Na Brandy Nelson na Lauden Mwambona, Mwananchi
Mbeya. Hofu imetanda kwa wakazi wa Mbeya na mikoa ya jirani baada ya kuzagaa kwa samaki wanaodaiwa kufa kwa sumu iliyotoka migodi ya nchi jirani ya Malawi kutokana na maji yake kutiririka kuelekea Ziwa Nyasa.
Taarifa za kuingizwa kwa samaki wanaodaiwa kuwa walikufa kwa sumu kwenye masoko mbalimbali wilayani Kyela, Rungwe na Mbeya zilitolewa jana kwa mtandao na baadaye kutolewa tamko na viongozi wa Serikali.
Mitandao hiyo ilisambaza ujumbe uliosomeka:-
Taarifa kwa watumiaji wa samaki: “Wilaya ya Kyela imepiga marufuku uingizaji na utumiaji wa samaki kutoka Ziwa Nyasa (Malawi) kuanzia leo tarehe 13.01.2015 hadi tamko lingine litakapotolewa. Hatua hii imekuja baada ya kupatikana taarifa toka Malawi kwamba wananchi wamezuiwa kutumia samaki wa ziwa hilo baada ya kugundulika majitaka yenye sumu kutoka mgodi wa machimbo ya uranium wa Kailekera uliopo Karonga na kuingia kwenye ziwa na kusababisha vifo vya samaki ambao wanaingizwa nchini kwetu na kuuzwa kwa bei rahisi kwa upande wa Tanzania. Sampuli itachukuliwa kwa uchunguzi. Tahadhari ichukuliwe kwa watumiaji wa samaki. Acheni kuagiza mbasa kwa muda huu.”
Samaki hao wanadaiwa kuanza kufa tangu Januari 10 nchini Malawi na kwa upande wa Tanzania wameonekana tangu Januari 11 na kwamba hivi sasa wapo wanaoelea majini kana kwamba wameanikwa.
Taarifa hiyo ilizua hamaki na taharuki kwa wananchi ambako msaidizi wa mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliyetajwa kwa jina la Marco Masaya alipoulizwa kama wanayo taarifa ya kuzagaa kwa samaki hao alijibu kuwa ni kweli.
Alisema bosi wake alikuwa ameshapata taarifa hizo na kwamba alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kyela (DC), Margreth Malenga mambo ya kufanya kwa haraka ili kuepusha madhara kwa wananchi.
Hata hivyo, DC Malenga alipopigiwa simu alikataa kuzungumza suala hilo kwa simu, akisisitiza kwamba yeye amejiwekea utaratibu wa kuzungumza na waandishi ana kwa ana.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyela, Clement Kasongo alipopigiwa simu kuhusu suala hilo alisema ni kweli wamewakuta samaki mpakani mwa nchi hizo na kwamba wamechukua sampuli watazipeleka kwa Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupimwa kubaini sababu za kufa kwao.
Aliongeza kuwa Serikali imezuia watu wasile samaki hao mpaka majibu yatakapotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mkazi wa Kasumulu, Kyela, Hebron Mwakapeja alipoulizwa kama amewaona samaki kwa wingi, alisema tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, makundi ya watu yanaelekea ziwani wanakosomba samaki kwa wingi na kuwauza kwa bei ya ndogo.
Alisema watu wengi wamepigwa butwaa kutokana na samaki hao kupatikana wakielea majini kwenye ziwa hilo.
“Siyo kawaida kwa samaki wa Ziwa Nyasa hasa mbasa ambao siku zote huuzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh25,000 kwa samaki mmoja kuuzwa kuanzia Sh5,000 hadi Sh8,000,” alisema.
Naye Anna Kapeje wa Itunge alipoulizwa kuhusu samaki hao alisema makundi ya watu yalihamia kwenye ziwa kuokota samaki kwa siku tatu zilizopita.
Mkazi wa Karonga nchini Malawi, Kassim Chimwemwe alipopigiwa simu alisema ni kweli samaki walikufa wengi ziwani tangu Januari 7 baada ya bomba la maji machafu lililopo kwenye kiwanda kupasuka na kumwaga maji yake ziwani.
Alisema Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi alifika eneo la tukio na kutoa siku 10 ili sampuli za samaki waliokufa zichukuliwe kwa uchunguzi.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment