BARAZA LA WAWAKILISI LA ZANZIBAR
MAONI YA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR JUU YA KATIBA MPYA
1.0Utangulizi
Kwa
niaba ya Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar naomba
kuchukua nafasi ya kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania
kwa umakini mkubwa inayochukua katika kupata maoni thabiti ya wananchi
kuhusiana na Katiba wanayoitaka. Pia naishukuru sana Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kutupa nafasi Baraza la Wawakilishi, kama taasis, kutoa maoni
yake kuhusiana na Katiba inayofaa itumike kwa ajili ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Badala ya Katiba iliopo sasa.
Baraza
la Wakilishi limekuwa linafatilia kwa makini utoaji wa maoni ya
wananchi mmoja mmoja na vikundi kuhusiana na Katiba inayohitajika katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kutafakari, katika kikao cha
Wajumbe wote na katika vikao mbali mbali vya Kamati yake ya Uongozi, na
kuona hali halisi ya maoni inavyoendelea na ufanisi mkubwa unaopatikana,
Baraza la Wawakilishi linaamini kuwa maoni yaliyotolewa tayari yameweka
wazi yale mambo muhimu ambayo wanachi wanapenda yazingatiwe katika
kupata Katiba mpya.
Na kwa kuzingatia pia kuwa,
katika hatua iliyopo sasa ya maoni ya wananchi ambapo hayajalolewa
mwelekeo wake rasmi ni vigumu sana kwa Wajumbe wa Baraza kufikia
makubaliano ya maoni ya Baraza kikamilifu (detailed opinion) hata kwa
yale mambo ambayo kwa ujumla wake Wajumbe wa Baraza wanakubaliana kwa
pamoja.
Kutokana na ukweli huo, Wajumbe wa
Baraza wameeonyesha mwelekeo wao wa kijumla juu ya mambo wanayoamini
kuwa yanahitajika kuingia kwenye Katiba mpya ya Jamhuri nya Muungano wa
Tanzania. Mambo ya msingi ambayo Wajumbe wa Baraza kwa ujumla wameyaona
na kuitaka Kamati yao ya Uongozi kuyawasilisha kwenye Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ni kama yanavyoelezwa hapa chini.
2.0Maoni Yenyewe
Baraza
la Wawakilishi la Zanzibar linaamini kuwa suala la namna ambavyo Katiba
mpya ya Tanzania inapaswa iwe litajitokeza wazi wazi zaidi katika maoni
ya wananchi. Kwa upande wake Baraza la Wawakilishi, kama Taasisi ya
kuwawakilisha wananchi, linajitayarisha kusimamia zaidi juu ya mambo ya
msingi ambayo Wanzibari na Watanzania walio wengi wameonyesha umuhimu wa
kuingizwa kwenye Katiba ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata
hivyo, Baraza la Wawakilishi lenyewe limeangalia baadhi ya mambo ambayo
linahisi ni muhimu ambayo kama Wanazibari wangependa yawe ni misngi
muhimu ya kikatiba katika Katiba ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:
2.1 Misingi ya Muungano na Utaifa
Kwa
sababu Wazanzibari ni waumini wa Muungano haukuondoa na hautoondoa
uwepo wa Zanzibar kama nchi, ni vyema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ijayo iweke wazi kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano
inayotokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Hali hii itahakikisha kuwepo na maeneo maalum ya mamlaka ambayo Zanzibar
ina uwezo nayo kama nchi (yaani, Mamlaka ya Dola ya Zanzibar).
2.2 Mgawanyo wa Mamlaka za Muungano
Kwa
sababu inapendekezwa kuwepo na Mamlaka ya Zanzbar huru na Mamlaka ya
Tanganyika huru ndani ya Jamhuri ya Muungano, Mamlaka ya Muungano iwekwe
wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake. Mambo yote
hayo yawekewe wazi na mipaka yake.
2.3 Usawa wa Ushirikishwaji katika Mamlaka ya Muungano
Uwepo
wa Muungano uonekane katika hali zote – uundwaji wa Mamlaka za
Muungano, ufanyaji kazi katika Mamlaka za Muungano, ufanyaji wa maamuzi
katika Mamlaka za Muungano, na uingizwaji na upunguzwaji katika orodha
wa mambo ya Muungano.
Kwa mfano, maamrisho kama
yale yaliyopo sasa kwenye Ibara ya 64(4) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania 1977, ambayo yanawezesha jambo kufanywa la Muungano
bila ya kuishirikisha katika maamuzi Mamlaka ya Zanzibar, yasiwe na
nafasi tena ya kutokea kwa mujibu wa Katiba ijayo ya Jamhuri ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Katika ushirikishwaji,
Katiba itamke wazi kuwa uwepo uwiyano ulio wazi wa viongozi na
watendaji katika utumishi wa Mamlaka za Muungano. Yaani, kwa mfano,
endapo Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, Makamo wa Rais
atoke upande mwengine.
Mamlaka ya viongozi
wakuu wa Muungano yawekwe bayana ndani ya Katiba; na uwepo utaratibu wa
kubadilishaji nafasi hizo kwa pande mbili za Muungano. Yaani, upande
unaotoa Rais kwa kipindi fulani, uje kutoa Makamo wa Rais kwa kipindi
kingine, na kadhalika.
2.4 Mfumo wa Kutunga Sera na Sheria za Muungano
Utungaji
wa sera na sheria za Muungano isiwe ni jambo la kuzingatiwa na
kutekelezwa na Mamlaka za Muungano pekee. Kama tulivyoelezea hapo awali
kuwa uwepo ushirikishwaji wa sehemu (Dola) mbili huru katika kufanya
maamuzi na uendeshaji wa Mamlaka ya Muungano.
Ushirikishwaji huo ni lazima udhihirike katika maamuzi yatakayopelekea kuundwa kwa sera na sheria zote za mambo ya Muungano.
2.5 Umiliki wa Rasilimali za Muungano
Rasilimali
za Muungano iwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilimali hizo
ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa
rasilimali ufanye kwa uwiyao maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande
mbili za Muungano. Neno rasilimali katika maudhui haya linajumuisha pia
miundombini inayojengwa kutokana na rasilimali za Muungano.
2.6 Kuwa na Muungano wa Dhati
Jambo
kubwa zaidi ya yote linalohitajika lionekane kwa maneno (maamrisho ya
Katiba) na vitendo ni haja ya kuwa na Muungano wa kweli, hata kama ni
kwa maeneo machache, kwa dhati ya wanasiasa na watanzania kwa jumla.
Hali inaweza kupatikana kwa kuzingatia Misingi ya Katiba iliyoainishwa
hapo juu ambayo yanaweka mkazo juu ya haki na maslahi ya pande mbili za
Muungano ya kujiamulia hatma za mambo yao yote, ya kiuchumi, ya kijamii
nay a kisiasa.
2.7 Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
Kuhusu
muundo unahitajika katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, Baraza la
Wawakilishi halikufikia maamuzi maalum. Katika mtazamo wa Baraza kama
taasisi, Muungano wa Tanzania unaweza kuchua muundo wo wote kwa
kuzingatia misingi ya Katiba iliyoelezewa hapo juu.
3.0 Hitimisho
Ni
imani ya Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, kuwa misingi ya Katiba
ambayo imeelezewa hapa kwa ufupi sana ni muhimu sana katika kujenga
Jamhuri ya Muungano iliyo imara na yenye kuonyesha dhamira halisi ya
kuwepo na Muungano endelevu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maoni
haya ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar yamewasilishwa na Spika wa
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa idhini ya Kamati ya Uongozi na
Shughuli za Baraza ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar leo Jumanne,
Februari 5, 2013.
………………………
Pandu Ameir Kificho
Spika
Baraza la Wawakilishi
Zanzibar
No comments:
Post a Comment