BARAZA KUU LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA
TAMKO LA WAISLAMU TANZANIA
KUHUSU KADHIA YA TANZANIA KUJIUNGA NA OIC NA KUREJESHWA KWA MAHAKAMA ZA KADHI
BARAZA KUU LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA
I. UTANGULIZI
Tanzania
inapita katika kipindi cha mivutano mikubwa kati ya Waislamu kwa upande
mmoja, na serikali na Wakiristo kwa upande mwingine.
Tafauti
hizo ni juu ya uhalalali wa urejeshwaji wa Taasisi ya Waislamu ya
Mahakama za Kadhi na mchakato wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya misaada
ya Waislamu duniani Organization of the Islamic Conference OIC.
Historia
inaonesha kuwa kufutwa kwa Mahakama ya Kadhi mwaka 1963 kunatokana na
maamuzi ya Bunge kupitia The Magistrates Courts Act, 1963.
Suala
jingine ni uhalali na ubora kwa Jamuhuri ya muungano wa Tanganyika na
Zanzibari (Tanzania) kujiunga na Shirika la misaada la Waislamu duniani
OIC.
Kutokana na madai ya muda mrefu ya
Waislamu ya kutaka kurejeshwa Mahakama ya Kadhi nchini, Bunge la
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilitoa jukumu kwa Kamati ya Katiba na
Sheria kushughulikia suala hilo chini ya uongozi wa Muheshimiwa Arcado
Ntagazwa mwaka 1994. Mwaka 2004 kamati iliendelea na jukumu hilo chini
ya uongozi wa Muheshimiwa Athumani Janguo.
Suala hili pia lilijitokeza katika Ilani ya Chama tawala CCM kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005.
Kamati
hiyo chini ya uongozi wa awamu zote mbili ilikutana na Jumuiya za
Kiislamu kwa uelewa halisi wa suala husika na vilevile wadau wengine kwa
faida za kiutendaji.
Taarifa tulizonazo ni kwamba waraka wa kamati hiyo uliwasilishwa kwa Spika wa Bunge (wa wakati huo) Mh. Pius Msekwa.
Novemba
11, 2007 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika hafla ya
‘kusimikwa’ Askofu mkuu wa Kanisa la KKKT Alex Malasusa aliwataarifu
watanzania kuwa mapitio ya vyombo husika juu suala la Mahakama ya
Kadhi yamekamilika, akaongeza kuwa wananchi watapatiwa jawabu ya suala hili Februari mwakani, yaani 2008.
Tokea
mchakato wa suala hili uanze, na mpaka Rais Kikwete alipotoa tarehe ya
kutoa jawabu katika hafla iliyotajwa hapo juu, ni zaidi ya miaka 13
sasa. Aidha, suala la OIC nalo limepewa urasimu wa aina yake.
Mwaka
1993 Zanzibar ambayo ni moja ya nchi zilizounda serikali ya muungano
inayoitwa Tanzania, iliamua kujiunga na OIC kama Zanzibar. Tanzania
bara ilipinga kwa hoja kuwa ni vema ufanyike utafiti wa kina ili maamuzi
ya kujiunga au kutojiunga yawe ya pamoja.
Baada
ya utafiti wa miaka 15 serikali ya Tanzania kupitia Waziri wake wa
mambo ya nje imetamka hadharani kuridhika kwake na sababu zote za
kujiunga OIC zikiwemo za kisheria na kiusalama.
Nchi
ambazo kwa muda mrefu raia wake wamekuwa wakifaidika kwa misaada ya OIC
ni pamoja na Benin, Cameroon, Cote d’Ivoire, Gabon, Guinea, Guinea
Bissau, Msumbiji, Nigeria, Sierra leone, Uganda, Urusi. Nchi hizi ni
sehemu ya nchi 57 wanachama wa OIC zikiwemo zenye idadi kubwa ya raia
Wakiristo.
Tarehe 24 Oktoba 2008 Maaskofu
Tanzania walitoa tamko kali kupinga Mahakama ya Kadhi na OIC. Wameionya
serikali kuwa endapo itaridhia kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi na nchi
kujiunga na OIC, mahusiano kati ya Wakristo na Waislamu yatavunjika na
uwezekano mkubwa wa kutokea umwagikaji wa damu.
Katika
masuala haya, Waislamu wameendelea kusimama kwenye rejea za Sheria,
Sharia, Mantiki na Historia. Wakristo wameendelea kusimama katika
wasiwasi wa kuwepo kwa itikadi yao na madai ya ‘uvunjwaji wa katiba’ ya
nchi. Serikali inaendelea kusuasua katika ahadi za muda mrefu na sura
isiyoeleweka.
Waraka huu ambao unakamilika kwa
Tamko la Waislamu, unapitia hoja zote tegemezi kwa Wakiristo, Waislamu
na mtazamo wa sheria za nchi ili kuitanabahisha serikali itekeleze ahadi
zote kama ilivyoahidi, kwa maslahi ya wananchi wote.
II. HOJA ZA MAASKOFU
1. Udini
Miongoni
mwa hoja za Maaskofu ni kuwa suala la Kadhi kutambuliwa na katiba ya
nchi ni kuleta udini miongoni mwa watanzania. Rejea gazeti la Msema
Kweli, na. 578 Jumapili, Septemba 28–Oktoba, 2008, uk. 5.
‘Akitoa
tamko hilo Jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Maaskofu wa Kipentekoste
nchini, Mwenyekiti wa PCT mkoani hapa Askofu David Mwasota alisema
katika awamu nne za uongozi wa nchi, kumekuwapo na juhudi za makusudi
kwa baadhi ya viongozi wa serikali, Wabunge na Viongozi wa Dini ya
Kiislamu kujaribu kushinikiza udini.’
‘Aliutaja
udini huo kuwa ni kutaka kuiingiza Mahakama ya Kadhi ndani ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano na pia Tanzania kujiunga na OIC.’
2. Ukiukwaji wa Katiba
Ukiukwaji
wa katiba ni moja ya madai ya Maaskofu katika kupinga kurejeshwa kwa
Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC. Rejea gazeti la Jibu la
Maisha, na.37, Jumapili, Septemba 28 Oktoba 4, 2008, uk. 2.
‘Na
wala hatutaki kabisa kuona kinaingizwa kipengele cha kuwa na Mahakama
ya Kadhi ndani ya Katiba, maana kwa kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la Novemba 1, 2000,
Sehemu ya Pili Ibara ya 9 kifungu ‘a’ na Ibara ya 20 (2) a. Kukiuka
vifungu hivyo, kutasababisha uvunjifu wa amani na kubomoa mihimili mikuu
ya utulivu iliyosimamishwa ndani ya nchi yetu.’
3. Uvunjifu wa Amani
Maaskofu pia wametowa hoja ya uvunjifu wa amani, rejea gazeti la Utatu, Na 044, Jumapili, Septemba 28 - Okotoba 4, 2008 uk. 5.
‘Kwa
kuwa Katiba ya nchi yetu hairuhusu serikali ya kidini hatujui
linalotafutwa ni nini hasa na serikali kuendelea kuachilia jambo kurudia
rudia bungeni, inaashiria nini, hata kama jambo limekubaliwa na chama
tawala katika ilani yake, lakini suala hili si la kichama, bali ni la
kitaifa na halina maslahi kitaifa maana lina malengo ya kuwagawa
Watanzania kidini, hivyo kuchafua amani tunayojivunia muda mrefu.’
4. Kunajisi Katiba
Maaskofu
pia wamefika mbali zaidi kwa kutowa hoja kuwa kuingizwa OIC na Mahakama
ya Kadhi ni kunajisi katiba ya nchi. Rejea gazeti la Utatu – Na 044,
Jumapili, Septemba 28 – Oktoba 4, 2008, uk. 5.
‘Akionyesha
wazi msimamo usioyumba wa baraza hilo, Mwenyekiti wa PCT, Dar es
Salaam, Askofu David Mwasota aliwaambia waandishi wa habari kuwa
uvumilivu wa Wakristo umefikia mwisho na sasa wanasema hapana, hawataki
Katiba ya nchi itiwe unajisi na sheria za dini.'
Aidha, kwenye Tahariri ya gazeti hilo Uk. 4. imeeleza kama ifuatavyo.
‘Tusikubali
kutia unajisi katiba ya nchi, iachwe ikibaki kama katiba na dini zetu
zibaki kama zilivyo, kwani kucheza na eneo hilo ni kuchezea aliyeumba
mbingu na nchi ambaye ana mamlaka juu ya yeyote na chochote.’
5. Kujitafutia laana ya Biblia, Tanzania
Imeelezwa
kuwa ‘Yabainika Tanzania kujiunga na OIC ni kujitafutia laana ya
biblia.’ Rejea gazeti la Msema Kweli Na. 579 Jumapili, Oktoba 5-11,
2008, Ukurasa wa mbele na Uk. 5,
‘Imebainika
kuwa malengo ya Shirika la Umoja wa Kiislamu (OIC) yatailetea laana
kubwa Tanzania iwapo itajiunga nalo, kutokana na moja ya malengo yake
kupinga uwepo wa taifa la Kiyahudi la Israeli katika eneo la Mashariki
ya Kati, huku tayari Biblia Tukufu ikiwa imetahadharisha kuwa yeyote
atakayekwenda kinyume na taifa hilo atakuwa amejipatia laana.’
‘Ukweli
wa laana ambayo Tanzania itajipatia ikiwa itajiunga na OIC inaelezwa
vyema katika Biblia kwenye Kitabu cha Mwanzo 12:3 ambapo baada ya Mungu
kumwahidi baraka kuu Nabii Abrahamu ambaye ni chimbuko la taifa la
Israeli, alisisitiza ahadi zake kwa kuweka Agano kwamba atawabariki wote
watakaombariki na kuwalaani wote watakaomlaani.’
6. Kuisilimisha nchi
Rejea
gazeti la Msema Kweli - Na. 578, Jumapili, Septemba 28 Oktoba 4, 2008,
Ukurasa wa mbele na Uk 5, chini ya kichwa cha habari:
‘Katiba ya OIC kuibadilisha Tanzania kuwa dola ya kiislamu.’
‘Juhudi
zinazoendelea hivi sasa za kutaka Tanzania ijiunge na Shirika la Umoja
wa Kiislamu maarufu kama Organization of the Islamic Conference (OIC),
huenda zikaigeuza kuwa dola la Kiislamu kutokana na katiba ya Shirika
hilo kueleza kuwa sifa ya kujiunga nalo ni nchi au dola husika kuwa la
Kiislamu.’
‘Hiyo inamaanisha kuwa ikiwa
Tanzania ina nia ya kujiunga na OIC ni lazima kwanza iwe dola la
Kiislamu na ndipo ipate ridhaa hiyo.’
7. Wakristo hawakubali kuhukumiwa na Qur’an.
Rejea gazeti la Msema Kweli Na. 579, Jumapili, Oktoba 5–11, 2008, Uk. 3.
‘Nchi
yetu ni ya amani na upendo kwa miaka mingi, hivyo endapo wataiweka
mahakama hiyo ndani ya katiba ni kutafuta kuingiza dini fulani kwenye
nchi na kufanya hivyo ni chanzo cha mafarakano kwani Mkristo hawezi
kuhukumiwa na Qur’an.’
8. Kutumia Siasa
Wakristo
watishia kutumia karata ya siasa kukataa kuja kwa OIC na mahakama ya
kadhi. Rejea gazeti la msema kweli Na. 579 Jumapili, Oktoba 5 – 11,
2008, Uk. 3.
‘Mchungaji wa Kanisa la Glory of
Christ lililopo Ubungo Kibo Jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima,
ameitaka serikali kubadilisha uamuzi wake wa kuiweka Mahakama ya Kadhi
katika Katiba ya nchi pamoja na kujiunga na umoja wa nchi za Kiislamu
duniani (OIC) na endapo itafanya hivyo, Wakristo hawatakuwa tayari
kukipigia kura chama chenye mambo hayo kwenye Katiba zake, wakati wa
Uchaguzi Mkuu ujao.’
Pia rejea gazeti Nyakati Na.408, Jumapili, Septemba 28, Oktoba 4, 2008–Uk. 7.
‘Sisi
kama Wakristo tunalichukulia jambo hili kuwa ni la kisiasa zaidi kuliko
la kitaifa na tunajua hatari yake kijamii, hata kama Waislamu
wanavyolazimisha kwamba haitawahusu WAKRISTO. Hivyo ikibidi
kuwatahadharisha waumini wetu kuwa waangalifu kwa, vyama vya siasa
vyenye sera na ilani zenye hatari kama hizi inapofika nyakati za
uchaguzi waone hatari zilizoko mbele kitaifa. Itakuwa haki kwetu mbele
za Mungu, mbele ya dunia, kikatiba na kama mwasisi wa taifa hili
alivyoona mbali akitutaka raia wote wa Tanzania tukumbatie suala la
kutoingiza mambo ya dini ndani ya Katiba na Serikali’
Mbali
na kauli hizi za makundi tofauti ya kikristo, walitowa tamko la pamoja
kupinga chini ya PCT na chombo kikuu kinachowaunganisha Baraza la
Maaskofu, CCT. Rejea gazeti la Nyakati Na. 408 Jumapili, Septemba 28
–Oktoba 4, 2008, uk. 6.
‘Kwa mujibu wa Askofu
Mwasota, wakati tamko lao lilipokuwa likitolewa mapema Jumanne,
iliyopita, harakati mbalimbali za kupinga azimio lililotangazwa hivi
karibuni na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Benard Membe, la Tanzania
kujiunga na OIC akisema itafaidika kiuchumi na kijamii, zilikuwa
zinaandaliwa.’
‘Habari zaidi zinaeleza kwamba
PCT mkoa wa Dar es Salaam, ni kundi tangulizi tu lililojitokeza lakini
msimamo wao ndio ule ule wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC) na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ambao walishatoa kauli zao kwa
mitindo tofauti kupinga swali hilo’.
III. MAKINZANO YA HOJA ZA MAASKOFU NA REJEA ZA KITAIFA NA KIMATAIFA.
1. Kujiunga na OIC hakuifanyi Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu
Kujiunga
na OIC hakuifanyi Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu kama Maaskofu
wanavyotaka ieleweke. OIC ina nchi wanachama wa aina mbili:
a)
Nchi ambazo Katiba zao zinatamka wazi kuwa serikali zao ni za
kisekula (hazina dini). Miongoni mwa hizo ni Albania, Benin, Burkina
Faso,
Cameroon, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Guinea, Guinea Bissau,
Guyana, Lebanon, Msumbiji, Niger, Nigeria, Senegal, Sierra leone,
Uganda, Urusi, Uturuki,
b) Nchi ambazo Katiba
zao zinatamka wazi kuwa ni nchi za kiislamu au Uislamu ndiyo dini
rasmi ya Taifa lao. Mfano Indonesia, Iran,
Malaysia, Misri, Pakistan, Turkimenistan, Saudia, Sudan na nyenginezo.
Kwa
hiyo, si kweli kwamba OIC inakutanisha nchi za Kiislamu tu na au nchi
ikijiunga hatimae huwa ni nchi ya Kiislamu. Kama hayo ni kweli,
tungeshuhudia nchi kama Cameroon, Msumbiji, na Uganda ambazo ni
wanachama wa OIC kulazimishwa kuwa nchi za kiislamu kama Maaskofu
wanavyodai. OIC ni taasisi ya kimataifa ya kiuchumi na kijamii
iliyoundwa na waislamu, na nchi kadha zikiwemo zenye raia wengi
wakiristo zimenufaika na uanachama huo.
2. Mahusiano na taasisi za kidini
Sio siri kuwa Tanzania ina uhusiano wa kibalozi na HOLY SEE ambayo ni mamlaka ya kidini yanayo tawalia Dola ya Vatikano.
Tanzania
pia imeingia Mkataba wa Maridhiano (Memorandum of Understanding) na
Makanisa ya CCT na TEC kwa ushirikiano na Makanisa ya Ujerumani (Germany
Churches Partners) tangu mwaka 1992.
Vilevile
Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ambayo
kiongozi wake ni Malkia wa Uingereza ambaye pia ni MKuu wa Kanisa
Anglikana duniani.
Kwa rejea hizi utaona wazi
kuwa dhana ya nchi ya Tanzania kuingizwa katika udini na uvunjaji wa
katiba inakuja pale tu mikataba ya kitaifa na kimataifa inapo tamka neno
uislamu.
Hatuwezi kuukataa ukweli kwamba OIC
ni Umoja wa nchi za waislamu kama Charter ya mkusanyiko huu
inavyoonyesha. Malengo mengine ya OIC ni ya kisiasa, kiuchumi na kijamii
kuliko kidini na ndiyo maana hata nchi zisizokuwa za kiislamu Gabon,
Cameroon, Msumbiji, Marekani, Uganda na Urusi- zimejiunga na umoja huo
kama wanachama kamili full membership au wanachama watazamaji observer
membership ili kupata faida hizo za kiuchumi na kijamii.
Kama
ambavyo serikali na wakiristo walivyoona si kinyume na katiba Tanzania
kuwa na uhusiano wa kibalozi na Papa Holy See ama Vatican, basi kwa hoja
hiyo hiyo si kinyume na katiba kwa Tanzania kujiunga na OIC.
Kuna
tofauti kati ya “The Vatican” na “Holy See”. The Holy See ni mamlaka
inayoitawala Vatican. Mamlaka hiyo ina madaraka kamili (sovereignity
entity) yanayoongozwa na Papa na huwakilisha Kanisa Katoliki katika
masuala ya kidunia.
Aidha, kwa mujibu wa tovuti ya ‘Holy See’, wanasema ifuatavyo:
‘The
Holy See should not be confused with The Vatican City State which came
into existence only in 1929 while the Holy See dates back to early
Christian times. Ambassadors are officially accredited not to the
Vatican City State but to “the Holy See” and Papal representatives to
states and international organizations are recognized as representing
the Holy See, not the Vatican City State’.
Mamlaka ya Upapa na Vatican ni vitu viwili tofauti kwa hoja zifuatazo:
Mosi, Vatican ilianzishwa 1929 wakati Holy See ipo toka zama za mwanzo za Ukristo baada ya Mkutano wa Nicaea 325 A.D.
Pili, Holy See ndiyo inayotawala Vatican City State.
Tatu, Mabalozi huchaguliwa na Papa na humuwakilisha Papa na si Vatican.
Nne, Mabalozi wa nchi zenye uhusiano na Holy See huwasilisha hati zao za ubalozi kwa Papa na sio Vatican.
Tano, Lugha rasmi ya Holy See ni Kilatini, wakati ile ya Vatican ni Kiitaliano.
Sita, Hata Pasi za kusafiria za Holy See na Vatican ni tofauti.
Ni
vema katika nukta hii ikumbukwe kuwa nchi inapokuwa na uhusiano na
Vatican, kimsingi, inakuwa na uhusiano na Papa (mamlaka ya kidini ya
Holy See) jambo ambalo kwa mujibu wa Maaskofu hao ni must be avoided at
all costs kwa sababu ni kinyume cha misingi ya kisekula. Kwa mfano
katika mwezi wa October 2008, Balozi wa ‘Vatican’ Tanzania, alifanya
ziara mkoani Mbeya ianyoitwa ziara ya kiroho kwa mujibu wa vyombo vya
habari.
Na kwa kuzingatia ukweli huu, na kama
Maaskofu hawa wangekuwa watetezi wa kweli wa Katiba, tungewasikia
wakipinga uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na Mamlaka ya Upapa moja
kwa moja au kupitia Vatican, jambo ambalo hivi sasa Tanzania
inalazimika kuwa na mabalozi wawili (Balozi wa Tanzania Italia na yule
wa Tanzania kwa Holy See) na pia kuna ubalozi mdogo (Consulate) wa Milan
katika nchi moja tu ya Italia.
Wakati hayo
yakijiri kwa Tanzania kuwa na mabalozi watatu katika nchi ya Italia
pekee kutokana na uhusiano wake na Holy See, nchi nyingi duniani zenye
umuhimu mkubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa nchi yetu, Tanzania
inawakilishwa na balozi mmoja tu, mfano, nchi za Saudi Arabia, Kuwait
na Qatar inawakilishwa na balozi mmoja tu.
Ulazima
huu wa kuwa na mabalozi wawili nchini Italia unathibitishwa na maandiko
yaliyo katika tovuti ya Holy See www.wikipedia/Holy_See yasemayo;-
“The
Holy See (not the State of Vatican City) maintains formal diplomatic
relations with 176 sovereign states, the European Union and the
Sovereign Military Order of Malta; 69 of the diplomatic missions
accredited to the Holy See are situated in Rome, though those countries
then have two embassies in the same city, since, by agreement between
the Holy See and Italy, the same person cannot be accredited
simultaneously to both”. (Ibid; Msisitizo wa kwetu).
Hivi
ndivyo walivyoona Maaskofu wenzao nchini Marekani. Katika Makala yake
Ambassadors to Vatican: Breaching the Church-State Wall, Mkurugenzi
Mtendaji wa Baptists Christian Life Commission huko Nashville Marekani,
Richard D. Land alimwandikia barua Rais Mteule wa Marekani wakati huo
Bill Clinton akisema hivi:
‘How does the United
States, our diverse democracy, justify the deployment of American
Ambassador to the Vatican? This is a gross abrogation of church-state
separation that relegates all other religions to a lesser status’.
Kisha
wakahoji mantiki hiyo kwa kusema ‘Why don’t we send ambassadors to
Canterbury, Mecca, Jerusalem-to all other religion headquarters
worldwide to difuse the smell of favouratism?)
Wameendelea
kusema: How does our government get away with meddling, both at home
and abroad, in any religious body at all? Danger! Stop! Why, oh why are
we not outraged and howling in protest? Here we sit, year after year,
watching our presidents and most of Congress who, greedy for votes, are
too chicken to call halt to this’. (Washington Post, December 5, 1992).
Izingatiwe
kuwa Marekani haikuwa na Ubalozi wowote Vatican toka 1776 mpaka mwaka
1984 wakati Rais Ronald Reagan alipoanza kutuma mabalozi Vatican.
Maaskofu
wa CCT walipaswa kuhoji kwanza kwa nini tuwe na Ubalozi Holy See na
Holy See iwe na Ubalozi Tanzania nchi ambayo ni ya kisekula kabla ya
kuhoji Tanzania kujiunga na OIC? Lakini pia walitakiwa kuona kuvunjika
kwa katiba pale ambapo wao wana uraia wa nchi mbili, Vatikani na
Tanzania, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi. Ajabu iliyoje kwa
wenzetu kuwa na hoja kengeza katika hili!
Kwa
Serikali kuendelea kuwa na Ubalozi wa Papa hapa nchini itakuwa na sura
mbili, jambo ambalo kama walivyosema Maaskofu wa Marekani tuliowanukuu
hapo juu linazidhalilisha dini nyingine na kuonyesha upendeleo wa wazi
kwa dini ya Kikatoliki dhidi ya waislamu, bali hata dhidi ya wakristo
wasiokuwa wakatoliki.
Uhusiano wa Tanzania na
Papa/Vatican, hauna maslahi ya kitaifa katika uchumi wala kijamii
ukilinganisha na historia ya OIC na nchi wanachama wake. Pengine hiyo
ndio picha ambayo Maaskofu wa Tanzania wasingependa ijulikane. Pia, wana
hofu jamii nyengine kupata nguvu zenye maslahi kupitia OIC kama wao
walivyopata nguvu kubwa kupitia mkataba uliopo baina yao na serikali
Memorandum of Understanding.
3. Wakiristo wanavyonufaika na Memorandum of Understanding.
Katika Makala “The Tanzania Catholic Church” iliyo katika tovuti ya Kanisa Katoliki (www.rc.net/tanzania)-tovuti ambayo
iko chini ya Askofu Method Kilaini, panazungumziwa faida wanazopata
wakristo peke yao kutokana na Memorandum of Understanding kama
ifuatavyo:
‘To strengthen their social services
sector, the two Church bodies that is the Protestants under Christian
Council of Tanzania (CCT) and the Catholics under the Tanzania Episcopal
Conference (TEC), in 1992 assisted by the German partner Churches
negotiated a
‘Memorandum of Understanding” with the Tanzania
government. In this memorandum, the government recognized the important
role played by the Churches in the social sector of the country, pledged
to help the Churches by sharing with them grants from foreign
government and promised never to nationalize church institution again’.
The
‘Memorandum of Understanding’ authorized the forming of ‘Christian
Social Services Commission’ (CSSC). TEC and CCT are each represented by
the Secretary and four bishops. The commission has two executive organs,
the Christian Medical Board of Tanzania (CMBT) and the Christian
Educational Board of Tanzania (CEBT) for health and education
respectively.
This commission formulates common
policies for the Education and medical services of the Churches and
negotiate with the Tanzania government in the name of the Churches. The
two executive organs run common programs. The churches together run more
than 50% of the Medical Services and secondary schools in the country’.
Kanisa
kupokea sehemu ya pato la taifa na kuliacha kundi jingine la dini
katika hali duni kiuchumi, kijamii na kielimu, je huku si udini kuvunja
Katiba? Mbona waliosaini makubaliano haya hawakuhisi kama hali hiyo
inaweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa kama ambavyo wanavyodai katika
suala la Kadhi na OIC.
Bila shaka Maaskofu
hawana hoja bali wana chuki dhidi ya Uislamu, (Islamaphobia), kiasi cha
kutoona boriti lililo katika jicho lao bali wanaona kibanzi kilikicho
katika jicho la wengine.
IV. MAHAKAMA YA KADHI NA ULIMWENGU WA KISEKULA
Moja
ya kadhia inayo athiri ustawi wa jamii ya Waislamu nchini Tanzania hivi
leo ni kuondolewa Mahakama za makadhi, ambazo mahakimu na majaji ni
wafasiri tu wa sharia (dispensers of law).
Kwa
waislamu, kuhukumiwa kwa sheria ya Allah (sw) ni sehemu ya imani yao.
Sheria za kiislamu zilikuwepo kabla ya katiba zinazotawalia nchi
mbalimbali hivi sasa.
‘Na ndivyo hivyo
tumekuweka juu ya sheria katika kila jambo, basi ifuate na wala usifuate
matamanio yao yakaja yakakutoa katika njia (dini) ya mola wako’.
(48:45)
‘Na wale wasiohukumu kwa aliyoyateremsha M/Mungu, basi hao ndio makafiri… Madhwaalimu… Mafaasiq’ (5: 44-47).
Uislamu
ni dini ya Allah Ambaye Habadiliki. Sharia zake hazitungwi na Mitume,
wala watu wa kawaida, na hazibadilishwi, kufutwa kuongezwa na wala
kupunguzwa. Waislamu watakapoishi pasina kutekeleza sheria za Mwenyezi
Mungu watakuwa wametoka katika misingi ya imani yao. Na ili sheria za
kiislamu zitumike katika jamii yao ni lazima pawepo mahakama za makadhi.
Ili suala hili lieleweke, ni vema nukta zifuatazo zikazingatiwa:
1. KADHI NI NANI KISHERIA?
Kadhi
kisheria ni ‘yule anayehukumu kwa kutumia sharia’. Hii ni kutokana na
neno la kiarabu ‘Qadhwaa’ ambalo lina maana ‘Hukumu’. Utaratibu wa kuwa
na “kadhi” pia umeelekezwa katika Biblia (Taz. Mathayo 5:25-27 na pia
Ezra na Matendo ya Mitume)
2. HISTORIA YA MAHAKAMA ZA MAKADHI.
2.1 Zama za Mtume (saw).
Wakati
wa uhai wa Mtume (SAW) hapakuwa na Makadhi. Hii ni kwa sababu Mtume
(SAW) mwenyewe alikuwa ndiye Kadhi. Alikuwa akihukumu kesi za aina zote
kwani ndio moja ya malengo ya kutumwa kwa walimwengu:
‘Basi
naapa kwa jina la Mola wako hawawezi kuwa waumini (wakweli) mpaka
wakufanye Hakimu katika yale wanayo khitilafiana baina yao kisha
wasipate uzito katika hukumu utakazohukumu’ (4 :65)
2.2 Zama za Makhalifa Waongofu.
Katika
zama za Makhalifa Waongofu; (yaani Waliongoza Uislamu baada ya Mtume
Muhammad saw) Abubakar, Umar, Uthman na Ali (r.a) waliteuliwa watu
waadilifu wenye kuielewa vema Qur’ani na Sunnah ya Mtume (saw) wakawa
wakihukumu watu kwa sheria ya Allah, hawa waliitwa Makadhi.
Miongoni
mwao ni; Al alama Iyaadh ambaye alitoa ile hukumu maarufu dhidi ya
Khalifa wa nne Ali Bin Abii Twaalib (r.a) kwa kumpa ushindi Myahudi
baada ya Ali (r.a) kukosa ushahidi wa kutosheleza katika kesi ya
kupotelewa na ngao.
Kipindi cha Mtume (saw) na
wakati wa Makhalifa, Misikiti ilibeba dhima ya majengo ya mahakama za
Kadhi. Hukumu zote zilitolewa msikitini.
Makadhi
walihukumu kwa Sharia hawakumuogopa yeyote isipokuwa Allah. walijua
hata kama wameteuliwa na mtawala lakini wao wanawajibika kwa Allah.
Mtawala (Khalifa) alipotuhumiwa alisimamishwa mbele ya Kadhi.
2.3 Baada ya Makhalifa Waongofu.
Kipindi hiki kilianza na dola ya Banuu Umayyah na kufuatiwa na Banuu Abbas na dola za wafalme wengine zilizokuja baadaye.
Katika
kipindi hiki mfumo wa Mahakama za Makadhi uliingia katika kipindi cha
tatu cha ukuaji wake. Majengo maalumu ya mahakama yalijengwa, uratibu na
udhibiti wa mashauri kwa mujibu wa uzito wake uliendelea kuzingatiwa.
2.4 Zama za Ukoloni.
Kimsingi,
Ukoloni ulikuja na agenda dhidi ya Uislamu. Agenda waliyokuja nayo ni
Ukristo kama Historia inavyothibitisha jambo hili: Katika mkutano
uliofanyika Berlin kuligawa bara la Afrika - maarufu “The Berlin
Conference of 1884-85”, wakoloni walikubaliana kuulinda ukristo.
Kipengele kimojawapo katika makubaliano ya Berlin kinasema;-
“Christian
missionaries, scientists, and explorers, with their followers,
property, and collections, shall likewise be the objects of especial
protection”. (http://en.wikipedia.org/wiki/ Berlin_Conference)
‘The
Christian missionary works paved the way for eventual colonization of
Africa’ (Walter Rodney - How Europe Underdeveloped Africa).
Kwa
hiyo, wakoloni ingawa walionekana kwa nje kuwa wasekula, mataifa yote
ya kikoloni yalijiita “Christian Powers” - Ujerumani, Uingereza,
Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Hispania na Italia. Hata ilipoundwa League of
Nations (mtangulizi wa UN) jina lake rasmi lilikuwa “The League of
Nations of Christian Powers”. Mpaka leo mataifa haya bado yanajivunia
Christian heritage.
Kwa hiyo wote waliapa
kupigana vita vya msalaba (Crusade) dhidi ya uislamu wakiuona uislamu
kuwa ni adui mkubwa anayepaswa kupigwa vita na kuangushwa kupitia mifumo
mbali mbali. Kwa maneno yake Mwanahistoria maarufu, W.W. Hunter (1871)
anasema kuwa:
‘the Mussalmans are in all aspects a race ruined under the British Rule’
‘Mohammedan
element in India is that which causes us most trouble and provokes the
largest share of our hostility. Our antagonism to the followers of
Mohamed is far stronger that that between us and the worshippers of
Shiva and Veshnu. They (muslims) are unquestionable more dangerous to
our rule” (W.H.Russel, My Diary in India, Vol.II, pp 73-74, London,
1890).
Kilele cha chuki za Wakoloni Wakristo
dhidi ya waislamu kinadhihirika pale Waziri Mkuu wa Uingereza Palmerston
(aliyeishi tangu 1784-1865) alipomwamuru Gavana Mkuu wa India Lord
Canning, ahakikishe kwamba kila nyumba ya muislamu nchini India
inavunjwa.
‘Raze to the ground every building
belonging to Muslims without regard to antiquarian veneration or
artistic predilection’ (W.W. Hunter, Indian Mussalmans, Are They Bound
in Conscience To Rebel Against The Queen, p.31, Calcuta (1871)).
Maana yake:
‘Bomoa kila jingo linalimilikiwa na Muislamu bila kujali thamani yake kwa ukale wake au mvuto wake wa kisanaa’
2.5. HISTORIA YA MAHAKAMA ZA MAKADHI TANZANIA.
2.5.1. Kuingia kwa Wareno (Wakatoliki):
Mahakama
za makadhi Afrika ya Mashariki zilikuwapo tangu uhai wa utawala wa
Makhalifa waongofu wanne. Wareno walipovamia Afrika ya Mashariki,
Waliwakuta waislamu wakitumia sharia zao ikiwemo Mahakama ya Kadhi.
Ingawa walifanya njama nyingi za kufisidi Uislamu, waliondoka na
kuziwacha Mahakama za Kadhi zikifanya kazi.
2.5.2. Kuja kwa Wajerumani (Walutheri):
Wajerumani
walipoingi Afrika mashariki waliwaajiri Waislamu katika mambo ya
kiutawala kwa kuwa ndio watu pekee waliokuwa wameelimika na kustaarabika
wakati huo, mfumo wa elimu uliokuwapo ulitumia lugha za Kiarabu na
Kiswahili.
‘In the early colonial period, the
Moslems being the only literate people in the country were used
everywhere as sub-officers’ (The Tanzania Catholic Church, www.rc.net/tanzania/ tec).
Maana yake:
‘Katika
kipindi cha awali cha ukoloni, Waislamu walitumiwa kama makarani kwa
kuwa ni wao peke yao ndiyo walikuwa wakijuwa kusoma na kuandika.’
Pia Wajerumani walipoondoka waliacha, mahakama za liwali ambazo zilikuwa ni sehemu ya mahakama za makadhi.
2.5.3. Zama za Waingereza (Waangalikana):
Muingereza
alipoingia Afrika ya Mashariki, alileta uzoefu alioupata bara Hindi
jinsi ya kuwadhibiti waislamu kama tulivyoona huko nyuma. Alichofanya
Muingereza ni kuwatenga Waislamu kutoka katika nafasi zote za utawala na
mfumo wa elimu.
Hata hivyo, Muingereza
hakutaka kuwakabili Waislamu moja kwa moja kwa sababu walielewa kuwa
kufanya hivyo ni hatari. Dr. Ambedkar alipata kunukuliwa akisema:
‘No
government can exercise its power in such a manner as to provoke
Muslims to raise in rebellion. I think it would be a mad government if
it did so. (Justice V.R Krishna Iyer, Reform of The Muslim Personal
Law, Bombay, p.17, 1970)
Maana yake:
Kwa hiyo, Muingereza alipanga kuwadhoofisha waislamu hatua kwa hatua. Kwanza, kielimu, Pili, Kiuchumi na hatimaye Kijamii.
Katika
kutekeleza mkakati huo, mfumo wa sheria ulitumika kama tunavyojifunza
kutoka India. Mbinu walizoitumia Wakoloni Waingereza ni hizi zifuatazo;
Kutunga Katiba na kufanya marekebisho ya katiba mara kwa mara
(Constitutional laws and amendments), Mfumo wa mahakama (Judiciary
System), Mfumo wa Elimu (Educational System), na Vyombo vya Habari (The
Mass Media). Jaji wa Mahakama Kuu nchini India alipata kusema kuwa;
‘Let
us tackle the job of mordenizing the Islamic law…Our Muslim brothers
should remember that matters of civil concern do not affect the core of
the Prophet’s religious teachings but fall under the great guidance
given by Jesus: Render to the Caesar what is due to him and to God what
belongs to Him’ (Justice V.R Krishna Iyer, Reform of The Muslim Personal
Law, Bombay, p.17, 1970)
Aidha, Jaji V.R Krishna aliongeza akisema kuwa;
‘Silent
but substantial reforms through judicial activism is an unexploited
field in India because they (the judges) are not militantly committed to
the secular mission of the constitution…Uninhibited judicial adventure
in open areas of Muslim law can be fruitful’ (The VII Constitutional
Assembly Debates (1949), pp 781-82, Calcuta, India).
Hapo
ndipo inapothibitika mkakati wa watawala kuhujumu sheria za kiislamu
kupitia mfumo wa sheria na mahakama. Mkoloni muingereza Mwaka 1920
akatunga sheria iliyojulikana kama “The Court Ordinance of 1920”.
Katika sheria hii, mfumo wa mahakama ukawa na sehemu tatu; Sheria za
Kisekula (The secular (common) laws), Sheria za Kiislamu (The Islamic
law), na Sheria za Mila (The Customary law)
Kwa
upande wa sheria za kiislamu, mahakama maalum zilizojulikana kama
“Mahakama za Liwali” ziliendelea kujengwa mbali na mahakama za serikali.
Mabaki ya majengo hayo yapo mpaka leo katika sehemu mbali mbali nchini
likiwemo lile lililopo Mjini Musoma. Majengo haya ni kumbukumbu kwamba
wakati Fulani Waislamu wa nchi hii walikuwa na hadhi na heshima yao na
walikuwa na mfumo wao wa sheria.
Hata hivyo,
katika miaka ya hamsini (1950’s), Waingereza walituma tume mbili hivi
zikiitwa “The Royal Commission” ili kuangalia namna ya kuziengua sheria
za kiislamu hatua kwa hatua kwa kuanzia na kupiga marufuku adhabu kadhaa
zilizokuwa zikitolewa na mahakama za kadhi. Tume hizi ziliweka msingi
ambao hatimaye ulipelekea kufutwa kwa mamlaka za machifu na mahakama za
kadhi.
2. 5. 4. Makahakama za Kadhi Katika Tanganyika huru.
Mahakama
za makadhi zilikuwepo hata mara tu bada ya uhuru wa Tanganyika na
hazikuleta faraka, ugomvi wala kuvunja umoja wa kitaifa. Bila shaka
wakati ambao umoja wa kitaifa ulidhihirika ni wakati wa kudai uhuru
ambapo ingawa waislamu ndio walioongoza harakati hizo, lakini
waliwapokea wakristo wachache waliojiunga nao kama Mwl Nyerere, John
Rupia, Kambona huku wakristo wengi wakichukua msimamo wa Kanisa
kutojiingiza katika kudai uhuru. (Reja tovuti ya RC www.rc.net/tanzania/tec).
Lakini
mara tu baada ya uhuru kupatikana, mwaka 1963, ikaanzishwa sheria
iitwayo ’The Magistrate Court Ordinance of 1963’ kuchukua nafasi ya ile
ya mwaka 1920. Sheria hii ndiyo inayodaiwa kuzivunja mahakama za kadhi
na za kimila, na hivyo kuwalazimisha Waislamu kufuata sheria zote za
kisekula kinyume na dini yao na mila zao jambo ambalo ni kuvunja haki za
binadamu kama zilivoaishishwa na tamko la Umoja wa Mataifa (The
Universal Declaration of Human Rights) ambalo Tanzania ilikwishalisaini
wakati huo.
Tangu mwaka 1963 mpaka sasa ni
miaka 45 , mambo ya waislamu, ndoa, mirathi, talaka, amana, wakfu
yanaendeshwa na serikali kwa kutumia sheria za kisekula kinyume cha
Katiba 19(1) na matakwa ya waislamu.
Sababu zilizoelezwa wakati wa kuondolewa mahakama za makadhi mwaka 1963 zilikuwa ni hizi zifuatazo;
1. Kuleta usawa, haki na umoja wa kitaifa.
2. Serikali haikuwa na fedha za kugharamia mahakama za makadhi.
3.
Ilikuwa ni katika maazimio ya vyama kadhaa vya kupigania
uhuru barani Afrika (Angalia kabrasha la tume ya kukusanya maoni kuhusu
adhabu ya kifo na kurejeshwa kwa mahakama za makadhi)
Sababu
hizi si za msingi wakati huo na hata leo, kwa sababu, kama waislamu
tungepewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi hayo ya kuondolewa Mahakama
za Makadhi mwaka 1963 kama ambavyo wakristo wanashirikishwa katika
mchakato wa kurejeshwa mahakama za makadhi hivi sasa tungehoji kama
ifuatavyo:
Mosi, kuwepo kwa mahakama za kadhi
kungehatarisha haki ipi na kwa vipi ambayo gharama yake ni kuondolewa
haki ya msingi ya Waislamu Tanzania?
Pili, Kama
kweli serikali haikuwa na fedha za kuendesha mahakama hizo si
wangewataka waislamu kuchangia mahakama hizo? Waislamu wangeweza
kuwasiliana na wenzao Afrika Mashariki wakati huo wanayo EAMWS au
kwingineko duniani kupata fedha hizo au kuchangia kwa njia ya sadaka,
zaka, wakfu kama walivyokuwa wakiziendesha kabla ya kuja wakoloni.
N.B:
Na hata sasa inatolewa hoja hii kwamba kama mahakama za kadhi
zitarejeshwa, fedha za kuendesha mahakama hizo zinatoka wapi? Sisi
twasema fedha zitatoka serikalini kwani serikali inapata wapi fedha za
kuendesha mashule, mahospitali na taasisi za kikristo kupitia Hati ya
Maridhiano kati ya Serikali na Makanisa (Memorandum of Undertanding)?
Tatu,
Maazimio ya vyama vya kupigania uhuru yalihalalishaje kuondolewa kwa
mahakama za makadhi? Vipi uhuru utafutwe kwa kuondoa uhuru wa ibada kwa
waislamu?
2.5.5. Kuwepo kwa Mahakama za Makadhi si Kuvunja Katiba
Hoja
kuwa kurejeshwa kwa mahakama za makadhi kutavunja katiba ya nchi haina
mantiki yoyote. Sababu yake ni kuwa katiba hiyo hiyo imewapa wananchi
wote uhuru wa kuabudu na kufuata dini wazitakazo. Katiba imefanya hivi
huku ikifahamika kuwa masuala ya namna ya kuoa, kuachana katika ndoa,
kurithisha, kutoa sadaka na kuweka mali wakfu, kulea watoto, na masuala
ya kifamilia kwa ujumla wake kimsingi ni mambo ya kiibada kwa kuwa
yanafungamana moja kwa moja na dini na imani ya mtu husika. Ruhusa na
uhuru huu wa kuabudu na kuamini dini kila mmoja anayoipenda ndiko kuliko
pelekea ruhusa ya kutumika kwa sheria za dini na mila katika masuala
haya.
Ni jambo la kimantiki kuwa iwapo sheria
fulani imeruhusiwa kutumika, basi na mahakama zifaazo kuamua masuala
yahusuyo sheria hiyo pia ziwepo. Kwani itakuwa haina maana kuwa na
sheria ambayo haina mahakama zifaazo kuamua migogoro ihusuyo sheria
hiyo.
Hali kama hiyo itaifanya sheria hiyo ikose maana, heshima na mwishowe itapuuzwa nakuacha kufuatwa.
Paragrafu
ya pili ya proviso ya fungu la 11(1) la Judicature and Application of
Laws Act, Sura ya 358, Mapitio ya mwaka 2002 inaeleza kuwa sheria ya
kiislamu itatumika katika masuala ya ndoa, talaka, usimamizi wa watoto,
mirathi, wakf na masuala kama haya kwa watu wa jamii inayofuata sheria
hiyo – yaani, waislamu.
Hakuna yeyote aliyepata
kusema kuwa fungu hili la sheria linavunja katiba ya nchi. Kinyume
chake ni kuwa fungu hili la sheria halivunji katiba bali linaikamilisha
kwa kuwapa haki waislamu kufuata taratibu za dini yao katika masuala
haya ya kiibada kama walivyorususiwa na katiba kuamini na kuabudu kwa
mujibu wa dini yao. Kutaka iwe kinyume na hivi ni kutaka kuvunja katiba
kwa kuwazuia waislamu kutekeleza mambo haya ya kiibada kwa uhuru.
Kama
tulivyotangulia kusema, hakutakuwa na maana kuweka sheria bila kuweka
mahakama zinazofaa. La kujiuliza hapa ni je, mahakama zilizoko kweli
zinafaa kusimamia utoaji maamuzi katika masuala yahusuyo sheria ya
kiislamu hapa nchini?
Jawabu la swali hili ni hapana iliyo bayana. Kwa uchache, sababu zifuatazo zinatosheleza kuonyesha kuwa mahakama hizi hazifai:-
Mosi,
Kwa mujibu wa imani ya kiislamu, asiye muislamu hapaswi kuhukumu kwa
sheria ya kiislamu kwa sababu sheria hizo ni imani ya waislamu kama
ambavyo hapaswi kufunga Ramadhani, kusali sala tano, kuhiji Makka na
mengineyo yaliyo ya dini ya kiislamu.
Pili,
hakimu au jaji asiyekuwa muislamu hawezi kutenda haki kwa muislamu kwa
sababu hakimu au jaji anatakiwa siyo tu kutumia sheria kuhukumu bali
aiamini sheria hiyo moyoni mwake vinginevyo anakuwa katika hali ya
kisaikolojia ambayo haifai kutoa hukumu kwa sheria husika.
Tatu,
mwenye kuhukumiwa naye si tu ahukumiwe bali anatakiwa awe na imani na
sheria inayotumika kumhukumu, mahakama na hakimu au/na jaji
anayemhukumu. Ndiyo maana mtuhumiwa anapokuwa hana imani na hakimu
huomba hakimu au jaji husika ajitoe kusikiliza kesi yake.
Nne,
hata katika mapungufu tuliyotaja hapo juu ya mfumo wa mahakama nchini
mintarafu ya waislamu, bado mahakimu na majaji wanahukumu kesi kwa
sheria za kiislamu hawana ujuzi wa kutosha katika sheria za kiislamu.
Kwa
hivyo basi, majaji na mahakimu wanaoamua kesi zihusuzo sheria ya
kiislamu hapa nchini hawastahiki kuhukumu kwa sheria hizo. Atahukumu
vipi kwa sheria mtu asiyejua sheria hiyo? Hii imekuwa sababu kubwa ya
kupindwa makusudi sheria za kiislamu katika mahakama hizi na
kusambaratishwa jamii ya kiislamu. Dr. Muhammad Ali Jinah, muasisi wa
Taifa la Pakistani na mwanasheria bobezi, alipata kusema:
‘The
privy councils have, on several occasions, absolutely slaughtered
Mohamedan law’ (Legislative Assembly Debates, Feb 1925, p.1175).
2.5.6 Njama za Kuwaritadisha (kuwabatiza) Waislamu Duniani
Katika
hili kuna ushahidi wa kutosha katika kuthibitisha kuwepo kwa njama za
kuwaritadisha (kuwabatiza) waislamu kupitia mlango wa sheria.
“Silent
but substantial reforms through judicial activism is an unexploited
field in India because they (the judges) are not militantly committed to
the secular mission of the constitution… Uninhibited judicial adventure
in open areas of Muslim law can be fruitful”. (VII Constitutional
Assembly Debates pp 781-82, (1949).
Kwa hiyo mahakama zinakuwa zinatumika kuingilia sheria za kiislamu za ndoa, talaka, mirathi n.k. kama ilivyotokea India. Mfano;-
Mwaka 1978 Mahakama Kuu ya Allahabad ilihukumu kwamba
‘Misikiti
inaweza kununuliwa kwa ajili ya matumizi ya umma. Kujengwa kwa misikiti
si jambo la lazima kwa ajili ya sala kwa sababu kwa mujibu wa uislamu
sala inaweza kusaliwa popote’. (Ibid).
Pia kwa mujibu wa hukumu nyingine iliyotolewa na Mahakama Kuu huko huko India
‘Makaburi
ya waislamu yataheshimiwa kuwa ni makaburi pindipo yatakapokuwa
yanaendela kutumika. Yakishaachwa kutumika kwa miaka zaidi ya 20,
wananchi kuyavamia na kujenga au kufanya shughuli nyingine kwenye
makaburi hayo watakuwa hawavunji sheria’ (Panchahat Deh V. Kucknow
Municipality 1978 Allahabad, AIR, p. 280).
Vilevile katika hukumu nyingine ya Mahakama Kuu huko huko India ilihukumiwa ifuatavyo:
‘The
second marriage of Muslim, is ipso facto amounts to mental cruelty for
the second wife, and on its basis she can claim divorce’ (Itwari V.
Asghari, AIR 1960 Allahabad, p.684.
Kwa kifupi,
izingatiwe kwamba mahakama zote katika nchi za Jumuiya ya Madola
(Common Wealth), Tanzania ikiwemo, hutoa hukumu dhidi ya sheria za
kiislamu kwa sababu nchi hizi hutumia sheria hizi kwa pamoja (common
law). Dr. Muhammad Ali Jinah, muasisi wa Taifa la Pakistani na
mwanasheria bobezi, alipata kusema:
‘The privy council have on several occasions absolutely slaughtered Mohamedan law’ (Ibid).
Mifano
ya athari mbaya za hukumu dhidi ya waislamu katika mahakama za hapa
nchini, ni kama ile iliyotokea katika shauru la Ust. Khamis Dibagula
aliyeshitakiwa na kutiwa hatiani kwa kusema Yesu sio Mungu, jambo ambalo
ni sahihi kwa mujibu wa imani yake ya kiislamu. (Angalia, ‘The Muslim
and State in Tanzania’ - Prof, Hamza Mustafa Njozi).
Kwa
hiyo, urejeshwaji wa mahakama za makadhi ni maamuzi ya busara kufanywa
na serikali kwani itakuwa inawarejeshea waislamu haki yao ya kidini na
kikatiba waliyoporwa kwa muda wa miaka 45 sasa.
Na
kwa kuwa, suala hili limechukua zaidi ya miaka 20 tangu waislamu kuanza
kudai haki hii, kuendelea kulichelewesha ni kuwanyima waislamu haki
yao, kwa mujibu wa kanuni ya kisheria isemayo “Justice delayed is
justice denied”. Aidha, kwa kuwa ajenda ya mahakama ya makadhi imevutia
wengi, jambo hili lisifanywe kuwa ni ajenda ya kiisiasa, bali ni haki
ya waislamu kwa mujibu wa katiba ya nchi ( 19 (1) na 20 (1 & 2).
Hata
hivyo, katika mchakato wa kurejeshwa kwa mahakama za Kadhi, utaratibu
wa kupatikana Makadhi na Kadhi Mkuu ni lazima usimamiwe na taasisi zote
za kiislamu nchini ili kupata uwakilishi wa waislamu wote na siyo
serikali au taasisi moja kupewa jukumu hilo.
V. TAMKO LA WAISLAMU
Ijumaa, Oktoba 31, 2008; Kidongo Chekundu, Dar es salaam
Ndugu
Waislamu kufuatia vikao vya Masheikh, Maimamu na Viongozi wa taasisi na
madhehebu mbalimbali za Kiislamu vilivyofanyika jijini Dar-es-salaam
kujadili masuala ya Tanzania kujiunga na OIC na kurejeshwa kwa Mahakama
ya Kadhi nchini na kwa kuzingatia matamshi ya kichochezi ya Maaskofu,
sisi Viongozi wa Kiislamu Tanzania tunalazimika kutoa tamko letu kama
ifuatavyo:
1. Tunasema kwamba Uislamu katika
nchi hii umekuwepo kabla hata ya vyama vya siasa vilivyopo kuwepo. Pia
Uislamu umekuwepo kabla ya Katiba ya Jamhuri na umekuwepo kabla ya hata
Ukristo na mashirika yake ya TEC, CCT na PCT. Hatukubali kudanganywa
wala kulaghaiwa na chama chochote cha siasa. Si CCM wala hicho
wanachodai Maaskofu kuwa watakiunga mkono ili kuiondoa CCM madarakani
kama itang’ang’ania kutekeleza ilani yake. Tunachotaraji ni kwamba
Serikali iliyoko madarakani itatekeleza ahadi zake kwa wapiga kura na
kuwa hatudhani kwamba utendaji serikalini unategemea matashi na ruhusa
ya Maaskofu.
2. Ni msimamo wetu kuwa suala
la kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi halitategemea huruma, utashi wa Chama
cha Siasa, Serikali au Kikundi cha Kikristo au asasi nyingine yeyote
ile. Kwa kuwa uzawa na uraia wa Waislamu katika nchi hii hautegemei kura
ya mtu mwingine yeyote, vivyo hivyo hata suala la kuwepo Mahakama ya
Kadhi litakuwa ni haki ya kuzaliwa (Birth Right) ya Waislamu wa Tanzania
na kuwa madhali Waislamu wanataka Mahakama hiyo basi ni msimamo wetu
kuwa Mahakama hiyo itakuwepo. Aidha tunaamini kwamba pande zote
zinazohusika zitatumia busara zake katika kufikia hatima hiyo kwa muda
mfupi na pia kwa gharama nafuu.
3. Madai ya
Maaskofu kwamba Wakristo nao watadai kuanzisha mahakama zao kama
serikali itaridhia kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi nchini hayana msingi
ndani ya Ukristo wenyewe, kwani Biblia pia inamtambua Kadhi. Tazama
Mathayo 5:25 ambayo inasema,
“Patana na mshtaki
wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani, yule mshitaki asije
akakupeleka kwa Kadhi , na Kadhi akakupeleka kwa askari ukatupwa
gerezani.”
Kwa hali hiyo basi kama na Wakristo
nao wanataka Kadhi wao kama huyo aliyetajwa katika Mathayo
5:25-27.Waislamu tunawaunga mkono. Sisi Waislamu tuwe na Kadhi wetu, na
wao Wakristo wawe na kadhi wao.
4. Kwa kuwa
Serikali imekwishafanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba OIC haina
madhara kwa taifa bali ina manufaa mengi ya kiuchumi kama vile misaada
na mikopo isiyokuwa na riba. Kwa hivyo, tunaitaka Serikali ijiunge mara
moja na OIC ili wananchi wote wafaidike. Kutokujiunga na OIC
kutamaanisha kuwa serikali hii inaendeshwa kwa utashi na udini wa
Maaskofu.
5. Waislamu tumeshtushwa na kauli
za Maaskofu kuwa endapo serikali itaachia mjadala juu ya OIC na mahakama
ya kadhi uendelee bungeni itakuwa mwanzo wa kuruhusu kuvunjika kwa
amani ya nchi yetu. Kwa kauli hii ya maaskofu waislamu tunalazimika
kuamini kwamba huenda maaskofu wamekwishajiandaa kuvuruga amani ya nchi
hii.
Tunatoa wito kwa serikali kulitupia jicho
suala hili na kufuatilia kwa karibu nyendo za makanisa haya ili kubaini
mapema iwapo yana mipango ya kuvuruga amani ya nchi ili hatua zinazofaa
kuepusha baa kama hilo kutokea zichukuliwe. Tahadhari hii si ya maneno
matupu kwani imebainika kuwa makanisa yameshiriki kikamilifu katika vita
na mauaji ya kimbari katika nchi ya Rwanda. Tunaitahadharisha Serikali
kuwa ispochukua hatua mapema itawajibika kwa maafa yatakayotokea
kutokana na tishio hili la uvunjifu wa amani nchini.
6.
Pamoja na kwamba Waislamu ndio walio wengi Tanzania (Tazama Sensa ya
1967 (63%), CIA Facebook 2005 (50%) na Encyclopaedia Britannica (More
than 60%)), siku zote wamekuwa wakionyesha uvumilivu pamoja na kuwa
wamekuwa wakibaguliwa katika elimu, ajira na madaraka serikalini na
katika mgawanyo wa rasilimali za nchi. Kwa Bahati mbaya au kwa makusudi
uvumilivu wetu na subira tuliyokuwa nayo vimechukuliwa kuwa ni udhaifu
na unyonge katika kudai haki zetu. Tunasema kuanzia Ijumaa ya leo
hatutavumilia tena ubaguzi, dharau, na vitisho vya aina yoyote ile.
Wabillahit Taufiiq
Kwa ridhaa ya Waislamu nchini, wafuatao tumesaini waraka huu.
1. Al-Haj Abbas K. Sykes, Mwenyekiti-Dar es Salaam Islamic Club_______
2. Sheikh Ramadhan Sanze – Katibu Mkuu- BARAZA KUU ________
3. Sheikh Sherali Hussein- Katibu Mkuu - BASUTA___________________
4. Sheikh Pazi Semili- Katibu Mkuu -TAMPRO_____________________
5. Sheikh Ramadhan Murtadha, Mwenyekiti wa Shura, Shia Ithnasheri___
6. Sheikh Nassor M. Majid, Sheikh Mkuu, ISTIQAMA (Ibadhi)__________
No comments:
Post a Comment