Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi wakati akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kabla hajavuliwa nyadhifa zote.
Alhaji Jumbe wakati alipotimiza miaka 93 mwaka 2013.
Na
Daniel Mbega
WAKATI
wajumbe wa Bunge la Katiba bado wanaendelea kutafuna kodi za wananchi kwa wiki
ya nne sasa bila hata kuanza kuijadili Rasimu ya Katiba Mpya, kuna jambo ambalo
naamini linahitaji tafakuri.
Tangu
mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya ulipoanza, Watanzania wengi (Wa Bara
na Visiwani) wameelekeza maoni yao kwenye muundo wa Serikali ya Muungano huku
walio wengi wakitaka serikali tatu.
Lakini
kuna mtu mmoja ambaye alikuwa sehemu kubwa ya utawala wa Visiwa vya Zanzibar kwa
takriban miaka 12 ambaye kwa hakika leo ama anaweza kuitwa shujaa au nabii kwa
haya yanayotokea.
Huyu
si mwingine bali ni Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Pili wa Zanzibar ambaye
pia alifanya jitihada kubwa wakati wa mapinduzi hayo na miaka nane baadaye.
Jumbe,
ambaye aliingia madarakani Aprili 11, 1972 ana historia ndefu ya siasa za Visiwa
hivyo, na mtazamo wake unawafanya mpaka leo wengi wajiulize kama ni shujaa,
mpinga Muungano ama mtu aliyekata tamaa.
Kwa
sasa kiongozi huyo, ambaye yuko kitandani kwake Mji Mwema akisumbuliwa na
maradhi mbalimbali, hasikiki kabisa na hakuna anayejisumbua kumzungumzia.
Tukio
la kujiuzulu kwake kwa shinikizo miaka 29 iliyopita linaweza kuwa ni historia
nyingine ngumu kuelezeka kwa siasa za Tanzania. Nakumbuka hata mimi, ambaye
wakati huo nilikuwa shuleni, sikuweza kuelewa kiini hasa cha kujiuzulu kwa
kiongozi huyo, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano.
Kwa
kipindi ambacho nchi nyingi zilikuwa ndiyo kwanza zimetoka katika makucha ya
ukoloni huku zikipigania kujenga chumi zao changa, tukio la kujiuzulu kiongozi
lilionekana geni sana, ingawa huko nyuma tulikuwa tumeshuhudia viongozi kadhaa
wakijiuzulu, akiwemo Alhaj Ally Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu mwaka 1978
kufuatia wimbi la mauaji ya watu, hasa vikongwe, kule Shinyanga.
Hata
hivyo, suala la kujiuzulu kwa Jumbe halikuweza kujadiliwa mitaani kwa kipindi
kile, tofauti pengine na kipindi hiki ambapo watu wangeweza hata kutoa hoja zao
nyingi kuhusiana na kiini cha kujiuzulu kwake.
Kwa
kipindi ambacho ilikuwa vigumu kunyoosha kidole hata kwa mtendaji wa kijiji,
hakika ingekuwa vigumu kama kuuhamisha Mlima Kilimanjaro kwenda Dodoma kuhoji
uamuzi wa kiongozi wa juu kama rais.
Jambo
la msingi kuhusiana na kujiuzulu kwake ni kutambua kwamba Jumbe alitaka, na
hata kesho angetaka, kuona Nyaraka za Muungano zinapitiwa upya ili kuleta usawa
wa pande zote mbili zilizounda Muungano huo, Bara na Visiwani.
Ingawa
yeye pia alishiriki katika maandalizi ya Nyaraka hizo, lakini hakuwa na mamlaka
ya juu kipindi hicho kwa vile alikuwa chini ya mtu, na miaka takribani 20
baadaye aliona kuna haja ya kufanya mapitio mapya kuona Zanzibar inapewa
heshima yake katika baadhi ya masuala yaliyoonekana kuingiliwa na Serikali ya
Muungano.
Ndiyo
maana hata katika kitabu chake cha Tanganyika and Zanzibar: The Partner-ship
alichokitoa mwaka 1994, miaka 10 baada ya kujizulu kwake, alielezea kwa kirefu
ni kwanini alitaka yafanyike mapitio ya Nyaraka za Muungano.
