Dk. Harrison Mwakyembe.
Mjadala mkali ulizuka kwa juzi na jana kwenye Bunge hilo, huku baadhi ya wajumbe wakitaka uhuru wa wananchi kupata habari uwapo kwa waandishi kuruhusiwa kuingia kwenye kamati na wengine wakiwamo wajumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekiti wakipinga vikali kwa kutaka waandishi wapewe taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kamati husika.
Kifungu cha 57 fasili ya kwanza ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, kinaeleza kuwa vikao vyote vya kamati vitakuwa vya faragha na hakuna mtu yeyote asiyekuwa mjumbe wa kamati, mtumishi wa Bunge au mtaalam aliyeitwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum atakayeruhusiwa kukaa katika sehemu yoyote ya ukumbi wa mikutano ya kamati wakati kikao cha faragha kinaendelea.
Fasili ya tatu, inaeleza kuwa bila kuathiri masharti ya kanuni hii Mwenyekiti wa Kamati ya mjumbe yeyote kwa idhini ya Mwenyekiti anaweza kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mambo yaliyojitokeza kwenye kikao cha kamati.
Baadhi ya wajumbe waliiomba kuwasilisha mapendekezo yao kwenye kifungu hicho, walitaka waandishi wa habari kuruhusiwa kwani kwa kuwazuia ni kwenda kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotaka kuwapo kwa uhuru wa kupata taarifa.
OLUOCH
Ezekiel Oluoch alisema anashauri vikao viwe wazi kwani hakuna jambo la siri la kujifungia kwani wananchi wana haki ya kujua kinachojadiliwa kwenye kamati na kwamba ni vyema kamati zikawa huru.
HALIMA MDEE
Halima Mdee alisema wenye jukumu la kuzitengeneza kanuni ni wajumbe na kwamba awali kamati ya kanuni na kumshauri mwenyekiti baada ya majadala mkubwa kamati ilipendekeza waandishi waruhusiwe kuingia kwenye vikao, na ikakubaliwa kwenye vikao vya kamati ambavyo vitakuwa na mijadala mikubwa na watakapokuja kwenye Bunge watafanya majumuisho kwenye manbo yaliyojadiliwa.
“Tulikubalina watu watakaokatazwa ni wananchi wa kawaida kutokana na
udogo wa kumbi, ila waandishi wa habari wakubaliwe, sisi ndiyo tunaopitisha kanuni na sisi tuliridhia ilikuwa ni matarajio yetu,”
alisema.
Alisema waliotajwa kwenye kanuni waruhusiwe kuingia na utaratibu utakaotumika uamuliwe na mwenyektii wa kamati kushauriana na makamu mwenyekiti.
“Waandishi wa habari waingie mnaogopa nini, mnaficha nini?...hii Katiba ni ya wananchi wana haki ya kujua kila kinachoendelea ndani ya kamati na nje ya kamati na kwenye ukumbi wa Bunge,” alisema Mdee.
MOSES MACHALI
Moses Machali alipendekeza fasili ya tatu ya kifungu hicho, ifutwe kwa kuwa inaweka kitanzi kwa uhuru wa wananchi kupata habari na hakimlazimishi mwenyekiti au makamu kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Alisema vikao vyote vifanyike kwa uwazi bila kuzuia mtu ingawa hawataruhusiwa kushiriki kwenye mjadala wa kamati.
“Hao wanaosisitiza kura ya wazi halafu mnaogopa na kuwakataa waandishi wa habari mnaficha nini, sioni sababu ya msingi,” alisema Machali.
MARIA SARUNGI
Maria Sarungi alisema vikao vya kamati viwe wazi kwa waandishi wa habari kwa kuwa Rasimu ya Katiba itakwenda kwao kwa ajili ya kuipigia kura.
“Mwanzo wa Rasimu ya Katiba unasema kwakuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua...Katiba hii si ya kwetu tuliokaa humu ndani bali ya wananchi wa Tanzania, mchakato ulivyoanza ilianza kwa wananchi hadi tulipofika,” alisema.
FREEMAN MBOWE
Freeman Mbowe alisema Katiba inayotungwa ni ya wananchi na wanaowakilishwa ndani ya Bunge hilo wanataka kujua kila kinachoendelea ndani ya Bunge hilo.
“Tusifikiri tunahitaji kuridhiana sisi wenyewe tulioko ndani ya Bunge hili kuna Watanzania kwa mamilioni wa vyama na taasisi mbalimbali wanatisikiliza,” alisema.
Wakati wajumbe huyo anazungumza, baadhi ya wajumbe walipiga kelele na kuzomea hali iliyomlazimu kuacha kuzungumza na mwenyekiti kumsihi kuendelea, lakini Mbowe alisema: “Siwezi kuendelea wakati wajumbe wanapiga kelele.”
MAHALU
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekti wa Muda,Prof. Costa Mahalu, alisema kamati yake inapeleka mapendekezo kwa wajumbe na wenye maamuzi ni wajumbe na baadaye wanaagizwa kurekebisha mwafaka uliofikiwa na kuonyesha msimamo wao kwa pamoja.
Mjumbe wa Kamati, Bakari Khamis Bakari, alisema hakuna uhuru usiokuwa na kinga kulingana na maelezo ya maeneo husika na kwamba kamati italichukua suala hilo na kujadailiana ili kupata namna bora ya kuruhusu waandishi wa habari kuchukua habari.
George Simbachawene, mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekiti, alisema maoni ya kamati ni kuwa hisia na sababu wanazotoa wajumbe hao zilikuwapo kwenye kamati yao na walipenda waandishi waruhusiwe ili mchakato huo uonekane kwa umma wote.
“Kilichotushinda na kufikia uamuzi wa maoni hayo ni utekelezaji wake...kwa busara yetu tukaliwekea utaratibu kwenye fasili ya tatu, vyombo vyetu vya habari ni vingi, kamati iko ukumbi wa Msekwa asubuhi anakuja mwandishi anachukua anapeleka, habari zitakazokwenda juu ya hoja moja jambo moja zitakuwa hazijakamilika zitawachanganya wananchi na si kuwasaidia,” alisema.
Alisema waandishi watachukua habari kivyao na kuwachanganya wananchi na ndiyo maana wameamua mwenyekiti wa kamati atoe taarifa kwa waandishi.
DK. MWAKYEMBE
Dk. Harrison Mwakyembe alisema kitaaluma ni mwandishi wa habari na mwanasheria na kwamba anaona hakuna haja ya waandishi wa habari kuruhusiwa kuwepo kwenye kamati na badala yake wapewa taarifa na mwenyektii wa kamati husika.
Hata hivyo, baadhi ya watoa hoja, walipinga hatua hiyo huku wanaopinga waandishi kuingia kwenye ukumbi wakishangilia kwa kupiga meza kusisitiza waandishi kunyimwa kuingai kwenye kamati hizo, huku wachache wa vyama wa upinzani wakipinga uamuzi huo.
DK. TULIA ACKSON
Mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri mwenyekiti, Dk. Tulia Ackson, alisema hakuna uhuru usiokuwa na mipaka na kwamba kamati inapendekeza kifungu hicho kubaki jinsi kilivyo.
Hoja hiyo ilimalizika kwa wajumbe kupitisha kifungu jinsia kilivyo kuwa waandishi hawataruhusiwa kuingia kwenye kamati na badala yake watapewa taarifa na mwenyektii wa kamati.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment