WAZIRI WA FEDHA ANATOSHA?
Rais Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri baada ya Mawaziri wanne kuachishwa kazi kutokana na kashfa ya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu uliotokea katika Operesheni Tokomeza na kifo cha Waziri wa Fedha. Katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Rais Kikwete hakuzingatia malalamiko ya Sekretariati ya CCM kuwa Mawaziri Mizigo wanakiathiri chama CCM hususani wakati huu tukielekea katika uchaguzi mkuu 2015.
Mawaziri walioanishwa na Katibu Mkuu na Katibu Mwenezi wa CCM kuwa ni mizigo na kuhojiwa na Kamati Kuu ya CCM na ambao wamebaki katika Baraza la Mawaziri ni pamoja na Dk Shukuru Kawambwa (Elimu), Christopher Chiza (Kilimo), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda), Celina Kombani (Utumishi wa Umma) na Hawa Ghasia (Tamisemi). Mhe. Saada Mkuya Salum akiwa Naibu Waziri alihojiwa kwa niaba ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ambaye kwa sasa ni marehemu. Rais Kikwete amemteua Mhe. Saada Mkuya Salum kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi.
Waziri wa Fedha na Uchumi ndiyo msimamizi mkuu wa sera za uchumi za nchi. Ana majukumu ya kusimamia uandaaji wa bajeti ya serikali ikiwa ni pamoja na kuandaa miswada ya sera za kodi na kuzitekeleza, kuandaa makadirio ya matumizi ya serikali na kusimamia utekelezaji wake baada ya kupitishwa na Bunge. Sera za serikali kupitia wizara ya fedha ni nyezo muhimu ya kukuza uchumi kwa kuhakikisha kuwa matumizi ya serikali yana tija ya juu, kuongeza ajira, kuhakikisha sekta za jamii hususan afya na elimu zinatengewa fedha za kutosha, kudhibiti mfumko wa bei kuhakikisha nchi ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, kudhibiti ongezeko la deni la taifa, kuhakikisha idara na mashirika ya serikali yanawajibika katika matumizi yao ya fedha za umma.
Waziri wa Fedha ndiye anayeongoza majadiliano na mashirika ya kimataifa yanayohusu sera za uchumi, fedha, misaada na mikopo kama vile Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mashirika ya Misaada ya Nchi zilizoendelea kama vile DFID (Uingereza), SIDA (Sweden), DANIDA (Denmark), USAID na MCC (Marekani) na kadhalika.
Tanzania imeanza kukopa katika masoko ya biashara kwa kasi na ari mpya. Waziri wa Fedha ana wajibika kuweka break nchi isije ikajikuta ina madeni isiyoweza kuyalipa.
Ndani ya serikali kuna mivutano mikubwa kati ya wizara ya fedha na wizara, idara na mashirika mengine. Kila wizara inataka itengewe fedha zaidi. Wizara ya fedha lazima isimamie matumizi yasizidi mapato. Waziri awe na uwezo wa kupambana na Mawaziri wenzake ambao wanakiuka bajeti zao. Awe na ujasiri wa kumueleza Rais kwa heshima na taadhima ofisi yake izingatie bajeti iliyopitishwa. Kuna taarifa kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Ofisi ya Rais ilitumia zaidi ya bajeti ya mwaka mzima ya safari za Rais. Waziri wa Fedha anapaswa kumueleza Bosi wake kwamba sote tunawajibika kuheshimu bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Waziri wa Fedha ndiye kiranja wa asasi nzito kama vile Benki Kuu BOT, Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Amana (Capital Markets and Securities Authority), Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority), Idara ya Usimamizi wa Bima (Insurance Supervisory Department), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (National Board of Accountants and Auditors) na kadhalika.
Wizara ya Fedha ndiyo inayosimamia hisa za serikali katika kampuni kama vile National Microfinance Bank (NMB), Tanzania Investment Bank (TIB), National Bank of Commerce (NBC), Tanzania Postal Bank (TPB), National Insurance Corporation (NIC) na mashirika mengine ya Umma. Wizara ya Fedha inasimamia mifuko ya Pensheni ikiwemo Public Service Pension Fund, Parastatal Pension Fund na Government Employees' Provident Fund.
