Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (aliyekaa kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (aliyekaa kulia) kwa pamoja wakisaini mkataba wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande hizo mbili. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja. (Na Mpigapicha Wetu).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (kulia) wakibadilishana mikataba ya kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande hizo mbili. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (kulia) wakishikana mikono punde baada ya kubadilishana mikataba ya kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja.
.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau akifafanua jambo kwa wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba kati ya shirika hilo na timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Dk. Dau alisema katika uendeshaji wa kituo hicho, Real Madrid itakua na dhamana ya kushughulikia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez akifafanua jambo kwa wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba kati ya timu yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitahusisha wanafunzi 108 watakaogawanywa kwenye timu za chini ya umri wa miaka 13, 15, 17, 19, kikosi cha pili na timu ya wakubwa.
Bw. Gerald Sondo (kushoto) kutoka idara ya uwekezaji ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akitoa ufafanuzi kwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (wa nne kulia) kuhusu ujenzi wa kituo cha michezo katika eneo la Mwasonga, Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati Bw. Gutierrez na ujumbe kutoka timu ya Real Madrid walipotembelea kuona eneo la ujenzi wa kituo hicho hapo jana. NSSF imeingia mkataba na klabu ya Real Madrid ya Hispania wa kujenga kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalisha vipaji.
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeingia mkataba na
klabu maarufu duniani ya Real Madrid ya Hispania wa kujenga kituo cha michezo
kwa ajili ya kuzalisha vipaji.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo wa miaka 18, Dar
es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi huo
utagharimu Sh bilioni 16 na unatarajiwa kuanza kujengwa Mei mwaka huu na kwamba
utakamilika baada ya miezi 18.
Dk Dau alisema kituo hicho ambacho kitajengwa kwenye kijiji cha
michezo cha shirika hilo (NSSF Sports City), kitakuwa eneo la Mwasoga,
Kigamboni, Dar es Salaam.
“Tuna eneo la zaidi ya ekari 400 ambapo tutajenga viwanja, shule
ya michezo, nyumba za kuishi na maduka. Lengo letu tuzalishe na kuuza
wachezaji. Tunakusudia kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13, 18,
20, timu B na timu ya wakubwa,” alisema Dk Dau.
Alisema utekelezaji wa kituo hicho utaanza hivi karibuni kwa
kutumia majengo ya kukodi wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.
“Hivi hapa baada ya kusaini mkataba, utekelezaji utaanza kwa
kutumia majengo ya kukodi ambayo tunadhani yatakuwa maeneo ya Temeke na
tutakuwa tukitumia viwanja vya Karume na Uhuru,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF alisema katika kuendesha kituo hicho,
kila kitu kitafanywa na Real Madrid kuanzia masuala yote ya ufundi, kuwatambua
wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba
wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
“Sisi tunachukulia huu mradi ni uwekezaji na hatufanyi
hisani, itazingatia misingi ya biashara na faida kubwa ni kwamba NSSF itaongeza
kipato, lakini pia kituo kitatumika kuitangaza Tanzania kwa sababu
yatakayofanyika yataoneshwa kwenye televisheni ya Real Madrid,” alifafanua Dk
Dau.
“Lakini pia wakati umefika sasa kwa Tanzania kushiriki Kombe
la Dunia Qatar 2022, kama unaandaa vizuri vijana wa miaka 13 sasa mpaka mwaka
2020 wanaweza kuwakilisha vizuri kwenye mechi za kufuzu na mwaka 2022
wakashiriki Kombe la Dunia, wakikosa la Qatar, basi hata hizo zinazokuja, hiyo
pia ni moja ya madhumuni ya kituo hicho.”
Akizungumzia namna walivyofikia uamuzi wa kujenga kituo, Dk
Dau alisema wazo hilo lilipatikana Agosti mwaka jana na kisha likapelekwa
kwenye Mkutano wa Wanachama uliofanyika Arusha ambako waliazimia NSSF iwekeze
rasmi kwenye michezo kabla ya kuwasilishwa kwenye bodi na utekelezaji kuanza
kufanyika.
“Tulitembelea sehemu nyingi kuona wenzetu wanafanyaje.
Binafsi nilitembelea nchi kadhaa za Ulaya, nilienda kituo cha Manchester
United, Sunderland, Real Madrid kwa hapa Afrika nilikwenda Asec Mimosas (Ivory
Coast) na TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC) kuona wanafanyaje,
ziara ikazaa matunda kwani tulikubaliana na Madrid na ndio wamekuja kusaini
mkataba leo (jana),” alifafanua Dk Dau.
Naye Mkuu wa Vituo vya Michezo wa Real Madrid, Rayco Garcia
aliishukuru NSSF wa kuwa na mpango huo na kuahidi kufanya kazi ili kuipatia
Tanzania mafanikio.
“Tukifanikiwa kuwatoa vijana hao, Tanzania itaweza kushiriki
kwenye michuano mikubwa kama alivyosema Dk Dau, inabidi tufanye kazi ili vijana
wafanikiwe, wafike mbali,” alisema Garcia.
Mbali na Garcia ambaye pia ni kocha wa timu ya vijana chini
ya umri wa miaka 18 ya Madrid, wengine walioambatana kwenye msafara huo ni
Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo, Ruben de la Red, Kocha Mkuu wa timu za
vijana, Francisco Martin Ramos na Juan Jose San Roman Milla. Mwaka jana,
wachezaji wa zamani wa Real Madrid walifanya ziara nchini.
No comments:
Post a Comment