Said Sued 'Scud' (wa tano kutoka kulia) akiwa na kikosi cha Yanga 1991
Na Daniel
Mbega
ZIKIWA
zimesalia siku tatu tu kabla ya pambano la Simba na Yanga, mashabiki wa timu
hizo walikuwa wamepamba moto kucharurana mitaani, lakini wadadisi wa mambo
walikuwa wamefikia uamuzi kwamba, pambano hilo lingekuwa kama fainali ya ligi
hiyo, kwa sababu, timu yoyote ambayo ingeshinda Jumamosi Agosti 31, 1991
ingekuwa vigumu kuzuiwa na timu nyingine huko mbele isitwae ubingwa wa Tanzania
Bara msimu huo.
Simba
ilikuwa inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 36 baada ya michezo 26, ikiwa
imeshinda 13, kutoka sare 10 na kupoteza mitatu tu, wakati Yanga ilishikilia
nafasi ya pili ikiwa na pointi 34 kwa michezo 25, ikiwa imeshinda 13, kutoka
sare 8 na kupoteza minne. Timu iliyokuwa inafuatia kwa karibu ilikuwa Pamba ya
Mwanza, ambayo ilikuwa na pointi 31 kutokana na michezo 25, ikiwa imeshinda 8,
kutoka sare 15 na kupoteza michezo miwili.
Tayari
bendera za kijani na njano, na zile nyekundu na nyeupe zilikuwa zimekwishatanda
jijini kuashiria kuwa, pambano la msimu lilikuwa limewadia. Tena safari hiyo,
bendera hizo hazikutundikwa kwenye mitaa ya Uswahilini tu, bali zilikuwepo hata
kwenye majumba ya Msajili katikati ya Jiji, nyingine zikiwa zimening’inizwa
kwenye antena za TV.
Simba,
ambayo ilikuwa bingwa mtetezi na kiongozi wa ligi, ilihitaji kutoka sare tu ili
iendelee kuiacha Yanga kwa pointi tatu, japokuwa ilikuwa imeitangulia kwa mechi
moja zaidi.
Kwa
upande mwingine, kama Simba ingeshinda mechi hiyo, basi ingeiacha Yanga kwa
pointi nne na ingekuwa vigumu kuzuiwa na timu yoyote ile kuhifadhi ubingwa
wake. Kama ingeishinda Yanga, basi Simba isingeweza kutishwa na Coastal Union
wala MECCO wala Ushirika katika mechi zilizokuwa zimesalia, kwani ushindi huo
ungekuwa umeipa nguvu za kutisha kiasi cha timu hizo tatu kuachia pointi
zenyewe bila ya kutaka.
Vivyo
hivyo, kama Yanga ingeishinda Simba, basi ingekuwa si rahisi kwa RTC Kagera
wala Pamba, African Sports au Maji Maji, kuizuia kutwaa ubingwa, ambao
iliupoteza mwaka 1990 kwa wapinzani wake. Hali hiyo ndiyo iliyolifanya pambano
hilo liwe na upinzani mkubwa zaidi.
Simba
ilikuwa inacheza Jumamosi huku ikiwa imefungwa na Pamba magoli 2-0 Agosti 24,
lakini Yanga ilikuwa inacheza huku ikiwa imeifunga Coastal Union 2-0 siku hiyo
hiyo. Hivyo, Simba ilikuwa inaingia uwanjani ikiwa inajaribu kuwaondolea
majonzi wapenzi wake huku Yanga ikiwa inataka kushinda mechi ya tatu mfululizo.
Timu zote
nne zililihama jiji la Dar es Salaam kabla ya mechi hiyo. Wakati ambapo Simba
ilikuja pole pole kutoka Mwanza ilikotoka kucheza na Pamba, Yanga ilikuwa
imekwenda tena Unguja, ambako ilikwenda kabla ya pambano la Mei 18. Agosti 26
Simba ilicheza na Milambo mjini Tabora
na kufungwa goli 1-0 na Agosti 27 iliwafunga mabingwa wa Kanda ya
Magharibi, Amka ya Nzega magoli 4-3 huko huko kwenye Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi, na Yanga, Agosti 26 ilifungwa na Mlandege goli 1-0 kwenye Uwanja wa
Amaan kabla ya kuzifunga Shangani 3-2 Agosti 27 na Small Simba magoli 2-0
kwenye uwanja huo huo.
Pamoja na
kwamba timu hizo zilikuwa katika mazoezi makali, lakini pia ukweli ni kwamba,
ziliamua kukaa mbali na Dar es Salaam ili kuepuka wachezaji wake wasipewe fedha
kwa nia ya kuwarubuni ili kupoteza ushindi na kambi zake zisiingiliwe
kimazingara.
Simba
ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, kwa sababu, mara kwa mara timu
hizo zikutanapo Simba ikiwa imenyongea, kama ilivyokuwa miaka ya 1986 na 1988,
mambo huwa mabaya kwa Yanga. Yanga ilitakiwa kujua kwamba, inacheza na golikipa
Mackenzie Ramadhani, ambaye msimu huo alikuwa hafungiki kirahisi.
Redio
Tanzania Dar es Salaam iliahidi kutangaza moja kwa moja pambano la Simba na
Yanga Agosti 31, lakini ikawataka wafanyabiashara nchini kote kujitokeza kutoa
matangazo yao kudhamini pambano hilo.
Habari
hizo ziliwaondolea wasiwasi wapenzi wa soka Tanzania ambao walifikiri RTD
ingeng’ang’ania msimamo wake wa kupata mdhamini mmoja tu wa kulipa shilingi
900,000/- kudhamini matangazo ya mpira wa miguu.
Agosti
24, mwaka huo RTD ilianza kutekeleza azma yake ya kutotangaza mapambano ya soka
mpaka ipate mdhamini baada ya kutolitangaza pambano kali la Yanga na Coastal
Union, na siku iliyofuata haikulitangaza pambano la Sigara na Tukuyu Stars.
Simba
imefungwa tena na Yanga? Kila mwanachama, shabiki na mpenzi wa Simba alikuwa
akijiuliza bila kupata jibu. Pengine msamiati sahihi ambao ungeweza kutumiwa
kuelezea hali ya wakati huo iliyoikumba klabu ya Simba ni kwamba, walikuwa
wamekubali kuitwa ‘Wateja wa Yanga’. Matokeo ya kufungwa tena goli 1-0 kwenye
mchezo huo wa ligi yalidumisha mambo kadhaa yahusuyo mechi za Simba na Yanga
katika kugombea ubingwa.
Kwanza;
mfungaji wa goli hilo moja lililoizamisha Simba Agosti 31, alikuwa yule yule
Said Sued ‘Scud’, ambaye alifunga goli lililoiangusha Simba Mei 18 katika
mchezo wa kwanza msimu huo.
Pili;
kocha Syllersaid Mziray alikuwa amezidi kutoka kifua mbele kwa mara ya nne
mfululizo baada ya mechi za Simba na Yanga, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Mei
26, 1990 wakati alipokuwa Kocha Msaidizi wa Simba, halafu ikaja Oktoba 20, 1990
akiwa kocha wa Yanga na Mei 18 na Agosti 31, 1991. Hivyo basi, ni kocha aliyejihusisha
na timu hizo mbili kongwe, ambaye hakuwa ameonja uchungu wa kufungwa na
mojawapo katika michezo minne iliyopita.
Tatu;
tangu aanze kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wanachama, Rashid Ngozoma Matunda,
hakuwa amefungwa na Simba katika mechi tatu alizosimamia.
Nne, hiyo
ilikuwa mara ya tatu kwa Yanga kuishinda Simba katika mechi zote mbili katika
msimu mmoja tangu mtindo huo wa ligi wa nyumbani na ugenini uanze kutumika
mwaka 1982. Mwaka 1982 Yanga iliifunga Simba goli 1-0 katika mechi ya kwanza na
kisha magoli 3-0 kwenye mechi ya marudiano, na mwaka 1987 Yanga iliifunga Simba
goli 1-0 katika mechi zote mbili.
