Dk. Hamisi Kigwangalla
Balozi Augustino Mahiga
Profesa Sospeter Muhongo
Dk. Harrison Mwakyembe
Komredi Mwigulu Nchemba
January Makamba
Na Daniel Mbega
RAIS Dk. John Magufuli amewapa uwaziri makada 6 kati ya 37
ambao walishindana naye mpaka hatua ya mwisho kuwania uteuzi ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Ndani ya makada hao sita, pia wamo wawili kati ya nane ambao
walikuwamo kwenye Kamati ya Kampeni ya CCM iliyoundwa na wajumbe 32.
Waliokumbukwa na Dk. Magufuli kwa utendaji wao makini ni Profesa
Sospeter Muhongo, Balozi Augustino Mahiga, Dk. Harrison Mwakyembe, Mwigulu
Nchemba, January Makamba na Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mwigulu na Dk. Mwakyembe walikuwemo kwenye Kamati ya Kampeni
iliyoundwa Agosti 17, 2015 ikiwahusisha makada wengine sita ambao pia waliwania
kuteuliwa kugombea urais.
Makada hao ni Dk. Asha-Rose Migiro, Bernard Membe, Samuel
Sitta, Makongoro Nyerere, Steven Wasira na Lazaro Nyalandu. Hata hivyo, Migiro,
Membe, Sitta na Makongoro hawakugombea ubunge safari hii, lakini Wasira
alibwagwa vibaya na Ester Bulaya wa Chadema katika Jimbo la Bunda Mjini, wakati
ambapo Nyalandu, licha ya kushinda ubunge Singida Kaskazini, ameshindwa
kurejeshwa kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo bado haijapata waziri
kamili.
Wajumbe wengine wawili wa kamati hiyo – Nape Nnauye na Ummy
Mwalimu – nao wamekumbukwa kwenye uwaziri.
Wajumbe
wengine kwenye kamati hiyo walikuwa Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana
(ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti), Rajab Luhwavi (Makamu Mwenyekiti – Bara),
Vuai Ali Vuai (Makamu Mwenyekiti - Z’bar), Sophia Simba, Mohamed Seif Khatib,
Amina Makillagi, Christopher Ole Sendeka, Abdallah Majura Bulembo, Hadija
Aboud, Mohamed Aboud, Issa Haji Ussi, Waride Bakari Jabu, Mahmoud Thabit Kombo,
Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Maua Daftari, Stephen Masele, Pindi Chana, Shaka
Shaka, Sadifa Juma Khamis, Antony Diallo na Livingston Lusinde.
Wajumbe watatu katika kundi hilo - Shamsi Vuai Nahodha (Kijitoupele), Livingstone Lusinde
(Mtera) na Stephen Masele (Shinyanga Mjini) – wamerejea bungeni, lakini Masele
na Nahodha ‘hawakukumbukwa’ licha ya kuwemo kwenye baraza lililopita.
Profesa Sospeter Muhongo amerejeshwa kwenye Wizara ya
Nishati na Madini ambako Januari 24, 2015 alijiuzulu kufuatia kashfa ya
uchotaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, lakini Balozi Augustino Mahiga
amekabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje, EAC na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk. Mwakyembe amerejea lakini akikabidhiwa Wizara ya Katiba
na Sheria, wakati Mwigulu Nchemba amekuwa waziri kamili na kukabidhiwa Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Katika baraza lililopita alikuwa naibu waziri wa
Fedha akishughulikia uchumi.
January Makamba amepandishwa na sasa ni Waziri katika Ofisi
ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira wakati Dk. Kigwangalla
ameingia kwa mara ya kwanza na kuwa naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Magufuli
kweli kiboko. Kati ya mawaziri 38 waliokuwemo kwenye serikali iliyopita kwa
nyakati tofauti amewachukua 12 tu na kuwatosa 26 katika baraza lake lenye
wizara 18.
Mbali
ya Dk. Mwakyembe, Profesa Muhongo, Makamba na Mwigulu, wengine waliobahatika
kuingia kwenye serikali ya awamu ya tano ni Dk. Hussein Ali Mwinyi (Kwahani) aliyerejeshwa Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Jenista Mhagama (Peramiho) ambaye amerudishwa Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, George
Simbachawene (Kibakwe) aliyekuwa Nishati na Madini, ambaye sasa atakuwa Ofisi
ya Rais pamoja na Angela Kairuki wakishughulikia Utumishi na Utawala.
Wengine ni William Lukuvi (Isimani) amebaki kwenye Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Makazi, Charles Kitwanga ‘Mawe Matatu’ (Misungwi) amepandishwa
na kupewa Wizara ya Mambo ya Ndani, Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), ambaye
alikuwa naibu katika Wizara ya Nishati na Madini, amepandishwa na kuwa Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, na Ummy Mwalimu aliyerejeshwa katika Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto lakini sasa atashughulikia pia Afya na
Wazee.
Waliotemwa
ni Juma Nkamia, Mahmoud Mgimwa, Prof.
Anna Tibaijuka (ambaye alifukuzwa
kufuatia kashfa ya Escrow), Diodorius Kamala, Daniel Nsazugwako, Prof. Jumanne
Maghembe, Dk. Mathayo David, Dk. Mary Nagu, Janet Mbene, Dk. Hadji Mponda, Dk.
Charles Tizeba, Dk. Seif Rashid, Lazaro Nyalandu, Andrew Chenge, Dk. Raphael
Chegeni na Ezekiel Maige.
Wengine
ni William Ngeleja, Sophia Simba, Hawa Ghasia, Kapteni George Mkuchika, Gerson
Lwenge, Dk. Shukuru Kawambwa, Margret Sitta, Shamsi Vuai Nahodha na Saada Mkuya Salum aliyekuwa Waziri wa
Fedha.
Lakini
Magufuli amehakikisha mrithi wake katika Jimbo la Chato, Dk. Medard Matogolo
Kalemani anaingia kwenye baraza hilo ambapo atamsaidia Profesa Muhongo katika
Wizara ya Nishati na Madini kama ilivyo kwa Angelina Mabula wa Jimbo la Ilemela
ambaye naye ni naibu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi akimsaidia Lukuvi.
Injinia Stella Manyanya (Nyasa) naye ameingia kwenye
baraza hilo akiwa naibu waziri wa Wizara
ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi huku waziri akiwa haijapatikana kama
ilivyo kwa Injinia Ramo Matala Makani (Tunduru Kaskazini), ambaye ni naibu
katika Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo
haijapata waziri.
Edwin Amandus Ngonyani (Namtumbo) amekuwa
naibu waziri katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano iliyokuwa ikiongozwa na Magufuli mwenyewe ambayo nayo bado haina
waziri, wakati Luhaga Mpina (Kisesa) atamsaidia Makamba katika Wizara ya
Muungano na Mazingira.
Mbunge
pekee wa CCM mkoani Arusha, William Tate ole Nasha (Ngorongoro) ameteuliwa kuwa
naibu waziri katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi akimsaidia Mwigulu,
wakati Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashantu Kijaji, amekuwa naibu waziri wa
fedha, wizara ambayo bado haijapata waziri.
Kwa upande mwingine, Balozi Mahiga atasaidiwa na Dk. Suzan
Kolimba katika Wizara ya Mambo ya Nje na EAC na Uhusiano wa Kimataifa.
0656-331974
www.brotherdanny.com
No comments:
Post a Comment