Kikao cha Pili cha Mkutano wa 18 wa Bunge la 10 kimeahirishwa muda huu mjini Dodoma baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka shughuli zote za serikali ziahirishwe mara moja ili kulishughulikia suala la kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba.
Katika hali ya mvutano, Spika Anne Makinda aliamua kuahirisha Bunge hadi saa 11 jioni kwa maelezo kwamba suala hilo ni zito.Profesa Lipumba alikamatwa jana jijini Dar es Salaam kwa madai kwamba aliongoza maandamano yasiyo rasmi na kukaidi amri ya polisi ya kusitisha maandamano hayo. Stori kamili ya tukio hilo la jana ni hii hapa kama ilivyoripotiwa na gazeti la Mwananchi:
Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam jana walifyatua mabomu ya machozi kutawanya viongozi na wafuasi wa CUF na baadaye kumtia nguvuni Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 32, tukio lililosababisha Ukawa kuunganisha nguvu kuwasaidia kuandika maelezo.
Profesa Lipumba na viongozi wenzake walikuwa wakienda Zakhem, Mbagala kuwatawanya kwa amani wafuasi wa CUF baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa mapema jana ya kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara uliopangwa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 14 tangu wafuasi wa chama hicho walipouawa kwa risasi na polisi wakati wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2001. Maandamano hayo yalipangwa kuanzia Temeke Mwisho na kuishia Mbagala Zakhem wilayani Temeke ambako chama hicho kina nguvu kubwa.
Lakini azima yao ilikumbana na mkono wa dola baada ya polisi kuwazuia viongozi hao eneo la Mtoni Mtongani na baadaye kutumia nguvu kutawanya wananchi.
Katika sakata hilo, polisi waliwaweka chini ya ulinzi viongozi wote akiwamo Profesa Lipumba na wafuasi hao walipokuwa wakijiandaa kwenda Viwanja vya Zakhem, ambako mkutano ungefanyika.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilithibitisha kukamatwa kwa Lipumba na wanachama 32 wa CUF kwa kufanya maandamano haramu na walikuwa Kituo Kikuu cha Polisi, ambako viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walienda pamoja na wanasheria waliotakiwa kuwasaidia kuandika maelezo.
Wakati polisi ikisema inawashikilia watu 32, CUF imesema watu 17 ndiyo wanaoshikiliwa.
Mbali na Profesa Lipumba, wengine ni Shaweji Mketo (naibu mkurugenzi wa mipango na uchaguzi na Abdul Kambaya, naibu mkurugenzi wa habari na uenezi (Taifa ).
Wengine ni Nurdin Msati, ofisa harakati na matukio, Rehema Kawambwa (mwenyekiti wa wilaya ya Temeke), Kais Kais (katibu wa Wilaya ya Temeke), Shaaban Kaswaka (mjumbe wa Baraza Kuu) na Mohamed Mtutuma ambaye ni katibu wa mwenyekiti wa chama hicho. Pia wamo Juma Kombo, Mohamed Zuber, Mohamed Ibrahim, Bakari Naleja, Athuman Hamed, Abdina Abdina, Shabani Ngulangwa na madereva; Hussein Alawi na Issa Rwabibi.
Wahaha kusaka dhamana
Mwandishi wa gazeti hili alikuwapo kituoni hapo hadi saa 1:35 usiku ilimshuhudia Mwanasheria wa Chadema, Fred Kimila, na wa CUF, Job Kerario, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Ubungo, John Mnyika wakihaha kuhakikisha Profesa Lipumba na wanachama hao wanaachiwa. Hata hivyo, Mbowe aliondoka muda mfupi baadaye.
“Chama (Chadema) kilimuagiza wakili Fred Kiwilo kufika kufika hapa kuja kutoa msaada wa kisheria kwa wapiganaji wenzetu wa Ukawa waliokamatwa kwenye maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF),” alisema msemaji wa Chadema, Charles Makene.
“Kwa hiyo Wakili Freddy tayari anasaidiana na mwenzake Kilerio Job kuhakikisha Profesa Safari na wengine akina Mketo, Kambaya na wenzake wanapata msaada wa kisheria wakati wa kuandikisha maelezo.”
Naibu kamishna wa Polisi Kanda hiyo, Simon Siro jana alisema: “Tumewakamata na tunaendelea kuwahoji... tulipewa taarifa ya maandamano hayo na viongozi wa chama na tuliwaandikia barua ya kuzuia maandamano hayo kwa kuhofia fujo kutokea.
“Sababu kubwa ya kuzuia maandamano hayo yasifanyike ni kuwa mwaka 2001 yalifanyika maandamano batili yaliyosababisha baadhi ya polisi na wananchi kufa.
“Polisi tumeona, tukiruhusu maandamano haya, kuna uwezekano wa kutokea fujo kama ilivyotokea mwaka 2001.”
Alisema sababu nyingine ya kuzuia maandamano hayo ni kwamba hivi karibuni walikamatwa watu wanaojihusisha na ugaidi na kwamba kutokana na mazingira hayo polisi inazuia mikusanyiko mikubwa kwa kuhofia kutokea mambo mabaya.
Walipotiwa nguvuni
Kabla ya kukamatwa, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwapiga virungu Lipumba na wafuasi hao na kisha kuingizwa kwenye magari ya polisi.
Lipumba aliingia kwenye gari aina ya Toyota Pick-Up huku akilindwa na askari wanne waliokuwa wameshikilia mitutu ya bunduki huku wafuasi wengine wakiwa wamepakiwa kwenye Land Rover Defender.
Lipumba na wafuasi hao walikamatwa katika eneo la Mtoni Mtongani ambako polisi walifyatua mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo mitaani, huku maduka na sehemu nyingine kufungwa.