Anasema
alimweleza Mwalimu Nyerere wakati wa kuadhimisha miaka 20 ya Mapinduzi Januari
12, 1984 kwamba kulikuwa na kero ambazo Wazanzibari waliona zilistahili
kuzungumzwa ili kuimarisha Muungano huo.
Alikuwa
amejiandaa kuelezea kwa kirefu kero hizo kwenye vikao husika, lakini kabla ya
hapo akaandaa waraka uliopaswa kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere.
Kwa kuwa waraka ule ulikuwa umeandikwa kwa mkono, tena kwa lugha ya Kiingereza,
alimpa mtu kuuchapa. Ukapotea katika mazingira ya kutatanisha.
Lakini
ajabu ni kwamba, siku chache baadaye aliitwa Ikulu kwa Mwalimu Nyerere na
alipokwenda akashangaa kuukuta waraka ule ule aliouandika mwenyewe kwa mkono
wake ukiwa mkononi mwa Nyerere! Namna ulivyofika mimi, wewe na hata yeye
mwenyewe hatujui, lakini Mwalimu angekuwa hai leo angeweza kutueleza
aliupataje, kama tungekuwa na haja ya kujua hilo.
Na
kwa vile tayari Jumbe alikuwa ameonyesha nia yake ya kujiuzulu wadhifa wa Rais
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu alimwambia
kwamba kama isingekuwa kwa waraka aliokuwa nao mkononi, katu asingekubali
kujiuzulu kwake, lakini kwa yale aliyokuwa ameyaainisha kuhusu Muungano, naye
alikuwa radhi kuona anajiuzulu.
Ndipo
Januari 30, 1984, katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kule Dodoma, akaamua
kujiuzulu nyadhifa hizo. Ali Hassan Mwinyi, mtu aliyekuwa akiiunga mkono
Tanzania Bara, akachukua madaraka na watu kadhaa walioonekana kuwa wapinzani
wakakamatwa.
Mwinyi
akaanzisha mfumo wa usawa Visiwani na Bara kabla hajawa rais wa Muungano mwaka
1985 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka huku Zanzibar ikiongozwa na
Idris Abdul Wakil Nombe. Mwaka 1990 Dk. Salmin Amour Juma akachaguliwa Rais wa
Zanzibar; akarejea tena madarakani katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi
mwaka 1995 ambao unadaiwa haukuwa huru na wa haki.
Aboud
Jumbe alipochukua urais baada ya mauaji ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume mwaka
1972, jamii yote ilitegemea kwamba mambo ya kale yalikuwa yamefikia kikomo.
Na
kwa kiasi fulani ndivyo ilivyokuwa, kwani utawala wake ulilegeza baadhi ya
mambo kuliko ule uliotangulia, lakini kwa kuwa alikuwa chini ya Baraza la
Mapinduzi, alipaswa kutekeleza baadhi ya sera ngumu zilizokuwepo, pale
ilipobidi, kwa utashi wa washirika wake katika uongozi.
Wazanzibari
wanakumbuka kwamba mlongo mmoja wa utawala wake ulitawaliwa na hali ya Zanzibar
kuegemea zaidi Bara na mwaka 1977 akaongoza muungano wa vyama vya Afro-Shiraz
na kile cha Tanganyika African National Union (TANU) cha Bara kuzaa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), chama ambacho bado kinaendelea kushika hatamu za uongozi hata
leo.
Lakini
kwa kiasi kikubwa, chini ya Jumbe watu walikuwa na uhuru na waliweza kusafiri
ulimwenguni bila matatizo makubwa tofauti na serikali ya ‘mkono wa chuma’ ya
hayati Karume. Hali hii ikamfanya kuwa kipenzi cha Wazanzibari wengi.
Jumbe
huyu pia akafungua taasisi mbalimbali za elimu Tanzania Bara kwa ajili ya
Wazanzibari waliopenda kuchukua elimu ya juu. Hali hii iliwawezesha Wazanzibari
kufika mbali zaidi kielimu badala ya kusomea ualimu, taaluma pekee ambayo
walikuwa na uwezo wa kuipata.
