Na Mwandishi Wetu, Arumeru
WAZEE Wilaya ya Meru wameomba ,Serikali na wahisani kuwasaidia kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayokabili ikiwa inachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi ,ambapo wamelazimika kuacha shughuli za kilimo walizokuwa wanazitegemea.
Wazee hao wakizungumza katika kijiji cha Sakila ,Kilombero wamedai kuwa maisha yao kwa sasa yanategemea msaada kutoka kwa wasamaria wema ambapo wamedai kuwa Taasisi ya Sakila Hope for Elderly imekuwa ni mkombozi wao kwa zaidi ya miaka 5 kupitia wadau wengine wa maendeleo .
Bibi Sara Noel alisema kuwa anapata nguvu na kuona maisha yanaendelea kutokana na huduma wanayopata kutoka kwa wasamaria kupitia Shirika la Sakila Hope for Elderly.
“Sisi tunashukuru angalau tunapata msaada lakini sote tunajua kuwa kuna kundi kubwa la wazee wanaoteseka wakikabiliwa na hali ya kukataliwa na jamii zao ,ni muhimu sasa ukawepo mpango wa kitaifa wa kuwasaidia wazee”alisema Bi Noel
Mratibu wa Taasisi ya Sakila Hope for Elderly Humphrey Mafie alisema kuwa wazee wengi katika siku hizi wanateseka na hata jamii zao zinawatenga na kuwaona ni mzigo.
Akigawa misaada ya vyakula ,nguo na mahitaji mengine kwa wazee 246 wanaolelelewa na taasisi hiyo katika eneo la Meru ,Mafie alisema kuwa idadi kubwa ya wazee wenye umri mkubwa wametelekezwa na familia zao na kugeuka kuwa omba omba katika jamii .
Aidha aliongeza kuwa wazee wengi ambao hutegemea kilimo wameathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi kufuatia kukosekana kwa mvua.
Alisema mazingira hayo yamewafanya wazee waishio vijijini kuwa na hali mbaya zaidi kwani wengi wameachwa na vijana ambao wamekwenda katika maeneo mengine kutafuta fursa za kiuchumi.
“Umefika wakati wa jamii kuanza mjadala kuhusu namna ya kuwatunza wazee ,hawa wazee ni hazina ,wengi wamelitumikia taifa na jamii zao hivyo ni muhimu familia kuwajali na kuwatunza” alisema Mafie.
Wakizungumzia misaada hiyo kwa niaba ya Wazee wenzake Ndetaniso Ndewario alishukuru Shirika la kuhudumia wazee pamoja na kampuni ya Sigara kwa kuwakumbuka na kuwasaidia.
“Tunashukuru tumepata nguo vyakula na hata msaada wa kila mwezi wa chakula na mahitaji mengine tunayopata ikiwemo ya huduma za kiafya” alisema Ndewario.
Naye afisa mahusiano wa kampuni ya Sigara Tanzania ambao ndio wametoa msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 10 Martha Saivoye alisema kuwa kampuni hiyo imetoa msaada kwa wazee hao kama moja ya majukumu yao ya kusaidia kijamii.
Kwa upande wake mlezi wa taasisi hiyo ya kuwatunza wazee wasiojiweza ,Mchungaji Amos Baruti alisema kuwa taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kumudu kusaidia wazee wengi wasiojiweza.
“Hili kundi la wazee wasiojiweza linaongezeka kila kukicha,hatuna rasilimali za kuweza kuwasaidia hivyo ni muhimu serikali na wadau mbalimbali wakatuunga mkono “alisema Mchungaji Baruti.
Alieleza kuwa wamejenga kambi maalum ya kuwatunza wazee ambayo itakuwa na uwezo wa kuwatunza wazee 24 itakapokamilika.
“Kambini tayari tuna wazee sita ,lakini ujenzi wa makazi hayo utakapokamilika tutaweza kuwahudumia wazee 24 tu na idadi nyingine itategemea misaada itakayopatikana kupanua mradi”alisema Mchungaji Baruti.
No comments:
Post a Comment