Wakazi wa maeneo hayo walionekana wakikimbia huku na kule wakitafuta maji kwa ajili ya kusafishia macho yaliyoathiriwa na moshi wa mabomu.
“Mtongani pameshageuka Iraq,” mzee mmoja alisema. Kina mama wengi waliokuwa wamekaa nje ya nyumba zao waliingia ndani na kufunga milango wakihofia Polisi.
Ilivyokuwa…
Profesa Lipumba alifika karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke saa 8:00 mchana na kukuta wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakimsubiri ili kuanza maandamano kwenda kwenye Viwanja vya Zakhem Mbagala. Baada ya kuteremka katika gari yake akiwa amevalia fulana nyekundu na suruali nyeusi, aliwasalimu wafuasi kwa salamu ya chama hicho.
Wakati hayo yakiendelea, polisi wakiwa kwenye magari matano aina ya Land Rover yaliyosheheni askari 10 kila moja likiwemo lori lenye maji ya kuwasha, walikuwa mita chache na walipokuwa wafuasi hao.
Askari hao walikuwa wamesimama katikati ya barabarani na wafuasi wa chama hicho nao walikuwa upande mwingine wa barabara.
Polisi walifunga barabara hiyo inayopita katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke na magari yote yalitakiwa kupita katika barabara za pembezoni.
Wafuasi wa chama hicho walikuwa wakihamasishana kwenda Zakhem kwa maandamano, lakini polisi walikuwa wakipinga huku wakisema hakuna kwenda kwa maandamano.
Katika hotuba yake, Lipumba aliwaeleza kuhusu barua ya kuzuia maandamano hayo na kwamba wenzao wa Zakhem waliokusanyika kusubiri mkutano, hawakuwa na taarifa hivyo alitakiwa kwenda kuwaambia kuwa mkutano umezuiwa na polisi.
Baada ya msafara wa CUF uliokuwa na magari saba kuondoka, Polisi nao wakaondoka kwa kasi na kwenda kuuzuia msafara huo. Kwanza waliwazuia eneo la Mtoni na baadaye Mtongani ambako ndiko kulipotokea mabomu kulipuliwa.
Kauli ya Lipumba
Akiwahutubia wanachama wa chama hicho kabla ya kuanza maandamano, Lipumba aliwataka wafuasi hao kuepuka makundi ndani ya chama na kuendeleza mshikamano hata kama watakosa nafasi za uongozi katika kura za maoni zinazotarajiwa kufanyika ili kuwapata wawakilishi wa nafasi za udiwani, ubunge na urais.
“Tunatoa agizo kuwa ni marufuku kwa wanachama na wapenzi wetu wote nchi nzima kujitokeza kwenda kupiga kura ya maoni kwani kushiriki kwa namna yoyote, hata kupiga kura ya hapana, ni kubariki mchakato haramu uliofanywa na mafisadi wa Chama Cha Mapinduzi,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema maadhimisho hayo yanatakiwa kuongeza mshikamano na umoja ili kupeana nafasi, kwa mujibu wa taratibu walizojiwekea kuwapata wagombea watakaokubalika.
Kauli ya CUF
Awali, Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya CUF, Buguruni, Mkurugenzi wa Mipango na Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Shaweji Mketo alisema kuwa wameshindwa kuizingatia kauli ya polisi kwa sababu ilichelewa.
“Tulipata barua ya polisi jana (juzi), saa moja usiku, ikitutaka tusitishe maandamano yetu wakati tulikuwa tumeshafanya maandalizi yote muhimu ili yafanyike leo (jana).
“Kwa muda waliotuletea barua hiyo, tunashangaa inawezekana vipi ofisi ya serikali ikawa wazi mpaka muda huo…tutaendelea na maandamano kama tulivyopanga na hatutorudi nyuma,” alisema Mketo.
Alifafanua kuwa, licha ya sheria kutaka taarifa ya maandamano kutolewa kabla ya saa 48, wao walifanya hivyo kwa muda mrefu zaidi kuliko huo, ila wanashangaa na amri hiyo iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini ambalo limetaarifu kuwa kama hawajaridhika basi wakate rufaa kwa waziri wa mambo ya ndani.
“Muda wa kukata rufaa haupo kwasababu maandamano hayo ni lazima yafanyike leo. Hii ni siku ya kumbukumbu na siyo sherehe hivyo hatuna budi kuyafanya. Nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maandamano na mkutano wetu wa hadhara,” aliongeza mkurugenzi huyo wa CUF.
Dk Slaa alaani
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alilaani kitendo hicho na kueleza kuwa ni mwendelezo wa serikali kuweka pamba masikioni kwa kuwazuia wananchi kuonyesha hisia zao.
“Watanzania wenzetu waliuwawa na leo (jana) wenzetu wanaandamana kwa lengo la kuwakumbuka, lakini polisi wanawashambulia waandamanaji ambao hawakuwa na silaha yoyote, hii ndiyo serikali isiyoheshimu maandamano katika taifa lake.”
“Juzi juzi wananchi wa Marekani tulisikia wameandamana na polisi hawakuwazuia wala kuwapiga bali iliwalinda, kwa nini sisi Serikali yetu isiwe inaheshimu hisia za wananchi wake, ubaya wa maandamano hayo ya CUF ni upi, kwani wangewalinda kipi kingeharibika,” alisema Dk Slaa.
Katibu Mkuu huyo alisema “Rais (Jakaya Kikwete) kwa kuwa amekuwa akitembea nchi mbalimbali anatakiwa kujifunza kutoka kwa wenzetu jinsi Serikali inavyoheshimu maandamano, hatupendi ifikie mahali wananchi wakaanza kujilinda wenyewe.”
No comments:
Post a Comment