Siku
za nyuma, nafasi za uongozi serikalini zilikuwa zikitolewa kwa watu waliokuwa
kwenye mfumo wa chama tu, na zaidi ya kazi ya ualimu hakukuwa na uwezekano
wowote wa watu kupata elimu ya juu zaidi.
Mnamo
mwaka 1979, Jumbe aliweka historia kwa kufungua taasisi ya kwanza ya
kidemokrasia, Baraza la Wawakilishi, lakini wajumbe wa baraza hilo walikuwa
wakiteuliwa badala ya kuchaguliwa na wananchi wenyewe. Pia alifungua utawala
wake kwa watu, ambao wangeweza kuwa pembeni kama kanuni ngumu za mapinduzi
zingezingatiwa kama ilivyokuwa awali.
Hatua
hii, ambayo baadaye alijikuta akiijutia, ndiyo iliyokuwa chanzo cha kuanguka
kwake. Alikuwa haelewani na wale waliojulikana kama ‘Kamati ya Watu 14’ ambayo
iliwahusisha watu wengi walioshiriki kwenye Mapinduzi. Ushawishi wao ulianza
kupungua na madaraka yao yakaanza kuhojiwa.
Katika
jaribio lake la kutaka kuokoa jahazi kutokana na matatizo hayo akawatema
wajumbe wengi katika serikali yake na kufanya jaribio la kujitenga kutoka
katika serikali moja kuu kwa Tanzania nzima. Lakini mwaka 1984 akalazimishwa na
Kamati Kuu ya CCM kujiuzulu.
Hatua
ya kujiuzulu kwake, kwa mwanamapinduzi inaweza kuchukuliwa kuwa ya kishujaa
kutokana na hoja zile alizokuwa akizitetea. Hakujutia uamuzi wake, ingawa
alisikitishwa kutokana na yale aliyokuwa ameyaainisha kushindwa kuwafikia
wananchi wengi, ambao ni dhahiri hata leo hii hawajui ni kipi hasa alichokuwa
akikipigia kelele.
‘Kwa
shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko’, ndivyo Waswahili wasemavyo.
Wale ambao hatukumwelewa Jumbe wakati huo tulimuona kama mtu aliyechanganyikiwa
kueleza kasoro hizo ambazo hazikuwa na mantiki yoyote kwa kipindi hicho huku
tukiendelea kuimba na kuzinadi sifa mbalimbali za viongozi wa chama na
serikali.
Lakini
leo hii yale ambayo alikuwa akiyasema Jumbe na kuyapigania tumeyaona Zanzibar.
Kero za Muungano zimekuwa nyingi mno kiasi cha kuifanya hali ya amani Visiwani
kuwa tete tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ambapo baadhi ya
wachunguzi wa masuala ya siasa wanadai kura ziliibwa ili Chama cha Wananchi
(CUF) kisitawale.
Kero
hizo ndizo zinazozidi kujenga ufa mkubwa hata ndani ya CCM Visiwani humo, na
ingawa viongozi wake wanajitahidi kuficha, ukweli bado unaendelea kubaki pale
pale kwamba kuna tatizo, tena kubwa.
Pengine
lingekuwa jambo la busara sasa kumpa heshima ya ushujaa Alhaj Jumbe kwa yale
yote aliyoyatenda enzi za utawala wake, pia hata kwa mawazo yake aliyokuwa
ameyaandika kwenye waraka ambao ulimfikia mhusika hata kabla ya kuusaini
mwenyewe.
Viongozi
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Muungano hawapaswi kupuuza kero
hizo kwa misingi ya kulinda chama, kwa sababu kama hazikutatuliwa siyo tu
zitauvunja muungano wenyewe, bali hata mustakabali wa chama utakuwa mashakani.
Binafsi
nasema Bravo Jumbe! Kwa sababu hoja zake alizozitoa ama kuziainisha miaka 30
iliyopita, ndizo zinazoonekana leo hii kutishia Muungano wenyewe.
No comments:
Post a Comment