa kuuza bidhaa zao zenye ubora, kwani kampuni yake inao uwezo wa kuzalisha
nguzo 12,000 kwa mwaka, lakini imekuwa ikiuza nguzo 700 tu kwa mwaka huku
akilalamika kwamba licha ya kuomba zabuni mara kadhaa, Tanesco hawajawahi
kuwapatia.
Sangito Sumari meneja wa Kiwanda cha Green Resources cha
Mufindi anasema kampuni hiyo inao uwezo wa kuzalisha nguzo kati ya elfu hamsini
na elfu tisini kwa mwaka, lakini kutokana na kukosa soko, wanazalisha nguzo
14,856 baada ya Tanesco kuacha kuagiza nguzo zao kutokana na deni kubwa la Shs.
2 bilioni kwa wakati huo.
Ukisimama pale Igumbilo mjini Iringa kwenye kizuizi, kila
siku utaona malori mengi yakiwa yamebeba nguzo kutoka ama Njombe au Mafinga,
lakini nguzo hizo haziishii Dar es Salaam, kwani ama zinaingizwa kwenye
makontena kupakiwa na meli kupelekwa Afrika Kusini au malori yanapitiliza
kwenda Mombasa na Nairobi, Kenya.
Lakini ukikaa Namanga au Horohoro, utashuhudia pia malori
yenye nguzo yakitoka Kenya na kuingia Tanzania. Ukiuliza unaambiwa hizo ni
nguzo za Tanesco wamenunua Kenya!
Inakuwaje tunajiibia kwenye mfuko mmoja na kuweka kwenye
mfuko wa pili? Biashara ya kujipiga makofi na kulia wenyewe itakwisha lini hii?
Nyingi kati ya nguzo zinazozalishwa na viwanda hivi vya
ndani zimethibitishwa na wataalamu kutoka nje ndiyo maana zinapata soko huko
kwamba ni bora na imara, zikiwa na uwezo wa kudumu kwa miaka zaidi ya 15.
Tunaposema tunatakiwa kutengeneza ajira nyingi kwa
Watanzania kupitia viwanda tutakuwa tunajidanganya wenyewe ikiwa bidhaa za
viwanda hivi hatuzithamini kwa sababu matokeo yake lazima uzalishaji utashuka
na viwanda hivyo kufungwa kwa sababu hakuna anayeweza kuendelea kufanya kazi kwa
hasara.
Mikoa ya Iringa na Njombe ndiyo inayoongoza kwa kilimo cha
miti tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Shamba kubwa la miti
la Sao Hill lina hazina ya kutosha ya kupata nguzo imara kabisa ambazo hata
mataifa mengine yanazitumia.
Hata hivyo, ufisadi uliotamalaki kila idara ndio
unaokwamisha maendeleo haya kiasi kwamba rasilimali zetu zinakosa thamani
nchini mwetu, lakini zinapokwenda nje na kugongwa mihuri, eti zinaonekana
zinafaa.
Imepata kuripoti huko nyuma kwamba, katika ufisadi huo wa
ununuzi wa nguzo za Tanesco, hata baadhi ya wabunge walikuwa wakihusika kwa
kutumia kampuni zao ama za jamaa zao kununua nguzo Mafinga na Njombe na
kuzipeleka nje, halafu wanakula njama na watendaji wa Tanesco ili kuzirejesha
tena nguzo hizo nchini kwa bei mbaya.
Siyo siri, mradi huo wa nguzo, kama ilivyo kwa mradi wa
mafuta ya kuendeshea mitambo kwa Tanesco, umezingirwa na harufu ya rushwa
iliyotamalaki na wabunge waliokuwepo wakati huo wanajijua ni namna gani
walivyokuwa wakihusika.
Haikushangaza hata Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
iliyokuwa chini ya January Makamba ilipovunjwa mwaka 2011 kufuatia kashfa ya
rushwa hasa wakati wa kuelekea kwenye Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Ni wakati muafaka kwa serikali, kama inataka kuziba mianya
ya rushwa na kubana matumizi ya hovyo kabisa ya idara zake, kuitupia macho
Tanesco na biashara hiyo ya nguzo, vinginevyo Rais John Magufuli atakuwa
anaweza fedha kwenye kapu lililotoboka bila kujua.
Wasalaam.
0656-331974
No comments:
Post a Comment