Waziri wa Fedha anastahiki kuwa na uelewa na uwezo mkubwa wa kuchambua sera za uchumi, kujenga hoja wakati wa majadiliano na mashirika ya kimataifa, kuweza kuonyesha uongozi katika mijadala na mawaziri wenzake na asasi nyeti kama vile Benki Kuu.
Rais Kikwete amemteua Mhe. Saada Mkuya Salum kuwa Waziri wa Fedha baada ya kifo cha Dr William Mgimwa. Uteuzi wa mwanamke kuwa Waziri muhimu ni jambo jema katika kupambana na mfumo dume. Mhe. Saada ni Mzanzibari. Moja ya kero za Muungano ni kuwa Wazanzibari hawapewi fursa kuongoza wizara muhimu kama vile Wizara ya Fedha. Mhe. Zakhia Meghji ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Fedha. Haidhuru yeye pia ana asili ya Zanzibar lakini alikuwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kilimanjaro. Kashfa ya uchotaji wa fedha za EPA Benki Kuu ilimlazimisha ajiuzulu. Kumteua Saada Mkuya Salum kuwa waziri kunaua ndege wawili kwa jiwe moja. Ni mwanamke na Mzanzibari wa Zanzibar.
Wasifu wa Mhe. Saada Mkuya Salum uliowekwa katika tovuti ya Bunge unaonesha kwa Mhe.Saada alijiunga na CCM mwaka 2000 na yeye ni mwanachaama wa kawaida. Bi Saada alimaliza kidato cha 6 mwaka 1995 Sekondari ya Lumumba Zanzibar. Shule ya Msingi alisomea Kisiwandui na sekondari ya kawaida (O level) alisomea Hamamni. Mwaka 1997 – 99 alifanya masomo ya biashara na akatunukiwa sitashahada ya juu. Kati ya 2000 – 2002 alifanya masomo ya shahada ya pili ya biashara (Courses for the Second Degree in Business) na akapata cheti (certificate). CV imetaja shule ya msingi alizosomea lakini vyuo alivyosomea havikutajwa.
Alianza kufanya kazi Hazina Zanzibar mwaka 2003 kama afisa. Mwaka 2006 alikuwa Afisa Tawala (Administrative Officer). Kati ya mwaka 2008 na 2010 alisomea shahada ya Master of Finance. Chuo alichosomea hakikuelezwa. Kutotaja Chuo kunaweka wasiwasi wa ubora wa shahada aliyoipata. Mwaka 2011 aliteuliwa kuwa Kamishna wa Fedha (Commissioner of Finance) na Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Baadhi ya Wabunge niliyozumgumza nao wamenieleza kuwa Mhe. Saada amefanya kazi nzuri Bungeni hasa katika kipindi ambacho Marehemu Dr Mgimwa alikuwa mgonjwa.
Ikiwa wasifu uliobandikwa katika tovuti ya Bunge ni sahihi ni wazi Mhe. Mkuya hana uzoefu wa kisiasa, kitaaluma na kiutawala wa kuongoza Wizara nzito na nyeti. Sina uhakika ana uelewa wakutosha kuhusu menejimenti ya fedha za umma (Public Financial Management), upembuzi yakinifu wa miradi ya umma, athari za nakisi ya bajeti katika mfumko wa bei, deni la taifa na upatikanaji wa mikopo kwenye sekta binafsi. Sera muhimu ya kukuza na kubadilisha mfumo wa uchumi, hususani kuendeleza viwanda vya ndani, kuongeza uuzaji wa bidhaa nchi za nje na hivyo kuongeza ajira ni kuwa na thamani halisi ya sarafu (real exchange rate) yenye kuongeza ushindani katika soko la dunia. Kuongezeka kwa tija na ufanisi katika uzalishaji bila kubadili thamani ya shilingi kunaongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia. Mfumko wa bei unapunguza ushindani wa bidhaa za Tanzania ndani ya nchi na kwenye soko la dunia na hivyo kuathiri ongezeka la ajira. Sera za riba na upatikanaji wa mikopo ni suala muhimu katika kuendeleza uwekezaji ambao utakuza uchumi na kuongeza ajira.
Serikali inakabiliwa na matatizo makubwa ya fedha. Matumizi yanaongezeka kwa kasi kubwa kuliko mapato. Bajeti inayowasilishwa na serikali Bungeni imekuwa na makadirio makubwa ya mapato kuliko ukusanyaji halisi. Matumizi ya kawaida yanaongezeka kwa kasi kubwa na kupunguza uwezo wa serikali kuchangia katika Bajeti ya Maendeleo.
Nakisi ya bajeti imeongezeka toka shilingi bilioni 389 mwaka wa 2007/08 sawa na asilimia 1.7 ya pato la taifa na kufikia shilingi bilioni 2992 mwaka 2012/13 sawa na asilimia 6.2 ya pato la taifa. Mwaka huu wa fedha 2013/14, bajeti imeishafumka. Mapato ni madogo kuliko makadirio. Matumizi ni makubwa. Serikali inalimbikiza madeni kwa makampuni yanayoiuzia bidhaa na huduma.
Serikali imekuwa inakopa katika masoko ya kibiashara kwa gharama kubwa na deni la taifa linaongezeka kwa kasi. Deni la taifa limeongezeka toka shilingi trilioni 5.9 mwaka 2007 sawa na asilimia 28.4 ya pato la taifa na kufikia shilingi trilioni 22 mwaka 2013 sawa na asilimia 42.5 ya pato la taifa. Tukiendelea na kasi hii ya kukopa Rais Kikwete ataiachia nchi tatizo kubwa la deni la taifa na hasa deni la nje.
Katika sekta ya ujenzi wa barabara kuna tatizo kubwa la makandarasi wengi kutolipwa kwa wakati na hivyo kucheleweshwa kukamilishwa kwa miradi. Wakati mwingine Wizara ya Ujenzi inatia sahihi miradi mipya hata kama hakuna fedha zilizotengwa ndani ya bajeti. Waziri wa Fedha ana wajibu wakuweka nidhamu katika matumizi ya serikali. Awe na uwezo wa kumueleza Waziri Magufuli asiweke sahihi miradi mipya ya barabara ambayo haijatengewa fedha.
Uendeshaji wa TANESCO una gharama kubwa katika bajeti ya serikali. Tanesco ilipata hasara ya dola milioni 240 na ina limbikizo ya madeni ya dola milioni 276
Katika kipindi hiki tuna mchakato wa katiba mpya ambao una gharama zake. Bunge la Katiba litaanza kukutana mwezi Februari. Bunge litafuatiwa na Bunge la Bajeti. Tume ya Uchaguzi inawajibika kuboresha Daftari la Wapiga kura kabla ya kura ya maoni. Tume haijaboresha daftari kwa sababu ya kukosa fedha. Uandikishaji wa vitambulisho vya taifa unasuasua kwa kutokuwa na fedha za kutosha.
Katika kipindi cha kueleka uchaguzi mkuu nidhamu ya matumizi ya serikali inatoweka. Rais na wapambe wake wanafikiria taratibu za maisha baada ya kuondoka Ikulu. Kuna kuwa na shinikizo kubwa za misamaha ya kodi na mikataba inayoweza kuwanufaisha katika kipindi cha kustaafu. Kuna shinikizo ya kupata fedha za kusaidia Chama Tawala wakati wa uchaguzi. Katika kipindi cha pili cha Rais Mkapa akielekea kun’gatuka aliuza nyumba za serikali kwa bei poa kwa mawaziri, viongozi wa CCM na watumishi wa serikali. Kashfa ya kuchota fedha za EPA ilitokea wakati tukielekea uchaguzi wa 2005. Waziri wa Fedha anawajibika kupambana na shinikizo hizo.
Baada ya kuchaguliwa kuwa Rais mwaka 2005, Mhe. Kikwete alieleza kuwa hakuna Chuo kinachofundisha Uwaziri kwa hiyo yeyote anaweza kuwa Waziri. Bila shaka mtazamo huu unachangia kuteua Mawaziri Mizigo wasiyokuwa na sifa au uwezo wa kutekeleza majukumu yao. Chanzo cha tatizo siyo Mawaziri Mizigo bali ni Rais Mzigo anayetokana na Chama mzigo.
Watanzania tunakabiliwa na matatizo ya gharama kubwa za maisha, ukosefu wa ajira, elimu duni, huduma mbovu za afya, kukithiri kwa rushwa na utawala mbovu. Tunapaswa kujipanga kukiondo Chama Mzigo madarakani.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti, Chama Cha Wananchi CUF.
CHANZO: Hii nimeitoa wanabidii
No comments:
Post a Comment