Rais Dk. Magufuli
Na Mwandishi Wetu, Pemba
Rais John Magufuli ameombwa kurudisha
maadili ya utumishi wa umma kwa kusimamia sheria za maadili kikamilifu ili watu
wasitumie siasa kupora uchumi na rasilimaili za taifa huku wakitumia nafasi
hizo kufanya biashara ya mihadarati na kujinufaisha misaamaha ya kodi kwa
asilimia 100 ambayo imewatajirisha wachache huku nchi ikiendelea kuwa maskini.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa madhehebu ya
dini nchini ambaye pia kiongozi wa Kanisa la Kipentekoste nchini, Mchungaji
William Mwamalanga ambapo pia alisisitiza kuwa kuna haja ya mawaziri wote
waliokuwemo kwenye utawala wa awamu ya nne kurudisha mali zote walizopora.
Mchungaji Mwamalanga alisema, kitendo cha
Rais aliyeondoka Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mwaziri wengine
kuondoka kimya kimyaa bila kueleza hadharani mali walizoingia nazo na
wanazotoka nazo kulingana na Sheria za Maadili ya Utumishi wa Umma kunaua
kabisa maana ya sheria hiyo na kugeuka wimbo wa danganya toto ambao
ulihimizwa kwenye serikali ya awamu ya
nne huku baadhi wabunge wakiitwa kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
ambapo hata ripoti zao hazijawahi kuwekwa hadharani.
Mchungaji Mwamalanga ambaye aliongoza
ujumbe wa viongozi wa dini wakiwemo maaskofu na mashekhe na wanaharakati wa amani
kutoka nchi za Maziwa Makuu, Afrika na Ulaya kwa lengo la kuhimiza uongozi wa haki,
amani na kupinga matumizi ya mihidarati kwa
vijana, alisema uwazi katika uongozi ndiyo njia pekee itakayodumisha amani na kulinda
rasilimali za nchi.
Viongozi wengine Sheikh Dk. Ahmad Mohammed,
Sheikh Ogowi Ramadhani na Bishop Dk. Mical Daniel wameonya kwamba Afrika kwa
sasa inakabiliwa tatizo baya la wanasiasa wengi kukimbilia kutawala badala ya kuongoza
huku wakibainisha kwamba uongozi ni kuonyesha njia. Wameonya kwamba, tamaa ya
kutawala inazifanya hata chaguzi nyingi barani humo kupoteza maana kutokana na
wanasiasa kutumia rushwa, hila na wizi ili waingie madarakani kwa nia ya
kujilimbikizia mali.
“Tunaona watu waliingia madarakani wakiwa
maskini lakini wanapotoka madarakani wanakuwa matajiri kufuru huku wakiwa
wamehodhi njia kuu nyingi za uchumi na kuwaachia wananchi kamkate kadogo ambako
huendelea kung’ang’aniana,” wanasema.
Kuhusu rushwa pamoja na mihadarati,
viongozi hao wameomba ziwepo sheria kali hata za vifo kwa wahusika kama ilivyo
kwa China na kwingineko kwani ndiyo njia muhimu kulinda uchumi wa pamoja na
maendeleleo ya kasi.
Wanasema mafanikio makubwa ya kupambana na
rushwa na mihadarati nchini China yametokana na uwepo wa sheria kali za vifo, hivyo
wamemuomba Rais Magufuli kuruhusu sheria hizo nchini Tanzania ili kutokomeza
hali hiyo.
Katika hatua nyingine, viongozi hao
walikutana na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na jamii ya kawaida ambao wamemuombea
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein kuruhusu hofu ya Mwenyenzi Mungu kwa
kuheshimu matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 badala ya kurudia
uchaguzi ambao kuna kila dalili kuwa hautakuwa huru wala haki haitasimamiwa.
Wanasema marudio ya chaguzi nyingi duniani yameleta
maafaa makubwa ambapo wananchi hugonganishwa wenyewe kwa wenyewe huku walafi wa
utawala wakijiongeza muda kama ilivyo nchini Burundi kwa kigezo kuwa hawawezi
kuacha nchi ikiwa kwenye vurugu.
No comments:
Post a Comment