Kwa kuwa
Simba na Yanga zilikuwa katika nafasi nzuri ya kucheza Ligi ya Muungano, basi
zilitarajiwa kukutana mara nne msimu huo. Hali hiyo ilikuwa inaipa ari Yanga ya
kutaka kushinda katika mechi zote nne mwaka 1991 na kuandika rekodi ya ajabu na
ngumu kuifuta kama Yanga ilivyoshindwa kuifuta rekodi ya kufungwa magoli 6-0.
Chama cha
Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kilimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe.
Augustine Lyatonga Mrema, kwa ushirikiano wake na chama hicho, ambao ulipelekea
mapato kuanza kuwa mazuri katika michezo ya kandanda kwenye Uwanja wa Taifa.
Katibu
Mkuu wa FAT wa wakati huo, Meshack Maganga, alisema kwamba, FAT inaishukuru
sana serikali kupitia kwa Mrema kutokana na juhudi za Waziri huyo katika
kuhakikisha kuwa, kuna ulinzi mzuri wa amani na udhibiti wa uingiaji uwanjani.
Pia
Maganga aliwashukuru polisi wote waliohusika na ulinzi katika mechi ya Simba na
Yanga na akatoa shukrani za pekee kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Temeke,
OCD Mhulo na Msaidizi wake, Matiku, ambao alisema, kazi yao ya kuhakikisha
usalama katika Uwanja wa Taifa ilikuwa nzuri mno.
Vile vile
aliwashukuru viongozi wa Simba na Yanga kwa kuanzisha vikundi vya sungusungu
ndani ya klabu zao kuangalia udhibiti wa malipo katika mechi zao. Alisema
utaratibu wa klabu kubadilisha wakaaji milangoni ni mzuri kuliko ule wa zamani
wa kuweka watu wale wale kila siku.
Maganga
pia alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi yao nzuri kwa kuutangaza mchezo wa
soka nchini.
Simba
safari hii haikukata rufaa kupinga kuchezeshwa kwa Issa Athumani kama
ilivyofanya katika mchezo wa kwanza uliofanyika Mei 18. Katika mechi hiyo ya
kwanza, Simba ilifungwa na Yanga goli 1-0 lililotokana na pasi ya Issa. Lakini
ingawa Issa alicheza tena katika mechi ya pili, hakuna rufaa iliyopokelewa na
Kamisaa wa Mchezo, Luteni Kanali Gwaza Mapunda, ambaye alikaa Uwanja wa Taifa
mpaka saa tatu usiku akisubiri malalamiko yoyote.
Baada ya
mechi ya kwanza, Simba ilikata rufaa kupinga usajili wa Issa kwa madai kwamba,
pia alikuwa amecheza ligi ya Oman, lakini kwa kutumia sheria za FIFA, FAT
iliikataa rufaa hiyo na hata Simba ilipoipeleka rufaa hiyo BMT, ilikataliwa kwa
misingi hiyo, na rufaa hiyo ikapelekwa kwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, ambaye
naye alikubaliana na maamuzi ya FAT.
SIMBA: Iddi Pazi, Raphael Paul, Azizi Nyoni, Method
Mogella, Frank Kassanga ‘Bwalya’, Iddi Selemani, Itutu Kigi/Jamhuri Kihwelu,
Khalfan Ngassa, Bakari Iddi/Issa Kihange, Hamisi Gaga, Zamoyoni Mogella/Ayoub
Mzee. Kocha: Hassan Affif.
YANGA: Stephen Nemes, Selemani Mkati/Freddy Felix
‘Minziro’, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Salum Kabunda, Jumanne Shango,
Abubakar Salum, Athumani China, Said Sued ‘Scud’/Joseph Machella, Issa Athumani
(nahodha), Thomas Kipese/Sanifu Lazaro. Kocha: Syllersaid Mziray.
Mwamuzi
alikuwa Taji Bakari wa Dodoma aliyesaidiwa na Joseph Mapunda wa Songea na
Kamisaa alikuwa Luteni Kanali Gwaza Mapunda. Mgeni rasmi alikuwa Athumani
Janguo, Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA).
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA
YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega,
ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa
simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment