Zanzibar. Wakati Kamati Kuu ya CCM, ikieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wake walio katika dhamana ya kisiasa kukumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, adhabu kali zitachukuliwa dhidi ya wagombea urais sita walioadhibiwa mwaka jana endapo walikiuka masharti ya adhabu zao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana baada ya Kikao cha Kamati Kuu kilichokutana Ofisi Ndogo ya CCM, Kisiwandui kuwa kamati hiyo imeagiza Kamati Ndogo ya Maadili kushauri na kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi watakaokuwa wamekiuka adhabu husika.
“Itakumbukwa kuwa kuna makada sita wa CCM waliopewa adhabu kwa kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais, watamaliza muda wa adhabu zao Februari mwaka huu.
“Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao na kama kuna ambao watakutwa hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao, wataongezewa adhabu,” alisema Nape.
Vigogo sita waliopewa adhabu ni; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira .
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Nape alisema kamati ndogo ya maadili inayoongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula itatoa ushauri kwa ngazi za juu za CCM na ikibidi hatua nyingine za kinidhamu na kiatiba zitafuata.
Makamba asema
“Binafsi sina wasiwasi, kwanza mwanzoni sikustahili kuwemo na hata sasa sina shaka kama kuna lolote nililofanya kinyume.”
Alisema kuwa wanaopaswa kuwa na wasiwasi ni wale wanaogawa pesa. “Sisi wengine hizo fedha hatuna...ninaamini wapo wengine ambao hawapo kwenye orodha lakini wamekiuka maadili. Nilitarajia na wao watahojiwa,” alisema Makamba.
Sumaye akumbushia rufani
Akizungumzia hatua hiyo ya Kamati Kuu, Sumaye alisema: “Mimi siwezi kujitathmini mwenyewe, tusubiri hiyo kamati tuone, sijui watasema nini na wala sielewi kosa langu na ndfiyo maana nilikata rufani.
“Labda watatumia muda huo kujibu pia rufani yangu. Sina mengine ya kusema.”
Sakata la Tegeta Escrow
Akizungumzia kashfa ya uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Nape alisema: “CCM kimesikitishwa na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
“Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu imeitaka Serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu suala hilo.
“Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha.
“Pia, imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya uamuzi vya chama.
Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika Jumatatu ijayo, Januari 19 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo,” alisema Nape.
Wanaotuhumiwa na uchotwaji wa fedha hizo ni pamoja na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Ngeleja na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mwingine aliyeko katika tuhuma hizo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Profesa Tibaijuka ameshavuliwa wadhifa wake.
Akizungumzia hatua ya Kamati Kuu, Profesa Tibaijuka alisema: “Kama wameamua tufikishwe Kamati ya Maadili, basi nitasubiri taarifa rasmi ili ajue kwa kina uamuzi huo.
“Sikuhudhuria kikao, sina la kuchangia na kwa sasa nasubiri nipate taarifa” alisema Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Prof Tibaijuka ambaye hakuhudhuria mkutano huo, alisema pia kuwa viongozi waliowekwa viporo sakata la Escrow, ni vyema mamlaka ya husika ikashughulikia suala hilo.
Alipotafutwa Ngeleja kuzungumzia suala hilo alisema, “Kwa sasa sipo kuzungumzia suala hilo kwa sababu linashughulikiwa na vyombo husika.”
Kwa upande wake Chenge alisema kwa ufupi kuwa hapendi kulizungumzia suala hilo.
Kamati za Bunge
Sakata hilo la Akaunti ya Tegeta Escrow lililodakwa na kamati hiyo ya CCM pia lilizusha mjadala mzito wakati wa vikao vya Kamati za Bunge, Katiba na Sheria inayoongozwa na Ngeleja na ile ya Bajeti chini ya Chenge.
Wenyeviti hao wa kamati tatu za Bunge waliotajwa kuhusika kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na kutakiwa kuvuliwa nyadhifa zao, wamezua mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa kamati zao kutokana na kuibuka kwa madai kuwa wamehukumiwa bila kuhojiwa.
Mvutano huo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inaongozwa na Ngeleja kubishana kuhusu suala hilo wakati wakiwa ndani ya kikao.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo zilieleza kuwa watuhumiwa hao, kutoitwa na kuhojiwa na badala yake kuhukumiwa moja kwa moja si jambo la kupongezwa, kwamba suala hilo huenda likachelewesha utekelezaji wa kung’olewa kwa wenyeviti hao.
Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema: “Hatukuwahoji wahusika kwa sababu kama tungefanya hivyo tungewapa hati ya kutoshitakiwa na hivyo wasingeadhibiwa na kufikishwa mahakamani.”
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi, kwamba anamsubiri Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Akifafanua Zitto alisema: “Kama kuna mtu analalamika kuwa hakuhojiwa na PAC ajue kuwa tulikwepa ujanja wao wa kutaka kupata kinga ya Bunge.”
Alisema Bunge liliazimia polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow na wengine watakaogundulika.
Juzi, baadhi yao, Ngeleja aliongoza Kamati ya Nishati na Madini na kusema kuwa uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili unaendelea na ikithibitika Bunge litachukua hatua.
Nape alisema Kamati Kuu imejadili na kufikia kuunda Kamati Ndogo ya Maadili ili kufanya uchambuzi na tahmini za wagombea waliohusika na adhabu waliopewa.
Alisema Serikali imetakiwa kutekeleza kwa vitendo maamizio yote ya Bunge kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kabla ya kikao cha Bunge Januari 27 na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana za uteuzi wachukuliwe hatua stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara moja.
Alisema Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli za chama mwaka 2015 ikiwamo ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa chama hicho kwenye uchaguzi ambao utapangwa na vikao husika.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment