Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 13 December 2015

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TPLB


Waheshimiwa viongozi wa vilabu vya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania, Waheshimiwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Waheshimiwa viongozi wa TFF Tanzania, Waheshimiwa wageni waalikwa,

Ndugu Wanahabari, Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote, napenda kumshukuru M/Mungu kwa kutufanikishia kukutana hapa leo, na namuomba atuongoze hadi mwisho wa shughuli yetu na awatangulie wale wanaosafiri, ili wafike salama. Pia napenda kuwashukuru ndugu wajumbe wa Baraza Kuu kwa kukubali wito wangu na kufika kwa wakati.
Ninaimani tutakitumia kikao hiki ambacho ni cha kikanuni, kutoa michango yetu ya hali na mali katika kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu Tanzania.
Bodi inapenda kutoa pongezi za jumla kwa uongozi imara wa nchi yetu, uliofanikisha kukamilisha uchaguzi mkuu, ambapo Mhe.  John Pombe Magufuli, amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunampongeza sana na pia kumshukuru Mhe. Rais, kwa kumteua Mhe. Nape Nnauye (MB) kuwa Waziri wa Wizara inayohusika na michezo. Tumefarijika sana kumpata kijana mwenzetu na tunaimani atakua mchango mkubwa katika kuendeleza Michezo, hasa Mpira wa Miguu.
Ndugu wajumbe, kikao hiki ni cha pili toka kuundwa kwa Bodi yenu na ndani ya kipindi tulichokaa madarakani kwa ridhaa yenu, Bodi imejitahidi kutekeleza majukumu  yake kama yalivyo ili kuendeleleza mchezo wa mpira wa miguu ambao unapendwa sana na Watanzania.
Bodi imeendesha Ligi Kuu (Vodacom Premier League) ya mwaka jana ambapo timu ya Yanga walitawazwa kuwa mabingwa, na vile vile imeendesha Ligi Daraja la Kwanza ambapo klabu tatu zilipanda daraja, na kwa mwaka huu, pamoja na kuendesha ligi hizo mbili, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeiomba Bodi pia iendeshe Ligi Daraja la Pili ambayo inaendelea hadi sasa.
Napenda kuchukua fursa hii,  kuipongeza Sekretarieti ya Bodi chini ya uongozi wa Bwana Boniface Wambura kwa kufanya kazi bila kuchoka kuona kwamba ligi hizi zinaendeshwa kwa ufanisi mkubwa pamoja na changamoto kadhaa walizokabiliana nazo. Pia nawapongeza kwa kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mkutano huu na mingine, naamini wajumbe mtakuwa mashahidi kwa hilo.
Ndugu wajumbe, utendaji wa Bodi yenu umeelezwa kwa kina kwenye taarifa ya utekelezaji ya mwaka ambayo imetayarishwa, lakini meza yangu kama Mwenyekikiti, ingependa kueleza kwa ufupi baadhi ya mafanikio ya Bodi pamoja na changamoto ilizokumbana nazo, kwa kipindi cha mwaka 2015.
Miongoni mwa mafanikio kwa mwaka 2015 ni kuhakikisha Bodi inakuwa mtendaji mkuu katika uendeshaji wa Ligi zote zilizo chini yake. Bodi imekuwa kiungo muhimu kati ya vilabu na TFF, na imekuwa tayari kutoa misaada mbalimbali kwa vilabu inapohitajika.
Kwa kushirikiana na Idara ya Masoko ya TFF, Bodi imefanikiwa kuhuisha mikataba ya udhamini na kupata mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza kwa mara ya kwanza katika historia ya ligi hii. Naamini udhamini uliopatikana ni mdogo sana na haukidhi gharama za uendeshaji, lakini ni mwanzo nzuri, ambao tunategemea kuwa kichocheo cha kupata wadhamini wengine.
