Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 2 January 2015

KWA TAARIFA YAKO: TANGA SCHOOL NDIYO SHULE YA KWANZA TANGANYIKA



Na Daniel Mbega
Tunazungumzia kuhusu maendeleo ya elimu nchini – kupanda au kuporomoka. Hata hivyo, hatuna budi kujikumbusha tu kwamba, elimu hii ilianzia wapi hasa.
Kwa kifupi, Wajerumani ndio walioanzisha elimu rasmi nchini mwetu, na hii ilikuwa mwaka 1892 wakati walipojenga shule ya kwanza kabisa, Tanga School, ambayo leo inaitwa Old Tanga High School. Jengo kubwa la shule hiyo lilikarabatiwa na Tanga Heritage Centre kutokana na fedha za msaada kutoka Serikali ya Ujerumani.

Mtu aliyeleta mabadiliko hayo ya elimu, ambaye kwa hakika hatajwi popote, ni Gavana wa Kijerumani Julius von Soden ambaye siyo maarufu ikilinganishwa na Wajerumani wengine waliohusika na utawala katika koloni la German East Africa kupitia kampuni ya Germany East Africa. Yeye ndiye aliyeleta elimu hapa nchini.
Sodden aliamini kwamba elimu wa vijana wa kiume, bila kujali imani zao za kidini, ingeweza kusaidia uwepo wa Wajerumani barani Afrika. Badala ya kuwalazimisha wananchi kufanya kazi au kutwaa ardhi yao, Soden alikuja na mtazamo chanya kwa eneo hilo ambalo lilikuwa nyuma kimaendeleo.
Julius Freiherr von Soden aliyezaliwa Februari 5, 1846 na kufariki Februari 2, 1921, alikuwa Gavana wa Cameroon na baadaye German East Afrika (Tanzania ya leo) kabla ya kuwa Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje.
Alizaliwa na kukulia katika mazingira ya kijeshi huko Ludwigsburg, ambapo baba yake, Julius, alikuwa Luteni Kanali. Alikuwa mfuasi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri.
Alipata elimu katika ngazi mbalimbali hadi Chuo Kikuu cha Tübingen alikosoma sheria kabla ya kuingia kwenye jeshi na hatimaye kupigana katika vita ya Austro-Prussia wakati wa utawala wa Otto von Bismarck mwaka 1866.
Aliwahi kuwa kamishna wa Ujerumani huko Togoland (Togo ya sasa) kuanzia Julai 1884, mwaka uliofuata akawa gavana nchini Cameroon. Otto von Bismarck alikuwa hamwamini Soden kuhusiana na masuala ya ukoloni, hivyo alimpa maelekezo machache sana. Hali hiyo ikafanya kazi yake kuwa ngumu.
Hata hivyo, Von Soden akiwa gavana wa Cameroon, aliona umuhimu wa kilimo na kuanzisha mradi mkubwa nchini humo kupitia taasisi ya Land- und Plantagengesellschaft.
Mwaka 1890, Chancela mpya Leo von Caprivi aliagiza utafiti ufanyike wa koloni jipya Afrika Mashariki. Von Soden akateuliwa kuwa gavana wa koloni hilo kuanzia Januari Mosi, 1891. Matatizo aliyokabiliana nayo ni miundombinu duni.
Bila kushauriana naye, serikali ikawateua makamishna watatu waliokuwa na nguvu: Eduard Schnitzer, aliyejulikana kama Emin Pasha, Carl Peters na Hermann von Wissmann. Von Soden hakuwa na namna ya kuandaa vikosi vya ulinzi na usalama.
Ndipo alipoamua kuanzisha shule ya kwanza, Tanga School, mwaka 1892, kinyume kabisa na matakwa ya serikali ya Kijerumani. Malengo yake yalikuwa kuwaelimisha vijana wa Kiswahili ambao wangemsaidia katika utawala hasa upande wa Pwani.
Hivi ndivyo shule ya kwanza ilipojengwa, lakini hakuna anayemkumbuka wala anayeienzi shule hiyo kama ndiyo ya kwanza kabisa ndani ya Tanzania ya leo.


No comments:

Post a Comment