Taarifa kwa Umma: “Kuendelea kwa ‘Kashfa ya IPTL’ mpaka hivi sasa ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa uongozi wa Bunge, ufisadi wa baadhi ya viongozi wa CCM na uongo wa Waziri Muhongo”.
Kwa
nyakati mbalimbali kati ya tarehe 27 Februari 2014 na tarehe 5 Machi
2014 vyombo mbalimbali vya habari vimeandika habari na kuchapisha
matangazo juu ya TANESCO na IPTL.
Umma
uzingatie kwamba ‘kashfa ya IPTL’ ni ya miaka mingi katika taifa letu
na inaendelea mpaka hivi sasa kutokana na udhaifu, uzembe, ufisadi na
uongo unaotawala.
Kumbukumbu
zangu zinanionyesha kwamba wakati wa kuanzishwa kwake IPTL ilikuwa ni
ubia wa kampuni mbili; Mechmar Corporation ya Malysia Bhd na VIPEM ya
Tanzania.
Udhaifu wa Rais unaendeleza ‘kashfa ya IPTL’:
Mwaka
1994 IPTL ilikutana na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini
wakati huo Jakaya Kikwete na aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO wakati huo
Simon Mhaville.
Mara baada ya mazungumzo hayo IPTL ilianza kupigiwa chapuo kuingia mikataba na TANESCO pamoja na kudaiwa kutokuwa na uwezo.
Mara
baada ya kuchaguliwa Urais mwaka 2005 Rais Kikwete aliahidi kuupatia
ufumbuzi mgogoro kati ya TANESCO na IPTL na washirika wake uliokuwa
umegubikwa pia na madai ya ufisadi mkubwa.
Huu
ni mwaka 2014 ‘kashfa ya IPTL’ inaendelea hivyo Rais Kikwete anapaswa
kulieleza taifa sababu za kuendelea kwa hali hiyo na hatua ambazo
unakusudia kuchukua kuondoa udhaifu huo.
Uzembe wa uongozi wa Bunge unakwaza uwajibikaji ‘kashfa ya IPTL’
Mwaka
2008 kufuatia ‘kashfa ya Richmond’ Bunge liliazimia katika Azimio Na.
3, kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC
(uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL,
SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema
iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na
Serikali”.
Uongozi
wa Bunge la tisa wa Spika Samuel Sitta ulizembea na kufunga mjadala
kuhusu ‘kashfa ya Richmond’ huku maazimio ya msingi yakiwa
hajatekelezwa. Uongozi wa Bunge la kumi wa Spika Anna Makinda
ukaendeleza uzembe huo hata tulipohoji Bungeni kwa nyakati mbalimbali
2011, 2012 na 2013 kutaka Serikali itakiwe kuwasilisha bungeni taarifa
za utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa za Richmond, IPTL na
nyingine nyingi katika sekta ya nishati.
Iwapo
Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji
TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na matatizo katika mikataba
zingepungua na hivyo kupunguza kuwaongezea mizigo ya bei ya umeme mara
kwa mara watanzania. Hivyo, kauli za hatua ambazo wanakusudia kuchukua
kuondoa uzembe huo za Waheshimiwa Sitta (katika Baraza la Mawaziri) na
Makinda (Katika Uongozi wa Bunge) zinahitajika kuepusha madhara zaidi
kwa nchi na wananchi.
Uongo wa Waziri Muhongo umechelewesha hatua bungeni
Katika Hotuba niliyotoa Bungeni tarehe 22 Mei 2013 kwa
nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nilieleza kwa kirefu
kuhusu kashfa hizo na hatimaye nikaeleza kwa niaba ya wenzangu kwamba
“Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwanini mpaka sasa
haijatekeleza maazimio hayo na bunge liweke muda wa ukomo wa kutekeleza
Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia katika sakata hili la
Richmond ili mara moja na daima sakata hili la Richmond limalizwe na
kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa ukamilifu. Ikiwa
maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika mpaka mwaka 2013
kwa miaka mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba maazimio mengine
mapya yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa wakati na kwa
ukamilifu?”
Aidha,
nikaendelea mbele kueleza kwamba “matumizi mabaya ya rasilimali za umma
hayako katika mikataba ya kukodi mitambo ya umeme tu, bali katika
ununuzi wa huduma za kisheria. Hivyo, narudia kutoa mwito kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni kiasi cha fedha kilichotumika
kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua
zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi
yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo
serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali”.
Katika
Hotuba hiyo bungeni nilikumbusha pia kwamba, “mwaka 2011 Benki ya
Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua
kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na.
ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na
riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya Mkono
(inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea
Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa
kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani
kuhusu suala hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye
usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa
Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama.
Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia gharama hizo na ni kiasi gani
Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na zingine mpaka hivi sasa?”.
Tarehe
25 Mei 2013 badala ya Waziri Muhongo kutoa majibu ya ukweli hatua
ziweze kuchukuliwa mapema kulinusuru taifa na mzigo wa madai akatoa
majibu ya uongo kwamba “sasa hivi tunaongelea uchumi na maendeleo na
ndiyo maana ukinitajia hapa mlolongo wa kesi ukategemea nikapukue
mafaili Wizarani, nadhani kuwa kwanza ni mbunge wa kuteuliwa na nikapewa
uwaziri nadhani hawakunituma pale kupekua mafaili”.
Matokeo
ya uongo huo ni Bunge kucheleweshwa kuingilia kati kabla ya hukumu
iliyotolewa tarehe 12 Februari 2014 ya kesi iliyofunguliwa na Benki ya
Standard Chartered (SCB) Hong Kong dhidi ya TANESCO kwenye Mahakama ya
Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) iliyopo nchini
Uingereza.
Kwa
kuzingatia kuwa hukumu hiyo imetoa miezi mitatu kwa pande mbili
kukubaliana nje ya mahakama hadi Mei 2014; Waziri Muhongo anapaswa
kujitokeza mbele ya umma kufuta kauli yake ya uongo aliyoitoa bungeni.
Waziri
Muhongo atumie fursa hiyo kueleza pia hatua ambazo yeye na wenzake
katika Serikali wanakusudia kuchukua kuhakikisha kwamba mazungumzo
yanayoendelea kwa siri hivi sasa kuhusu taratibu za kukokotoa gharama
halisi hayabebeshi mzigo kwa nchi na wananchi.
Waziri
Muhongo akiendelea kusema uongo kuhusu ‘kashfa ya IPTL’ na zingine
nitawataja kwa majina vigogo wa Serikali na CCM walionyuma ya kashfa
hizo ili waweze kuhojiwa kwa umma.
Nitachukua
hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka ni ya wananchi,
Serikali inafanya kazi kwa niaba ya wananchi; hivyo pale ambapo Serikali
inachelewa kuchukua hatua kutokana na udhaifu, uzembe, ufisadi au uongo
ni muhimu wananchi wakashiriki kutaka uwajibikaji.
John Mnyika (Mb)
05/03/2014
No comments:
Post a Comment