Bodi imekua ikipokea fedha toka kwa wadhamini na kuziwasilisha kwa vilabu vyote kwa wakati, jambo ambalo lilikua tatizo sugu wakati Ligi ilipokuwa chini ya Shirikisho. Bodi imekua ikiwakilisha vilabu katika mikutano na majadiliano yanayohusu maslahi ya vilabu na wachezaji, na itaendelea kuwa muhimili wa vilabu kwa maendeleo ya mpira.
Pamoja na mafanikio hayo, kuna changamoto ambazo Bodi imekumbana nazo katika kipindi cha mwaka huu. Itakumbukwa katika kikao cha mwaka jana, moja ya majukumu niliyopatiwa kama Mwenyekiti ni kupeleka wazo la kubadilisha muundo wa Bodi kuelekea kuwa chombo huru. Kwa ufupi, imeonekana muundo wa vilabu vyetu kwa ujumla unahitaji marekebisho ili kuweza kuunda chombo huru cha kujiendesha. Kamati ya uongozi ya Bodi, imeunda kamati ndogo ili ifuatilie maswala hayo, na kutoa taarifa itakayotusaidia kutoa mwelekeo.
Changamoto nyingine ni hali ngumu ya kiuchumi ya vilabu pamoja na ufinyu wa udhamini kwa vilabu. Kutokana na hali hii Bodi huwa inalazimika kusaidia klabu kwa kutoa mikopo ya muda mfupi ili kuziokoa. Pia gharama za uendeshaji ziko juu kulinganisha na kipato cha Bodi, kama inavyoonekana kwenye mahesabu ya mwaka.
Ndugu wajumbe, changamoto nyingine ni kwa viongozi wa vilabu kutohudhuria miito ya mikutano ambayo inaandaliwa kwa faida za vilabu, naomba niwaombe, ndugu wajumbe tuwe na utayari wa kushiriki kila tunaposhirikishwa. Mfano wa mahudhurio hafifu ni semina ya maelekezo kuhusu leseni za vilabu, yaliyoandaliwa na CAF kupitia Bodi ya Ligi. Naamini hali itabadilika kwa kipindi kinachokuja.
Bodi ina changamoto ya kujenga Ligi zetu ili kuwa chapa (brand) inayojiuza. Jambo hili linahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa vilabu vyote katika maeneo yote muhimu kama weledi katika uendeshaji wa vilabu pamoja na kuhakikisha nidhamu ya kiwango cha juu inakuwepo kwa timu na washabiki kwa ujumla.
Bodi kupitia Kamati yetu ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi zetu imekuwa ikitoa adhabu za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kinidhamu ya timu ambayo yako ndani ya mamlaka yake kikanuni.
Hii ni changamoto kwetu kuhakikisha matatizo ya kinidhamu kwa timu zetu na washabiki yanapungua kwa kiasi kikubwa kama hatuwezi kuyaondoa yote. Hii ni moja ya njia za kuzijengea heshima timu zetu.
Ndugu wajumbe, michango yenu katika Mkutano huu wa Baraza Kuu itasaidia kuboresha uendeshaji wa Ligi zetu, na kwa ile itakayohitaji marekebisho ya Katiba ya Shirikisho, Kanuni za Uendeshaji wa Bodi ya Ligi pamoja na kanuni za
Ligi tutayafikisha katika vyombo husika. Pamoja na jitihada za kushughulikiwa kwa changamoto zilizojitokeza, bado Bodi inaendelea kuhakikisha inaboresha maeneo yote yanayohitajika zikiwemo changamoto mpya zitazojitokeza pamoja na kuendelea kushughulikia ambazo hazijarekebishika ipasavyo.
Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadhamini wote waliojitokeza kudhamini Ligi zetu na tunatoa nafasi kwa kampuni nyingine kujitokeza kudhamini kwani bado tunahitaji udhamini zaidi ili kuzijenga klabu kiuchumi na kuimarisha uendeshaji wa Ligi zetu, na Bodi kwa ujumla.
Ahsanteni
Yahya Hamad

No comments:

Post a Comment