WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu
elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za
Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais
John Magufuli.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu
bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo
kuwa ni
- Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Diamond (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam);
- Shule ya Msingi Iringa (Iringa) na
- Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
- Shule ya Msingi Angaza (Mbeya);
- Shule ya Msingi Nuru (Mbeya);
- Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma);
- Shule ya Msingi Tanga (Tanga);
- Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na
- Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na
mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu
sawa na shule za binafsi.
Katika waraka huo, Wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na
Wizara hiyo, TAMISEMI, Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri ya wilaya,
wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi
Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo,
vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa
wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa
kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka,
vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na
wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa
taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi
na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
Katika waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia
utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya
wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga
fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila
malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo
unaielekeza wizara hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa
wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata
mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya
elimumsingi bila malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na tathmini
za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo inatolewa kwa
ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule
ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na
vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa
mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi,
kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati,
vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga
na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni za kugharimia wanafunzi wenye mahitaji
maalumu waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu maalumu kwa kuwapatia
chakula yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo mitatu kwa
wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule
Waraka huo unawataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina
ya vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, sare
za michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia wanafunzi ili
wazazi wanunue wenyewe.
Pia wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali
inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za Serikali
na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na mahitaji
mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule
Wizara katika waraka huo inataka kamati za shule kufuatilia na kusimamia
matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze kuleta tija;
kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali
inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.
Kuwashirikisha wazazi, walezi, walimu na wanafunzi katika maamuzi na
maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule
kwa ujumla.
Pia waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni
kusimamia sera na miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi ambao ndio
walengwa wakuu wa utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo
shule katika kipindi chote cha masomo.
No comments:
Post a Comment